Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Katika miaka ya zamani, mipira ya kuchezea soka ilikuwa inajazwa upepo tu, na kisha timu kuchezea, lakini sasa hali imekuwa tofauti.
Sasa hivi ipo mipira ya kiteknolojia ambayo kabla ya kutumika uwanjani, lazima uifanyie vitu viwili ambavyo ni kujaza upepo na kuchaji.
Teknolojia hiyo ilianza mwaka jana mwishoni katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Qatar.
Mipira hiyo ndani yake imewekewa ‘chip’ maalumu, ambazo zinahitaji kuwa na nishati ya umeme ili kufanya kazi kwa usahihi.
Mipira hiyo ya kuchaji ilitengenezwa na kampuni ya Adidas, ina sensa ndani yake, ambayo inakusanya takwimu mbalimbali, kasi na uelekeo wa mpira, na kutuma ujumbe kwenye mashine za VAR kutambua kama kuna mchezaji ameotea (offside) au la.
Mfano kwenye fainali za mwaka jana, mipira ilikuwa ikichajiwa kama simu za mkononi, ambazo zilichomekwa kwenye umeme kabla ya mechi za Kombe la Dunia kuanza huko Qatar, na baada ya hapo waamuzi husika walikuwa wakikagua kila kitu na kuruhusu itumike. Hii ni tofauti na zamani ambapo kazi ya mwamuzi ilikuwa kukagua kiwango cha upepo tu.
Sensa iliyopo ndani ya mpira huo, inapewa nguvu na betri ndogo, ambayo uwezo wake wa kukaa na chaji wakati ukitumika ni saa sita na chaji itadumu kwa siku 18 kama hautakuwa unatumika.
Uzito wa sensa hiyo ni gramu 14 ambayo kazi yake ni kufanya uwelekeo wa mpira, huku ikiwa imeunganishwa na kamera mbalimbali zilizopo uwanjani ili kuwasaidia waamuzi juu ya mchezaji kuotea, na mambo mengine.
Mpira utakapopigwa kwa mguu, kichwa, kurushwa hata ukiguswa tu, meseji 500 zinakuwa zimetumwa ndani ya sekunde moja.
Data zinatumwa kwa wakati na haraka, kupitia antena za mtandao zilizowekwa kuzunguka uwanja wa mchezo, na hivyo kuhifadhiwa kwenye kompyuta kwa ajili ya matumizi inapohitajika.
Kama mpira utatoka nje ya eneo na kuingizwa mpira mwingine uwanjani, mfumo unakamata haraka na data zinanaswa zenyewe bila ya kuhitaji usaidizi wa kibinadamu.
Adidas imetengeneza mpira mwepesi na wenye kasi kubwa, kitu ambacho kilimfanya beki wa England, Kieran Trippier kufichua kuwa umekuwa ukimpa shida kwenye kupiga mipira ya adhabu ndogo.
Alisema kwamba kila alipojaribu kupiga mpira wakati wa adhabu ndogo, aligundua kuna utofauti, lakini hata hivyo hicho hakiwezi kuwa kisingizio katika jambo lolote.
Alisema kuwa mipira ipo tofauti, siyo suala la joto wala kitu kingine, na kwamba ikitumika nguvu kubwa kupiga mipira hiyo, ni rahisi kupaa.
Kwa miaka kadhaa, kampuni hiyo ya Adidas imekuwa ikitengeneza mipira mbalimbali yenye teknolojia ya kushangaza watu katika michuano mikubwa.
Kuna wakati walishawahi kutengeneza mipira yenye ‘sensor’ ndani yake, ambayo ilikuwa maalum kwa ajili ya kugundua kama mpira umevuka mstari wa goli.Na hii ilikuwa inaambatana na saa maalum anayovaa mwamuzi, ambayo ilikuwa inatetemeka kama ishara kwamba mpira umevuka mstari wa goli.
Kama saa ya mwamuzi haitetemi, ni dhahiri kwamba mpira haujavuka mstari, na mwamuzi hawezi kukubali goli.

