Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Fransis wa Asizi, Kongowele, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyofanyika parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakristo wametakiwa kuepuka kuwapenda wanzao kwa sababu ya vitu au misaada wanayopata, bali wafanye hivyo kwa sura na mfano wa Mungu.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Padri Dickson Sambala- OCARM, wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuwashukuru Wanaparokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kwa kumlea katika kipindi cha Uchungaji wake, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Unaposali, unatengeneza matunda ya upendo, kwani unapopenda, unatengeneza matunda ya huruma kwa ajili ya kuwahudumia wengine, na unapowahudumia wengine, unatengeneza amani ndani ya mioyo ya watu….;
“Unatakiwa kuondoa matabaka kati ya walio nacho na wasio nacho. Unawaheshimu watu kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini siyo kwa sababu ni matajiri, siyo kwa sababu wanatusaidia hiki au kile,” alisema Padri Sambala.
Katika homilia yake, Padri Sambala aliwaasa Wakristo kuepuka kuwa na upendo wa masharti, kwani upendo huo huchagua baadhi ya watu.
Aliongeza kuwa upendo wa kweli ni ule wa kidugu unaowafanya watu kuwa kitu kimoja, na kuwafanya kupokea baraka za Mungu.
Aidha, Padri Sambala aliwashukuru waamini wa Parokia hiyo kwa ushirikiano waliompatia na kuipongeza Tumaini Media kwa kazi kubwa ya uinjilishaji kupitia vyombo vyake vya habari.
Naye Roselinda Msele, Katibu wa Kamati ya Liturjia Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, aliwaomba watu wenye mapenzi mema kuchangia ujenzi wa kanisa jipya la Parokia hiyo, ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Naye Diana Peter, Mlezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu wa Parokia hiyo, aliwasihi wazazi kuendelea kuwalea watoto katika maadili ili kupata watu wema.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari – Bombambili, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Sheejan Kallarakkal- MSFS, amesema kwamba uwepo wa wazee katika Kanisa, jamii, na hata familia, ni hazina kwa sababu wana uzoefu wa kimaisha.
Padri Sheejan alisema hayo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa Wazee na Wastaafu wa Dekania ya Pugu, kwa mengi aliyowatendea, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Uwepo wao wazee katika Kanisa, jamii, na hata familia, unaleta maana kubwa, na una faida kwa sababu wana uzoefu mkubwa katika kusimamia mambo…Kwa hiyo, ukiwa mzee una fursa fulani katika maisha yako, hivyo tumia uzee wako kurithisha imani kwa vijana na watoto,” alisema Padri Sheejan.
Aidha, aliwakumbusha wazee kutambua kwamba wana jukumu la kusambaza ukweli na mafundisho ya Kanisa kwa vijana, kwani wanakubalika kwa matendo na sauti zao.
Awali akitoa homilia yake, Padri Sheejan aliwaomba wazee hao kuwakemea vijana wanapokengeuka, ili kujenga heshima kwa watu wote.
Aliwasihi wazee na wastaafu hao kumwomba Mungu ili waendelee kuwa watu wa hekima na maarifa, yaani busara ndani ya Kanisa na jamii zao kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Wazee na Wastaafu wa Dekania ya Pugu, Cosmas Sokoni, aliwashukuru wazee wote walioshiriki Misa hiyo, akiwasihi wazidi kushirikiana ili chama cha Wazee na Wastaafu katika Dekania hiyo kikue zaidi.
“Kwanza, nichukue nafasi hii kuwashukuru wazee wenzangu wote tulioshiriki katika Misa hii Takatifu. Niwaombe tu kwamba tuzidi kushirikiana ili chama cha Wazee na Wastaafu katika Dekania yetu ya Pugu, kizidi kukua na kusonga mbele,” alisema Sokoni.
Aidha, Sokoni aliwahimiza viongozi wenzake kushirikiana na kusaidiana, ili wawe na umoja uliokamilika, na hivyo waweze kwenda pamoja.

