Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Dekano wa Dekani ya Mtakatifu Thomas More, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Romwald Mukandala, amewataka waamini kuwa na upendo kwa majirani zao.
Padri Mukandala ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kizito, Kilongawima, jimboni Dar es Salaam, alisema hayo hivi karibuni wakati wa Misa Takatifu ya Alhamisi Kuu iliyofanyika parokiani hapo.
Alisema kuwa waamini inabidi muoneshane upendo, hasa kwa majirani zetu…mkitambua kwamba sisi sote ni Watoto wa Baba Mmoja, ambaye ni Mungu Mwenyezi,” alisema Padri Mukandala.
Alisema kuwa jambo lingine ambalo waamini hao wanatakiwa kulisimamia ni kuwa na Imani na Mapadri wao wanaowaongoza katika Imani.
Padri Mukandala alisema kuwa Mapadri ni watumishi wa Mungu, ambao hawapaswi kutetwa na kusemwa kama inavyofanyika kwa baadhi ya waamini, akiwasihi waendelee kuwaombea Mapadri ili waweze kutekeleza vyema utume wao.
Akizungumzia Alhamisi Kuu, Padri Mukandala alisema kuwa hiyo ni Siku ya Mapadri, kwani ndiyo siku ambayo Bwana Yesu Kristo alisimika rasmi Misa Takatifu kwa njia ya karamu ya mwisho, alipokula pamoja na wanafunzi wake.
“Sisi ni wafuasi wa Kristo. Je tunapomfuata yeye, tunayaishi hayo? Mungu atusaidie tuache tabia ya ubinafsi, uchoyo, tujitoe kwa wenzetu,”alisema Padri Mukandala.
Ahimiza utunzaji wa mazingira
Kwa mujibu wa Padri Mukandala, waamini wote wanatakiwa kuhakikisha wanatunza mazingira katika maeneo yao kwa kupanda miti katika kutekeleza Waraka wa Baba Mtakatifu Fransisko wa ‘Laudato Si’ unaohitimiza utunzaji wa mazingira.
Alisema kuwa kuna kila sababu kwa waamini kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha anatimiza wajibu wa kupanda miti kwa wingi katika maeneo yake, na hata katika Maparokia ili kutunza mazingira ili yawe katika hali bora.
Naye Mlezi wa Seminari Kuu ya Segerea, Padri Siegried Ntare aliwataka Wakristo kuishi Ukristo wao kwa kumpenda Mungu kwa kusali na kuyashika Maandiko Matakatifu.

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, amewaonya watu wenye tabia ya kusengenya, kuponda na kuwachafua wengine kwa maneno mabaya ya kashfa.
Askofu Mchamungu alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Ibada ya Ijumaa Kuu, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Daima, Kimara Korogwe.
“Katika jamii pia watu wengine kazi yao ni kuponda wengine na kusengenya watu wengine. Wanatumia midomo yao vibaya kusema mabaya juu ya wengine, hawa hawana tofauti na wale waliomtemea mate Yesu Kristo,”alisema Askofu Mchamungu.
Askofu Mchamungu alisema kuwa katika jamii ya sasa pia wapo watu wengine ambao kazi yao ni kuchafua sifa za watu kwa kuwashuhudia maneo ya uongo, jambo alilosema ni baya katika maisha.
Ataka wenye mamlaka kutoa haki
Aliwataka waamini kuhakikisha wanatetea haki za wengine, na kutoogopa maneno ya watu kama alivyofanya Pilato, hasa wanapokuwa katika nafasi za kutetea haki za wengine.
“Kila mmoja kwa nafasi yake ajitahidi kutetea haki za jamii, hasa wanapoona kitu kimekuwa siyo sahihi,”alisema Askofu Mchamungu.
Kwa upande wake Ibrahimu Meresho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Kimara Korogwe, alisema kuwa wapo katika mkakati wa ujenzi wa Kanisa kubwa jipya na la kisasa, kwani kila kitu kimefanyika.
“Kwa sasa vibali vyote vya ujenzi vimeshapatikana. Tunatafuta mtu wa kurekebisha tu ramani yetu, na baada ya hapo tutaipelekea kwa Baba Askofu ili naye aiangalie na kutoa baraka zake ili ujenzi uanze kufanyika,”alisema Meresho.
Parokia ya Kimara Korogwe haina Kigango hata kimoja, na ina mwaka mmoja tu tangu itangazwe kuwa Parokia kamili, ikiwa na Kanda tano na Jumuiya 20, ikiongozwa na Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Dar es Salaam

