Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha
Japhet

Japhet

Waamini wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam wakiwa katika maandamano ya Ekaristi Takatifu baada ya adhimisho la Misa Takatifu ikiwa kama ishara ya kumtangaza Yesu wa Ekaristi kwa jamii nzima.Waamini wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam wakiwa katika maandamano ya Ekaristi Takatifu baada ya adhimisho la Misa Takatifu ikiwa kama ishara ya kumtangaza Yesu wa Ekaristi kwa jamii nzima.

Na Angela Kibwana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa mchango wa Sh milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa Kuu la Mt. Patrick jimboni Morogoro.
Mchango wa Rais Samia umewezesha kuezeka upya Kanisa hilo kongwe ambao ukarabati wa Kanisa hilo umefikia asilimia 98. 
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Lazarus Msimbe (SDS) ametoa shukrani kwa Serikali na wadau mbalimbali kwa ushirikiano walioonesha tangu kuanza kwa shughuli za ukarabati wa Kanisa kuu la Mtakatifu Patris jimboni humo.
Mhashamu Askofu Msimbe ametoa pongezi hizo kwa mahojiano maalum na Tumaini Letu ofisini kwake akisema kuwa anawashukuru pia waamini wa Kanisa hilo walioshiriki kuchangia ukarabati wa Kanisa hilo huku akiwapongeza uongozi wa Halmashauri Walei kwa umoja na mshikamano wao.
Aidha Mhashamu Askofu Msimbe alisema kuwa baada ya hatua zote muhimu kukamilika kukarabati Kanisa hilo ikiwa ni pamoja hatua itakayofuata ni kutabaruku kutokana na kugusa sehemu mbalimbali za Kanisa hilo nje na ndani, maeneo matakatifu ya Kanisa hilo kuguswa wakati wa ukarabati huo.
“Napenda kutoa shukurani kwa Mwenyezi Mungu ambaye ametupa nguvu na kutuwezesha kimawazo, ni Mungu mwenyewe amefanya hii kazi kwa ajili ya nyumba yake. Nipende kutoa shukurani nyingi kwa ushirikiano tuliokuwa nao kwa Serikali katika suala zima la ukarabati wa Kanisa, niwashukuru viongozi na waamini wote walioshiriki kuchangia ukarabati huu,” alisema Askofu Msimbe.

Na Waandishi Wetu

Waamini wameaswa kutopokea Ekaristi Takatifu kimazoea huku wakia hawana maandalizi mazuri kiroho.
Ujumbe huo umetolewa na maaskofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo Mhashamu Sana Jude Thaddeus Ruwa’ichi na Askofu Msaidizi Mhashamu Henry Mchamungu kwa nyakati tofauti wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana Wetu Yesu Kristo
Akiwa katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu, Mhashamu Sana Jude Thaddeus Ruwa’ichi alisema waamini wanapaswa kukumbuka kuwa Ekaristi Takatifu si kitu cha kupokelwa kimazoea bali kinahitaji tafakari na maandalizi ya kiroho.
“Mnatakiwa kutambua kuwa Ekaristi siyo kitu cha mazoea wala cha kubahatisha bali ni adhimisho Takatifu sana na kuu la wokovu wetu,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Aidha alisema kuwa kila mtu anatakiwa kufahamu ni nini anafanya pale kwenye adhimisho la Misa Takatifu kwa sababu ndipo kwenye kiini cha imani.
Mbali na hayo aliwasisitiza waamini kuziishi Sakramenti kwa imani, upendo na ibada kwa ajili ya kupata uzima wa kimungu.
 Alisema kwamba wana wa Israeli walipokuwa jangwani walimlalamikia Musa kwa kuwa na njaa na kusema ni bora angewaacha utumwani kuliko kuwapeleka jangwani jambo ambalo alisema lilionesha jinsi binadamu walivyo vigeugeu.
Askofu Ruwa’ichi aliwataka waamini wafahamu kwamba utumwa ni mateso japo kuwa wanadamu wengi ni vigeugeu wanaoweza kutakani kurudi utumwani wanapopata shida katika safari ya ukombozi.
Askofu Ruwa’ichi aliwataka waamini watambue kuwa wao ni Taifa jipya la Mungu na wako hivyo kwa sababu ya sadaka ya Yesu Kristu ya kukubali kujishusha na kutwaa ubinadamu na kufa kifo cha aibu.
Sambamba na hayo alisema kuwa Yesu Kristu alikubali kuteswa na kufa msalabani kwa ajili ya kutaka kukomboa ulimwengu kutoka katika dhambi na kabla ya kufa kwake aliweka Ekaristi Takatifu ikiwa alama ya upendo wake mkuu kwa wanadamu.
Pia alisema kuwa Ekaristi ni ukumbusho wa mateso,kifo  na ufufuko wa Yesu Kristu kwani katika Ekaristi kila mtu amepewa sadaka ya ukombozi yenye kuwapatanisha watu na Mungu.
Askofu Ruwa’ichi aliendelea kusema kuwa Ekaristi ni Sakramenti Kuu ya wokovu ambayo Yesu Kristu aliitoa kama zawadi kwa mitume wake kwa ajili ya kuiadhimisha na kupokea mwili na damu ya Yesu Kristu.