DAR ES SALAAM

Na Editha Mayemba

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, anatarajiwa kuadhimisha Misa Takatifu ya kutabaruku kanisa jipya la Parokia ya Mt. Vincent wa Paulo, Kibamba, Septemba 23 mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Katibu wa Parokia hiyo, Victor Rweyongeza, amesema kuwa Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 3:00 asubuhi, ikiwashirikisha Mapadri, Watawa, Waamini Walei na waalikwa kutoka Parokia jirani, na Jimbo kwa ujumla.
Amebainisha kuwa maandalizi kwa ujumla yamekamilika, ikiwemo kiroho na kimwili, yaani maungamo, semina na mafundisho  kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya WAWATA, UWAKA,VIWAWA na Wanandoa, kwani siku hiyo kutakuwa na ndoa nyingi zitakazofungishwa.
Amekumbusha pia kuwa mwaka uliopita waliadhimisha Sakramenti ya Ndoa Takatifu kwa Wanandoa jozi 30, ikiwa ni maandalizi ya waamini hao kuingia katika Kanisa jipya wakiwa wametakatifuzwa.
Kuhusu ujenzi wa kanisa hilo la kisasa ulioanza mwaka 2013, Rweyongeza amesema kuwa wanafanya maandalizi ya mwisho, ikiwemo kupaka rangi ndani na nje, na kumalizia maeneo madogo madogo yaliyobaki.
Amewashukuru Waamini na watu wenye mapenzi mema kwa niaba ya Kamati Tendaji na Kamati ya Ujenzi kwa majitoleo yao na michango iliyowezesha kazi hiyo kukamilika kwa mafanikio makubwa na kwa wakati.

SINGIDA

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wananchi watakaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga mkoani Singida yenye urefu wa Kilometa 77.6, kutohujumu mradi huo kwa kutokuiba vifaa ili kufanikisha ujenzi huo kukamilika kwa wakati.
Bashungwa aliyasema hayo katika hafla ya kukabidhi mradi huo kwa Mkandarasi Henan Highway Engineering Group Ltd ya nchini China, kuanza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
“Serikali imetoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali kote nchini ikiwemo ya Mkoa wa Singida, hivyo niwapongeze wananchi kwa ushirikiano mnaowapa wakandarasi. Hata hivyo, nitoe tahadhari ya wizi wa mali na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi, naomba viongozi muwasisitize wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi kuepukana na uhalifu wa aina yoyote kwa vifaa hivyo, badala yake wavilinde,” alisema Bashungwa.
Katika hatua nyingine, Bashungwa aliwataka Wakala wa Barabara nchini (Tanzania National Roads Agency: TANROADS), kuhakikisha wanamsimamia kikamilifu mkandarasi huyo ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na ubora.
“TANROADS nyie ndio wenye dhamana ya kusimamia ujenzi wa barabara hapa nchini, jipangeni vizuri ili ujenzi ukamilike ndani ya muda uliokusudiwa na kwa ubora, na si vinginevyo,” alisema Bashungwa.
Bashungwa alisema kwamba ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh.Bilioni 88.583 bila kujumlisha kodi ya ongezeko la thamani VAT Sh. Bilioni 15.944, chini ya kampuni hiyo.
Bashungwa alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta na watendaji wenzake, pamoja na viongozi wote wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa vizuri hafla hiyo, na kueleza kuwa Singida imefungua njia, na sasa ataanza ziara ya kwenda kuwakabidhi wakandarasi miradi iliyopo katika wilaya mbalimbali, akiambatana na Wabunge wa maeneo ilipo, ambayo imekwishatengewa fedha na Serikali.
Naye Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, naye alikuwa mwenyeji wa makabidhiano hayo ya barabara hiyo, pamoja na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, aliwataka Watanzania kuwa wamoja, hasa katika suala la kuinua uchumi wa nchi, kazi ambayo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeianza kwa kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa uchumi.
“Mimi kitaaluma ni mchumi, hakuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza kukuza uchumi wake pasipo kuwekeza kwenye sekta binafsi, na katika jambo hili hatutarudi nyuma, kwani litaongeza mapato ya nchi na kutuwezesha kutoa ajira nyingi, ikiwa ni pamoja na za wauguzi ambao watakuwa wakifanya kazi kwenye vituo vya afya tulivyovijenga nchi nzima,” alisema Mwigulu.
Alisema kwamba kumekuwa na tofauti katika jambo hilo la uwekezaji hadi kufikia hatua ya kutaka kufarakana kati yao, ambao wapo wanaoamini kwamba kupitia uwekezaji, watapiga hatua, na wenzao ambao hawautaki, wakidai Serikali inaweza kufanya kazi hiyo peke yake.
Mwigulu alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambayo alikuwa ameanza kuiomba tangu alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza, barabara ambayo inakwenda kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya za Ikungi, Iramba, Mkoa wa Singida na nchi kwa ujumla, kutokana na kupata masoko ya mazao yao.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, licha ya kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo, alitoa onyo kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe aache kumsakama Rais Samia kwa kumteua Mohamed Mchengerwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) si kwa sababu ni mkwe wake, bali inatokana na uchapa kazi wake uliotukuka kabla hajawa waziri, na baada ya kuwa Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akitoa taarifa fupi ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta, alisema kwamba barabara hiyo inapita katika maeneo yenye uchumi wa kilimo, misitu, madini na rasilimali nyingi ambazo hazichangii kikamilifu kwenye Pato la Taifa, kutokana na kutopitika kiurahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya mkoa huo, alisema una vijiji 441, kati ya vijiji hivyo, vijiji 341 tayari vina umeme, na vijiji 100 ambavyo havina, wakandarasi wapo kazini.
Alisema pia kwamba mambo hayo yote yanafanyika kwa ufundi na ustadi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya mambo mengi katika miradi ya maji, sekta ya elimu na mingine mingi, ikiwemo minara ya simu na kilimo cha mazao yote ya alizeti, mpunga, mahindi, dengu, vitunguu, pamba, na kueleza kuwa anaamini sasa kwamba Mkoa wa Singida unakwenda kuwa kinara wa uzalishaji wa mafuta ya kula, na mazao yote ya chakula na biashara yanayolimwa mkoani humo.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo iliyopewa kazi ya kujenga barabara hiyo, Huang Lele, alisema kwamba wamejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa, na akaomba kupewa ushirikiano kwa kuzingatia kuwa China na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu.