DAR ES SALAAM

Na Nicolaus Kilowoko

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza kuandaa mkakati wa kuisuka timu ya Taifa kwa lengo la kufanya vyema katika michezo yake mbalimbali ya kimataifa.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerson Msigwa (pichani) aliuzungumzia mwelekeo wa michezo kwa nchi ya Tanzania kwa sasa, huku wakiwa wanaendelea kupata nguvu mara baada ya kupewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, (African Cup of Nations: AFCON).
Alisema kuwa kwa sasa wanaandaa mipango ya kukaa na wadau mbalimbali wa michezo kwa lengo la kuanza mchakato wa kuiandaa timu ya Taifa ili iwe bora zaidia, kwa siku za usoni.
Msigwa alisema kuwa kufanya vizuri kwa timu ambazo zinashiriki Ligi Kuu Tanzania na michuano mbalimbali ya Kimataifa kumesaidia kuwa na timu bora ya Taifa, na hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupata maendeleo kwenye michezo.
“Mwaka 2027 sisi ndio wenyeji wa michuano hiyo, hivyo hatutakiwi kuwa na timu ambayo haina mwelekeo, bali kuandaa timu ambayo itakuwa na ushindani, ila hata kuchukua hilo kombe lenyewe, inawezekana. Wewe si unaona vijana wanaoshiriki kwenye vilabu mbalimbali vya Ligi wanavyoubonda?” Alisema Msigwa.
Alisema pia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa sasa imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya michezo, kwani tayari Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametengeneza muunganiko mkubwa wa viongozi katika maeneo mbalimbali.
Msigwa alidai kuwa mikakati ambayo inaendelea kuwekwa, ni kwa ajili ya kuipa hadhi nchi ya Tanzania katika sekta hiyo ya michezo ili ipate heshima yake.
Msigwa aliapishwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye hafla fupi iliyofanyika  Septemba 26 mwaka huu, Ikulu, Jijini Dar es Salaam akichukua nafasi ya Said Yakubu ambaye amepewa majukumu mengine.
Miundombinu kuelekea katika fainali hizo imeanza kuwekwa sawa, ambapo Visiwani Zanzibar ukarabati wa uwanja umeanza, huku jijini Arusha ukitarajiwa kujengwa uwanja mpya wa kisasa.
Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam utafanyiwa marekebisho madogo ili kuendana na viwango vya kimataifa.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akibariki kanisa la Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Kibamba, jimboni humo, katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa na Altare yake iliyofanyika parokiani hapo. Kushoto ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Prijo Joseph, na kulia ni Kansela wa Jimbo, Padri Vincent Mpwaji.  (Picha na Yohana Kasosi)