Na Mwandishi Wetu

Serikali imeendelea kuimarisha hatua za kudhibiti, na kutokomeza tatizo la mbegu feki nchini, kupitia mifumo ya kisasa ya uthibitishaji wa ubora, ukaguzi wa mara kwa mara, pamoja na utoaji wa elimu kwa wakulima.
Akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Onesmo Merdson Mnkondya, kuhusu mpango wa Serikali wa kukomesha mbegu feki nchini, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema kwamba, kwa mujibu wa Kifungu cha 15 cha Sheria ya Mbegu (Sura ya 308, Toleo la Urekebu la mwaka 2023), mbegu zote zinazouzwa nchini, zinapaswa kuthibitishwa ubora wake, na Taasisi ya Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
Silinde amesema kuwa, TOSCI imeanzisha matumizi ya lebo za kielektroniki, zinazotolewa kwa kampuni za mbegu, ili kuwasaidia wakulima, kuhakiki uhalisia wa mbegu wanazonunua. Kupitia mfumo huo, mkulima anaweza kukwangua lebo maalumu, iliyowekwa kwenye kifungashio cha mbegu, na kuingiza namba husika kwenye simu yake ya mkononi, ili kupata taarifa za uthibitisho wa mbegu hizo.
Matumizi ya teknolojia hiyo, yameleta mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya mbegu feki, ambapo matukio yaliyoripotiwa yamepungua kutoka 325 mwaka 2014/2015, hadi kufikia matukio 10 pekee mwaka 2023/2024.
Mbali na matumizi ya teknolojia, Serikali kupitia TOSCI, inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, katika maduka yanayouza mbegu nchini. Katika ukaguzi uliofanyika kati ya Julai 2025 na Januari 2026, wafanyabiashara 13 walibainika kujihusisha na uuzaji wa mbegu feki, au mbegu zisizokidhi viwango vya ubora.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Silinde, kesi moja tayari ipo mahakamani, huku uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wengine 12 ukiendelea, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wakulima, kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora, na namna ya kutambua mbegu feki. Kupitia Kampeni ya Mali Shambani, wakulima 5,822 walipatiwa elimu hiyo, huku wakulima wengine 6,763, wakipata huduma na ushauri kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call Center), katika kipindi cha Novemba 2025 hadi Januari 18, 2026.
Silinde amesisitiza kwamba, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya mbegu, ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na salama, sambamba na kuwalinda dhidi ya wafanyabiashara, wanaojihusisha na uuzaji wa mbegu feki.

Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watumishi wa Umma kote nchini, watambue na wathamini nafasi za kazi walizonazo, kwamba ni huduma wanazotakiwa kuzitoa kwa wananchi.
“Ninapokuwa kwenye hizi ziara, nimekuwa ninawaambia watumishi wenzangu walioko maofisini kwamba, kuwa kwenye hizi nafasi ni huduma, ni utumishi, na kuwazungusha watu wanapotaka hizo huduma ni ushamba,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa wito huo Ijumaa, Juni 05, 2026, wakati akizungumza na wakazi wa Jimbo la Isimani, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kijiji cha Isimani, Kata ya Kihorogota, Wilaya ya Iringa, Mkoani Iringa.
“Tutahakikisha hoja zote zinazotolewa na wananchi zinafanyiwa kazi, kwa sababu huo ndio wajibu wa Serikali, kuwatimizia wananchi yale yaliyo mahitaji yao ya kila siku, ili waweze kufanya kazi wakiwa na utulivu. Nitoe rai kwa ofisi zote za umma, tuyazingatie hayo,” alisisitiza.

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa vijana wakishapokea Sakramenti ya Kipaimara, hawawi watoto tena, bali wanakuwa Wakristo wakomavu, na wenye kuwajibika katika kuishuhudia Injili ya Yesu Kristo.
Hayo yalisemwa hivi karibuni, na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi - OFMCap, wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara, katika Parokia ya Mtakatifu Nicholaus wa Tolentino - Msingwa, jimboni humo.
“Kama kwenye Ubatizo walizaliwa, kwenye Kipaimara wanakamilishwa, wanafanywa kuwa Manabii, wanakabidhiwa Utume, wanapewa jukumu la kuishuhudia Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo;
“Kwa hiyo vijana wapendwa, wanangu wapendwa, leo mnaanza ngwe mpya, ngwe mpya ya safari yenu ya imani. Kuanzia leo mkiwa mnarudi nyumbani, mkiwa mmepata Kipaimara, jitambueni kuwa ninyi sio watoto tena, utoto mtaucha pale kwenye mlango wa Kanisa. Na Paroko naomba kuanzia leo usiwaite tena watoto, waite Waimarishwa, waite watu wakomavu, waite watu wenye kuwajibika,” alisema Askofu huyo.
Aidha, Askofu Mkuu aliwasihi vijana hao kutokumhadaa Kristo, na kwamba wamshuhudie kwa maneno, matendo na kwa maisha yao yote.
Sambamba na hayo, aliwasisitiza kutoona aibu kusema mbele za watu kwamba, wanamuungama Kristo katika maisha yao, kwani kazi kubwa wanayotumwa kuifanya, ni kuitetea imani yao.
“Nanyi vijana wapendwa, hakikisheni kwamba hamumhadai Kristo, bali mnamshuhudia kwa maneno, kwa matendo, na maisha yenu yote. Na msione haya kujibainisha kuwa Wakristo, msione haya kusema kwamba, ‘Mimi namuungama Kristo Mwokozi wangu aliyeteswa, aliyekufa na aliyefufuka’. Simameni imara, simameni kidete kuujenga Ufalme wa Kristo,” alisema Askofu huyo.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitoa wito kwa wazazi, kushirikiana na watoto wao, katika kuuendeleza utume huo unaowapasa.
Pia, aliwasihi Mapadri, Makatekista pamoja na Viongozi wa Kamati Tendaji, kuhakikisha kuwa wanashikamana na kusindikizana na vijana hao, katika safari ya kuujenga Ufalme wa Mungu.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Msingwa, Padri Geofrey Mtitu - OSA, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi, kwa kufika parokiani hapo, na kuadhimisha Misa hiyo Takatifu.

