Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Canberra, Australia
Bingwa wa Olimpiki wa discus Roje Stona na mchezaji wa kimataifa wa Rugby wa Australia Jordan Petaia, watakuwa miongoni mwa kundi la hivi punde la wanariadha watakaoshiriki katika Njia ya Wachezaji wa Kimataifa ya NFL.
Tangu programu ya IPP ianzishwe mwaka wa 2017, wachezaji 41 wa kimataifa wamejiunga na timu za NFL, huku 23 wakiwa na timu kwa sasa, na sita wameingia kwenye orodha inayotumika ya timu.
Mpango wa IPP hutambua vipaji vya kimataifa, na huwapa wanariadha fursa ya kukuza ujuzi wao wa soka wa Marekani, na uwezekano wa kupata nafasi kwenye orodha ya NFL.
Mnamo Januari, wanariadha 14 wataenda kwenye kambi ya mafunzo ya wiki 10 huko Florida, inayojumuisha vipindi vya uwanjani na darasani, kabla ya kuonyesha ujuzi wao kwa maskauti wa NFL kabla ya rasimu ya NFL ya mwaka ujao.
Stona, 25, alifanya mazoezi na timu mbili za NFL majira ya kuchipua mwaka jana, kabla ya kushinda medali ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki ya Jamaica katika mchezo wa kutupa tufe huko Paris 2024.
Petaia, 24, alikuwa tayari amehusishwa na kuhama chama cha raga na atalenga kumwiga Mwaustralia mwenzake Jordan Mailata.

NEW YORK, Marekani
Juan Soto anatazamiwa kusaini mkataba ambao unadaiwa kuwa mkubwa zaidi katika historia ya michezo baada ya kukubali mkataba wa $765m (£600m) kwa miaka 15 na New York Mets ya Ligi Kuu ya Baseball.
Vyanzo vingi vya habari nchini Marekani vimefichua maelezo ya mpango huo, ingawa Mets bado hawajathibitisha hilo kwa sababu raia huyo wa Dominican mwenye umri wa miaka 26 anahitaji kukamilisha uchunguzi wa kimatibabu.
Soto aliwekwa kuwa wakala wa bure anayetafutwa zaidi na MLB katika msimu huu wa nje baada ya kuwa na msimu bora wa maisha yake akiwa na Yankees ya New York, tena akionyesha uwezo wake wa hali ya juu wa kupata msingi.
Ana asilimia kubwa zaidi ya kazi kwenye msingi kati ya wachezaji wanaocheza (0.421), ni mchezaji mwenzake wa Yankees Aaron Judge ndiye aliyekuwa na OBP bora zaidi mnamo 2024 na ni wachezaji watatu pekee waliopiga mbio zaidi za nyumbani.
Tovuti ya MLB ilisema, Soto nje ya mshahara wake lakini atapata bonasi ya kusaini ya $75m, bila pesa iliyoahirishwa, katika mkataba ambao unaweza kuwa na thamani ya hadi $800m (£627m).
Thamani ya jumla ya mkataba huo inapita mkataba wa miaka 10 wa $700m (£558m) ambao Shohei Ohtani alisaini na Los Angeles Dodgers mwaka jana, huku nyota huyo wa Japan akikubali kuahirisha $680m (£541m) ya kiasi hicho.
Baadhi ya wachezaji wengine wakubwa ni pamoja na beki wa Dallas Cowboys Dak Prescott kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi katika historia ya NFL mnamo Septemba kwa kukubali kuongezwa kwa mkataba wa miaka minne wenye thamani ya $240m (£183m).

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Visiwani Zanzibar nako wana michezo yao inayopendwa zaidi kama Tanzania Bara ilivyo na michezo yake ikiwemo ya asili.
Ni michezo ambayo huchezwa kwa kuhusisha rika la watu tofauti, na hufanyika haswa wakati wa mapumziko ikiwemo jioni baada ya watu kumaliza shughuli zao za kujitafutia kipato.
MAKACHU
Makachu ni mchezo wa asili ya Kizanzibari unaochezwa zaidi na vijana wenye ujuzi wa kujitupa majini kutoka umbali mrefu wa nchi kavu, na kisha kuogelea.
Zamani, mchezo huo ulikuwa kama wa kujifurahisha lakini sasa hivi unatumika kuwaingizia pesa vijana ambao hufanya matangazo kwa kubeba mabango yenye maandishi ama bendera, na kisha kukimbia nayo kwenye usawa wa bahari, na kujitupa majini. Tukio hilo husindikizwa na kamera ili kunogesha tangazo.