Mbinga

Na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imefanikisha mpango wa kumtua ndoo kichwani mama baada ya kuanzisha huduma ya maji.
Hatua hiyo imetokana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Mbinga kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaohudumia zaidi ya wakazi 3,600 wa kijiji hicho, na kijiji cha Mangwangala.

Songwe

Na Mwandishi wetu

Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, mkoani Songwe imepatiwa magari matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulances) ili kutoa huduma za dharura na kwa rufaa za matibabu kwa wananchi.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu (pichani) alitoa taarifa hiyo wakati akizungumza na Madaktari, Wauguzi na timu ya usimamizi wa Afya ngazi ya Halmashauri katika ziara yake mkoani Songwe.

DAR ES SALAAM

Na Esther Ngubes- TUDARCO

Wakatoliki wametakiwa kuepuka dhuluma, wizi na rushwa kwa sababu ni matendo maovu mbele ya Mungu.
Aidha, wameaswa kuacha kujihusisha na vitendo vya utoaji mimba, na wenye kushiriki vitendo hivyo vya uuaji yawapasa kufanya toba kwa Mwenyezi Mungu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri wa Jimbo Katoliki la Shiyanga, Padri Dunstan Sita, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokozi, Sinza, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Tunaalikwa kuwa na moyo mkuu, moyo hodari, na hatupaswi kuwa na deni…baadhi ya familia hususan wazazi na walezi, wanawasaidia mabinti kutoa mimba, jambo hilo ni baya na watu wanatakiwa wakatubu,” alisema Padri Sita.
Padri huyo alisema kwamba waamini wanapaswa kuwa sababu ya watu wengine ili kufikia malengo na mafanikio yao, na kuwa taa kwa kuwaonya watu wanaokosea katika ngazi za familia hadi Jumuiya.
Aliendelea kusema kwamba Kanisa lina wajibu mkubwa wa kuonya na kuwasaidia watu wanaokosea na wale wenye kwenda kinyume na maadili.
Padri Sita alisema pia kuwa dhambi ni chukizo kwa Mungu, hivyo waamini wasiwe wanatakiwa kuanza kuishi kwa mazoea, na badala yake waonyeshe upendo kwa wenzao.

