Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha
Makala

Makala (78)

VATICAN CITY

Wakristo wameitwa kuleta chachu ya ukarimu kwa ulimwengu, hasa katika ulimwengu unaoathiriwa kila mara na mantiki ya ubinafsi, huku wakifikiria na kuishi kulingana na mantiki ya kweli zaidi, ile ya ukuaji fungamani wa mwanadamu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Leo XIV, huku akiwaelekea Waamini katika kituo cha IFEMA, Madrid, ikiwa ni hotuba yake ya mwisho, kabla ya kuanza sehemu ya Pili ya ziara yake ya kitume nchini Hispania.
Hitaji la kufikiria na kuishi, kulingana na mantiki ya maendeleo fungamani ya binadamu, limesikika katika hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV, akihitimisha hija yake mjini Madrid, kwa kukutana na watu wa kujitolea 17,000, katika Ukumbi wa 3 wa IFEMA, kabla ya kupanda Ndege kuelekea kwenye Mji wa Barcelona, ikiwa ni sehemu yake ya Pili ya ziara ya 4 ya Kitume nchini Hispania, iliyoanza tangu Juni 6 na kuhitimishwa Juni 12, kwa kutembelea pia Visiwa vya Kanari na Tenerife.
Banda hilo la 3 ni moja ya taasisi tano muhimu zaidi, za maonyesho ya biashara barani Ulaya, moja kuu nchini Hispania, ambapo alifika kwa gari katikati ya watu wa kujitolea, waliotambulika kwa rangi ya machungwa.
Katika hotuba yake Askofu huyo wa Roma, alianza na shukrani kwa Mwadhama José Kardinali Cobo Cano, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Madrid, kwa kaka na dada wapendwa katika Jimbo hilo.
Hapa wote walisikika wakitoa ukelele wa kusikitika, na Papa akaendelea. “Kila mmoja wenu na wengine wengi, ambao hawakuweza kuwa hapa asubuhi ya leo, wanastahili “shukrani” maalumu sana, kwa sababu mmetoa uwepo wenu na huduma yenu, na mmefanya hivyo kwa upendo kwa Bwana, Kanisa na Papa.”

Na Pd. Gaston George Mkude

Amani na Salama!
Injili ya leo, tunakutana na Yesu mbele ya makutano, waliokuwa wamechoka na kutawanyika. Makutano si tu wanawakilisha watu wa nyakati zile za Yesu, bali hata katika siku zetu leo hii.
Ni watu wangapi leo wanapitia magumu na mahangaiko, pamoja na mateso ya kila namna, labda hata baadhi yetu tumechoka, na kutawanyika kama kondoo tusio na mchungaji.
Wangapi leo wanaishi maisha yenye kila majeraha na maumivu! Wangapi leo wamechoka kimwili, kiakili na hata kiroho, kiasi cha kutawanyika na hata kutangatanga kiimani.
Wapo wanaokwenda kila siku, kwa wanaojiita mitume na manabii, na wengine kwa waganga wa kienyeji na wapiga ramli! Yesu anamuona kila mmoja wetu, na moja tu kutoka kwake, anatuhurumia!
Labda mara nyingi tunajiuliza, kwanini Mungu aliye upendo na huruma, anaruhusu wana na watoto wake tupitie magumu kiasi hicho?
Je, Mungu hawezi kutukinga na mateso na magumu? Au je, Mungu hatupendi hata anatuacha tukipitia kikombe hicho cha mateso na mahangaiko?
Ni maswali msingi na ya haki kabisa, kutuingiza katika tafakari ya fumbo la mateso, katika maisha ya ufuasi wetu.
Ni katika Injili ya leo, tunaona Yesu anapokutana na makutano wale, hata anapokutana nasi katika hali ngumu na taabu, anajawa na moyo wa huruma.
Yesu alipowaona, aliwahurumia! Huruma kama alivyokuwa anatukumbusha daima, hayati Baba Mtakatifu Fransisko, ndio haswa sura na utambulisho halisi wa Mungu wetu.
Mungu ni upendo na huruma! Papa Fransisko daima alipenda kurudiarudia na kusema ni sisi tunaochoka kuikimbilia huruma na upendo wa Mungu, kwani Mungu kamwe hachoki kutuhurumia na kutukumbatia tena na tena!
Shime katika kuikimbilia huruma na upendo wa Mungu! Jina na utambulisho wa Mungu ni Huruma!
Nabii Isaya anapotambulisha wema na huruma ya Mungu, anajaribu kutuonesha Mungu anatupenda zaidi ya mama anavyopenda watoto wake.
Sisi ni watoto wa Mungu kwa nafasi ya kwanza, na hivyo Mungu kwetu anajifunua kama upendo na huruma. (Isaya 49:14-16).