Na Israel Mapunda

Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu, Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Vitalis Kassembo, amesema kwamba kila muamini anatakiwa kuwa shuhuda wa Imani.
Padri Kassembo alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalumu yaliyofanyika baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Pasaka, iliyofanyika parokiani hapo.
Alisema kuwa waamini wanapaswa kuendelea kusherehekea Pasaka kwa amani na upendo kwa kumtafuta Bwana Yesu Kristo.
“Tunapaswa tuendelee kuumbwa upya, kwa njia ya Sala, kutenda matendo mema, na kupokea masakramenti,”alisema Padri Kassembo na kuongeza,
“Neema hizi za Pasaka zisikae kwetu tu bali tuwashirikishe na wenzetu kile ambacho Mungu ametujalia, furahini na wengine,”alisema Padri Kassembo.
Naye Katibu Msaidizi wa Parokia ya Mburahati, Edward Alex, alisema kuwa mwaka huu Parokia hiyo inatarajia kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia, hivyo wapo katika harakati za maandalizi kuelekea kwenye jubilei hiyo.
Alisema pia kuwa kila muamini anatakiwa kushirikiana na wenzake katika kutenda matendo mema kwa kusaidia wahitaji kile ambacho wamejaal;iwa na Mwenyezi Mungu.
Naye Katibu Msaidizi wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa Parokia hiyo, Magreth Charles, alisema kuwa wanawake wanatakiwa kutulia na kuendelea kulea familia zao.
Alisema kuwa waamini pia nao wanatakiwa kuendelea kushikamana katika kuiishi Imani yao Katoliki, hasa katika kipindi hiki cha Oktava ya Pasaka.

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Bonaventura, Kinyerezi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Francis Hiza, amewasihi wanaume kuhakikisha wanajitoa kwa dhati katika kuhudhuria Jumuiya na kanisani, kwani uwepo wao ni mihimu kwa kuwa wao ni nguzo ya Kanisa.
Padri Hiza alitoa wito huo hivi karibuni wakati akizungumza katika hafla fupi ya Wanaume Wakatoliki Parokia ya Kinyerezi (UWAKA DAY), iliyofanyika Jumatatu ya Pasaka parokiani hapo, ikiwa ni utaratibu wa Parokia kuadhimisha UWAKA Day.
“Katika kuwatia moyo kwa mara ya kwanza nimeaandaa  sherehe kwa pesa ya Parokia kwa mwaka huu ili kila kitu wafanye wenyewe. Kwa hiyo hii inanipa mwanga kwamba tunasonga mbele kama wanaume,”alisema Padri Hiza.
Padri Hiza alisema pia kuwa  malengo makuu ya kuwakutanisha Wanaume Wakatoliki kukaa pamoja na kujadiliana maisha ya kiimani, ni kuwajenga ili washiriki kikamilifu shughuli za Kanisa, kwani wao ni nguzo ya Kanisa.
Alisema kuwa kila Mwanaume Mkatoliki anatakiwa kuhakikisha anauishi uamaume wake, hasa kwa kutambua kwamba wao ni kichwa cha famiilia, hivyo uhalisia huo lazima udhihirishwe kwa vitendo.
“Mwanaume ni kichwa cha familia, hivyo ni wajibu kwetu lazima tujipange ili tusije kuzidiwa na wanawake na hata katika Kanisa,”alisema Padri Hiza.
Kwa mujibu wa Padri Hiza, wanaume wasikubali kuuza haki zao za kuzaliwa wa kwanza, na kuliacha Kanisa likaangamia, kwani kufanya hivyo wataiangamiza pia jamii.
Kwa upande wake Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, Padri Benson Mapunda, aliwataka Wanaume hao waamke katika maisha ya sala na maisha ya ibada kila mara.
Alisema kuwa UWAKA wanatakiwa kujitahidi walau kila mwezi kusali katika Jumuiya na Misa za Dominika walau mara moja na kufanya maungamo, kwani ni jambo muhimu katika maisha yao.
Padri Mapunda alisema kwamba kila Baba anatakiwa kuhakikisha anazungumza na mwenza wake katika maisha yao ya kila siku, hasa katika mambo ya kiroho, na kuhimizana kufanya maungamo ili kuzirudishia roho zao uhai.
Alibainisha pia kuwa maungamo ya pamoja yanasaidia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha mahusiano yao ya ndoa.
Naye Didas Ndyemela-Mwenyekiti wa UWAKA Parokia ya Mtakatifu Bonaventura, Kinyerezi, alisema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida unaofanyika kila mwaka katika Siku ya Jumatatu ya Pasaka, ili kutafakari nguvu ya upendo kwa Wanaume Wakatoliki.
“Tunabadilishana mawazo ili tuweze kuona namna gani ya kuendeleza Parokia yetu sisi kama UWAKA,”alisema Ndyemela.
Hata hivyo alisema kuwa UWAKA imefanya kazi kubwa katika kufanikisha ujenzi wa kanisa, nyumba za Mapadri na vituo vya njia ya Msalaba, kwani Kituo cha Tano kimejengwa na UWAKA.

