Print this page

Simbu atoa neno kifo cha Papa

Dar es Salaam

Na Arone Mpanduka

Mshindi wa pili wa mbio za Boston Marathon Alphonce Felix Simbu, amesema kuwa kifo cha Baba Mtakatifu Fransisko kimeleta simanzi kubwa ulimwenguni, hasa kwa Wakatoliki.
Akizungumza na Tumaini Letu kwa njia ya simu, Simbu alisema kwamba kifo chake pia kimeleta pigo kubwa kwa wanamichezo kwa kuwa alikuwa mpenda michezo enzi za uhai wake.
“Sijapata nafasi ya kumfuatilia sana kwa upande wa michezo, lakini nimekuwa nikisikia kwamba alikuwa mdau mkubwa wa michezo mbalimbali. Mimi ninamuombea kwa Mungu apate pumziko la milele,”alisema.
Hivi karibuni Simbu aliandika historia mpya katika mbio za kilomita 42 kwa kushika nafasi ya pili, mbio za Boston Marathon zilizofanyika huko Massachusetts, Marekani.
Alimaliza mbio hizo kwa muda wa saa 2:05:04, akitanguliwa kwa sekunde chache na Mkenya John Korir aliyeibuka kidedea kwa muda wa saa 2:04:45, ikiwa ni muda wa pili kwa kasi zaidi katika historia ya mbio hizo.
Katika mbio hizo, Simbu alionesha ushindani wa hali ya juu, akiibuka kinara kutoka kwa kundi kubwa la wanariadha waliotabiriwa kufanya vizuri, akiwemo Cybrian Kotut wa Kenya aliyeshika nafasi ya tatu na Mmarekani Conner Mantz aliyemaliza wa nne.

Rate this item
(0 votes)
Japhet