Dar es Salaam

Na Celina Matuja

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, amewaasa Mapadri, Watawa na waamini kwa ujumla kutambua kwamba wanapokabiliana na kifo, hawapaswi kughafilika, kukata tamaa na kuona mambo yote yameharibika, bali watambue kwamba kifo cha Mkristo ni sehemu ya safari yake ya kuungana na Kristo katika ushindi wake.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kumwombea marehemu Padri Novatus Mbuya-ALCP/OSS, aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mtume, Kijitonyama, jimboni humo, iliyofanyika parokiani  hapo, ikihudhuriwa na Maaskofu Wasaidizi Mhashamu Stephano Musomba na Mhashamu Henry Mchamungu.
Alisema kuwa Mkristo wakati wote anatakiwa kuwa tayari kwa kuweka mahusiano mema na Mungu katika maisha yake yote, na asingoje kesho kwa sababu maisha ya mwanadamu hayapo katika mamlaka binafsi.
“Nikiwauliza kwa sasa wangapi wapo tayari kuungana na Kristo, wachache mtanyoosha, na baadhi mtajificha kwa sababu mnataka kuniambia kwamba ‘ndiyo’, lakini siyo sasa. Ila tutambue kwamba hakuna hata mmoja wetu anayepanga siku zake,”alisema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi aliongeza kwamba huo ni mwaliko muhimu kupitia Maandiko Matakatifu, kwa habari ya Mlima Zioni, ambao unadokeza Mji Mtakatifu wa Yerusalem kwa maana ya Maisha ya Mbinguni, ambayo yameandaliwa na Mungu Mwenyezi kwa ajili ya Mwanadamu.
Alisema pia kuwa kwa Zioni ya Mbinguni, Mwandamu atafika huko ikiwa tu amepatamani, amepatafuta, na amepashughulikia maisha yake yote kwa kuweka mahusiano yake vizuri kiroho na Mwenyezi Mungu.
Aliongeza kwa kusema kwamba Zioni ni kushirikishwa Mwanadamu na Ushindi wa Kristo aliyeteswa, aliyekufa, aliyefufuka, na ambaye kila amwaminiye ameunganishwa kwa njia ya Ubatizo na kuwekwa kuwa shahidi wake.
Aliongeza kusema kuwa kitendo cha kukusanyika waamini kumwombea na kumuaga Marehemu Padri Novatus Mbuya, ni upendo, lakini pia ni kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwani kibinadamu wanaweza kusema amefariki akingali kijana.
Padri Novatus Mbuya alifariki dunia Septemba mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Muhimbili National Hospital: MNH), kwa ugonjwa wa saratani ya tumbo.
Padri Mbuya alizaliwa Juni 25 mwaka 1978 katika Jimbo Katoliki la Moshi, na alipata Daraja Takatifu la Upadri Februari Mosi mwaka 2012. Hadi anakutwa na umauti mwaka huu, Padri Mbuya alikuwa anafanya Utume wake akiwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu Mtume, Kijitonyama, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa Wachungaji wema ni wale wenye kutenga muda wao kwa ajili ya kuwafahamu kondoo wao kwa majina, ili wasisambaratike.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu la Upadri kwa Mashemasi saba wa OSA, katika Parokia ya Mtakatifu Ambrosi – Tagaste, jimboni humo.
Aliwataka Mapadri hao wapya kutambua kwamba wanatakiwa kujitosa bila kujibakiza, kwani ndiyo sifa ya uchungaji mwema, kuwakusanya kondoo wanaowachunga.
“Sifa ya uchungaji mwema ni kujitosa bila kujibakiza. Wachungaji wema ni wale wenye kuwafahamu kondoo wao, tena kwa majina, ili wasisambaratike. Mumwombe Mungu awape nguvu ya kuifanya kazi yake ili muwe vyombo vya neema yake,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa kila mbatizwa alizawadiwa wito wa kumtambua na kumfuata Kristo, akiwasisitizia Wakristo kuitambua fursa hiyo.
Aliwasihi Wakristo kuthubutu kumkimbilia Mungu, kwani kwa kufanya hivyo, watapata faraja na kusamehewa dhambi zao.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mungu ndiye chimbuko la kila jema, na pia ndiye anayetoa kila wito ulio sahihi katika maisha ya mwanadamu.
“Ndugu zangu, Mungu ndiye chimbuko la kila jema, na pia ndiye anayetoa kila wito ulio sahihi. Wapo baadhi ya watu wanaolala na kuamka, kisha kujitangaza kuwa wana wito. Mtu anaamka asubuhi anamwambia mke wake kwamba ‘usiku nimeoteshwa’. Huo siyo wito ulio sahihi, kwani wito ulio sahihi hutoka kwa Mungu Mwenyezi,” Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliongeza kuwa Mungu ni mwenye huruma, ndiyo maana licha ya mapungufu ya wanadamu juu ya dhambi zao, yeye huwahurumia.