Na Mwandishi Maalumu

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa Bunge la Hispania, ameitaka Hispania kuendelea kuwa ni mahali pa watu kukutana, katika utamaduni ili hatimaye, kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, chemchemi ya Injili ya matumaini.
Katika hotuba yake hiyo, Papa alikazia utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuongozwa na kauli mbiu ya Umoja wa Ulaya umoja katika utofauti, mambo yanayounda amana na utajiri wa watu wa Mungu.
Hija hiyo ya 4 ya Kitume nchini Hispania imebebwa na kauli mbiu: “Alzad la mirada” Yaani “Inueni macho yenu.” Yn 4:35.
Baba Mtakatifu Leo XIV, alikutana na Waziri mkuu wa Hispania Pedro Sánchez Pérez-Castejón, ambaye amekuwa madarakani tangu Juni 2, 2018 na ndiye kiongozi mkuu wa Serikali ya Hispania.
Papa pia amekutana na kuzungumza na Bunge la Hispania na baadaye amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania na baadaye jioni wakakutana kwa sala na Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Almudena “Santa María de la Almudena” ambaye ni Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania na kila mwaka ifikapo Novemba, 9, mwaka huu, anakumbukwa na Mama Kanisa nchini Hispania. Baadaye usiku, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Jimbo kuu la Madrid, Hispania, Waswahili wanasema, siku hii ilikuwa “full shangwe.”
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa Bunge la Hispania, ameitaka Hispania kuendelea kuwa ni mahali pa watu kukutana, katika utamaduni ili hatimaye, kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, chemchemi ya Injili ya matumaini.
Amekazia utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuongozwa na kauli mbiu ya Umoja wa Ulaya “In varietate concordia” yaani “Umoja katika Utofauti” kwa kusimikwa katika tofauti za tamaduni, mapokeo na vipaumbele tofauti; mambo ambayo kwa pamoja yanaunda amana na utajiri mkubwa wa watu wa Mungu nchini Hispania.
Mama Kanisa anatembea bega kwa bega na binadamu, anashiriki matumaini na madonda yake, anaendelea kusikiliza na kujibu maswali msingi ya binadamu wa kila nyakati na kwamba, kuna tofauti ya utendaji kati ya Kanisa na Serikali; na kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kuzingatia kwamba, uhuru ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu.

Na Dk. Philip Komba

inaadhimishwa ifikapo Juni 3, kila mwaka nchini Uganda, na inakumbusha sadaka ya watu kadhaa, kutoka mahakama ya Mfalme Mwanga II, waliouawa kati ya mwaka 1885 na 1887, kwa kubadili dini na kuwa Wakristo.
Dini hiyo, Mfalme aliiona kama tishio kwa mila za kikabila, na kikwazo cha maisha yake.
Hivyo, kutokana na hilo, Papa Paulo VI mwaka 1969, huko Kampala nchini Uganda, akihutubia Bunge alisema kwamba: “Ninyi Waafrika mnajua maana kubwa ya jumuiya, ni mojawapo ya sifa zenu nzuri na za kibinadamu.”
Kundi la watumishi 22 Wakatoliki (karibu wote ni Waganda), wa mahakama ya Mfalme (Kabaka) Mwanga II wa Buganda, ambao Mama Kanisa aliwatangaza kuwa Watakatifu, waliteswa sana na baadaye kuuawa kishahidi kati ya 1885 na 1887, kwa kutetea imani yao ya kidini.
Watu wengine 150 walikufa katika mapigano kati ya vikundi tofauti, vilivyohusishwa na ushawishi wa wamisionari Wakatoliki au Waprotestanti, na wafanyabiashara wa Kiswahili au Wamisri.
Kifo cha kwanza cha shahidi mnamo Januari 1885, kilifuatiwa mnamo Oktoba, na kile cha Askofu wa Kiingereza J. Hannington na Joseph Mukasa Balikuddembe. Kundi la Waislamu lilimshawishi Mwanga, kuhusu kuhusika kwa Wakristo katika kuchomwa moto, kwa eneo la kifalme (1886), na kwa hiyo ukatili wa mfululizo mpya wa mauaji, uliwashtua sana viongozi wasio Wakristo, kiasi kwamba walizuia mauaji zaidi na hata kusababisha ongezeko la ubatizo. Mashahidi 22 Wakatoliki, walitangazwa kuwa Watakatifu mnamo 1964 na Papa Paulo XIV, ambaye pia alifanya ziara ya Kitume nchini Uganda.
Mtakatifu Paulo VI, alitimiza ziara hiyo kuanzia tarehe 13 Julai hadi tarehe 2 Agosti 1969.  Ziara hiyo ya Uganda mara nyingi, imekumbukwa kwa kutia moyo Kanisa changa la Afrika, kukua katika ukomavu, kwa ajili ya kukuza ubinadamu na kwa ajili ya kutafuta amani.
Papa Mtakatifu akikutana na baadhi ya Waamini wa Kiislamu, katika Ubalozi wa Vatican mjini Kampala alieleza kuwa:
“Tuna uhakika wa kuwa katika ushirika nanyi, tunapomwomba Mwenyezi Mungu, aamshe mioyoni mwa Waamini wote barani Afrika, hamu ya upatanisho na msamaha, ambayo mara nyingi hupendekezwa katika Injili na Kurani.
Na tunawezaje kushindwa kuhusisha na ushuhuda wa uchamungu, na uaminifu wa mashahidi Wakatoliki na Waprotestanti, kumbukumbu ya wale wanaoungama imani ya Kiislamu, ambao historia yao inatukumbusha kwamba, walikuwa wa kwanza mnamo 1848, kulipa kwa maisha yao kwa kukataa kukiuka maagizo ya dini yao?”
Hotuba ya Papa Paulo XIV kwa Uganda
Ndugu msikilizaji na msomaji, vilevile Mtakatifu Paulo VI akikutana na Rais, Mamlaka za kiraia na kikosi cha Kidiplomasia cha Uganda, katika Ukumbi wa Bunge huko Kampala tarehe 1 Agosti 1969, wakati wa hija yake ya kitume alitoa hotuba yake.
Katika muktadha huu wa maadhimisho ya Mashahidi, tunapenda kukumbusha hotuba hii ya Kinabii, katika ziara yake ya kwanza barani Afrika. Maono yake na utabiri wake, ulikuwa kama wa watangulizi wake, na wale ambao walifuata hadi leo hii. Mapapa wote kilio ni kimoja. Katika ulimwengu uliogawanyika vipande vipande na vita, unahitaji amani, haki na usawa.