DAR ES SALAAM

Na Eva Paul – TUDARCO

Wananchi wa Mtaa wa Mikongeni, Manisipaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi na usalama ili kudhibiti vitendo vya uhalifu vilivyokithiri katika eneo hilo.
Akizungumza na gazeti la Tumaini Letu katika mahojiano maalumu, Mjumbe wa nyumba kumi katika mtaa huo, Sara Malimbwi, alisema kuwa mtaa huo unakabiliwa na makundi ya vijana wanaovamia watu majumbani, na kuwaibia mali zao.
“Ni watoto wadogo tu, ambao walipaswa wawe shule, lakini wamejiingiza kwenye makundi ya wahuni, yaani ukiwaona utasikitika, kwani ni watoto wadogo, wengine hata darasa la saba hawajamaliza, lakini tayari wameshaacha shule, kutwa wanashinda vijiweni… Sisi kama wazazi tunaumia sana kuona watoto wanaharibika kiasi hiki, lakini hatuna cha kufanya,” alisema Sara.
Aliwasihi wazazi na walezi kuwaonya na kuwadhibiti watoto wao ili waache vitendo vya wizi.
Baadhi ya wananchi hao walisema kwamba vijana hao wanaotembea kwa makundi, wamekuwa wakiwavamia wananchi, hata nyakati za mchana.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walisema kuwa wanashangazwa kwa kukithiri uhalifu huo, licha ya kuwepo kwa ulinzi shirikishi unaochangiwa na malipo ya Shilingi 1000/= kwa mwezi kwa kila kaya.
“Tunalipa pesa ya ulinzi, lakini bado tunaibiwa, sasa walinzi wanafanya kazi gani?...” alihoji Hassan Selemani mkazi wa mtaa huo.
Naye Anna Lucas, mkazi wa eneo hilo alisema kuwa vitendo hivyo vimewachosha, kwani vimekithiri mtaani hapo.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema kuwa Kanisa halihitaji Mapadri wanaolaza damu katika utume wao, hivyo Padri anapopokea Daraja hilo Takatifu, anapaswa kuwa mchakarikaji katika Kanisa la Mungu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Daraja Takatifu la Upadri kwa Shemasi Emmanuel Mushi -P.O.C.R, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu – Buza, jimboni humo.
“Tunamwomba Mungu aliyekujalia wito wa kuwa Mtawa na kuwa Padri, akujaze Roho wake Mtakatifu, akujaze nguvu na neema, akupe mvuto na ari ya kuwa Padri mwema, Padri mwadilifu, Padri Mtakatifu, Padri mchakarikaji katika Kanisa la Mungu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi, na kuongeza,
“Hatuhitaji Mapadri wanaolaza damu, na wewe ujitahidi usiwe kuwa Padri wa kulaza damu…, uwe Padri wa kujitosa, kwa sababu anayekuita anataka uwe Padri unayefurahi kuwa Padri, uliye tayari kuuishi Upadri wako kiadilifu, kuuishi Upadri wako kiheshima, kuuishi Upadri wako ukichuchumilia utakatifu.”
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi, aliwataka waamini kumwombea Padri Emmanuel ili akue na kuimarika katika utakatifu kama Kuhani na Kasisi wa Bwana.
Wakati huo huo, Askofu Ruwa’ichi aliwasihi Wakristo kumwomba Mungu ili aendelee kuwaita vijana wengi wenye afya, akili timamu, walio watakatifu na waadilifu, ili wapokee wito wa kumtumikia Kristo ndani ya Kanisa lake kwa kuwa Mapadri.
Aliwakumbusha pia kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Padri Emmanuel, kwani amepata wito huo si kwa mastahili yake, bali kwa mastahili ya Mungu Mwenyezi.
Padri Emmanuel ametakiwa kujibidiisha kuwakusanya waamini kuwa familia moja, ili waweze kusimama katika misingi ya kumpendeza Mungu.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alilipongeza Shirika la Mapadri la Aldorin, kwa kupata Padri mpya.
Aliwashukuru wazazi wa Padri huyo kwa kumzaa, kumlea na kumtoa kwa Mungu kwa ukarimu, kwani wapo baadhi ya wazazi wasio na mtazamo sahihi, mathalani huwakataza watoto wao kutumikia miito yao.
“Kila mtoto ni mali ya Mungu… kwa hiyo kazi ya wazazi ni kuwalea watoto wao kama atakavyo Mungu, siyo kama watakavyo wao. Jifunzeni kuwalea watoto wenu ili watimize yale ambayo ni mpango wa Mungu kwa maisha yao, siyo mpango wenu kwa maisha yao,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi aliziasa familia zote ziwe ni kitalu cha kulea Miito Mitakatifu, kwani katika shamba la Bwana, mavuno ni mengi, ila watendakazi ni wachache.