Aliwasisitiza Mashamasi hao kuwa wakawe Mapadri wenye kujituma bila kulaza damu, bali watumie kila muda wao kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu.
Aidha, aliwataka pia Wakristo kutambua kwamba Yesu Kristo hashabikii dhambi, bali humwokoa mdhambi na kumzawadia wokovu maishani mwake.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa kama Kanisa, wanamshukuru Mungu kwa kupata Mapadri wapya watakaosaidiana nao kufanya utume kwa ajili ya kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Kwa upande wake Padri Laurent Temanya- OSA, mmoja wa waliopokea Daraja hilo Takatifu, alisema kwamba wao kama Mapadri, wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Upadri.
Alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kuongoza Adhimisho hilo, huku wakiwashukuru wazazi wao kwa kuwaleta duniani pamoja na kuwaruhusu kuuitikia wito huo.
Waliwashukuru walezi wao katika maeneo yote waliyopita kwa mchango mkubwa katika safari yao hiyo, huku wakiwashukuru pia wote waliowaombea, na kusema kwamba bado wanahitaji sala zao.
Aliwaasa wazazi kuendelea kuziombea familia zao, hasa zenye watoto wanaowiwa kuufuata wito, ili katika shamba la Bwana, watendakazi wawe wengi.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Kanisa la Parokia ya Kibamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, limetabarukiwa, huku Waamini wakionywa kutotumia vibaya kanisa hilo, kwani linapotabarukiwa, linawekwa maalumu kwa ajili ya Mungu na mambo Matakatifu.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, alisema hayo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Kibamba, jimboni humo.
“Kanisa linatabarukiwa ili liwe tu kwa ajili ya Mungu na watu wake, pamoja na mambo yote matakatifu. Hapa si mahali pa disko, disko pelekeni ukumbini. Msipafanye hapa kuwa jalala,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi alisisitiza kuwa kanisani si mahali pa kupumzishia mifugo, ikiwemo mbuzi wala kondoo, kwani likifanywa hivyo, hilo litakuwa jalala, badala ya kanisa.
Aliwapongeza waamini wa Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Kibamba, kwa moyo wa majitoleo waliouonyesha, hadi kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.
“Wapendwa familia ya Mungu katika Parokia ya Kibamba, nianze kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri na nzito mliyoifanya kwa kipindi cha miaika kumi. Kwa mshikamano wenu, imani yenu, mmemjengea Mungu kanisa zuri,” alisema Askofu Mkuu.
Aidha, Askofu Mkuu aliwakumbusha Wakristo kufahamu kwamba yeyote aliyebatizwa anatakiwa kutojiruhusu kuwa jalala, bali afahamu kwamba yeye ni ndugu yake Kristo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwaasa waamini kutambua kwamba biashara yoyote yenye sura ya dhambi, Yesu Kristo haitaki, wala haiungi mkono biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka Waamini wa Parokia hiyo kutobadilisha mwonekano wa kanisa hilo, kwani tayari limeshatabarukiwa.
“Kwa hiyo, ninyi sitegemei kwamba mwakani mtapenda kuja kurefusha upande huu na upande ule, au mtakuja kulibadilisha liwe tena la shughuli tofauti. Hili litakuwa ni mahali pa sala, mahali pa ibada, mahali penu pa kumtukuza Mungu kwa miaka yote. Hivyo, tunalipa hati ya kutabarukiwa,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Prijo Joseph alimshukuru Mungu kwa kuwawezesha na kuwapa nguvu katika kipindi chote, hadi kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.
Aidha, Padri Prijo alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa mawazo na ushauri aliowapatia hadi kuweza kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo lililotabarukiwa.
Vile vile, Paroko aliwapongeza Wanaparokia hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha, kwani walikuwa bega kwa bega katika kipindi chote cha ujenzi huo wa kanisa.
Naye Padri Augustine Paikkatt, Mkuu wa Shirika la MC BS (Superior General MC BS), alisema kuwa anafurahi sana kushiriki katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa.
Padri Augustine aliwapongeza waamini wa Parokia ya Kibamba, kwa michango na majitoleo yao hadi kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.