Hata watalii wanapokwenda Visiwani humo huwalipa pesa vijana na kisha huandika majina yao kwenye bango, mfano “Welcome Mr John,” na kukimbia na hilo bango baharini na kujitupa nalo kwenye maji.
NGWARE
Ngware ni mchezo wa kupiga mtu mtama.Kwa ujumla, ni mchezo unaotumia miguu na mikono katika uchezaji wake.
Mchezo huu unaweza kusema hauna tofauti na mieleka kutokana na uchezaji, ukamataji wake, hata watu kuangushana kwao hadi kupatikana mshindi.
Katika kisiwa cha Pemba Wilaya ya Micheweni, ndiko mchezo huo unakochezwa tangu miaka 30 iliyopita. Katika Bara la Afrika ni mchezo mkubwa sana, na zaidi huchezwa Senegal. Kidunia huchezwa Japan, na hutumiwa na wachezaji wanene.
Kwa sasa, mchezo wa ngware haumo tena kwenye mashindano ya Olympiki, mara ya mwisho mchezo huo uliondolewa mwaka 2020.
Ulingo wake unatakiwa ujengwe juu kidogo kama wa ‘boxing’, ili kuwafanya watu weweze kuona pande zote.
Mchezo hushirikisha timu mbili A na B, kila timu inatoa mchezaji mmoja, ambapo watakuwa katikati, na mwamuzi mmoja wa kuamua mshindi wa mchezo huo.
Anasema wachezaji hukamatana mikono kwa ukakamavu wa hali ya juu, hapo tena ndipo wanapopigana Ngware (mtama), ili mmojawapo amwangushe mwenzake chini na hivyo kuwa mshindi.
NAGE
Nage ni mchezo mwingine unaochezwa sana Zanzibar.Zamani watoto waliucheza sana vijijini lakini sasa hivi hata watu wazima wanaocheza, hasa wanawake.
Mchezo huu unafanana na rede, lakini unashirikisha wanawake wanne na kuendelea, na ukaaji wao ni tofauti, kwa kuwa wachezaji hujipanga pande nne, na mchezeshaji mmoja hukaa katikati, ili apate mpira ambao walio nje ya duara, wanarushiana. Akifaulu kuudaka, hujiunga na wachezaji walio katika duara, na aliyeurusha anaingia katikati badala yake.
BAO
Ni mchezo ambao hupendwa sana Visiwani humo, ambapo wanaume huucheza sana hasa wanapomaliza shughuli zao za uvuvi na biashara za pweza na samaki.
Kiutamaduni wengi hucheza wakiwa wamevaa misuli, huku wakisimuliana mambo mbalimbali.
Ikumbukwe zamani Hayati Abeid Aman Karume alikuwa anapenda sana kucheza mchezo huo, na hata tukio la kupigwa risasi na kusababisha kifo chake, lilitokea wakati akiwa anacheza mchezo huo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wapinzani wa Yanga katika kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Hilal ya Sudan, wameliandikia barua Shirikisho la Soka Afrika CAF kuomba mechi zao za kimataifa zichezwe nchini Libya.
Al Hilal kwa sasa wanatumia nchi ya Maurtania kama nyumbani katika mechi za kimataifa ambapo hivi karibuni ilimualika TP Mazembe na kumnyuka 2-1.
Kwa mujibu wa mtandao wa michezo wa Libya Observer, Al Hilal imeandika barua kisirisiri kwenda CAF ikitaka kutumia uwanja wa Benghazi.
Kama endapo CAF watakubali ombi la Al Hilal, mechi ijayo ya hatua ya makundi kati yao na Yanga itachezwa nchini Libya katika dimba la Benghazi.
Mechi ya marudiano ya makundi kati ya Al Hilal na Yanga imepangwa kuchezwa Januari 10 mwakani 2025.
Yanga bado ina kisasi kikubwa na Al Hilal baada ya kufungwa mara mbili na timu hiyo, ambapo mwaka juzi ilikwama kule nchini Sudan katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa ya kuwania nafasi ya kuingia hatua ya makundi kwa kufungwa 1-0.
Safari hii Yanga alifungwa tena katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi kwa kupokea kichapo cha 2-0 nyumbani kwenye dimba la Benjanim Mkapa, huku kocha akiwa yule yule Florent Ibenge.
