Na Remigius Mmavele
“Chef Djouna anataka kuniuzia gari ili nishuke nalo Kinshasa.” Pepe Kalle hakumjibu kwa hasira bali alimwita mbele yake, akamgeukia Dokolos na kuuliza: Kwani tatizo liko wapi sasa kwa ndugu yako kukuuzia gari?
Mwisho wa yote, Dokolos alinunua gari na walipofika jijini Kinshasa ikawa gumzo ya mjini Dokolos anajivinjari na gari lake BMW pande zote za Jiji la Kinshasa. Kuona hivyo, Pepe Kalle hakusita kwenda kwenye vituo vya radio na televisheni huku akisema: “Huyu hapa Dokolos anaendesha gari lake hovyo hovyo. Anazunguka na gari lake kila mahali. Asije akafanya makosa barabarani ikaja kusababisha ajali.”
Pepe Kalle aliliomba Jeshi la Polisi lifanye kazi yake, akawaambia mkamateni huyo maana naamini anaendesha gari wakati hata leseni hana. Alieleza kwamba ameshawahi kushutumiwa bure kuhusiana na kifo cha Emoro akasema nikabebeshwa msalaba kana kwamba mimi ndiye niliyemuua.
Alisikika akisema wala sitopendelea tena kuhusishwa na mambo ambayo sina hatia nayo na wala siyajui, Bileku anasisitiza kwamba naweza kusema wazi kwamba mali niliyoipata katika maisha yangu, niliipata kutokana na kazi yangu, lakini zaidi pia kwa ushauri wa Pepe Kalle.
Anasimulia kwamba pesa aliyoipata aliizidisha kupitia biashara ndogo ndogo na siku moja walipokuwa Uswisi alikuwa ametoka jijini Kinshasa akiwa na kiasi cha fedha Yuro 15,000. Walipotakiwa kwenda nchini Ufaransa maafisa wa forodha waliwazuia kwa sababu alikuwa na zaidi ya Yuro 10,000 taslimu wakati kiwango kinachoruhusiwa ni Yuro 10,000 pekee. Ilibidi azigawe kwa wenzake zile Yuro 5,000 za ziada akawapatia Vieux Boeing, Papillon, Gode Lofombo na Dokolos.
Wengine hawakuamini kwamba pesa hizo zilikuwa za kwake wakawa wanasema kimya kimya kwamba ni pesa za kundi amepewa na Pepe Kalle ili awapatie wanamuziki wenzake. Mwisho wake hapo mpakani wala hawakuweza kupita maana baada ya uchunguzi walikamatwa kwa kutumia pasipoti bandia.
Bileku anasema kuwa yeye alikuwa mtu wa karibu zaidi sana na Pepe Kalle kuliko mwanamuziki yeyote, anakumbuka kwamba Pepe Kalle alikua akipendelea sana wakati anaimba, sauti yake iwe nakaukwaruzo kidogo, isiwe laini kupita kiasi. Mara nyingi alikua akizungumza na Bileku kwa macho pekee naye akawa anamwelewa vilivyo.