KASESE, Uganda
Askofu wa Jimbo Katoliki la Kasese, Mhashamu Francis Aquirinus Kibira Kambale amewataka  Wakristo kuiga mfano wa marehemu Bi. Augustino Muhindo, “anayejulikana kama Kithabutsunde” aliyemtaja kama nguzo ya ukuhani, elimu, na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika wilaya ya Kasese.
Askofu Kambale alisema hayo wakati wa Misa Takatifu ya kumbukizi ya miaka 10 ya Marehemu Bi. Muhindo aliyemtaja kuwa ni watu wa kwanza wa Mukonzo kutawazwa kuwa Kasisi katika Kanisa Katoliki la Roma, Desemba 14, mwaka 1958.

ADDIS ABABA, Ethiopia

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia (CBCE) limemteua Padre Asfaw Ketema kuwa Katibu Mkuu mpya.
Ataanza rasmi jukumu hilo Juni mwaka huu, akimrithi Askofu Lukas ambaye alihudumu kwa miaka sita kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi wa Eparchy ya Emdibir.
Padri Ketema, kutoka Vicariate ya Nekmete, analeta usuli dhabiti katika theolojia, masomo ya maendeleo, usimamizi wa biashara na usimamizi huko Dublin, Ireland.
Alitawazwa mwaka wa 1994, uzoefu wake mbalimbali unajumuisha huduma ya parokia, usimamizi wa shule, na uratibu wa mradi. Alionyesha uzoefu wa kiutawala kama Makamu wa Rais wa Utawala na Utawala katika Ethiopia.

LiLONGWE, Malawi

Baba Mtakatifu Fransisko amemtambua Padri Henry Chinkanda wa Jimbo Katoliki Dedza na Padri Patrick Thawale wa Lilongwe, kuwa Mamonsiyori.
Heshima hii ilitolewa kwa Mapadri hao wawili kama shukrani ya huduma yao ya kipekee kwa Kanisa la mtaa kwa ujumla na hasa majimbo yao ya Dedza na Jimbo Kuu la Lilongwe.
Cheo cha ‘monsignor’ ni alama ya tofauti inayotolewa kwa makasisi fulani kwa kutambua michango yao ya kujitolea, imani thabiti, na miaka ya utumishi wa kujitolea.
Si cheo au kiwango tofauti cha ukuhani, bali ni cheo kinachotoa heshima na heshima ndani ya muundo wa daraja la Kanisa.
Watawa wanaweza kukabidhiwa majukumu au majukumu maalum ndani ya Jimbo au Kanisa, kulingana na uwezo wao na mahitaji ya Kanisa.
Sehemu mbili za Kanisa la Malawi zina sababu zote za kusherehekea heshima hii kwa Padri Bi. Thawale, anafuata nyayo za Padri Bi. Charles Maida huku Padri Bi. Henry Chinkanda akifuata nyayo za Padri Bi. Joseph Masandi, ambao vile vile walitunukiwa cheo hiki na Baba Mtakatifu wakati wao.
Wakatoliki kutoka majimbo husika na kote Malawi na kwingineko wametuma ujumbe wa pongezi za dhati kwa Watawa wawili Padri Bi. Henry Chinkanda na Padri Patrick Thawale, akiwatakia huduma ya upadre iendelee katika Kanisa zima.
Padri Thawale alipewa daraja la Upadri Jimboni Lilongwe mwaka 1984.
Tangu kutawazwa kwake, alihudumu katika parokia, na kwa miaka mingi, alifundisha katika seminari nchini Malawi, ikiwa ni pamoja na Seminari Kuu ya Kachebere ambako aliwahi kuwa Mhadhiri na Mkuu wa Chuo; Seminari ya AMECEA Bakanja nchini Kenya ambako pia aliwahi kuwa Mhadhiri na Mkuu wa Chuo; na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) kwa zaidi ya miaka 13.
Padri Thawale baadaye aliteuliwa kuwa Mratibu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Malawi, kampasi ya Lilongwe kabla ya kuteuliwa kuwa Kasisi Mkuu wa Jimbo Kuu na Hayati Askofu Mkuu Ziyaye.
Baadaye Padri huyo akawa Msimamizi Mkuu wa Jimbo Kuu wakati wa mpito kabla ya kusimikwa kwa Uwaziri mkuu.
Padri Chinkanda alitumikia si Jimbo la Dedza pekee, bali Kanisa katika ngazi ya kitaifa, akianza kama mhadhiri na Mkuu wa Seminari Kuu za Saint Peters na Saint Anthony Kachebere mtawalia.
Pia alihudumu katika Tume ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu la Malawi kwa miaka mingi, na yeye ndiye Mratibu wa Kitaifa wa Sinodi.
Yeye pia ni Kasisi wa Kitaifa wa Chama cha Waseminari wa Zamani. Tarehe 26 Agosti 1979, alipewa daraja la Upadre.

