Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

L’Orchestra African Fiesta, mara nyingi ilijulikana kama African Fiesta, ilikuwa bendi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye mtindo wa soukous, iliyoanzishwa na Tabu Ley Rochereau na Dk. Nico Kasanda mnamo mwaka 1963.
Tabu Ley Rochereau(kwa sasa marehemu) ni mwanamuziki mwenye historia ndefu katika tasnia hiyo, aliyezaliwa Novemba 13, 1940 huko Bandundu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC).
Kwa kushirikiana na mpiga gitaa Dr. Nico Kasanda, waliasisi muziki wa Soukous ambao uliwafurahisha Waafrika kwa muda wa miongo minne, wakiutangaza muziki huo kimataifa kwa kuunganisha muziki wa asili ya Kongo na Cuba, Caribbean na Rumba ya Latin America (Amerika ya Kusini).
Tukianzia mwaka 1954, akiwa na umri wa miaka 14, Tabu Ley aliandika wimbo wake wa kwanza ulioitwa ‘Bessama Muchacha’ aliourekodi akiwa na Bendi ya African Jazz ya Joseph Kabasele (Grand Kale ama Pepe Kalle), na baada ya kumaliza elimu ya juu, alijiunga na bendi hiyo kama mwanamuziki kamili.
Tabu Ley aliimba wimbo wa kupigania uhuru wa watu weusi ulioitwa ‘cha cha’ ambao ulitungwa na Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ wakati Congo ilipopata uhuru mwaka 1960, wimbo ambao ulipelekea yeye kupata umaarufu mkubwa.
Alibakia na bendi ya African Jazz mpaka mwaka 1963 wakati yeye na Dr. Nico Kasanda walipounda kundi lao lililoitwa African Fiesta.
Miaka miwili baadaye, Tabu Ley na Dr. Nico walitengana, na Tabu Ley aliunda kundi lake lililoitwa African Fiesta Nationale, pia bendi hiyo ilifahamika kama African Fiesta Flash. Kundi hilo lilikuwa na mafanikio kwa kuongoza mauzo katika historia ya Afrika.
Mwaka 1970 alirekodi wimbo uliokuwa umeshika chati za juu za Kiafrika uliojulikana kama Afrika Mokili Mobimba, na uliuza zaidi ya nakala milioni moja.
Mzee huyo alifyatua nyimbo zingine kali za Ibragimu, Sukaina, Ponce Pilate, Cadance Mudanda na Boya Ye. Zingine zilikuwa Mbanda ya Ngai, Maze,Nzale, Sima Mambo Revens Itou, Nalingi yo Linga, Nadina, na nyingine nyingi.
Papa Wemba na Sam Mangwana walikuwa ni miongoni mwa wasanii maarufu wa muziki wa Kiafrika ambao walikuwa sehemu ya kundi hilo.
Sambamba na kundi la Franco Luambo Lwanzo Makiadi lililoitwa T.P.OK. Jazz, kundi la Afrisa lilikuwa moja kati ya makundi makubwa ya Kiafrika. Walirekodi nyimbo kama vile Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon, na Mose Konzo.
Katikati ya miaka ya 1980, Tabu Ley alivumbua vipaji vya waimbaji na wachezaji.Mwanamama M’bilia Bel ndiye aliyesaidia kuipa bendi yake umaarufu zaidi. M’bilia Bel alikuwa mwimbaji wa kwanza wa kike wa muziki wa Soukous, na kukaribishwa kwa shangwe Afrika nzima.
Baadaye Tabu ley na M’bilia Bel walioana, na harusi yao ilifungwa ndani ya ndege wakati wakiwa hewani, na baada ya harusi, wakafanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike waliyemwita Melodie kwa jina.
Mnamo mwaka 1988, Ley alimtambulisha mwimbaji  mwingine wa kike Faya Tess. Lakini baada ya ujio wa Tess katika bendi hiyo, kulimfanya M’bilia kuondoka kwa kile kilichoelezwa kuwa wivu wa kimapenzi baina ya wana ndoa hao ulioingilliwa na Faya Tess.
Mara baada ya M’bilia Bel kujitoa katika kundi la Afrisa  Intrenationale, pamoja na upinzani mkubwa na kundi la T.P.OK. Jazz, Bell aliendelea kupoteza umaarufu.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tabu Ley aliishi Kusini mwa California nchini Marekani, na alianza kurekebisha muziki wake ili uendane na mashabiki wa kimataifa kwa kuingiza lugha ya Kiingereza katika mashairi yake.
Alipata mafanikio kwa kutoa albamu kama vile Muzina, Exile Ley, Africa Worldwide, na Babeti Soukous.
Mwaka 1996, Tabu Ley alishiriki katika albamu ya Gombo Salsa iliyotengenezwa na Salsa Music Project Africando. Wimbo uliojulikana kwa jina la ‘Paquita’ kutoka katika albamu hiyo, ikiwa ni toleo jipya alioimba mwishoni mwa miaka ya 1960 katika bendi ya African Fiesta, na ulishika chati katika medani ya muziki.
Mwishoni mwa miaka ya 1990 Rais Mobutu Sese Seko Kuku Ng’endu Wazabanga alipoondolewa madarakani (mwaka 1997), Tabu Ley alirudi Kinshasa na alipewa nafasi ya Uwaziri katika Baraza la Mawaziri katika Serikali mpya ya Rais Laurent Kabila.