Msisitizo walionao Yanga kwa sasa ni kuhakikisha wanashinda mechi zilizo karibu yao kwa mujibu wa ratiba, na kisha waanze kuipigia hesabu Al Hilal ambayo imekuwa mfupa mgumu msimu huu.
“Tupo kwenye kipindi kigumu, lakini hatupaswi kuangalia yaliyopita, sisi kazi yetu ni kusonga mbele kama kaulimbiu yetu inavyosema, ya ‘Daima Mbele, Nyuma Mwiko’. Tunaomba mashabiki wetu waendelee kuwa nasi. Malengo yetu bado ni yaleyale ya kufika mbali katika mashindano ya kimataifa,”alisema Alex Ngai, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Yanga.
Yanga hadi sasa imepoteza mechi mbili za Ligi Kuu na mbili za kimataifa ndani ya muda mfupi.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewataka Waamini kuuishi Ukristo wao, huku wakilishika Neno la Mungu.
Kardinali aliyasema hayo hivi kalibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa Vijana 112 katika Parokia Teule ya Mtakatifu Stephano wa Hungaria – Makurunge, jimboni humo.
“Sakramenti hii ya Kipaimara ni muhimu sana kwa Mkristo kuipokea, kwa sababu inakupatia uwezo mkubwa wa kumtangaza Kristo mahali,popote pale bila hofu. Pia, inakupatia nguzo kubwa ya kuwa askari hodari wa imani ya Kristo,” alisema Kardinali.
Alisema pia kuwa Waamini wengi hawasikilizi sauti ya Kristo, na hawafuati maneno yake, akiwasisitiza kuepuka kupotoshwa kwa maneno ya uongo, bali wafahamu kwamba sauti ya Mungu ndiyo inatakiwa kufuatwa.
“Sijui wamepotoshwa na kitu gani kibaya, bali utakuta wanafuata sauti za watu waongo ambao hawawezi kuwafikisha safari ya kuelekea kwa Baba Mungu. Ndugu zangu Waamini, nawaomba sana fuateni sauti ya Kristo, ambayo itawasaidia katika safari yenu ya kumtangaza Yesu Kristo ili baadaye muwe watu wema machoni mwake.
“Pia, tutambue kwamba Mungu ametuambia tusikilize sauti ya mwanaye. Huyu ndiye mwanangu niliyependezwa, naye msikieni, Mungu alikuwa na maana kubwa sana kutamka maneno haya. Tuwe watu wa kupendana, kuheshimiana, na kusaidiana kila wakati,” alisema Kardinali.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Watakatifu Wote – Kiluvya, Padri Danipaso Bitegeko, ambaye pia ni Msimamizi wa Parokia hiyo Teule, alimshukuru Kardinali Pengo kwa kufika parokiani hapo, na kuwapatia Vijana Sakramenti hiyo ya Kipaimara.
Naye, Mwenyekiti wa Parokia Teule, Gabriel Mwalo alisema kuwa kwa sasa wapo katika ujenzi wa nyumba mpya ya Mapadri, ili Padri aweze kukaa hapo hapo, kwani kwa sasa Waamini wanazidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo wanahitaji huduma ya kiroho kwa karibu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ametoa wito kwa Vijana wanaopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kumweka Mungu maanani siku zote za maisha yao.
Kardinali aliyasema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyoambatana na Sakramenti hiyo katika Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu Mtume – Kijitonyama, jimboni humo.
“Wanakipaimara tambueni kwamba katika maisha yenu ni lazima mumuweke Mungu Mwenyezi maanani. Na ndilo Neno lililotukusanya leo hapa, mlipotualika tuje kuadhimisha, kushuhudia adhimisho lenu la Sakramenti ya Kipaimara, ni ninyi mmetualika. Huwa hamumwoni Askofu anakuja hapa kanisani, lakini ni kwa sababu yenu ninyi mnaopokea Sakramenti ya Kipaimara, mimi niko hapa…
“… na hawa wote waliopo hadi Wanakwaya, huwa wanakuwepo sawa, lakini kwa leo ni kwa sababu yenu kuonyesha kwamba tunaweka maanani tendo mnalolifanya siku hii ya leo. Ni tendo kubwa lenye manufaa, siyo kwenu tu, ni tendo kubwa ambalo mnalifanya kwa niaba ya Kanisa zima. Kwa hiyo tunawaombea kwa Mungu Mwenyezi atekeleze maombi yanayokuwa ndani ya moyo wa kila mmoja wenu,” alisema Kardinali Pengo.
