Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa kazi ya Msimamizi katika Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, ni kuwasaidia wazazi wa mtoto anayemsimamia, ikiwemo kujua maendeleo ya kiroho ya mtoto huyo, na kwamba siyo tu kumuwekea mkono begani wakati wa kupokea.
Ufafanuzi huo ulibainishwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Vijana 49 katika Parokia ya Mtakatifu Simon Stock – Mbezi Mageti, jimboni humo.
“Pengine watu wanaweza kujiuliza kwamba nini majukumu ya msimamizi wa mtoto wakati wa kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara. Msimamizi ni mzazi wa mtoto huyo kiroho, na anatakiwa kujua maisha ya mtoto huyo baada ya kupokea Kipaimara.”
“Kwa hiyo, wewe msimamizi jitahidi kuulizia maendeleo ya mtoto uliyemsimamia. Tambueni kwamba mna kazi ya kuwalea watoto hawa, siyo tu kuwabandikia mikono begani wakati wa kupokea Sakramenti hii ya Kipaimara,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu huyo aliwasihi Waamini kuchangia katika shughuli za kimungu, ikiwemo ujenzi wa kanisa, kwani kufanya hivyo si kama kuchangia katika sherehe za harusi, bali ni kufanya jambo litakalowapatia baraka.
Hata hivyo Askofu Mchamungu aliwaasa Waamini kutokuoneana wivu katika maisha yao, bali waweke kipaumbele suala la kusaidiana, huku wakiwa katika misingi ya kumpendeza Mungu.
‘Kwa hiyo ndugu zangu, hakuna sababu ya kuoneana wivu. Tunaona katika maeneo mbalimbali watu wanaoneana sana wivu. Kwa Mkristu, hiyo siyo tabia nzuri kabisa,” alisema Askofu Mchamungu.
Vile vile, Askofu Mchamungu aliwapongeza Wanaparokia hiyo kwa hatua nzuri waliyofikia ya ujenzi wa kanisa, akiwaomba kuongeza umoja na mshikamano ili waweze kukamilisha.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Nelson Osmond alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kufika parokiani hapo, na kuwaimarisha Vijana 49 kwa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara.
Padri Nelson aliwapongeza Waimarishwa kwa kupokea Sakramenti hiyo, akiwasihi kuendelea kuyaishi yale yote waliyofundishwa ili yaendelee kuwasaidia katika maisha yao.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Walei Parokia, Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Dk. Felix Sukuma   alimshukuru Askofu Mchamungu, akisema kwamba wamefarijika kutembelewa na Askofu aliyewaongoza katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba amewataka Waamini kuwa wanyenyekevu, kwani utawasaidia kuuona ukuu wa Mungu.
Askofu Musomba alisema hayo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 na 50 ya Upadri, iliyoadhimishwa katika viwanja vya Kituo cha Msimbazi, jimboni Dar es Salaam.
“Katika hilo ni kwamba sifa zimwendee Mungu kwa makuu aliyowatendea ndugu zetu Wajubilanti kwa miaka 25 na miaka 50. Si rahisi hivyo, na ndiyo maana haya yote yanahitaji sana unyenyekevu. Katika unyenyekevu, ndipo tunapotambua ukuu huu wa Mungu katika maisha yetu,” alisema Askofu Musomba.
Musomba aliwaasa Wakristo kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Makuhani, akiwasihi kutambua kwamba Makuhani hao ni Kristu mwingine.
“Tunapoadhimisha haya yote, tunathamini sana wito huu mkubwa wa Ukuhani. Kwa maneno mengine hawa Makuhani ambao ni Yesu mwingine. Na katika kumshukuru huyu Kristo, tumshukuru Mungu tumeona makuu anayotutendea kwenye maisha yetu. Na katika kuyaona hayo makuu, siyo kwamba tunajivunia kwamba tumeweza, ila tunamshukuru Mungu, na tunamsifu yeye peke yake,” alisema Askofu huyo.