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliangazia jinsi Uislamu ulivyoteka Afrika ya  Kaskazini. Leo tunawaletea jinsi gani Ukristo ulivyoinjilishwa Barani Afrika chini ya Wareno. Sasa endelea....

(Sehemu ya kwanza)

Kanisa la Afrika mwaka 1500
Mwaka 1500, Kanisa Barani Afrika lilikuwa limedhoofika sana. Misri, ingawa Ukristo ulidumu, Kanisa lilifanya kazi zake katika mazingira magumu sana, kwani waamini wake walinyanyaswa na Waislamu. Kila mwaka Wakristo wengi walihamia katika Uislamu.

Nubia sasa Sudan, ilipigana vizuri na kustahimili kwa miaka mingi lakini ufalme wake wa mwisho wa Alodia ulitekwa na Waislamu mwaka 1504 na polepole kufuta Ukristo wote.

Afrika ya Kaskazini inayojumuisha nchi za Tunisia, Libya, Algeria na Morocco, Ukristo ulitoweka kabisa chini ya utekaji wa Waislamu. Mfalme wa Ethiopia alikuwa amekimbilia milimani kwa sababu ya mashambulizi ya Waislamu, na ni kwa msaada wa Wareno mwaka 1543 ndipo alipoweza kujiimarisha tena.

Hivyo Ethiopia ikabaki nchi ya Kikristo hadi leo hii. Kusini mwa sehemu hizo zilizotajwa hapakuwepo na Ukristo. Ni katika hali hii ya Ukristo Afrika, tunaingia kipindi cha pili cha uinjilishaji chini ya Wareno.
                     
Misioni za Wareno Afrika (1400 – 1750)

Safari za Uvumbuzi:
Mhimili Mkuu wa uvumbuzi wa Ureno, alikuwa Mtoto wa Mfalme Henri Navigatores (1394-1460).  Mwaka 1415 aliteka Kisiwa cha Ceuto toka kwa Waislamu, na kwa mara ya kwanza Wareno walitawala bahari.  

Kutoka kisiwa hicho, alituma meli zake Kusini kwa uvumbuzi, licha ya simulizi za vitisho kwamba Kusini kuna mto wa moto, mtu atageuka mweusi, au kuna majitu makubwa wala watu.  Mafanikio ya safari hizo yalikuwa mazuri sana.  Kufikia  mwaka 1498 Vasco Da Gamma aliweza kuzunguka Afrika na kufika India.  

Kuna sababu kubwa zilizomtuma Henri na wenzake kufanya safari za utambuzi:

- Kwanza, ilikuwa ya kisayansi, alitaka kujua kulikoni huko Kusini.
       
- Pili, baada ya Ureno na Hispania kuwafukuza Waislamu kutoka nchi yao, walikuwa bado na mori ya vita vitakatifu. Walitaka kuwazunguka kupitia baharini na kuwashinda toka nyuma, kiasi kwamba wasingeliwasumbua tena.

Wakati huo palikuwepo simulizi nyingi juu ya ufalme wa Kikristo chini ya Mfalme Presta John. Walitumainia kuunganisha nguvu naye dhidi ya Waislamu. Wengi wanadhania kwamba ufalme huo ulikuwa ule wa Ethiopia.

- Tatu, ilikuwa sababu ya kibiashara. Walitegemea kugundua njia ya kufika India kupitia baharini. Kule kulikuwako na biashara ya dhahabu na vito ambavyo wangeliifanya bila kupitia nchi za Waislamu zenye hatari na ushuru mkubwa.
 
Vile vile waliona ugunduzi huu kama umisionari kwa ajili ya kuwainjilisha wapagani wa Afrika na Mashariki kwa ujumla.