Aliongeza kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kufanya kitu na kufanikiwa bila kumtanguliza Mungu, akisisitiza kuwa kila mmoja ahakikishe anamtanguliza Mungu katika mipango yake.
Sambamba na hayo, Kardinali alitoa mfano wa watu waliotaka kujenga mnara mrefu ili wakamwone Mungu mbinguni, na kwamba Mungu hakuona wivu juu ya maamuzi hayo, bali lengo ni kuwaonyesha kuwa hakuna kitu kinachofanywa na mwanadamu bila kumweka Mungu maanani.
“Waliotaka kujenga mnara ili uwe kumbukumbu yao hata kama hawapo, Mungu Mwenyezi alipogundua kwamba hawa watu wanataka kujenga kitu cha namna hii, akaamua kuwachanganya kwa lugha, hawakuweza kuelewana tena; mmoja akitumwa na mwenzake lete jiwe, yeye analeta maji; naomba mchanga, yeye analeta maji, kwa hiyo hawakuweza kuendelea kwa sababu hawaelewani tena…
“Si kwamba Mungu Mwenyezi aliwaonea wivu kwamba watafanya kitu kikubwa hivyo, lakini Mwenyezi alitaka kumwonyesha mwanadamu kwamba ‘ukitaka kufanya kitu chochote bila kuniweka mimi Mungu maanani, haiwezekani, hutafanikiwa,” alisema Kardinali Pengo.
Vile vile, alitoa wito kwa Vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara katika Adhimisho hilo, pengine wana mipango mikubwa iliyopo katika maisha yao, bali watambue kwamba hawataweza kufanikiwa bila kumweka Mungu mbele.
Aliwasisitiza kufahamu kuwa hakuna anayeweza kuwazuia kupanga mipango, hasa ya kimaendeleo maishani mwao, bali wakumbuke kwamba bila kumweka Mungu maanani, hakuna kitakachofanikiwa.
Wakati huo huo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwakumbusha Vijana hao kuendelea kuishi maisha yanayompendeza Mungu, kwani hayo ndiyo yatakayowasaidia kupokea baraka katika kila wanaloliomba kwake.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu, na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Aretas Lyimo, alisema  kuwa mpaka sasa watuhumiwa 58 wamekamatwa kwenye operesheni hiyo.
“Katika dawa za kulevya tulizozikamata, ni pamoja na mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, na tumeweza kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi, na lita 19,804 za kemikali bashirifu,”alisema Kamishna Lyimo
Aidha alisema kuwa kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja (01) ya hashishi, zilikamatwa katika eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
Alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake, ambao hudai kutumia dawa hizo kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.
“Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inayosababisha madhara makubwa kiafya. Vile vile, hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka. Mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa, na magonjwa haya wamerogwa,”alisema Lyimo.
Adiha, alisema kwamba katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
“Dawa hizi ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka, ili kuepuka kubainika. Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, Hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya, na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya,”alisema Kamishna Lyimo.
Kamishna Lyimo alisema kuwa mkoani Dodoma, Mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili Suleiman Mbaruku Suleiman (maarufu Nyanda), mwenye umri wa miaka 52, na Kimwaga Msobi Lazaro (miaka 37) wakazi wa mtaa wa Kinyali, Kata ya Viwandani.
“Watuhumiwa hao walikamatwa na jumla ya gramu 393 za heroin. Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo, na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu,”alisema.
Kupitia operesheni za kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba wananchi waendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya, na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano na taasisi ya Henan Polytechnic Institute, kutoka Nanyang, China, ili kushirikiana kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika nyanja za kilimo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, (TEHAMA).
Makubaliano hayo yamesainiwa, ambapo katika makubaliano hayo VETA Kihonda kitanufaika katika nyanja ya kilimo na Chuo cha VETA Kipawa, kitanufaika katika sekta ya TEHAMA.
Aidha, waalimu na wanafunzi kutoka vyuo vya VETA Kihonda na Kipawa watajengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo katika maeneo ya Kilimo na TEHAMA, ili kuboresha elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kuhakikisha wanazalisha wahitimu bora wenye kukidhi ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya Tanzania.
Katika mpango huo, waalimu na wanafunzi kutoka pande zote mbili, watapata fursa za kutembeleana na kubadilishana uzoefu baina yao, ili kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa katika ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, ameishukukuru taasisi ya Henan Polytechnic kutoka China kwa kuona VETA ndiyo sehemu sahihi ya kuleta teknolojia mpya katika masuala ya kilimo na TEHAMA.
