Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, akimpatia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara mmoja wa vijana waliopokea Sakramenti hiyo, katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Imakulata, Upanga, Jimboni humo, (kulia kwa Kardinali) ni Paroko wa Parokia hiyo Padri Casmir Kavishe. (Picha na Mathayo Kijazi)

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardnali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewasihi Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kutambua kwamba kwa sakramenti hiyo wanatumwa kuitangaza habari njema kwa Mataifa.
Kardinali Pengo aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 37, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Imakulata, Upanga, Jimboni humo.
“Ndugu zangu mnaoimarishwa leo katika Sakramenti hii Takatifu, tambueni kwamba mnapopakwa mafuta, mnatumwa kwenda kuifanya kazi ya Mungu ya kuitangaza habari njema kwa Mataifa, yaani mnatumwa kuwatangazia masikini habari njema,” alisema Kardinali Pengo, na kuongeza,
“Masikini hao wanaotangaziwa habari njema, siyo umasikini wa kukosa fedha, kwa sababu kama ni umasikini wa fedha, hata Yesu Kristu mwenyewe alikuwa ni masikini.”
Aidha, Kardinali Pengo aliwasihi vijana hao kufahamu kwamba hata kama ni masikini na wenye kujiona kuwa hawana thamani maishani mwao, lakini Mungu hajawaacha, hajawatupa na wala hajawalaani.
Kardinali Pengo aliongeza pia kuwa heri watu walio masikini ambao wanamtegemea Mungu, kuliko matajiri ambao wanadhani kwamba wana kila kitu, na hivyo hawahitaji uwezo wa Mungu katika maisha yao.
Alisema pia kuwa kuitangaza habari njema ni pamoja na kuyaishi Maandiko Matakatifu, kwani mtu hawezi kuitangaza habari njema kwa kutenda kinyume na mafundisho ya Mungu.
Kardinali Pengo aliwasihi wazazi na walezi kuwasindikiza watoto wao katika kumsifu na kumtukuza Mungu, ili waendelee kudumu kuwa Askari hodari wa Kristo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Casmir Kavishe alimshukuru Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kufika Parokiani hapo na kuwapatia Sakramenti hiyo Takatifu vijana 37 katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Padri Kavishe aliwashukuru Makatekista na waalimu wote walioshiriki katika kuwafundisha vijana hadi kuwa imara na kuweza kupokea Sakramenti Takatifu, huku akiwasihi vijana hao kuendelea kudumu katika yale yote waliyofundishwa.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wadau na Watetezi wa Uhai kutoka Shirika la Kutetea Uhai, Pro-Life Tanzaania, wamesema kwamba mengi yaliyoandikwa katika Barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II (Familiaris Consortio 1981) kuhusu Nafasi ya Familia katika Ulimwengu wa leo, hayaonekani katika maisha halisi, kwani dunia ya sasa ni ya kizazi kipya.
Hayo yamejiri katika Kongamano la  Shirika hilo liliofanyika Jijini Dar es Salaam, na ambalo lilijadili barua hiyo ya Kichungaji.
Katibu wa Pro-life Tanzania, Godfrey Rahabu Mkaikuta amesema kuwa maisha yamebadilika, hivyo wamefikiri ni vema kupeleka ujumbe wa barua hiyo ya Kichungaji kwa vijana, na hivyo wamelenga kuanza na Vijana katika Vyuo Vikuu.
Alisema pia kuwa mpango huo unakusudiwa kuanza kutekelezwa mapema Januari mwakani katika Vyuo vya Kati, Vidogo na Vyuo Vikuu vya Kanisa Katoliki, na tayari wameshajipanga katika makundi namna ya kufikia Vijana hao katika Vyuo.
Mkutano huo uliokuwa ukijadili Insikliko ya Baba Mtakatifu, ulishirikisha watetezi wa uhai kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda Zambia, Zimbabwe na Rwanda, uliotanguliwa na Misa Takatifu wakati wa ufunguzi iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu.
Askofu Mchamungu aliwapongeza watetezi hao wa uhai kwa juhudi na hamasa kubwa wanayofanya katika kutetea uhai bila kuchoka wala kukatishwa tamaa, na hivyo kuwataka kuendelea na moyo huo bila kuchoka.
Katika mahubiri yake, Askofu Mchamungu alieleza umuhimu wa ndoa na familia katika maisha ya binadamu, kwani familia lazima imsaidie mwanadamu kutambua wito wake mwenyewe, na kuishi kadri ya maongozi ya Mungu.
Kanisa lazima litambue muhimu wa kuweka programu zinazolinda uhai, na kustawisha ndoa na familia kwa ajili ya ustawi wake, na pia ustawi wa taifa kwa ujumla wake.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Afisa Habari wa Klabu ya soka ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kuwa timu yake imeanza maandalizi ya sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu ya msimu huu, licha ya kwamba bado ni mapema.
Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano maalum, Bwire alisema kwamba wanajivunia maandalizi waliyofanya kabla ya msimu kuanza na sasa wana kikosi imara.
Alisema pia kuwa wamesajili kikosi kizuri ambacho kinaweza kuhimili ushindani katika Ligi ikilinganishwa na timu zingine.
“Sisi tuna kikosi kizuri, na falsafa yetu siku zote ni kuwa na wachezaji wazawa.Hicho ndicho kitu tunachojivunia.Wanaotudharau wakija kucheza na sisi watakiona cha mtema kuni,”alisema Bwire.
Alisema kwamba hakuna timu iliyoandikiwa kupata ubingwa siku zote kwa sababu ubingwa ni haki ya kila timu inayowania, na kwamba hawapo kwenye Ligi kwa ajili ya kupoteza muda au kusindikiza tu timu zingine.
“Huwa tunasikia tu eti kuna timu zimesajili Wazungu, zingine Wabrazil, zingine Wajapan, lakini sisi hatutetereshwi na mbwembwe zao.Sisi tutawaonyesha uwanjani”       
Alisema kuwa kuna timu zinawadharau, lakini mechi inapokaribia matumbo yao yanavurugika kwa hofu ya kufungwa.