Sambamba na hayo, alikumbusha kile kilichoendelea katika Kongamano la 5 la Kitaifa la Ekaristi Takatifu juu ya Ukuu wa Adhimisho la Misa Takatifu, na kwamba wanaojongea mbele za Mungu, Mungu hawezi kuwaacha.
Wakati huo huo, Askofu Musomba aliwapongeza Mapadri hao kwa Jubilei yao ya Miaka 25 na 50 ya Upadri, akisema kwamba wamefanya kazi kubwa kwa kuweza kukaa katika utume wao, pamoja na kudumisha utambulisho wao kama Makuhani.
Askofu huyo aliongeza kwamba kama Wanajimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wameziona kazi pamoja na utume kwa ujumla uliofanywa na Mapadri hao katika Parokia pamoja na Taasisi mbalimbali jimboni humo, hasa katika malezi yao ya kuwapeleka watu kwa Mungu.
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Henry Mchamungu, akiwasilisha salamu za Askofu Mkuu, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, aliwapongeza Mapadri hao kwa Jubilei yao ya Miaka 25 na 50, huku akiwapongeza kwa kazi kubwa wanazozifanya katika utume wao.
Askofu Mchamungu alibainisha kwamba hakuna mtu yeyote duniani mwenye mamlaka au uwezo wa kumwondolea mtu Daraja Takatifu la Upadri, bali binadamu anao uwezo wa kumwondolea mtu hadhi ya Uklero.
“Nadhani itabidi siku moja tuboreshe lugha. Kusema miaka 25 au 50 ya Upadri kwa tukio kama hili, je utawezaje kutofautisha na tukio ambalo ni Padri ambaye hayupo katika utumishi, lakini na yeye anakumbuka kwamba ametimiza miaka 25 au miaka 50 ya Upadri?
‘Kama mnavyojua, kuna Sakrementi tatu ambazo zinaweka alama isiyofutika, ambazo ni Ubatizo, Kipaimara, na Daraja Takatifu la Upadri. Tunapoongelea kuhusu Daraja Takatifu la Upadri, ni kwamba hakuna binadamu yeyote duniani ambaye anao uwezo wa kumwondolea mtu Daraja Takatifu la Upadri, ila binadamu anao uwezo wa kukuondolea ile hadhi ya Uklero. Lakini anayekuwa Padri, anakuwa Padri milele.
Askofu huyo alibainisha kwamba neno Utumishi ni muhimu sana, na ndilo neno linalofaa kutumika kwa Mapadri, kwani linaonyesha kwamba wanapongezwa kwa miaka hiyo wakiwa katika utumishi wao, na si nje ya utumishi kama ilivyo kwa wengine.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema kuwa hali ya uwekezaji nchini imeongezeka katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kwamba TIC ilisajili miradi 198 yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.69 sawa na zaidi ya Shilingi trilioni tatu, itakayoajiri watu 9600 kote nchini.

Dar es Salaam

Na Israel Mapunda

Meneja wa Maabara Kuu ya Veterinari kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dk. Geofrey Omarch amefanya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula hivuo Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar Es Salaam ili kufuatilia ubora wa vyakula hivyo.
Dk. Omarch aliongeza kuwa TVLA kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inalenga kuwalinda watumiaji wa vyakula hivyo ili kulinda ubora wa vyakula vinavyozalishwa vitokanavyo na zao la Mifugo pamoja na kuongeza soko la Mifugo kimataifa.
“Tumekuwa tukifanya ukaguzi huu mara kwa mara kwa wasindikaji, wauzaji na watumiaji wa vyakula vya Mifugo ili watumiaji wa mazao hayo wawe salama wakati wote. TVLA imedhamilia kuwapitia wazalishaji wote Tanzania nzima kwa nyakati tofauti ili kujiridhisha kile kinachozalishwa kama kinakidhi ubora, kukagua marighafi za uzalishaji, hatua za uzalishaji pamoja na kukagua vibali vya uzalishaji,” alisema Dk. Omarch.
Baadhi ya wazalishaji wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Kinondoni waliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwafanyia ukaguzi wa mara kwa mara kwani ukaguzi huo unaowaongezea umakini kwenye uzalishaji wa vyakula.