Kufuatia kifo cha Laurent Kabila miaka miwili baadaye, Tabu Ley aliendelea na wadhifa huo chini ya Rais Joseph Kabila.
Katika miaka ya 2000, Tabu Ley alianza kupatwa na maradhi, ikiwemo ugonjwa wa kiharusi ambao ulisababisha kufariki kwake ulipofika mwaka 2013.
Tabu Ley alikuwa katika hali mbaya kiafya toka mwaka 2008 baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi, na alikutwa na umauti wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja nchini Ubelgiji.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Mpira wa kikapu ni aina ya michezo inayopendwa katika sehemu nyingi za dunia, na watu wengi hutamani mchezo huu.
Kila timu huwa na wachezaji watano uwanjani, na hadi wachezaji wa kando 7 walio tayari kuchukua nafasi ya mchezaji mwingine muda wowote.
Mchezo huu ulianzishwa na mwalimu James Naismith kwenye Chuo cha Springfield College huko Massachusetts mwaka 1891. Alibuni mchezo huo kwa ajili ya wanafunzi wake ili wapate mazoezi wakati wa kipupwe waliposhindwa kucheza nje.
Mpira wa kikapu ulienea haraka kwenye vyuo vya Marekani, na katika karne ya 20, pia nje ya vyuo.Mwaka 1936 mchezo huu ulikubaliwa kwenye michezo ya Olimpiki.
Mpira unaotumiwa kimataifa ni mpira wa ngozi wenye kipenyo cha milimita 749 hadi 780, na uzito wa gramu 567 hadi 650.
Vipimo vya uwanja wa mpira wa kikapu huwa ni wa mita 28 urefu kwa mita 15 upana.
Wakati wa mchezo, kuna marefa wawili hadi watatu uwanjani. Kando ya uwanja hukaa waamuzi wengine wanaohusika na muda, kuhesabu pointi na makosa ya uwanjani.
Mchezo huu huchezwa kwa dakika 48  zenye vipindi vinne, ambapo kila kimoja huwa ni cha dakika 12.
TURN OVER
Katika mpira wa kikapu, ‘turn over’ hutokea wakati timu inapoteza umiliki wa mpira kwa timu pinzani, kabla ya mchezaji kushuti golini. Hili linaweza kutokea kutokana na mchezaji kuibiwa mpira, na mchezo kuwa chini ya umiliki wa timu pinzani, ama kutoka nje ya mstari wa uwanja, ama kufanya faulo, na mpira kulazimika kwenda kwa timu nyingine.
Turn overs zipo za aina kuu mbili, ambapo ya kwanza ni ya kulazimisha, na ya pili si ya kulazimisha.Turn over ya  kulazimisha ni ile ambayo mchezaji anaingia kwa nguvu na kuiba, ama kumpokonya mpira mpinzani, na kuufanya uwe kwenye umiliki wake.Na turn over isiyo ya kulazimisha ni ile inayotokea wakati timu inayoshambulia kufanya makosa yenyewe, ikiwemo kucheza rafu, ama kutoa mpira nje kwa bahati mbaya, au makosa mengine madogomadogo yatakayolazimu mpinzani auchukue mpira.
BLOCKS
Hii inatokea wakati mchezaji wa eneo la ulinzi la timu anapomzuia mshambuliaji kushuti mpira kwenye goli lake.Tukio hili huhusishwa pia katika takwimu za mchezo huo.
REBOUND
Hili ni tukio ambalo hutokea wakati mpira uliorushwa kuelekea kwenye goli, kugonga ubao wa goli, na kisha kurudi uwanjani ama kupitiliza upande wa pili wa chuma cha goli ikiwa ulirushwa na mfungaji kutokea pembeni mwa uwanja.Wakati mwingine, rebound huwa faida kwa mfungaji ambaye huwahi kuudaka mpira ulioshindikana kuingia wavuni, na kisha kufunga, ama beki anayezuia kuuwahi ule mpira usirudi tena kwa mpinzani, na kisha kuanzisha mashabulizi.
STEAL
Hii hutokea wakati mchezaji anapoiba mpira kutoka kwa mpinzani.Mara nyingi haitumiki nguvu kubwa zaidi ya akili ya mlinzi kuona namna ipi bora ya kuuchukua mpira kwa haraka kutoka mikononi mwa mpinzani.
FREE THROW
Hutokea hasa kwenye faulo ambapo timu inayofanyiwa faulo hupewa fursa ya kuwa na mrusho huru, ambapo mchezaji mmoja husimama akiwa anatazamana na goli, na kisha anahurusha mpira kuelekea golini. Na mpira unapoingia golini, faida yake ni pointi moja.
POINTI
Kwa kawaida, matokeo ya kwenye mchezo wa mpira wa kikapu hutokana na kuhesabiwa pointi, na si kuhesabu mara ngapi mpira umeingia golini.
Kila goli katika kikapu linahesabiwa kama pointi 2 au 3, kutegemeana na umbali wa kurusha.Kama ni karibu na goli, zinatolewa pointi mbili, na kama ni mbali na goli, zinatolewa tatu.Goli la penati (adhabu), huzaa pointi moja tu.
ASSIST
Hii ni pasi ya mwisho anayotoa mchezaji mmoja kwenda kwa mfungaji, nayo ni sawa tu na ilivyo kwenye mchezo wa soka.
FAULO
Hii hutokea wakati mchezaji anapomchezea vibaya mpinzani, na adhabu yake ni ‘free throw’ ambayo imeelezwa hapo juu.

