Print this page

Simameni kulinda tunu msingi za ndoa na familia - Papa

VATICAN CITY

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni, Baba Mtakatifu Leo XIV, amewataka Wahispania kuendelea kuwa ni mahali pa watu kukutana katika utamaduni, ili kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, chemchemi ya Injili ya matumaini, huku wakisimama kidete, kudumisha na kulinda tunu msingi za ndoa na familia.
Aliyasema hayo katika hotuba yake kwa Bunge la Hispania, akiwa katika ziara yake ya kitume nchini humo, huku akikazia utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuongozwa na kaulimbiu ya Umoja wa Ulaya, umoja katika utofauti, mambo yanayounda amana na utajiri wa watu wa Mungu.
Ikumbukwe kuwa Baba Mtakatifu Leo XIV, kuanzia Juni 6 hadi 12, 2026, anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania, kwa kunogeshwa na kaulimbiu: “Alzad la mirada” Yaani “Inueni macho yenu.”
Sambamba na hayo, Papa alikutana na Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez Pérez-Castejón, ambaye amekuwa madarakani tangu Juni 2, 2018, na ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Hispania, ambapo alitumia nafasi hiyo pia, kukutana na kuzungumza na Bunge la Hispania, na baadaye kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania (Conferencia Episcopal Española: CEE)”.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Leo XIV, alikutana pia na kuzungumza na Jumuiya ya Jimbo Kuu la Madrid, nchini Hispania, ambapo Mama Kanisa anatembea bega kwa bega na binadamu, anashiriki matumaini na madonda yake, anaendelea kusikiliza na kujibu maswali msingi ya binadamu wa kila nyakati, na kwamba kuna tofauti ya utendaji kati ya Kanisa na Serikali.
Aliongeza kwamba utu, heshima na haki msingi za binadamu, ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia kuwa uhuru, ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu.
Alibainisha kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya sheria, kanuni maadili na utu wema, na kuongeza kuwa uongozi unabeba dhamana kubwa ya haki na uwajibikaji.
Alisisitiza kuwa vijana wa kizazi kipya, wanapaswa kufundishwa kutafuta na kupenda ukweli, na kwamba watu waondokane na tabia ya ubaguzi na maamuzi mbele, bali wajitahidi kujenga haki jamii.
Sera na mikakati ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji inajikita katika misingi mikuu minne: Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha, ambapo mwongozo huo unalenga kutetea utu, kuzuia nyanyaso na kuleta mshikamano kupitia huduma za kiroho na kijamii.
Papa alisema kuwa wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaokosa haki, amani na usalama; ni watu wanaosiginwa na umaskini, njaa, maradhi sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi, akitoa wito kujenga utamaduni wa mshikamano wa dhati.
Ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, Papa Leo XIV alisema kwamba, kuna haja ya kuheshimiana na kuthaminiana, kwani ulimwengu umekumbwa na mgogoro wa maisha ya kiroho na kitamaduni.

Rate this item
(0 votes)
Japhet