Na Mathayo Kijazi
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Vincent Mpwaji, ametoa wito kwa waamini kutotaka kusukuma makosa yao kwa wengine, badala yake wawe na nia thabiti ya kuyakubali na kuyasahihisha makosa hayo.
Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa homilia yake katika adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 107 katika Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga - Yombo Dovya, jimboni humo.
“Hata ukiwa umefanya kitu pale nyumbani, mama akikuuliza kwa nini umefanya hivi, unakataa unasema ‘Hapana, sio mimi’. Kwa hiyo tunakuwa na hiyo hali ya kusukumia makosa kwa wengine. Kwa hiyo ndugu zangu tunaalikwa kutokusukuma makosa yetu kwa wengine. Tuwe na nia thabiti ya kuyasahihisha makosa yetu pale tunapokosea,” alisema Askofu Mpwaji.
Askofu huyo aliongeza kuwa Mungu daima hutoa nafasi kwa mtu anayetaka kubadilika na kuanza upya, akiwaalika kila mmoja kubadilika na kuanza kufanya matendo mema ya kumpendeza Mungu.
Pia, aliwasihi vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kusema ‘Ndiyo’ ya kweli pale wanapopokea Sakramenti hiyo, ili kwa kusema hivyo, wasiwe watu wa kubadilika.
Pia, aliwasisitiza kuwa na nia moja katika maisha yao, ili lengo lao liwe moja la kumtangaza Kristo popote pale wanapokuwa.
Aliwasisitiza kila mmoja baada ya kupokea Sakramenti hiyo, kuwa mstari wa mbele katika kusema ukweli popote pale walipo, huku wakiepuka hofu wala woga, akitolea mfano wa ‘Nani amfunge paka kengele’.
