Mtwara

Na Mwandishi wetu

Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mkombozi - Magomeni, Jimbo Katoliki la Mtwara, Padri Silvanus Chikuyu, amesema kuwa mtu yeyote anapouona Msalaba, anatakiwa asipite bila kutafakari upendo wa Yesu Kristo kwa wanadamu.
Padri Chikuyu alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Somo wa Kutukuka kwa Msalaba, Kigango cha Lyenje, Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni – Luagala, Jimbo Katoliki la Mtwara.
“Na naomba kila mmoja anapouona Msalaba, asiishie tu kuuona na kupita zate, bali atafakari. Katika msalaba tuone mambo mawili makuu, kwanza kabisa tuone upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu….hakuna upendo ulio mkuu kama wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengine.
“Yesu Kristo ametupenda, akatoa uhai wake kwa ajili yetu sisi, ili sisi tuwe nao tele. Hilo ni jambo kubwa sana, usiupite tu Msalaba hivi hivi bila kutafakari upendo wa Mungu kwa wanadamu wote. Jambo la pili ni utii na unyenyekevu wa Yesu Kristo, ambaye alikubali kuachilia hali yake ya Kimungu, akajinyenyekesha akatwaa hali yetu ya kibinadamu,” alisema Padri Chikuyu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi.
Aidha, Padri Chikuyu aliongeza kuwa ni haki kwa kila Mkristo kuwa na msalaba nyumbani kwake, kwani kwa kufanya hivyo, milango ya baraka na mafanikio itapatikana katika maisha yao.
Padri huyo alisema kuwa wapo baadhi ya Wakristo ambao wanaishi na wenza wao katika familia, lakini wamekuwa wagumu kufunga ndoa, akisema kuwa ni vyema wakawa na misalaba majumbani mwao, ili baraka ziwafikie, na waweze kufunga ndoa.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni – Luagala, jimboni humo, Padri Andrew Chitanda alisema kuwa amefurahi kuona maadhimisho hayo yamekwenda vizuri.
“Maadhimisho haya yatie hamasa kwa ndugu wengine wote kutoka Parokia zote, Wakristo kutoka Vigango mbalimbali, kutoka Jumuiya mbaimbali, ili waweze kuthamini na kuadhimisha siku maalumu za Somo wa Kigango, au wa Parokia. Kwa hiyo, nawahisi Vigango vingine waweze kuiga mfano huu,” alisema Padri Chitanda.
Kwa Upande wake, Sista Elvira Lilungulu wa Shirika la Masista wa Mkombozi, Jimbo Katoliki la Mtwara, aliwaomba wazazi kuwaruhusu watoto wao wa kike na wa kiume wajiunge katika Mashirika mbalimbali ya Kitawa ili wamtumikie Mungu, kwani Mungu ndiye anayewaita kwa ajili ya kumjua na kumtumikia.
Naye Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Kigango cha Kutukuka kwa Msalaba - Lyenje, Regina Mtanda, aliwaasa akinamama kuwalea watoto katika maadili mema ili wale wenye wito waweze kuikimbilia miito hiyo.

LIRA, Uganda

Uamuzi wa kujenga Parokia nyingi katika Jimbo la Lira nchini Uganda, umetajwa kuleta msisimko na shangwe miongoni mwa Wakristo ndani na nje ya nchi hiyo.
Wazo la kufungua Parokia zaidi chini ya uongozi wa Askofu Sanctus Lino Wanok wa jimbo hilo, unalenga kuleta Sakramenti karibu na watu wa Mungu katika maeneo yao.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Parokia nyingine tano zilijengwa kwenye jimbo hilo.
Parokia hizo ni Parokia ya Mtakatifu Francis wa Assisi ya Abuli katika Wilaya ya Kwania; St. Peter Clever Ober katika mji wa Lira; St. Mary’s Catholic Parish, Loro, katika wilaya ya Oyam; St. Luke Mwinjilisti, Parokia ya Kikatoliki Aputi, katika wilaya ya Amolatar; na Parokia ya Mama Yetu wa Rozari Takatifu, ya Anyeke.
Kabla ya kujengwa kwa parokia hizo, Parokia zingine mbili za Mtakatifu Joseph Agweng, na Mama Yetu Malkia wa Amani katika Wilaya za Lira na Otuke, zilijengwa rasmi mwaka 2018.
Maendeleo haya yanaleta jumla ya parokia 27 za Jimbo laLira, na ndogo zaidi, yaani Parokia zinazolelewa na kuwa parokia siku zijazo.
Ndani ya jiji la Lira pekee, Parokia tatu Ndogo za St. Peter Anai; St. Leo the Great Boroboro; na St. Philip Neri Erute; mtawalia, zinatayarishwa kuwa Parokia katika siku zijazo.
Parokia nyingine Ndogo ni; Parokia ya Adyeda All Saints, itajengwa nje ya Parokia ya Bala Katoliki; Parokia Ndogo ya Gomi; Parokia ya Onek Gwok-Ngai; Parokia Ndogo ya Abakuli huko Dokolo; Parokia Ndogo ya Etam huko Amolatar; na Parokia ya Mtakatifu Francis wa Assisi, Ayago, inajengwa nje ya Alenga Katoliki.
Kujenga Parokia Ndogo kama hizo hapo juu kumezua shangwe na msisimko zaidi miongoni mwa Wakristo katika Dayosisi ya Lira.
Hivi majuzi katika Parokia Ndogo ya Assisi, Ayago, katika wilaya ya Apac, jumuiya ya Kikristo haikuweza kuficha furaha yao katika hafla ya mapokezi rasmi ya kasisi wao, Mchungaji Denis Okello Odyek, Msimamizi mpya wa Parokia Ndogo ya Ayago, akisaidiwa na Mchungaji Deacon Moses Opio.
Tarehe 2 Septemba 2023 katika ufunguzi rasmi wa Parokia Ndogo ya Ayago, Wakristo waliwajumuisha viongozi wa mitaa, kiraia na kisiasa, na viongozi wa kitamaduni walitoa shukrani zao kwa Askofu wa Jimbo la Lira kwa uongozi wake wa maono unaowezesha kujengwa kwa Parokia nyingi. ili kuwezesha ustawi wa kiroho wa watu wa Mungu.
Jovino Akaki Ayumu, Waziri wa zamani wa Jimbo la Utalii kwa Wanyamapori na Mambo ya Kale ni makamu mwenyekiti Baraza la wachungaji la parokia hiyo, Ayago alifichua kuwa kama Wakristo wamepokea wachungaji kwa furaha na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea na kuendeleza Parokia hiyo.
Kutoka mji wa Lira hadi Parokia Ndogo ya Ayago katika mwelekeo wa Kusini-Magharibi kupitia Manispaa ya Apac, inachukua takriban muda wa saa mbili, ikiwa na umbali wa kilometa 91, kuwa na makanisa 35 yaliyoenea ndani ya Kanda Saba chini ya Parokia Ndogo ya Ayago.