Uinjilishaji na Udhamini wa Serikali (Padroado):

Toka mwanzo, Serikali ya Ureno ilidhamini na kusimamia shughuli zote za uinjilishaji.
Kila meli ya uvumbuzi iliyoanzia safari yake Ureno, ililazimika kuchukua Wamisionari.  

Papa Martin V mwaka1418 alizipa safari za ugunduzi hadhi ya vita vya msalaba kiasi kwamba walioshiriki safari hizo wote walipewa hadhi ya Kikanisa na neema zake.

Papa Callistus wa III mwaka 1456 aliwapa wafalme wa Ureno na Hispania madaraka ya Kikanisa ya kuanzisha majimbo na kuweka Maaskofu katika nchi zote walizozigundua.

Ingawa udhamini huu ulisaidia wamisionari kwenda misioni kwa bajeti ya serikali na ulinzi. Kuchanganya misioni na ukoloni pamoja na  biashara ilikuwa hatari sana.  

Mwishowe hali hiyo ilichangia sana kushindwa kwa missioni za Ureno Barani Afrika. Sasa nchi hizo zilikuwa na ukiritimba wa kuwatuma wamisionari wao katika nchi hizo watakaoweza kulinda maslahi ya taifa lao.

Vilevile kama wenyeji waliichukia serikali ya Ureno na ukoloni wake, vilevile walichukia wamisionari na imani ya Kikristo waliyoihubiri.

 Uinjilishaji Afrika ya Magharibi:

(a) Visiwa:
Visiwa vilikuwa rahisi kuinjilisha kwa sababu visiwa vingi hapakuwepo watu, na hivyo Wareno waliingia humo ambao tayari walikuwa Wakristo na kuwaleta watumwa waliofuata dini ya mabwana wao.

Visiwa vya Canary viligunduliwa na Hispania mwaka 1433.  Kule walipelekwa Mapadre Wafransiskani. Vilikaliwa na makaburu wa Hispania pamoja na watumwa ambao kwa kuoana waliingizwa katika utamaduni wa Hispania.

Ingawa visiwa hivyo viko Afrika, bado hadi leo ni sehemu ya Hispania. Wakazi wake ni wachache zaidi ya milioni moja, na na asilimia 80 ni Wakatoliki.
       
Visiwa vya Azores and Madeira viligunduliwa na Wareno mwaka 1420 na kukaliwa na wao pamoja na watumwa. Hadi leo ni sehemu ya Ureno, na asilimia 90 ni Wakatoliki.

Visiwa kumi vya Cape Verde viligunduliwa na Wareno mwaka 1460. Tofauti na visiwa vingine, hivi vilikuwa kwa ajili ya kulima pamba na miwa, na hivyo watumwa waliofanya kazi hiyo waliwazidi Wareno kwa wingi.

Hivyo mwaka 1975 walidai na kupata uhuru kama nchi ya Kiafrika licha ya kuwa na chotara wengi. Wakazi wake ni zaidi ya nusu milioni, asilimia 90 ni Wakatoliki.

Visiwa vya Sao Tome na Principe viligunduliwa mwaka 1470 siku ya Mtakatifu Tomaso, ndiyo sababu vikaitwa jina hilo. Sao Tome ilikuwa kituo maarufu kwa biashara na sukari. Askofu wake kwa miaka ya mwanzo alikuwa Askofu wa mwambao wote wa Afrika ya Magharibi.

Kisiwa kiliinjilishwa na watumwa huru kutoka Ureno. Mwaka 1975 pamoja na koloni nyingine za Wareno, kilidai na kupata uhuru wake. Kikiwa na wakazi 133,000 huku asilimia  88  wakiwa ni Wakatoliki.