Wameiomba Serikali kutochoka kwenda kuwakagua na kuwapa ushauri na kuendelea kuwadhibiti baadhi ya wazalishaji ambao sio waaminifu wanaowaharibia soko la vyakula kwa kuzalisha vyakula vyenye mapungufu na kuvipiga chapa za kampuni zingine.
Wakala ya Maabara ya Veterinali Tanzania (TVLA) imekuwa ikifanya ukaguzi wa vyakula vya mifugo mara kwa mara kwa wazalishaji, wauzaji na pamoja na wanunuzi wa vyakula vya Mifugo kwa kushirikiana na wakaguzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi za Wakuu wa Mikoa pamoja na Halmashauri.

MTWARA

Na Mwandishi wetu

Serikali imesema kuwa itajenga Kongani ya Viwanda vya kuchakata mazao ya Mikoa ya Kusini kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 300.
Akizungumza katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Mtwara, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, kuwa alisema iwe jua ama mvua itajenga Kongani ya Viwanda vya kuchakata mazao ya Mikoa ya Kusini eneo la Maranje Mkoani Mtwara yenye gharama ya zaidi ya sh. Bilioni 300.
Kongani ya Viwanda (Industrial Park) inajengwa katika kijiji cha Maranje na Tulia, Kata ya Mtiniko, Nanyamba Mji, Mkoani Mtwara
Alisema eneo la mradi lina jumla ya ekari 1,572, ambapo eneo linaloendelezwa kwa sasa ni ekari 354, na ekari 1,218 zilizobaki zitasafishwa na kuwekewa uzio mwezi ujao.
Waziri Bashe alieleza kuwa, Kongani hiyo ya Viwanda ndilo suluhisho la changamoto walizonazo wakulima wa mikoa hiyo.
“Wapo watu walisema ni ndoto, haitawezekana leo, nawaambia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni msikivu na mtendaji, ameamua iwe jua iwe mvua, Kongani itajengwa hapa na itahusisha viwanda mbali mbali vya kuchakata korosho, ufuta, mbaazi na mengine,”alisema Waziri Bashe.
Alisema, Serikali imeanza hatua za awali za ujenzi wa Kongani hiyo, na zaidi ya sh. Bilioni 7 zimewekezwa.
“Mradi huu mkubwa unaoitwa Dkt Samia Suluhu Hassan, unalenga kujenga viwanda vya kubangua korosho visivyopungua 30 kwa awamu, na tayari zaidi ya shilingi bilioni saba zimetumika kujenga maghala mawili na kisima kimoja,”allisema Bashe.
Aliongeza pia kuwa maghala hayo mawili ya awali, yenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 za korosho, yanatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu, ili msimu wa korosho wa mwaka kesho uanze kwa ufanisi.
alisema huo pia utatoa fursa za ajira kati ya watu 33,000 mpaka 35,000 ambapo ajira za kwanza zitanufaisha wananchi wenyeji .
“Mradi huu unatarajiwa kuajiri kati ya watu 33,000 mpaka watu 35,000 na utakuwa suluhisho la changamoto ya muda mrefu juu ya bei ya korosho kwa mikoa yote inayolima korosho, ikiwemo Mtwara, Ruvuma, na Lindi. Serikali yenu ni sikivu haitarudi nyuma, hiki kiwanda kitajengwa kwa maslahi ya wananchi wa kusini,”alisisitiza Bashe.
Aidha, Waziri Bashe alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kurejeshwa kwa agenda ya ushuru wa mauzo ya nje, lengo ni kuwezesha upatikanaji wa ruzuku na pembejeo, ili kumuinua mkulima.
Bashe alisema kuwa fedha hizo za ushuru huo zikikusanywa, zinarudi Bodi ya Korosho ili kusimamia mahitaji ya korosho.