CPA. Kasore alisema kupitia makubaliano hayo, VETA inatarajia kunufaika kwa kiasi kikubwa, hasa katika kupata utaalam mpya ambao utawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi bora na yenye viwango vya kimataifa ambayo yatakidhi ushindani katika soko la ajira.
“Ninaamini, kwamba kupitia ushirikiano huu, ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujikwamua kimaisha inaenda kutimia, naomba ushirikiano huu uwe chachu katika kuzalisha vijana ambao wataweza kushindana katika soko la ajira kimataifa katika kujenga uchumi wao na taifa la Tanzania,” alisema CPA. Kasore.

MOSHI

Na Mathayo Kijazi

Wakristo wametakiwa kuwa wanyenyekevu na wenye hekima katika maisha yao, kwani hiyo itawasaidia kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Hayo yalisemwa na Padri Festo Tingo wakati wa homilia yake katika Misa Takatifu ya kumwombea marehemu Mzee Michael Lesio Kissoka, baba mzazi wa Padri Bonaventura Kissoka AJ, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Anna – Kirima, Jimbo Katoliki la Moshi.
Padri Tingo aliwasihi Waamini walioshiriki katika Adhimisho hilo, kuiga mfano wa maisha ya Mzee Kissoka, yakiwemo ya unyenyekevu na kuwajibika, kwani ni katika jitihada tu ndipo wanafanikiwa.
“Ukimya ni jambo lenye tafsiri nyingi katika maisha ya binadamu, ambapo pia ndani yake ukimya huashiria busara. Mzee Kissoka alikuwa mkimya, mnyenyekevu, mwenye busara, na mwenye kupenda kusali. Kwa hiyo ndugu zangu, ni vema kila mmoja akatumia muda wake vizuri kufanya matendo yaliyo mema, kwa sababu kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmeitengeneza njia ya kwenda mbinguni,” alisema Padri Tingo.
Alisema pia kwamba hata kama Mzee huyo amefariki, bali watoto pamoja na ndugu kwa ujumla, wasiache kwenda kusalimia, kwani Kirima bado ina watu wanaostahili kwenda kusalimiwa.
“Usiseme kwamba siendi tena Kirima kusalimia kwa sababu mzee wangu hayupo, hapana. Endelea kuja kusalimia kwa sababu Wanakirima wapo, na Kirima ipo,” alisema Padri huyo.
Kwa upande wake Padri Bonaventura Kissoka aliwashukuru Mapadri wenzake, Waamini kutoka Majimbo mbalimbali, pamoja na watu wengine kwa kushiriki na kuwafariji katika msiba huo.
Padri Kissoka alisema kuwa wao kama familia, wanamshukuru Mungu kwa maisha ya baba yao kwa kuwalea katika misingi iliyo bora, ikiwa ni pamoja na kuwasomesha.
Akisoma wasifu wa marehemu, Michael Kissoka ambaye ni mjukuu wa Mzee Michael Lesio Kissoka, alisema Mzee huyo alizaliwa Septemba 26 mwaka 1926, Kibosho - Kirima Kati, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Alipata elimu ya watu wazima mwaka 1954, pamoja na elimu ya ufundi seremala na udereva.
Aliongeza kuwa Mzee huyo aliwafundisha kusali, kwani alipenda kusali kabla ya kufanya chochote, desturi ambayo aliipata kwa Masista, ambapo kwa kuishi hivyo, alijenga familia ya maisha ya sala, jambo lililomfanya kuwahimiza watoto wake kuwa na desturi ya kusali kila mara.
Kuhusu ugonjwa, mjukuu huyo alisema kwamba babu yake hakuwahi kusumbuliwa na ugonjwa wowote katika utu uzima wake hadi mwaka 2015, ambapo alikabiliwa na tatizo la koo na kuanza matibabu katika hospitali ya KCMC iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, na baadaye kupata matibabu zaidi katika hospitali ya OCEAN ROAD, Dar es Salaam baada ya kugundulika kuwa na saratani ya koo.
Aliendelea kusema kuwa mwezi Juni mwaka 2015, alipatiwa matibabu katika mji wa Ahmedabad nchini India, na baadaye aliendelea na matibabu katika klinik ya BESTA iliyopo Kinondoni Dar es Salaam, ambapo baada ya vipimo, alionekana kupona ugonjwa huo, na hivyo kuendelea na maisha yake kama kawaida.