VATICAN CITY, Vatican
Kitabu kuhusu maisha ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI (2005-2013:wa 265-hayati), kimewekwa hadharani baada ya matayarisho yake kukamilika.
Kitabu hicho kinachofahamika kwa jina la El Sucesor, ikiwa na maana “Mtangulizi”cha mahojiano kati ya Papa na mwandishi Javier Martínez-Brocal, ambapo Papa Fransisko (2013 hadi sasa-wa 266)anamkumbuka Mtangulizi wake Papa mstaafu Benedikto XVI kuwa:”Daima alinitetea, na kamwe hakuniingilia.”
Papa Benedikto XVI alikuwa mtu mkuu kwa upole. Katika kesi nyingine baadhi ya watu walimtumia, labda bila ubaya, na walipunguza harakati zake. Kwa bahati mbaya, kwa maana nyingine, walikuwa wanamzunguka. Alikuwa ni mtu nyeti sana, lakini hakuwa mdhaifu, alikuwa mwenye nguvu.
Lakini kwake mwenyewe alikuwa mnyenyekevu, na  alipendelea kutojilazimisha. Kwa njia hiyo aliteseka sana. Haya ni baadhi ya meneno ambayo Papa Fransisko anayakumbuka ya Mtangulizi wake Benedikto XVI, katika kitabu cha mahojiano na Mwandishi Javier Martínez-Brocal (“El Sucesor”, Editorial Planeta), kitakachochapishwa Jumatano tarehe 3 Aprili, 2024.
“Aliniacha nikue na alikuwa na uvumilivu”, anaeleza Papa Fransisko. Na ikiwa aliona jambo lisilo sawa, alikuwa anafikiria mara tatu, au mara nne kabla ya kuniambia. Aliniacha nikue na alinipatia uhuru wa kuchukua uamuzi. ” Papa amesimulia, uhusiano ambao alifanya uzoefu wa karibu ya miaka 10 ya kuishi mjini Vaticani, na Papa Mstaafu kwamba: “Aliniacha huru, na hakuniingilia kamwe.”
Katika fursa ambayo kulikuwa na maamuzi ambayo hakuelewa, aliniomba maelezo kwa namna ya kawaida kabisa. Alinieleza: “Tazama sikuelewa hilo, lakini maamuzi yako mikononi mwako,” na mimi nilimweleza sababu, na yeye alifurahi.” Papa Fransisko katika kitabu ameeleza kwamba mtangulizi wake kamwe  hakuwahi kupinga uamuzi wake wowote kwamba: “Hakuwahi kuniondolea msaada wake. Labda kulikuwa na jambo ambalo hakulikubali, lakini hakulisema kamwe.”
Papa Fransisko aidha, alikumbuka wakati mwingine hata katika kumuaga Papa Mstaafu  Benedikto XVI, Jumatano tarehe 28 Desemba mwaka 2022, alipomuona kwa mara ya mwisho kwamba: “Benedikito alikuwa amelala kitandani. Alikuwa bado na fahamu, lakini alishindwa kuzungumza. Alinitazama, alinishika mkono, alikuwa anaelewa kile ambacho ninasema, lakini hakuweza kueleza neno lolote. Nilibaki kwa muda kitambo, kwa kumtazama na kumshika mkono. Ninakumbuka kabisa macho yake mang’avu… Nilimwambia maneno machache kwa upendo, na nilimbariki.’’
Papa Fransisko amekumbuka na kusimulia kesi maalum ambazo alitetewa na Papa Benedikto XVI: “Nilipata mazungumzo mazuri sana na yeye wakati alipokuwa Kardinali, na nilikwenda kukutana naye kwa kushangazwa na maneno yake juu ya ndoa kwa wanandoa, ambapo yeye alikuwa wazi kabisa na wao.
Siku moja walifika nyumbani kwake ili kunishtaki mbele yake eti  nilihamasisha ndoa za mashoga. Papa Benedikito hakuwa na wasi wasi  kwa sababu alikuwa anajua kabisa kile ambacho mimi ninafikiri.