“Faida zake ni kubwa kwa kuwa ushuru huu sasa unarudi bodi ya Korosho ili kuwezesha wakulima wa zao hilo. Sasa tumetoka kuzalisha tani 180,000 hadi tani 310,000 na tunatarajia kufikia tani 500,000”, alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota alimpongeza Waziri Bashe kwa mapambano ya kutetea maslahi ya wakulima wadogo nchini.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam amewaasa Vijana 129 waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kuishi katika viapo walivyoweka kwa Mungu kwa ajili ya kazi ya kuhubiri Injili kwa mataifa.
Alitoa wosia huo hivi karibuni wakati wa homilia yake katika adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Mtakatifu Maria Faustina, Lulanzi-Kibaha, Jimboni humo.
“Inawapasa mtambue kuwa mkiishi vyema, ahadi zenu mlizo weka kwa Mungu, basi tambueni mtapewa uwezo wa kujua na kutambua lile analolitaka Mwenyezi Mungu kwa wakati na kwenye mazingira ya wakati huo”Alisema Kardinali Pengo
Aliwataka Waamini watambue Pentekoste ya kwanza ya Mitume, ambao walipewa uwezo wa kuhubiri injili kwa mataifa bila ya uwoga na wasiwasi, hata Mwinjili Yohane anasimulia kuwa Mitume walikuwa wakijificha ndani kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi, lakini waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, uwoga uliondoka, kwani Roho huyo aliwafanya kuwa na ujasiri.
Kardinali Pengo alisema kuwa viongozi wa Kiyahudi hawakupenda na hawakutaka kusikia habari za Yesu na yeyote aliyekuwa akitangaza imani ya Kristo, alikuwa ni adui kwa viongozi hao.
Sambamba na hayo alisema jambo ambalo kwa sasa linatia hofu, ni kuhusu watu wanaopotea katika mazingira ya kutatanisha, na kesho yake kukutwa wameshauawa, na kwamba hali hiyo inawasukuma watu kujiuliza matendo kama hayo yanafanywa na nani.
Kardinali Pengo alisema kuwa hayo yanayotendeka ya watu kuuawa na mtu akijitokeza kusema ukweli naye anauawa ndiyo sababu ya watu wengine kuogopa kusema ukweli, na kuwataka Waimarishwa wazidi kumwomba Roho Mtakatifu awatoe hofu katika kufanya kazi zao, na kuwataka wamtumie vyema Roho wa Mungu.
Pia, aliwataka Waamini wote watambue kuwa chimbuko la maafa yote ni dhambi, na wakati mwingine dhambi hizo ni katika kutafuta utajiri, au ukosefu wa imani, wazazi kwa watoto wao kwa kutambua kuwa watoto wao ni chimbuko la Utajiri.
Kardinali Pengo aliwataka Waamini wajitahidi kuishi bila dhambi na kushuhudia imani huku wazazi na walezi wakiwaombea vijana wanaopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara ili waweze kuishi imani yao na kutangaza habari njema ya wokovu bila uwoga.
Vilevile aliwataka waamini kuwakumbusha vijana hao mambo yote watakayo yaahidi na kuwasaidia kwa kukaa nao siku zote za maisha yao ili wasisahau kumuomba Mungu awasimamie katika vita yao ya kupambana na dhambi.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Paroko Msaidizi wa Parokia Mtakatifu Maximiliam Kolbe, Mwenge, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,  Padri Daniel Mapunda amewataka Waamini kuachana na wivu, kwani huo ni ushamba wa kutojitambua.
Alisema hayo katika homilia yake wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu iliyoadhimishwa  parokiani hapo.
“Wivu ni ile hali ya mtu kutokupenda mafanikio ya mwenzako, lakini inawapasa kutambua kuwa wivu kwa maana nyingine ni ushamba wa mtu kumtolea mwenzako kijicho kwa yale mafanikio aliyopewa na Mungu,”alisema Padri Mapunda.
Padri Mapunda aliwaasa Waamini wazidi kumwomba Mungu ili wajitambue kuwa wao ni nani, na kufahamu uwezo wao waliopewa na Mungu.
