Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Viongozi wa Halmashauri ya Walei na Waamini wa Parokia ya Bikira Maria wa Mateso - Mbezi Msakuzi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Ekaristi Takatifu kwa watoto 90, iliyoadhimishwa parokiani hapo hivi karibuni.

Waamini wa Kanda ya Bethlehemu, Parokia ya Thomas More, Mbezi Beach, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika maandamano ya kutembeza Msalaba wa Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndogo, baada ya kukabidhiwa kutoka kwa Paroko wa Parokia hiyo, Padri Ladislaus Kapinda (mwenye kanzu).

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Mikael Malaika Mkuu, Kawe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Bonus Ngoo, akiwapaka waamini Majivu wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jumatano ya Majivu, iliyoadhimishwa parokani hapo.

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Roho Mtakatifu, Segerea, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Amedeus Babu akiwapaka waamini Majivu wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jumatano ya Majivu iliyoadhimishwa parokani hapo.

Mwalimu na Mlezi wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua – Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba, Padri Roland Kashaga (katikati kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa Komunio ya Kwanza baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya watoto 90 kupokea Ekaristi Takatifu, iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Mateso - Mbezi Msakuzi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Kulia katikati ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Fregiel Massawe. (Picha na Yohana Kasosi)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan akimpatia Baba Mtakatifu Fransisko zawadi wakati Rais na Ujumbe wake wa Tanzania ulipofanya ziara ya kitaifa, na kuzungumza na Baba Mtakatifu mjini Vatican. (Picha kwa Hisani ya Ikulu)

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Wakati Mfungo wa Kwaresma ukiwa umeanza, Wakristo wametakiwa kujikita katika toba, sala, kufanya matendo ya huruma na upendo katika kipindi chote cha mfungo huo wa siku 40.
Wito huo ulitolewa na Maaskofu, na Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakati wakitoa homilia katika Maadhimisho ya Misa Takatifu zilizoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu; Parokia ya Mtakatifu Petro – Oysterbay; Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja – Boko; na Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, aliyeadhimisha Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, alisema kuwa ni vyema kujikita katika matendo ya huruma na upendo, huku wakimrudia Mungu.
“Ndugu zangu, Neno la Mungu kwa msisitizo mkubwa, litatualika na kutuasa kujikita katika toba, kujikita katika sala, kujikita katika huruma na upendo tukimrudia Mungu. Hizi ni zama za mtandao. Kishawishi kikubwa, ni kule watu kutaka kufanya mambo yaonekane mtandaoni,” alisema Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu alisema kuwa toba ya kweli siyo mambo ya mtandao, bali ni mabadiliko ya ndani, kuongoka rohoni, kumrudia Mungu kwa dhati, pamoja na kuanza upya, kwani hilo ndilo waliloaswa katika masomo waliyoyapitia katika Misa hiyo.
Pia, aliwasisitiza Waamini kufahamu kwamba majivu ni kielelezo cha toba, akisema kuwa watu wa kale walipofanya toba, walijipaka majivu, wakajivika magunia, na wakatembea katika unyofu na uadilifu.
Aliongeza kuwa Wakristo wanapopakwa majivu na kufanya toba, hawatakiwi kufanya maonyesho, bali wamwombe Mungu kwa mioyo radhi ili awahurumie dhambi zao, awajaze neema yake, na awajalie wajikite katika safari ya kipindi cha Kwaresma, huku wakimrudia Mungu.
“Sisi tunapojipaka majivu tukifanya toba, hatutaki kufanya maonyesho, bali tunataka kumwomba Mungu kwa mioyo radhi, atuhurumie dhambi zetu, atujaze neema yake, atujalie tujikite katika safari ya kipindi cha Kwaresma, tumrudie Mungu tukimwomba toba kwa ajili ya dhambi zetu, kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, na yote yale yaliyo machukizo kwake.
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Parokia ya Mtakatifu Petro – Oysterbay jimboni humo, aliwataka Wakristo kuwa wanyenyekevu, huku wakitambua mipaka yao, udhaifu wao, na kufahamu kwamba Mungu ni muhimu katika maisha yao.
Katika homilia yake, Askofu Msaidizi Musomba aliwataka Waamini katika kipindi hiki cha Kwaresma, kuombana msamaha pale wanapokoseana, na pale wanapomkosea Mungu, ili waanze upya na waendelee vizuri na maisha yao.
Naye Paroko wa Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja – Boko, jimboni humo, Padri Emmanuel Makusaro aliwaalika Waamini kufunga matendo ya dhambi pamoja na kuwasaidia wahitaji, kwani hapo Kwaresma ndipo itakuwa na nguvu zaidi.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo, Padri Cornelius Mashare alitoa wito kwa Waamini kutafakari, huku wakiishi maisha ya unyenyekevu na yenye kumpendeza Mungu katika kipindi hiki cha Kwaresma.

