Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Baadhi ya Waamini wa Parokia ya Kung’ara kwa Yesu Kristo, Mbezi Mshikamano, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

Masista wanaofanya kazi za kitume kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Mahafali ya Darasa la Saba ya Shule ya Msingi ya Golden’light, Mbezi Mpigi Magohe, jijini Der es Salaam. (Picha na Yohana Kasosi)

Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari – Bombambili, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Sheejan Kallarakkal MSFS (mwenye kanzu nyeupe), akiwa katika picha ya pamoja na Wazee na Wastaafu, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa Wazee na Wastaafu wa Dekania ya Pugu, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bombambili. (Picha na Mathayo Kijazi)

Padri Dickson Sambala- O.CARM, akibariki vipaji wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, iliyofanyika parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

Baadhi ya Waamini wa Parokia mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuhitimisha Ziara ya Kuitembeza Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo, Vikindu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, na baadaye waliikabidhi kwa Jimbo Katoliki la Lindi. (Picha na Yohana Kasosi)

Mdau wa Tumaini Media, Anitha Kihwele na mumewe Joseph Kihwele, wakitabasamu baada ya kukabidhiwa cheti cha shukrani na Padri Cornel Mashare (kushoto), Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kutokana na mchango wa Mama Kihwele katika kuhamasisha majitoleo ya tegemeza Tumaini Media. Cheti hicho kimetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi. Nyuma yao ni Meneja Utawala Tumaini Media, Joseph Kessy.

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Fransis wa Asizi, Kongowele, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyofanyika parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakristo wametakiwa kuepuka kuwapenda wanzao kwa sababu ya vitu au misaada wanayopata, bali wafanye hivyo kwa sura na mfano wa Mungu.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Padri Dickson Sambala- OCARM, wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuwashukuru Wanaparokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kwa kumlea katika kipindi cha Uchungaji wake, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Unaposali, unatengeneza matunda ya upendo, kwani unapopenda, unatengeneza matunda ya huruma kwa ajili ya kuwahudumia wengine, na unapowahudumia wengine, unatengeneza amani ndani ya mioyo ya watu….;
“Unatakiwa kuondoa matabaka kati ya walio nacho na wasio nacho. Unawaheshimu watu kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini siyo kwa sababu ni matajiri, siyo kwa sababu wanatusaidia hiki au kile,” alisema Padri Sambala.
Katika homilia yake, Padri Sambala aliwaasa Wakristo kuepuka kuwa na upendo wa masharti, kwani upendo huo huchagua baadhi ya watu.
Aliongeza kuwa upendo wa kweli ni ule wa kidugu unaowafanya watu kuwa kitu kimoja, na kuwafanya kupokea baraka za Mungu.
Aidha, Padri Sambala aliwashukuru waamini wa Parokia hiyo kwa ushirikiano waliompatia na kuipongeza Tumaini Media kwa kazi kubwa ya uinjilishaji kupitia vyombo vyake vya habari.
Naye Roselinda Msele, Katibu wa Kamati ya Liturjia Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, aliwaomba watu wenye mapenzi mema kuchangia ujenzi wa kanisa jipya la Parokia hiyo, ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Naye Diana Peter, Mlezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu wa Parokia hiyo, aliwasihi wazazi kuendelea kuwalea watoto katika maadili ili kupata watu wema.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari – Bombambili, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Sheejan Kallarakkal- MSFS, amesema kwamba uwepo wa wazee katika Kanisa, jamii, na hata familia, ni hazina kwa sababu wana uzoefu wa kimaisha.
Padri Sheejan alisema hayo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa Wazee na Wastaafu wa Dekania ya Pugu, kwa mengi aliyowatendea, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Uwepo wao wazee katika Kanisa, jamii, na hata familia, unaleta maana kubwa, na una faida kwa sababu wana uzoefu mkubwa katika kusimamia mambo…Kwa hiyo, ukiwa mzee una fursa fulani katika maisha yako, hivyo tumia uzee wako kurithisha imani kwa vijana na watoto,” alisema Padri Sheejan.
Aidha, aliwakumbusha wazee kutambua kwamba wana jukumu la kusambaza ukweli na mafundisho ya Kanisa kwa vijana, kwani wanakubalika kwa matendo na sauti zao.
Awali akitoa homilia yake, Padri Sheejan aliwaomba wazee hao kuwakemea vijana wanapokengeuka, ili kujenga heshima kwa watu wote.
Aliwasihi wazee na wastaafu hao kumwomba Mungu ili waendelee kuwa watu wa hekima na maarifa, yaani busara ndani ya Kanisa na jamii zao kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Wazee na Wastaafu wa Dekania ya Pugu, Cosmas Sokoni, aliwashukuru wazee wote walioshiriki Misa hiyo, akiwasihi wazidi kushirikiana ili chama cha Wazee na Wastaafu katika Dekania hiyo kikue zaidi.
“Kwanza, nichukue nafasi hii kuwashukuru wazee wenzangu wote tulioshiriki katika Misa hii Takatifu. Niwaombe tu kwamba tuzidi kushirikiana ili chama cha Wazee na Wastaafu katika Dekania yetu ya Pugu, kizidi kukua na kusonga mbele,” alisema Sokoni.
Aidha, Sokoni aliwahimiza viongozi wenzake kushirikiana na kusaidiana, ili wawe na umoja uliokamilika, na hivyo waweze kwenda pamoja.

DAR ES SALAAM

Na Editha Mayemba

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, anatarajiwa kuadhimisha Misa Takatifu ya kutabaruku kanisa jipya la Parokia ya Mt. Vincent wa Paulo, Kibamba, Septemba 23 mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Katibu wa Parokia hiyo, Victor Rweyongeza, amesema kuwa Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 3:00 asubuhi, ikiwashirikisha Mapadri, Watawa, Waamini Walei na waalikwa kutoka Parokia jirani, na Jimbo kwa ujumla.
Amebainisha kuwa maandalizi kwa ujumla yamekamilika, ikiwemo kiroho na kimwili, yaani maungamo, semina na mafundisho  kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya WAWATA, UWAKA,VIWAWA na Wanandoa, kwani siku hiyo kutakuwa na ndoa nyingi zitakazofungishwa.
Amekumbusha pia kuwa mwaka uliopita waliadhimisha Sakramenti ya Ndoa Takatifu kwa Wanandoa jozi 30, ikiwa ni maandalizi ya waamini hao kuingia katika Kanisa jipya wakiwa wametakatifuzwa.
Kuhusu ujenzi wa kanisa hilo la kisasa ulioanza mwaka 2013, Rweyongeza amesema kuwa wanafanya maandalizi ya mwisho, ikiwemo kupaka rangi ndani na nje, na kumalizia maeneo madogo madogo yaliyobaki.
Amewashukuru Waamini na watu wenye mapenzi mema kwa niaba ya Kamati Tendaji na Kamati ya Ujenzi kwa majitoleo yao na michango iliyowezesha kazi hiyo kukamilika kwa mafanikio makubwa na kwa wakati.