Marehemu Mzee Michael Lesio Kissoka aliyefariki dunia Jumamosi Novemba 2 mwaka 2024 siku ya kuwakumbuka na kuwaombea Waamini Marehemu Wote; ameacha watoto.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, amewaasa vijana watambue kuwa wao ni Taifa la leo na si taifa la kesho, akiwasihi kuwa na uchungu na taifa lao.
Padri Kitima alisema hayo hivi karibuni katika Kongamano la Vijana lililofanyika katika Chuo cha ufundi Don Bosco, Oysterbay, Jijini Dar es salaam.
“Unatakiwa kuwa na uchungu na taifa lako kwa kuitambua vyema nchi yako ya Tanzania pamoja na ‘focus’ yaani nchi inapolenga kwa ajili ya maendeleo ya uchumi huku ukifahamu malengo ya viongozi”. Alisema
Alikumbusha kipindi cha nyuma ambapo kulikuwa na sera kama Tanzania ya viwanda au Kilimo kwanza lakini cha ajabu kwa sasa hakuna focus yeyote ya nchi ambayo itasaidia katika maendeleo.
Hata hivyo Padri Kitima alisema kuwa unapojengewa ‘physical skills’ unapewa mbinu ya kujitambua kama Mtanzania ni vyema kutumia maarifa ili uweze kufikia malengo ya nchi.
Mbali na hayo alizungumzia‘Development plan’ ya Hayati Rais Benjamin Mkapa iliyolenga kwa kila mtu kujitegemea, Mkapa aliwekeza katika kuanzisha taasisi zilizoweza kumuongoza katika sheria kama Tanroads, Takukuru, Tanzania Revenue Authority na zingine nyingi ambazo aliweza kusaidiana nazo katika kuingoza nchi”.
Vilevile Padri Kitima alisema nchi yetu imelenga kwa vijana ili kutoa taarifa zilizo sahihi kwa kuwasimulia matukio ya nyuma kwani 1884-1885 kulitokea na tukio kubwa ambalo lilibadili siasa zote za Tanzania ambalo ni Mkutano wa Berlin ambao uliligawa bara la Afrika na kuunganishwa na makoloni mengine ya ujerumani na kuanza kutumia siasa ya pamoja.
Hata hivyo alieleza kuwa hapo ndipo ushirikiano wa makabila ulianza kwani waliwekwa pamoja na kuanza kazi kwa umoja japo wajerumani walikuwa na lengo la kuwanyonya waafrika.
Padri Kitima alisema Tanzania ina wawekezaji wengi wa nje kuliko wa ndani lakini India wawekezaji wao wengi ni wahindi ambao wanasaidia mapato yao yasiende mbali bali yazunguke ndani ya taifa lao kutokana na wawekezaji wao.
Pia aliwataka vijana watambue kuwa Marekani matajiri wazawa ndiyo wanao ikopesha serikali na kusema inasikitisha kwa Tanzania hakuna hata Mzawa mmoja anayeimiliki hoteli kubwa kwani waliokuwa wakimiliki kipindi cha nyuma wamezibinafsisha kwa sera ya kusema hawawezi kuziendesha.
Padri Kitima aliwataka vijana kuwa na malengo na jambo Fulani kwa kuiga mfano wa Rais Obama wa kutamani kuongoza Marekani na lengo lake kutimia hivyo basi aliwaasa vijana kuwa na ndoto ya siku moja kuja kuondoa mfumo wa chama kimoja bungeni na kuruhusu vyama vingi.
Aliendelea kusema aliyepita kwa wizi wa kura hawezi kuwatetea wananchi wake, na kuwataka vijana kukataa dhambi ya kuchukua pesa kwa ajili ya kutangaza majibu ya uwongo wakati wa uchaguzi.
Aliwataka vijana kutoruhusu nchi ya vyama vingi kutawaliwa na chama kimoja kwa kusema kitashika serikali na bunge hata mahakama itashindwa kufanya kazi yake kwa haki.
Padri Kitima alisema vijana wanawajibika kuamka sasa kabla hawajaingia maofisini na baadaye kuanza kulia machozi wakati watu hao wameanza majukumu.
Alitoa wito kwa vijana kuchagua kiongozi muwazi na muwajibikaji ili aweze kutekeleza wajibu kwa haki.