DAR ES SALAAM

Na John Kimweri

Imeelezwa kuwa kiburi cha elimu ni sababu mojawapo inayowafanya watu kuacha kumwamini Mungu, na kutegemea utashi wao na mali walizonazo, kama jawabu katika maisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 125, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Martin wa Porres, Mwananyamala.
Askofu Musomba (pichani) alisema kuwa kiburi ni dhambi na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani, akiwataka waamini  kuhakikisha licha ya elimu walizonazo, lakini watambue uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa sababu bila yeye, hawawezi kufanya kitu chochote.
“Kiburi cha usomi kinaweza kusababisha mtu akaona kuwa hakuna Mungu, na eti anajiweza yeye mwenyewe bila ya msaada wa Mungu, kiburi ni dhambi kubwa sana na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani,” alisema Askofu Musomba.
Askofu  Musomba, alieleza kuwa kiburi kingine ni cha maendeleo na kiroho, akiwaonya waamini wanaojiona kuwa wamekamilika kuliko wengine kuacha kufanya hivyo.
Aliwakumbusha wazazi kuhakikisha kuwa wanapowarithisha  watoto wao mali na vitu vingine vya thamani, wasisahau kuwarithisha imani, kwani hilo ni jambo lisiloharibika wala kuchakaa.     
Aidha, aliwataka waimarishwa kutambua kwamba wanapopokea Sakramenti hiyo, Roho Mtakatifu anaingia ndani mwao na kuwafanya kuwa wapya katika kila jambo, huku akiwaasa wazazi nao kuwa na desturi ya kusali pamoja, na pia kusoma Neno la Mungu na watoto wao.  
Alisema kwamba Roho Mtakatifu ni nyenzo ya utume ya kuwasaidia waamini kuinjilisha hapa duniani, na kudai kuwa utume wa kweli unatakiwa kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Kwa mujibu wa Askofu  Musomba, utii unamfanya mtu akabidhi utashi na kuwa mtii kwa Mungu mwenyewe, na kuongeza kwamba pia utii huendana na usikivu, ambapo mwisho wake huleta unyenyekevu kwa mtu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia hiyo, Jeremia Mchomvu, alisema kuwa Parokia hiyo ina jumla ya waamini 6757, kutokana na sensa iliyofanyika Januari mwaka 2020.
Alisema kuwa Parokia kwa sasa ina mpango wa kununua nyumba mbili, ili kupanua eneo la kanisa.