Aidha, aliwataka Waamini wafahamu, vizuri jinsi ya kuzitumia karama zao walizojaliwa na Mungu na kuzifahamu kwani hata kama ndugu wamezaliwa tumbo moja hawawezi kufanana karama zao.
Kwa mujibu wa Padri Mapunda, Waamini wanapaswa kufahamu kuwa utajiri wa Mungu hauna mipaka, na kuwataka watambue kuwa Mungu aliwapa Manabii utajiri wa kuhubiri Injili kwa watu wake.
Aliwataka Waamini hao kila mmoja kwa nafasi yake kuonesha utu kila mahali, na kuziheshimu kazi  zao.
Padri Mapunda alisema hata katika somo la Injili inaonyesha namna Mungu alivyotoa, talanta na kuwataka Waamini wasizitumie vibaya.
Hata hivyo, aliwaomba Waamini hao kuachana na tabia za kuwakwaza wenzao kwa kuwafabyia matendo ambayo kwa upande wao hawayapendi.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane wa Mungu – Vituka, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Patrick Bwakila amewataka watoto kutokuufananisha mkate uletao uzima (yaani Mwili wa Kristu) na mikate mingine, kwani wanapokula Mkate huo, wanamla Kristu mwenyewe.
Aliyasema hayo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyokwenda sanjari na kuwapatia watoto hao Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika Parokia ya Yohane wa Mungu – Yombo Vituka, jimboni humo.
“Ndugu zangu wanangu wapendwa, Mama Kanisa alitufundisha kwamba Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu, Mungu kweli na Mtu katika maumbo ya mkate na divai…
“Kumbe, mkate tunaokula leo, siyo ule wa mama mpika chapati, hapana, ni Kristu mwenyewe ndiye mnayemla leo. Na Kristu mwenyewe anatuambia, aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, huyo hukaa ndani yangu, na mimi hukaa ndani yake. Huu ni mkate wa uzima, mkate uletao uponyaji, afya ya roho, mkate unaotustahilisha sisi huurithi na kupata uzima wa milele,” alisema Padri Bwakila.
Padri Bwakila aliwaonya watoto hao kuepuka kumuasi Kristu mara baada ya kupokea Sakramenti hiyo Takatifu, na kuongeza kwamba atakayefanya hivyo, atatakiwa kuacha kushiriki sakramenti, kwani amemkana na kumkimbia Kristu.
Pia, aliwataka kukumbuka kwamba kwa Sakramenti hiyo ya Ekaristi Takatifu waliyoshiriki katika adhimisho hilo la Misa Takatifu, wametengeneza mahusiano ya kudumu na Yesu Kristu, ambaye ndiye waliyemla.
Mmisionari huyo wa Shirika la Watumishi wa Wagonjwa(Wakamiliani), aliwasihi watoto hao kujitahidi kujibidiisha siku zote, ili watamani na waendelee kupokea chakula hicho ambacho ni kitakatifu.
Aliongeza kwamba haipendezi kwa mtoto ambaye amepokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, na baada ya hapo, haonekani kanisani kushiriki katika Adhimisho la Misa Takatifu.
“Leo umepokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, baada ya hapo unasema sasa Kanisa ‘bye bye’. Ukifanya hivyo, na Yesu naye atakwambia ‘bye bye’. Utatoroka kanisani, utaliacha kanisa, utaenda kuhangaika, baadaye likikupata tatizo, utaanza kusema ‘Mungu wangu mbona umeniacha,” alisema Padri huyo.
Aliwasisitiza kutokumwacha Mungu ambaye tayari wameshatengeza mahusiano mazuri naye, kwani faida ya kuwa karibu na Mungu wataiona mbinguni.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi akiadhimisha Misa Takatifu ya Shukrani ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kwenye viwanja vya Seminari ya Mtakatifu Maria, Visiga-Kibaha jimboni humo. (Picha na Michael Ally)

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi akiadhimisha Misa Takatifu ya Shukrani ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kwenye viwanja vya Seminari ya Mtakatifu Maria, Visiga-Kibaha jimboni humo. (Picha na Michael Ally)