Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea historia ya kuibuka kwa Madhehebu mengine ya Kiprotestanti. Leo tunaendelea kuwaletea kuibuka kwa Madhehebu ya Kiprotestanti, hususani Uprotestanti chini ya John Calvin. Sasa endelea…
John Calvin 1509-1564:
Kati ya Waprotestanti waanzilishi, Calvin ndiye aliacha nyuma mafundisho ya msingi kwa Waprotestanti. Calvin alizalilwa mwaka 1509 huko Ufaransa. Alijifunza elimu dunia ya wakati huo (humanist), vilevile akajifunza Kilatini, Kiyunani na Sheria.
Mwaka 1533, anasema aliongoka na kuitikia wito wa Mungu kuwa “Chombo cha kutangaza ukweli”. Alipokea wito huo kwa moyo wake wote na kuanza kuhubiri.
Mwaka 1535, ilimbidi akimbie kutoka Ufaransa na kwenda Basle-Uswizi, kwa sababu ya upinzani dhidi ya mafundisho yake.
Akiwa Basle, Uswizi, aliandika mafundisho yake ya dini, Teologia, ambayo baadaye aliyaboresha. Ni muhimu kujua mafundisho haya ya Calvin, kwa sababu madhehebu mengi ya Kiprotestanti hata yale ambayo hayamkubali kama mwanzilishi wake, mafundisho yao yameingiliwa na teolojia yake.
Calvin kimsingi alifundisha yafuatayo:
1. Kwanza ya yote, Mungu ni mwenye mamlaka yote. Yeye ni Muumbaji, Mtegemezaji na Mtawala. Yeye yuko juu sana na mwenye uamuzi wote.
Yeye huamua anavyotaka, hana sheria inayombana. Hivyo, binadamu hawezi kuungana naye kama walivyofundisha watakatifu, bali la kufanya ni kujiweka chini ya utashi wake na maagizo yake. Kwa hilo alikuwa karibu na mafundisho ya Waislamu.
2. Alifundisha kwamba, tangu milele, watu wengine walipangiwa tayari kwenda mbinguni na wengine kwenda motoni (predestination). Mtu hawezi kufanya lolote kugeuza hilo.
Kwa wale waliopangiwa kwenda mbinguni, kuna ishara tatu za kuwatambua. (a) Kushika imani ya kweli (b) Maisha ya uadilifu (c) na kushiriki chakula cha Bwana.
Yeye na wafuasi wake, kwa sababu walikuwa na ishara hizo, ilikuwa ni wazi kwamba wamepangiwa mbinguni. Hapo mtu anaweza kusema “Nimeokoka” kwa sababu kama mtu amepangiwa kwenda mbinguni haiwezi kugeuka.
Mtu hana uhuru wa kutenda mabaya au mema, kwa sababu yeye ni mwovu, bali Kristo anamhesabia wokovu. Hata hivyo yule anayekosa lazima aadhibiwe kwa sababu hakulazimishwa na mtu kutenda mabaya.
3. Biblia ndio chanzo pekee cha ufunuo, na ishikwe na kufuatwa neno kwa neno kama ilivyoandikwa.
4. Kuna Kanisa lisiloonekana na Kanisa linaloonekana. Kanisa lisiloonekana, ni la wale wote waliopangiwa kwenda mbinguni, tangu mwanzo wa nyakati hadi mkamilisho wake. Kanisa linaloonekana ni la watu wale wanaotimiza masharti anayoyafundisha.
5. Anazitambua Sakramenti mbili tu Ubatizo na Ekaristi; lakini sakramenti hizo siyo za lazima kwa wokovu. Katika ibada mbalimbali, anakataza nyimbo, pawepo zaburi tu, vilevile anakataza ibada nzuri, hija, maandamano, sanamu nk.
6. Katika mafundisho yake alisisitiza sana juu ya umisionari. Alitayarisha watu ambao walikuwa tayari, bila kujali shida kwenda kuhubiri na kuwaongoa watu, kwa mafundisho yake.
Walifundisha vikundi na watu binafsi nyumba hadi nyumba.
7. Hawakumtambua Papa, Maaskofu au Mapadri. Kwao, kila mmoja aliyebatizwa ni Padri. Hivyo, kiongozi wa ibada huchaguliwa na watu, au huteuliwa na yeye na anaweza kumfukuza wakati wowote.
8. Kwake mwisho wa dunia, uko mbali, hivyo lazima binadamu afanye kazi sana na kuendeleza ulimwengu. Faida inayopatikana katika kazi hiyo, isitumike kwa anasa na starehe, bali iwekezwe au kusaidia maskini.
Hii iliwapa Waprotestanti, nguvu za kipesa na kuhamasisha ubepari. Hadi leo Waprotestanti wanajua biashara, kuwekeza na kuzalisha kuliko Wakatoliki.
