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliendelea kuwaletea historia ya Uasi wa Martin Luther na historia ya maisha yake ya uasi.

Leo tunaendelea kuwaletea historia ya uasi wa Luteri hata kwa Shirika lake, na mafundisho yake ya dini. Sasa endelea…

Februari 3, mwaka 1518, Luteri aliitwa na Mkutano Mkuu wa Shirika lake, lakini kwa kulindwa na Frederick, hakuudhiwa na hata ndugu zake wengine shirikani walimshangilia.
Tarehe  16/05/1518, Luteri  akiogopa kutengwa na Kanisa, alihubiri akipinga uwezo wa Papa kumtenga Mkristo.
Hapo Papa alimwita afike Roma kwa hukumu, lakini Frederick wa Saxony, aliweza kumfanya Papa akubali, asikilizwe huko huko Ujerumani na Kardinali Kajetani.
Luteri alikataa kuacha uzushi, na baadaye akakimbilia kwa Frederick asikamatwe. Bahati mbaya Papa hakufanya lolote, akihofia kupoteza urafiki wa Frederick.
Mambo yalifikia kilele mwaka 1519, Luteri alipobishana na Mdominikani makini sana John Eck, aliyemzidi akili na utundu.
Kabla ya hapo, Luteri alikuwa akijificha katika maneno magumu ya teolojia, lakini sasa ilibidi aseme wazi, kujibu maswali makali ya John Eck.
Pale alikiri, mawazo yake na kusema kwamba, siyo tu Papa lakini hata Mtaguso Mkuu, unaweza kufanya makosa na mtu binafsi akaupinga.
Sasa ikawa wazi kwamba, ni mzushi na vyuo vikuu vikubwa vikamkana kama mzushi.  Ni tokea wakati huo, sasa Luteri akahesabika rasmi kama mzushi katika Kanisa.
Tarehe 15/06/1520, Papa Leo X, alituma hukumu ya kumtenga na Kanisa kwa Luteri, akimpa siku 60 akane uzushi.
Luteri badala ya kukana uzushi, akaichoma ile hukumu hadharani, kama dharau kwa Papa.   Mwaka 1521, aliitwa na Mfalme Mkuu Karoli V, kukana uzushi na alipokataa alihukumiwa,  lakini akakimbizwa na Frederick na kufichwa.
Wakati huo, ambapo Mfalme Mkuu Karoli angefuatilia kwa matendo, ilimbidi aondoke haraka kurudi Hispania kwa shida maalumu.
Hispania ilikuwa ikigombana na Ufaransa, na wakati huo huo Waturuki walitaka kuiteka Ulaya. Mfalme Mkuu Karoli, hakuweza kurudi Ujerumani mpaka baada ya miaka 9, yaani mwaka 1530.
Katika muda huo, Luteri aliachwa kueneza mafundisho yake, kwa sababu hakuna mwingine ambaye angelimsema au kumshika, kwa sababu alilindwa na Frederick wa Saxony.