Padri Germine Laizer akiwavisha rozari baadhi ya wanachama wapya wa Chama cha Wajane na Wagane

Dar es Salaam

Na Benedikto Agostino

Wajane na Wagane nchini wametakiwa kuendelea kuishi fadhila za Mtakatifu Monica bila kukata tamaa, na kumshukuru Mungu kwa maisha ya wenzi wao waliotangulia mbele ya haki, bila kusahau kuwaombea hao na watoto waliochwa na wazazi wao kila mara.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kamili, Yombo Kiwalani, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaaam, Padri Germine Laizer, wakati akihubiri katika Adhimisho la MIsa Takatifu ya Somo wa Wajane na Wagane, Mtakatifu Monica, iliyofanyika kwa ngazi ya Jimbo katika Parokia hiyo.
Katika homilia yake, Padri Laizer aliwakumbusha wajane na wagane kutambua maisha ya Mtakatifu Somo wao, Monica, kama mjane aliyeishi katika mateso na maisha mabaya ya mwanae Augustino, lakini licha ya kupitia changamoto hizo, hakukata tamaa hadi mtoto wake alipoongoka, na sasa ni Mtakatifu.
Alisema kwamba pamoja na ujane na ugane wao, ni muhimu kuishi fadhila ya unyenyekevu, kwani ni ishara ya itii mbele ya Mungu na watu, na hasa kila mmoja anapojishusha na kuwa kama mtoto mdogo.
“Maisha yetu yana maana kubwa kila tunapojinyenyekeza na kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani kila mmoja wetu anadaiwa kadri anavyokuwa mkuu kunyenyekea,” alisema Padri Laizer.
Aliongeza kusema kwamba watu wengi walioishii fadhila hiyo ya unyenyekevu wamepata kibali mbele za Mungu, na kujibiwa sala na maombi yao na kumbukumbu lao linaishi hata hivi leo.
“Tabia ya kiburi na majivuno ni kinyume cha unyenyekevu, na mara baada  ya mtu kuwa na maisha hayo, hali ya mtu hubadilika na kuharibika kabisa,” alisema Padri Laizer.
Alisema kuwa tukiongozwa na unyenyekevu ni lazima tufike mbali, kwani fadhila hiyo inalipa, na hakuna aliyeishi hali hiyo ambaye hakufanikiwa kamwe.
“Ni wazi unyenyekevu unapokosekana popote, yanatawala mafarakano, uogomvi na majigambo, hali inayotawanya kundi na kupoteza amani na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu,” alisema padri huyo.
Aliwataka waamini kuiga mfano mzuri wa mtu pekee aliyeishi fadhila ya unyenyekevu, ambaye ni Bikira Maria ambapo pamoja na magumu aliyoyapitia, aliyaweka mengi moyoni mwake.
Naye Mwenyekiti wa Wajane na Wagane Jimbo, Sweetbeter Mzungu alimshukuru Paroko wa Parokia hiyo, kwa utayari wake wa kupokea ujio wa sherehe hizo, na kuwapongeza wanachama wote waliojitokeza kufanikisha shughuli hiyo muhimu ambayo hufanyika mara moja kila mwaka.
Sweetbeter alisema kwamba moja ya mafanikio makubwa kwa sasa ni hatua waliopiga kutoka kutambuliwa kama kikundi na kuwa chama cha kitume ingawa bado changamoto kubwa ni mwitikio, hasa wa kupokelewa katika Parokia zote.
Alibainsha kuwa mara nyingi watu wengi hawapendi kujitambulisha kama wajane au wagane, na hali hiyo hutokana na kutokujikubali au kuipokea baada ya kuondokewa na wapendwa wao, na hasa wagane.