NEW YORK, Marekani
Ligi ya National Basketball Assocation (NBA) imeanzisha sheria mpya zitakazoruhusu timu kumpumzisha mchezaji wao nyota mmoja pekee katika kila mchezo msimu huu.
Bodi ya Magavana wa Ligi hiyo inataka kuhakikisha wachezaji wake nyota wanaonekana kwenye michezo zaidi, haswa mechi za luninga za kitaifa na mashindano ya msimu, ambayo yanaongezwa mwaka huu.
Ligi hiyo itakuwa na uwezo wa kuadhibu timu zitakazokiuka sera hiyo kwa kuzitoza faini ya $100,000 (£80,000) kwa ukiukaji wa kwanza, na $250,000 (£250,000) kwa kosa la pili, na kwa kila ukiukaji utakaofuata, faini itaongezeka hadi $1 milioni (£800,000).
Kamishna wa NBA Adam Silver (pichani) alisema kuwa wanataka timu kudumisha uwiano kati ya idadi ya kutocheza mchezo mmoja mchezaji nyota nyumbani na ugenini, na pia kujiepusha na kufungiwa kwa muda mrefu ambapo mchezaji nyota anakuwa haruhusiwi kucheza.
Alisema pia kuwa ligi itaruhusu timu kuwasilisha maombi ya maandishi mapema kwa wachezaji wakubwa kwa michezo ya kurudi nyuma, na hii ni kwa kundi dogo la nyota ambao wana umri wa miaka 35 au zaidi mwanzoni mwa msimu, au wamecheza kwa zaidi ya dakika 34,000 za msimu wa kawaida, au michezo 1,000 katika maisha yao ya soka, wakiwemo LeBron James, Kevin Durant na Stephen Curry, ambao wote wanafaa katika kitengo hicho.