LIRA, Uganda
Askofu wa Jimbo Katoliki la Lira Kaskazini mwa Uganda, Mhashamu Sanctus Lino Wanok, ameonya dhidi ya unywaji pombe kupita kiasi unaofanywa na Makatekista na maajenti wengine wa wachungaji.
Akizungumza katika hafla ya uzionduzi wa Parokia ya Kanisa Katoliki ya Mama Yetu wa Rozari Takatifu, Anyeke wilayani Oyam, Askofu Wanok alibainisha kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi unasababisha madhara kwa huduma ya kichungaji katika Kanisa hilo.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amesema kwamba wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuombewa na kupewa hifadhi wanapoomba hifadhi.
Kauli hiyo ya Baba Mtakatifu imo katika tafakari yake kwa waamini waliofurika kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, wakati Baba Mtakatifu akikumbushia Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana.
Alisema kwamba kuna umuhimu wa kuwa na uhuru wa kukaa au kuondoka katika nchi, pamoja na ule wa kukaribishwa popote mtu anapokwenda.
Baba Mtakatifu akiwageukia waamini na mahujaji kutoka pande zote za Dunia waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro akisema, “Leo (Jumalipi ya Septemba 24) ni Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani, yenye kaulimbiu: ‘Huru kuchagua kuhama au kubaki,’ ili kukumbusha kwamba kuhama kunapaswa kuwa chaguo huru, na kamwe, si jambo pekee lisilowezekana.
Alisema kuwa haki ya kuhama sasa imekuwa wajibu kwa wengi, na hasa mahali ambapo panapaswa kuwepo haki ya kutohama, ni kubaki katika nchi ya mtu mwenyewe.
Baba Mtakatifu alisema kuwa ni lazima kwa kila mwanaume na mwanamke kuhakikishiwa haki ya kuishi maisha yenye heshima katika jamii anamojikuta.
Aliongeza kusema kuwa kwa bahati mbaya, umaskini, vita na mgogoro wa tabianchi, huwalazimisha watu wengi kukimbia nchi zao.
“Sote tunatakiwa kuunda jumuiya ambazo ziko tayari na wazi kukaribisha, kukuza, kusindikiza na kuunganisha wale wanaobisha hodi kwenye milango yetu,” alisema Baba Mtakatifu Fransisko.
Baba Mtakatifu aliikumbuka ziara iliyompeleka Kusini mwa Ufaransa ambapo alisema, “Changamoto hii ilikuwa katikati ya Rencontres Méditerranéennes, yaani Mikutano ya Mediteranea ambayo ilifanyika katika siku za hivi karibuni huko Marsiglia, na katika kikao chake cha kuhitimisha, nilishiriki jana, nikisafiri hadi jiji, njia panda ya watu na tamaduni.”