DAR ES SALAAM

Na Edvesta Tarimo

Katika jamii nyingi, viatu vyenye kisigino kirefu vimejijengea nafasi ya kipekee kama alama ya urembo, hesima, hadhi na kujiamini kwa mwanamke. Kwa muda mrefu, kuvaa kiatu chenye kisigino kirefu kumechukuliwa kama sehemu ya mwonekano wa kitaaluma na kifahari, hususani katika mazingira ya kazi na hafla rasmi. Hata hivyo, nyuma ya mvuto huo wa nje, tafiti za kisayansi zinaendelea kuibua hoja nzito, kuhusu gharama ya kiafya inayoweza kujificha kwenye mtindo huu.
Kihistoria, kumbukumbu zinaonesha kuwa viatu vyenye kisigino havikuanza kama vazi la wanawake. Tafiti za kihistoria za mitindo zilizokusanywa na Fashion Institute of Technology, zinaonesha kuwa takribani mwaka 1000 BK, wanaume wa Uajemi waliokuwa wakipanda farasi, walitumia viatu vyenye kisigino, ili kuimarisha mshikamano wa mguu na farasi.

DAR ES SALAAM

Na David Mpangile

Ili kutimiza wajibu wao Wakristo, ikiwa ni sehemu ya matunda ya ubatizo, Waamini hujaliwa karama mbalimbali. 
Mafundisho ya Kanisa yanasisitiza kuwa karama yoyote itokayo kwa Roho Mtakatifu, yafaa katika kumsaidia mwamini katika safari yake ya kuutafuta utakatifu. 
Karama hiyo pia inaweza kuchangia katika ustawi wa Kanisa, na ni msaada kwa ndugu wengine katika Kristo. Hivyo ni makosa kuacha kuitumia. Hata hivyo, bado kuna kishawishi cha Walei wengi kushindwa kutumia vipawa walivyo navyo, kwa sababu wanatafsiri kwamba karama ni zile tu zinazohesabika kuwa kubwa, kama vile kutenda miujiza na kunena kwa lugha.

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliendelea kuwaletea historia ya Papa Gregori Mkuu, ambaye alikuwa Baba wa Kanisa wa mwisho na kiungo kati ya dola ya Kirumi ya zamani na ulimwengu mpya wa kishenzi. Leo tunawaletea historia ya maisha ya Mtume Muhammad na mwanzo wa Uislamu.  Sasa endelea…

Maisha ya Muhammad:
Katika kipindi cha ghasia na uvamizi wa Ulaya, ndipo Muhammad alizaliwa mwaka 570. Wazazi wake walikufa akabakia yatima na akalelewa na baba mdogo. Akiwa kijana alifanya kazi katika misafara ya ngamia ya mjane mmoja tajiri aliyeitwa Khadija.
Alifanya kazi vizuri, hata baadaye Khadija alimfanya Muhammad kuwa Mkuu wa misafara yake. Muhammad akiwa na umri wa miaka 25, alimwoa mwajiri wake Khadija aliyekuwa na miaka 35. Ndoa yao ilikuwa nzuri na ilidumu.

Mwanza

Na Paul Charles Mabuga

Simulizi ya Amos Katama (sasa marehemu) ni kioo cha maumivu ya kizazi kizima. Kauli yake kuhusu “soli ya 20 ya kiatu kuchakaa akitafuta ajira” si dhihaka, bali ni kovu la kisaikolojia linalowatafuna wahitimu wengi. Amos aliondoka duniani akiwa na Shahada ya Uandishi wa Habari mkononi, lakini mfuko ukiwa mtupu. Hali hii inatufanya tujiulize: Je, vyuo vyetu vinazalisha wasomi au vinazalisha watafuta kazi waliofungwa pingu za kifikra?

Na  Askofu Mstaafu Method Kilaini

Wahuni:    
Wahuni walikuwa wapiganaji wakali sana, na ndio walioleta matatizo yaliyozusha uvamizi. Wahuni walikuwa watu wa Mashariki ya mbali (Mongoliani, waasia wa ngozi ya njano). Wahuni walikuwa wachungaji wakiishi Kaskazini ya Milima ya Himalaya. 

Malisho yalipoisha, hawa wapanda farasi, walianza kuvamia nchi nyingine. Mwaka 200 Baada ya Kristo (BK), walikwea ukuta wakaivamia China na kusambaratisha himaya yake, na tangu hapo ikawa nyakati za giza kwa miaka 400 iliyofuata kwa China. 

Page 1 of 6