MOSHI

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspector General of Police: IGP) nchini, Camillus Wambura amesema kwamba takwimu za makosa makubwa ya jinai nchini yameongezeka katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2022.
IGP Wambura aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa wa waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, na makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, akisema kuwa makosa hayo yameongezeka kutoka 24,848 kipindi kama hicho mwaka 2021 hadi makosa 27,848, sawa na ongezeko la asilimia 11.2.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wamesema wamekumbwa na mashaka kuhusu matumizi ya michango yao.
Kwa nyakati tofauti, wanachama hao  wamesema hawana imani kama michango yao bado ipo salama kutokana na hali ya namna ilivyokuwa ikiendeshwa ndani ya CWT.

DODOMA

Na Ndahani Lugunya

Wakristo nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo, kuchangia Pato la Taifa, na kutatua changamoto katika maeneo yao.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, wakati akizunguma katika sherehe ya kumweka wakfu Askofu wa  tatu wa Kanisa  la Anglikana, Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto, iliyofanyika Jijini Dodoma, baada ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa hilo, Askofu Donald Mtetemela kustaafu.
Simbachawene alisema kuwa changamoto nyingi za kiuchumi katika jamii zitatatuliwa endapo wananchi watajituma kufanya kazi na kuwa wabunifu  kwa kuanzisha miradi mbalimbali, kama ambavyo Maandiko Matakatifu yanavyoagiza watu kufanya kazi.
“Lazima Wakristo wa sasa tufanye kazi, lazima tutatue changamoto kwenye maeneo yetu kwa sababu imeandikwa katika Biblia, ‘asiyefanya kazi na asile’, kwa hiyo kufanya kazi ndio uhai wako, heshima yako na ukizalisha, utaweza kuendesha maisha yako binafsi,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za Dini, kwani zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo, kusimamia maadili na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watu wasio na hofu ya Mungu.
Aidha, alibainisha kwamba Serikali inaendelea  kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ufisadi, utovu wa nidhamu kwa watumishi wa umma, pamoja na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk. Maimbo  Mndolwa, aliipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele kuziunga mkono Taasisi za Dini  katika nyanja zote, huku akimtaka Askofu Chiteto kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu, hatimaye kufikia malengo ya Kanisa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary  Senyamule  aliwataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa ya Serikali  kushusha bei ya  mbolea kwa kujikita katika kilimo.

Washington DC, USA
Mwanasiasa wa Kamanda wa Washington, Brian Robinson amefanyiwa upasuaji baada ya kupigwa risasi wakati wa jaribio la wizi wa kutumia silaha, au wizi wa gari.
Nyota huyo wa Washington Commanders, Brian Robinson alipata majeraha yasiyo ya kutishia maisha, baada ya kupigwa risasi.
Idara ya Polisi ya Washington DC ilisema kwamba Robinson alipata majeraha mawili ya risasi kwenye chini ya mguu wakati wa tukio hilo lililotekea Jumapili.
Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa 18:00 kwa saa za huko, katika mji mkuu wa Marekani. Polisi walisema washukiwa wawili walitoroka eneo la tukio, na bunduki ilipatikana karibu.
Siku ya Jumatatu, Robinson aliandika kwenye Instagram kwamba “upasuaji ulikwenda vizuri.”
Kocha wake mkuu Ron Rivera alimtembelea Robinson Jumapili jioni, na kusema Robinson “anaendelea vyema”.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi (mwenye Fimbo ya Kiaskofu), akiwa na Maaskofu Wasaidizi wake, Mhashamu Henry Mchamungu (mbele kulia), na Mhashamu Stephano Musomba (mbele kushoto), wakiwa katika Maandamano ya kuingia katika viwanja vya Seminari Ndogo ya Visiga, kwa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kilele cha Miaka 50 ya Jubilei ya WAWATA, Jimboni humo. (Picha na Yohana Kasosi)