Dar es Salaam

Na Edvesta Tarimo

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (World Bank -2023), inakadiriwa kuwa uzalishaji wa taka utaongezeka kwa 70% kutoka tani bilioni 2.01 hadi bilioni 3.40 ifikapo mwaka 2050.
Kulingana na ripoti ya taarifa ya kiuchumi ya Urejelezaji wa Marekani
(U.S Recycling Economic Information - REI), San Francisco, Marekani, ni jiji la kijani kibichi hasa, na linatajwa kama kinara kwa urejeshaji wa taka (recycling), kwa zaidi ya asilimia 80 ya taka zake.
Urejelezaji wa taka na mifumo mizuri ya kushughulika na majitaka, utasaidia kuongeza ajira, kuongeza viwanda vidogo vidogo, kuongeza teknolojia mpya, pamoja na kipato ambacho kimekuwa kikipotea, ikiwa ni pamoja na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Majiji mengine yanayofanya vizuri kwenye urejeshaji wa takataka ni pamoja na Curitiba - Brazil, iliyofanikiwa kwa asilimia 70, pamoja na Vancouver-Canada, waliofanikiwa kwa asilimia 60 wakiwa na lengo la kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2040.
Wanafanyaje? Kwa kushikamana na mipango madhubuti ya kuchakata taka na sera ya kulipa fedha kadri wakazi wake wanavyotupa taka zisizoweza kutumika tena, huwafanya wananchi wawe na ufahamu zaidi wa mazingira, hasa kuhusu bidhaa wanazonunua katika kuepuka kulipishwa fedha zaidi za taka.
Nini kifanyike kukabiliana na hili?
Jiji la Dar es salaam ambalo linatajwa kuwa kitovu cha biashara, lenyewe linakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,252 za taka kwa siku moja. Kati ya taka hizo, ni asilimia 50 tu ndizo zinazopokelewa kwenye maeneo maalumu, nyingine zikisalia na kutupwa kwenye mitaro, maeneo ya wazi, na hata barabarani.
Hapa Tanzania, baadhi ya wadau wa mazingira wamekuja na mpango mkakati wa kuweka mazingira katika hali safi kwa kukusanya takataka, na kwa kupita baadhi ya masoko katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama vile Ilala, Buguruni. n.k.
Alpha Ntibachunya  ameamua kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwa kuanzisha kampuni ya LIMA ya kurejeleza taka ngumu katika matumizi mengine, badala ya kutupwa na kuchafua mazingira.
Ntibachunya anasema kuwa yeye na mwenzake walifanya utafiti wa kujua takataka zinazotupwa zinapelekwa wapi baada ya kukusanywa, na baada ya utafiti, waligundua kuwa kuna fursa nyingi zinazopatikana kwenye takataka.
“Kilichotupelekea tukaanzisha huu mradi, tulikaa tukafanya utafiti na kugundua kwamba kuna changamoto, baada ya hapo tukapata wazo linguine, tukaja na wazo hili la kuzalisha chakula cha kulishia mifugo, na mbolea ambayo tulitazama zaidi wakulima wadogo, hasa wa vijijini,” anasema Ntibachunya.
Anaongeza kusema kuwa njia mbili tofauti wanazotumia katika kukusanya taka, kwa kwenda sokoni, mfano soko la matunda Buguruni, hotelini na kutumia njia ya boksi hai ambalo hupeleka majumbani mwa watu kwa ajili ya kukusanyia mabaki ya vyakula majumbani mwa watu, kisha wanakwenda kuzichukua na kwenda kuzichakata.
Anasema kuwa wametumia changamoto ya mlundikano wa takataka katika maeneo tofauti tofauti katika jiji kugeuza kuwa sehemu ya kujipatia ajira, na kuajiri vijana wengine katika kukusanya na kuzichakata na kuwa chakula cha kulishia mifugo, na mbolea ambayo ni halisia isiyokuwa na makemiko ya aina yoyote.
Ntibachunya anasema kwamba uchakataji wa taka katika matumizi mengine umekuwa mchango mkubwa wa nafasi ya ajira kwa vijana wengi, kwani uzalishaji wake hauhitaji kiwango cha elimu, bali utayari wa kijana wa kuelekezwa kufanya kazi hiyo.
Kuchakata taka kunanufaisha mazingira, na kunatoa ajira kwa vijana, kunakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Kwa kutenganisha taka zinazoweza kutumika tena kama karatasi, nguo chakavu, glasi, plastiki, aluminium na mabaki ya vyakula na taka za elektroniki, watumiaji wanaweza kusaidia kuunda kijani kibichi kwenye majiji makubwa duniani.
Anitha Erasmi ni mama wa watoto wanne, anasema kuwa uchakataji wa taka umekuwa sehemu yake ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha ya familia yake, licha ya ndugu kumwona kama amechanganyikiwa.
“Mwandishi, ndugu zangu na jamii, iliniona kama chizi, lakini mimi sikujali kwa sababu mjini kama huna kazi, ukichagua kazi utashindwa kuishi. Nakusanya mamboga mboga nazipeleka kuziuza, napewa pesa,” anasema Anitha.