DODOMA

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameiagiza Taasisi zote za ununuzi nchini (Serikali na Binafsi) kuhakikisha zinatoa kipaumbele katika manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa Watanzania, na wazingatie kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo na makundi maalum.
Dk. Biteko alisema hayo Jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (Public Procurement Regulatory Authority: PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (National Economic Empowerment Council: NEEC) ili kujenga ushirikiano unaolenga kuchochea ushiriki wa Wafanyabishara Wadogo, wa kati na Makundi Maalum, katika masuala ya ununuzi wa umma.
“Kusainiwa kwa hati hii leo, kunazidi kuboresha mazingira ya Watanzania kushiriki kwenye uchumi wa nchi yao, hasa watu kutoka makundi maalum. Haya ni  maelekezo ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wote wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, hivyo NEEC, PPRA, Taasisi nyingine za Serikali na Binafsi, wawezesheni Watanzania kushika uchumi wa nchi na muone fahari katika hili,” alisema Dk. Biteko.
Kupitia hafla hiyo, Dk. Biteko aliitaka PPRA kuzidi kuboresha huduma zake kwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa rufaa zinazowasilishwa kwenye mamlaka hiyo, hususan zile zinazohusisha waombaji wa zabuni kutoka makundi maalum ili kuchochea kasi ya ukuaji wa Uchumi wa mtu mmoja mmoja, na hatimaye Uchumi wa Taifa.
Alizitaka mamlaka hizo kujikita zaidi katika uwezeshaji wa wananchi kwa kutoa elimu, badala ya kubaki kuwa wadhibiti pekee.
Dk. BIteko aliongeza kusema kwamba NEEC na PPRA kufanya tathmini na kutoa tuzo kwa watoa huduma wanaofanya vizuri katika uwezeshaji wa makundi maalum suala litakalochagiza ushindani miongoni mwa watoa huduma, na hatmaye kukuza uchumi.
Alisema kuwa makubaliano hayo yatatumika kama jukwaa la kuwahamasisha watu wa kundi hilo kushiriki na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja, kuimarisha wigo wa walipa kodi, na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Aliipongeza PPRA kwa kuweka kanuni ya ushirikishaji makundi maalum kwenye manunuzi ambayo imeelekeza kuwa asilimia 30 ya zabuni zote zitolewe kwa washiriki kutoka makundi maalum, ambao ni wanawake,vijana, wazee na wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, alisema kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya PPRA na NEEC ni ushahidi wa namna Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kwa dhati kushikirisha makundi ya watu maalum kwenye uchumi na ujenzi wa Taifa.
Alisema kuwa makubalinao hayo yataongeza ushiriki wa makundi maalum kwenye manunuzi ya umma, na hii itaongeza uwezo wa Watanzania katika uzalishaji malighafi na bidhaa pamoja na utoaji wa huduma ndani ya nchi.

TUNDURU

Na Salimu Juma

Wananchi wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Rural Water Supply and Sanitation Agency: RUWASA) kwa kutimiza ahadi yake ya kuwapatia maji safi.
Walisema kuwa kwa miaka mingi vijiji vya Wilaya ya Tunduru vilikabiliwa na changamoto kubwa ya huduma ya maji safi na salama kutokana na wananchi kutumia maji ya visima na mito, ambayo hayakuwa salama kwa afya zao.

VISIGA, PWANI

Na Mwandishi wetu

Wabatizwa nchini wametakiwa kuitambua hadhi yao, kwani wao ni hekalu la Mungu, hivyo hawatakiwi kuligeuza hekalu hilo kuwa jalala la dhambi.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi alitoa wito huo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa la Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria – Visiga, mkoani Pwani.
“Tusimshangae sana Suleimani, tuchote fundisho kutoka kwake, kwa nini? Kwa sababu hata sisi tuna kibali machoni pa Bwana, siyo tu kwamba Mungu ameturuhusu tujenge hekalu, bali ametupa haki ya kuwa hekalu lake. Kila Mbatizwa anayo hadhi ya kuwa hekalu la Roho Mtakatifu…
“Kwa hiyo, ewe Mbatizwa, tambua hadhi yako, tambua wito wako, tambua heshima yako, na tunza utakatifu wako mbele za Mungu. Usikubali kukengeuka na ukaligeuza hekalu la Mungu kuwa jalala la dhambi,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu aliwaasa Waamini kumbeba Kristo na kumpeleka kwa wengine, kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wameinjilisha na wamekuwa wajumbe wa Habari Njema katika maisha yao.
“Maria huyu ni mfano wetu, kwani sisi pia tunaitwa tumbebe Kristo na tumpeleke kwa wenzetu. Kwa maneno mengine, tunaitwa tuwe wainjilishaji, tuwe wajumbe wa Habari Njema,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aliwashukuru Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), kwa majitoleo yao yaliyoweza kujenga kanisa hilo lililotabarukiwa, akisema kuwa kujituma kwao na kwa ukarimu wao, ndiko kumefanikisha kukamilika kwa ujenzi huo.
Vile vile, Askofu Mkuu aliagiza kuwa kanisa hilo lililotabarukiwa, lisigeuzwe kuwa ukumbi, bali liwe tu kwa ajili ya mambo ya Mungu na Taifa lake Takatifu.
Wakati huo huo pia, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliialika Jumuiya ya Seminari kulitunza kanisa na altare hiyo, ili viendelee kutumika kama ilivyokusudiwa.
Aliwataka Waseminari kutokuona aibu ya kutoa ushuhuda wao, bali wajivunie kwamba wamepata heshima ya kuwa Wakristo, hivyo hawana budi kuutunza uwakfu wao.
“Kwenu Waseminari, tunza uwakfu wako, jilinde kama hekalu Takatifu, toa harufu ya utakatifu na usione aibu kutoa ushuhuda wa Ukristo wako. Jivunie ya kwamba umepata heshima ya kuwa Mkristo, ishi heshima hiyo na shuhudia heshima hiyo na lijenge Kanisa la Kristo,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake, Gombera wa Seminari Ndogo ya Visiga, Padri Philip Tairo, alisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwapa nguvu ya kufanya kazi hiyo ya ujenzi wa kanisa ambayo waliianza Novemba mwaka 2022.
Naye Mwenyekiti WAWATA jimboni humo, Stella Rwegasira alimshukuru Askofu Mkuu kwa kuunganisha tukio lao la shukrani pamoja na la kutabaruku kanisa hilo, huku akisema kuwa kwao kama WAWATA, hiyo ni siku ya furaha kubwa.