LONDON, England
Emma Raducanu amefichua kuwa anapanga kurejea kwa kishindo mwaka 2024 huku akiendelea kupata nafuu, baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye vifundo vya mikono na kifundo cha mguu mmoja.
Raducanu alikosa michuano ya French Open, Wimbledon na US Open mwaka huu, baada ya kufanyiwa upasuaji mwanzoni mwa mwezi Mei.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, ambaye alitoka nje ya 200 bora duniani wiki hii, alikuwa na matumaini ya kurejea msimu wa vuli, baada ya kurejea katika mahakama ya mazoezi mwezi uliopita.
Bado hajavuka raundi ya pili ya Grand Slam tangu ashinde US Open 2021, na pia amekuwa na majeraha kadhaa.
“Msimu ujao nitarejea.Msimu huu slam zote zilikamilika, hivyo ilikuwa vigumu kuzitazama zikipita, lakini nilikuwa najaribu kukaa kwenye mstari wangu kadri niwezavyo, na kuweka mkazo katika kupona kwangu”, alisema Raducanu.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (Tanzania Football Federation:TFF), Wallace Karia amesema kuwa wapo kwenye mchakato wa kuongeza idadi ya makocha katika timu ya Taifa Stars ili iweze kufanya vizuri.
Taifa Stars kwa sasa inasubiri upangaji wa timu(team draw) ya kujua kundi gani litakalokuwa la wapinzani watakaokutana nao katika fainali za Afrika zitakazofanyika kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 mwakani 2024, nchini Ivory Coast.
Akizungumza na Kituo cha Redio cha UFM jijini Dar es salaam kwenye mahojiano maalum, Karia alisema kwamba wamepanga kufanya maandalizi makubwa ili Tanzania ifike mbali katika fainali hizo.
Alisema pia kuwa timu hiyo ina makocha wasaidizi wakiongozwa na Adel Amrouche, lakini kuna ulazima wa kuwa na benchi pana la ufundi, kama zilivyo timu za mataifa mengine.
“Tunaamini na Serikali itatusaidia katika eneo hili muhimu.Tunataka tupate wataalamu wa kutosha.Unakuta wenzetu benchi lao la ufundi lina wataalamu 15, na kila mmoja anafanya majukumu yake.Kwa kuwa tunakwenda kushindana na watu wa ngazi ya juu, tunataka walau tuwe na makocha saba,”alisema Karia.
Alisema pia kwamba wanataka hadi kufikia kwenye mechi za kalenda ya Federation of International Football Assocation(FIFA) za mwezi Oktoba, timu iwe na benchi pana la ufundi, na kwamba tayari hao makocha wapo, na kilichosalia ni kuwasainisha tu mikataba.
Alisema pia kwamba kuna makocha wengine walishaanza kuonekana kwenye benchi hilo, ingawa wamekuwa kama wanajitolea. Hivyo mipango ikikamilika na wao kusainishwa mikataba, watakuwa tayari kutangazwa makocha wapya.
Akizungumzia maandalizi ya jumla kuelekea fainali hizo, Karia alisema kuwa wameshaongea na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo imewataka kuwasilisha mpango mkakati wa maandalizi, ili waangalie sehemu ipi Wizara inaweza kuwaunga mkono.
“Mwezi Oktoba kuna mechi za Kalenda ya FIFA ambazo tutazitumia kuiandaa timu yetu, na mwezi Novemba kuna nafasi pia ya mechi za timu za taifa, nako pia tutaangalia uwezekano wa kuiandaa timu yetu kuelekea michuano hiyo ya Januari,”alisema Rais huyo wa TFF.
Katika fainali zake mbili za Afrika zilizopita za miaka ya 1980 na 2019, Stars iliishia hatua ya makundi, na kutolewa pasipo kuingia 16 bora.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi (kushoto), akibariki visakramenti wakati wa ziara yake ya Kichungaji aliyoifanya hivi karibni katika Kituo cha Hija, Pugu. (Picha na Yohana Kasosi)

Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Cornel Mashare (kushoto), na Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Frederick Akilimali, wakionesha cheti cha shukrani kutoka kwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi kwa kufanya vizuri katika kuitegemeza Tumaini Media mwaka 2023.

Mgeni rasmi katika Mahafali ya Darasa la Saba ya Shule ya Msingi Golden’light, jijini Dar es Salaam, John  Magwisha (kulia), akikabidhi zawadi kwa Gladness Jonathan (kushoto),  mmoja wa Waalimu wa shule hiiyo, wakati wa sherehe za Mahafali hayo zilizofanyika shuleni hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

Baadhi ya Waamini wa Parokia ya Kung’ara kwa Yesu Kristo, Mbezi Mshikamano, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

Masista wanaofanya kazi za kitume kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Mahafali ya Darasa la Saba ya Shule ya Msingi ya Golden’light, Mbezi Mpigi Magohe, jijini Der es Salaam. (Picha na Yohana Kasosi)