Philbert Alphonce mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam, anasema kwamba amekuwa anakikusanya taka ngumu kutoka soko na kuzipeleka sehemu wanakozichakata na kuzirejelesha katika matumizi ya kulisha baadhi ya mifugo, na pia mbolea asilia ambayo hutumiwa na wakulima wadogo wadogo kuweka kwenye mashamba ya mboga na maua.
Alphonce anasema amekuwa akiendesha familia yake ya mke na watoto wawili kupitia kazi yake ya ukusanyaji wa mabaki ya mbogamboga na kwenda kuziuza, ambapo kwa wiki anakwenda sokoni mara mbili, huku siku nyingine akizitumia kwa shughuli zake nyingine.
NEMC,Wadau watoa neno
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (National Environment Management Council – NEMC), Dk. immaculate Sware Semesi anasema NEMC, na taasisi ya mazingira, kituo cha Sayansi cha Mazingira (Centre for Science and Environment - CSE), kutoka India, wamekutana nchini Tanzania kujenga uelewa wa nini kifanyike katika taka ngumu, kuchukua takwimu ni taka kiasi gani zinazalishwa na zinatunzwaje, ili ziwe fursa badala ya kuwa uchafuzi wa mazingira.
Dk.Semesi anasema sambamba na hilo, kutambua ni teknolojia gani itumike ili kufanya taka zisiwe kero katika manispaa na jiji, bali ziwe fursa ya kuzalisha ajira au nishati kutokana na taka.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika moja ya hotuba yake alisema kwamba anaiona fursa kubwa kwenye wingi wa taka hizo, na tayari alisafiri mara moja kwenda kwenye jiji la Bursan nchini Korea Kusini kujifunza namna wenzetu walivyofanikiwa kwenye urejelezaji wa taka, na kuzifungamanisha na fursa kwa vijana wa rika mbalimbali.
Chalamila anasema kwamba jiji la Dar es salaam linaweza kuwa mfano kwa majiji mengine nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa fursa ya ajira kwa njia ya urejeleshaji wa taka, endapo juhudi za makusudi zitachukuliwa na kufanyiwa kazi kwa vitendo.
Anaongeza kuwa urejelezaji wa taka (recycling) ni mchakato wa kutibu taka kwa lengo la kuokoa malighafi zilizopo ndani ya taka na kuzirejesha kwenye matumizi ya kiuchumi.
Vifaa vya kielektroniki kama simu na kompyuta hurejelezwa na kutumika tena katika kutengeneza matofali, saruji na vyombo vipya vya glasi.
Taka za kaboni kama maganda ya matunda na mbogamboga, zinatumika kutengeneza mbolea na karatasi zikirejelezwa na kutumika kama makasha ya mayai na vifungashio vya bidhaa mbalimbali.
Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu maendeleo ya miji, inaonesha kuwa Afrika huzalisha tani milioni 70 za taka kwa mwaka.
Wakati huu ambapo ongezeko la watu wanaohamia mijini linaongezeka kwa kiasi kikubwa, Benki ya Dunia inasema kuwa kufikia mwaka 2025, uzalishaji wa taka huenda ukafikia tani milioni 160 kwa mwaka.
Tafiti zinasema kwamba ni rahisi kutengeneza bidhaa kutoka nyenzo zilizorejelezwa, kwani bidhaa kama ya aluminium iliyorejelezwa inaweza kuandaliwa tena na kuuzwa kwa bei nusu, kutokana na kuhitajika nishati kidogo ya kuchakata aluminium iliyorejelezwa, kuliko kutumia aluminium mbichi ya kiwandani inayotumika kwa mara ya kwanza.
Urejelezaji pia huepusha gharama ya utupaji wa taka kwenye dampo na vichomaji (incinerators), kwani baada ya kuanza kwa urejelezaji, dampo chache zitahitajika, na ardhi zaidi zilizokuwa zimetengwa kuhifadhi taka huweza kutumika kiuchumi.
Aidha, mapato ni sehemu nyingine aliyoiona Chalamila, kwani urejelezaji huimarisha tasnia ya uchakataji, na hivyo kutengeneza nafasi mpya za kazi kwenye viwanda vidogo vitakavyoundwa, kama viwanda vya chuma, karatasi, glasi, pamoja na ajira kwenye vituo vya ukusanyaji taka, na hata warejeshaji husika.
Utafiti wa U. S Recycling unaonesha kuwa nguvukazi ya kuchakata na kutumia tena malighafi zinazotokana na taka, imekuwa kubwa zaidi kwenye mataifa mengi, zaidi ya nguvukazi inayotumika kwenye uchimbaji wa madini na usimamizi wa taka zisizorejelezwa.Mashirika yanayorejeleza taka, huzalisha takribani dola bilioni 240 kwenye mapato ya kila mwaka.
Huko Carolina kusini pekee, zaidi ya wafanyakazi 15,000 na dola za Marekani milioni 69 za ushuru, hutokana na uchakataji wa taka, huku Carlifonia urejelezaji wa taka ukiajiri watu 85,000.
Kila mwaka, dunia inageuka kuwa makao ya takribani tani bilioni 2.01 za taka ngumu, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia bilioni 3.40 miaka 30 ijayo, sawa na ongezeko la 70%.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, (World Bank – WB), mataifa yenye kipato cha juu inaonesha kwa siku kuna ongezeko la 19%, huku mataifa yenye uchumi wa kati na chini, ukiongezeka kwa 40% au zaidi.