Na Mathayo Kijazi

Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) ngazi ya Taifa, kimefanya Uchaguzi Mkuu, na hivyo kuwapata viongozi wapya, watakaoongoza chama hicho hadi mwaka 2029.
Akizungumza hivi karibuni, katika Mkutano wa makabidhiano, uliofanyika katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwenyekiti mpya wa VIWAWA Taifa, Elia Mshana, alisema kwamba Dira Kuu waliyonayo ni kumjenga kijana mwenye nafasi katika jamii na katika Kanisa.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa walezi, wanaowalea vijana hao kuanzia ngazi za Parokia pamoja na Majimbo, kuwapa nafasi vijana katika Halmashauri za Walei, kwani wanaweza kufanya kazi katika maeneo hayo.
“Wito wangu kwa walezi wanaowalea vijana, kuanzia ngazi za Parokia mpaka Majimbo, Wakurugenzi wote wawape nafasi vijana. Lakini pia katika Halmashauri za Walei kwenye Parokia zao, vijana wapewe nafasi kubwa zaidi, kwa sababu wakiaminiwa wanaweza,” alisema Mwenyekiti, Elia Mshana.
Aliongeza kwamba, imekuwa ni desturi ya Viongozi wa VIWAWA Taifa, kukutana Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kufanya makabidhiano kati ya Viongozi Wastaafu na Viongozi wapya, kwa ajili ya kuanza rasmi majukumu yao ya kiuongozi.
Mwenyekiti huyo aliwashukuru viongozi waliomaliza muda wao, kwani wamefanya kazi kubwa, katika kipindi chote cha uongozi wao, wakiahidi kwenye kuendeleza yale yaliyoanzishwa na uongozi uliopita.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mstaafu VIWAWA Taifa, Mwalimu Leonard Mapolu, alimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufanya shughuli zao za kitume, katika Chama hicho tangu walipoanza mwaka 2023 mpaka 2026.
Mwalimu Leonard Mapolu kutoka Jimbo Katoliki la Shinyanga, ambaye pia ni Mratibu wa VIWAWA Afrika, alisema kwamba katika utume wanashirikishwa, hivyo wana wajibu wa kutii na kufuata miongozo ya Kanisa, lengo likiwa ni kumpeleka Kristo kwa wengine.
Pia, alitoa wito kwa vijana kuendelea kushiriki Makongamano mbalimbali ya Kanisa, pamoja na Semina pale wanapopata nafasi, kwani kupitia matukio hayo, wanapata utatuzi wa changamoto zao.
Mwalimu Mapolu alitoa wito kwa Viongozi wapya wa VIWAWA, kuendeleza mradi wao wa kitenge cha VIWAWA, hasa katika kukizalisha kwa ubora mzuri, kwani kwa kufanya hivyo, watakiendeleza vema Chama hicho.
Naye Katibu Mstaafu wa VIWAWA Taifa, Benedict Agustino, alimshukuru Mungu kwa kutumikia katika mihula miwili, ambapo alianza mwaka 2020–2023, kisha 2023-2026, akisema kuwa katika vipindi hivyo, walijitahidi kutekeleza majukumu yao kama ilivyokusudiwa.
Kwa mujibu wa Benedict, miongoni mwa miradi waliyofanikiwa kuitekeleza, katika kipindi cha uongozi wao, ni pamoja na kununua shamba la VIWAWA, lenye ukubwa wa ekari 50, lililopo katika Jimbo Katoliki la Singida, pamoja na shamba jingine lililopo Kibiti, ndani ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu

Wakurugenzi na wawakilishi wa vyombo vya habari vya Kanisa nchini Tanzania wamekutana na wawakilishi wa Kurugenzi ya Mawasilano ya Vatican na kujadili kuhusu ushirikiano wa pamoja kwa lengo la kukuza na kuimarisha mawasiliano kati ya Kanisa Katoliki ulimwenguni na jamii.
Kikao hicho kimefanyika hivi karibuni katika Ubalozi wa Vatican nchini uliopo Jijini Dar es Salaam.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi wa Mawasilano  wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC)  Padri Faustine Furaha ameeleza namna vyombo vya habari vya kanisa vinavyofanyakazi hapa nchini.
Alisema kupitia vyombo hivyo Kanisa limefanikiwa kuwafikia zaidi ya waamini Mmilioni 30 na kuwapatia ujumbe wa Injili.
Kupitia kikao hicho wawakilishi hao kutoka Vatican walieleza miradi ya kuboresha ushirikiano na mawasiliano baina ya Kanisa Katoliki na jamii ikihusisha vijana wenye umri usiozidi miaka 35.
Walieleza kuwa wahusika katika mradi huo mradi huo watatakiwa kuwa Shahada ya Mawasiliano,  wafanyakazi wa taasisi ya Kanisa Katoliki na wenye uwezo wa kuzungumza lugha ya Kiingereza.
Wameutaja mradi wa pili kuwa ni Mafunzo ya Muda wa miezi mitatu kwa Masista wa Kanisa Katoliki ulimwenguni ambao wana taaluma ya Mawasilano, wenye uzoefu wa kazi kwenye radio, Televisheni, gazeti na mitandao ya kijamii.
Vyombo vya mawasiliano vilivyoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Kurugenzi ya mMawasilino TEC, Tumaini Media, Jugo media, Radio Maria, Radio Habari Njema Mbulu, na gazeti la Kiongozi.

Dar es Salaam

Na Mathayo Kijazi

Mkurugenzi wa Utume wa Walei Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Vitalis James Kassembo amezindua kitenge cha Chama cha Kitume cha Wajane na Wagane, akiwataka kuutumia vema mradi huo katika kuendeleza utume kupitia chama chao.
Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika ofisi ya Halmashauri ya Walei iliyopo katika  viunga vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jimboni humo.
Padri Kassembo aliwaasa wote watakaonunua kitenge hicho kuwa waaminifu, akisema kwamba anayechukua vitenge vya idadi fulani, arudishe fedha inayolingana na idadi ya vitenge hivyo.
“Mradi huu utusaidie pia kuendeleza utume. Lakini pia kama wanautume kuweza kujitawala vizuri sisi kama wanachama wa chama hiki. Maana yake tunaongea kuhusu uaminifu katika yale ambayo tutakuwa tumekabidhiwa, kama umekabidhiwa vitenge kumi, basi urudishe fedha ya vitenge kumi, usilete kona kona, kwa sababu ukileta kona kona, tunakwama wote,” alisema Padri Kassembo.
Aliwasisitiza kuutumia mradi huo kuwaunganisha na kuwafanya wawe wamoja zaidi, akiwaasa kutotengana kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kutokuwa waaminifu.

LILONGWE, Malawi

Chansela wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha Malawi, Askofu Martin Anwel Mtumbuka, ametoa mwito wa kuanzishwa kwa wahitimu, wanaozingatia uadilifu na maadili thabiti, pamoja na ubora wa kitaaluma.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa 25 wa Chuo Kikuu, kwa ajili ya utoaji wa Astashahada, Stashahada na Shahada, uliofanyika Ijumaa iliyopita, Askofu Mtumbuka alieleza wasiwasi wake, kuhusu idadi inayoongezeka ya watu walioelimika, ambao hawana uadilifu katika majukumu yao ya kitaaluma na utumishi wa umma.
“Tayari tuna watu wa kutosha walioelimika, lakini kwa kusikitisha, tuna watu wengi sana waliopotoka. Tunachohitaji sasa ni wanaume na wanawake walioelimika, ambao watahudumu kwa uaminifu, uadilifu na huruma,” alisema Askofu Mtumbuka.
Msemaji wa kuanza kwa Sherehe hiyo, Mheshimiwa Jaji Annabel Mtalimanja, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC), pia aliwasihi wanafunzi waliohitimu hivi karibuni, kukataa ufisadi na rushwa, akielezea kuwa ni vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya taifa.