Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Pd. Gaston George Mkude

Amani na Salama!
Mwinjili Marko wakati anaandika sehemu ya Injili ya leo, himaya ya Kirumi ilikuwa imetoka katika vita na mabalaa mengi, mfano magonjwa ya milipuko na uvamizi wa wadudu katika mashamba yao.
  Si tu himaya ya Kirumi, bali hata Jumuiya ya Wakristo katika himaya ile walikuwa wametoka kupitia kipindi kigumu cha mateso na madhulumu ya Mfalme Nero, aliyewatesa na kuwaua Wakristo wale wa kwanza. Hivyo katika mazingira ya namna hii magumu na yenye mateso mengi waamini walikuwa wanajiuliza nini maana ya haya yote na kwa nini wanapitia hayo yote. Hata nasi leo dunia nzima tunajiuliza maswali mengi mintarafu majanga mbali mbali, kwa nini Mungu anaruhusu tujaribiwe, tupatwe na kupitia kipindi kigumu namna hii? Nini hasa maana na lengo lake?
Mwinjili Marko ni katika mazingira ya namna hii anaandika sehemu ya Injili hii ya leo yenye aina ya uandishi ya kiapokaliptiko. Apokaliptiko ni neno lenye asili ya Kigiriki litokanalo na maneno mawili ambayo ni apo likimaanisha kuweka mbali au tenganisha, pamoja na kaliptiko likimaanisha weka bayana.
Hivyo aina ya uandishi ya kiapoliptiko ni ile inayotumia lugha isiyo kuwa wazi sana, ni lugha ya mficho hivyo kupata ujumbe wake ni lazima kufunua au kufumbua mafumbo na lugha ile ya mficho. Tunaweza kutumia lugha ya vijana ya kileo ni kufungua code (decodification)!
Na ndio mwaliko wa Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo anapotuonya tusidanganyike tunapoona mambo hayo yakitokea katika ulimwengu na nyakati zetu. Hata katika nyakati zetu kuna mengi yanayotokea, na hata mara kadhaa kushawishika kusema mwisho wa dunia umekaribia. Hiyo pia ilikuwa ni hofu ya Wakristo wale wa mwanzo, hivyo mwinjili anaona hitaji la kuwaandikia ujumbe huu wa kiapokaliptiko.
Marko mwinjili anatumia lugha ya picha ya kiapokaliptiko kama vile jua na mwezi na ishara nyingine za angani. Kwa watu wa mashariki ya kati walikuwa wanaabudu ishara za angani kama jua na mwezi kama miungu yao, na hivyo hata kutolea sadaka pale wanapoona kuwa mambo yao yanakwenda kinyume na matarajio yao.
Musa anawaalika Wanawaisraeli kumwabudu Mungu wa kweli na sio nyota au jua au mwezi wa angani. (Kumbukumbu la Torati 4:19) Hata Nabii Isaya pia anaawalika kumwabudu Mungu wa kweli na si nyota wala jua wala mwezi. “Nyota na vilimia vyake angani hazitaangaza; jua linapochomoza litakuwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake” (Isaya 13:10)
Ujumbe huu haukuwa kwa ajili ya kuwatisha na kuwaogofya, kuwa jua na mwezi na nyota zitaacha kutoa mwanga wake wa asili, bali kuwatia matumaini kuwa nuru na mwanga wa kweli unatoka kwa Mungu mwenyewe na si katika vitu vya angani. Hivyo ni ujumbe wa furaha na matumaini. Mwanga na nuru ya kweli ni Yesu Kristo mwenyewe katika maisha ya kila mfuasi wake.
Na ndio mwinjili Marko anaandika sehemu hii ya Injili, ambapo Yesu Kristo anatumia pia lugha hii ya kiapokaliptiko kwa lengo la kuwafariji waamini wanaopitia kipindi kigumu cha mateso na madhulumu. Na kwetu leo ni neno la faraja na matumaini hata kama tunapitia katika kipindi chenye magumu na changamoto nyingi katika maisha.
Ni kawaida kujiuliza maswali nini maana ya magumu na mateso katika maisha yetu, na hata tunapojibidisha kusali na kuwa waaminifu katika imani yetu, bado tunakutwa na mahangaiko katika maisha ya siku kwa siku. Nini maana ya mateso, kwa nini mateso na magumu katika maisha ya ufuasi?
Tunaalikwa kunyanyua vichwa juu kwani wokovu wetu unakaribia, ulimwengu mpya wa ufalme wake Mungu. Mwanzo mpya ambapo mtawala mpya ni Mungu mwenyewe anayetaka kukaa na kuwaongoza watu wake. Ni mwanzo wa ufalme wa Upendo, Amani na Haki.
Dhiki, jua kutiwa giza, mwezi kukoma kutoa mwanga wake, nyota zikianguka na nguvu za mbinguni kutikisika, zote hizi ni ishara ya yule muovu na uovu ulimwenguni. Ni kwa ujio wa Yesu Kristo ulimwenguni basi yule muovu na uovu hauna nguvu tena, hauna nafasi tena kwani tunaalikwa kuunda ulimwengu mpya, ndio ufalme wa Mungu kati yetu, katika maisha yetu.
Ni ujumbe wa faraja kuwa Mungu mwenyewe atamtuma malaika wake, hapa malaika pia ni lugha ya kiapokaliptiko likimaanisha mjumbe wa Mungu ambaye ujio wake sio kuja kuhukumu ulimwengu, bali kuwaunganisha wana wake kutoka pande zote za dunia baada ya kutawanywa na yule mwovu.
Mwana wa mtu hataruhusu wapotee bali atawakusanya wote. Ni mjumbe wa Habari Njema ya wokovu kwa watu wote bila ubaguzi wa aina yeyote, mjumbe huyu ndio kila mmoja wetu anaposhiriki katika kueeneza Ufalme wa Mungu hapa duniani, kuwa wajumbe wa kweli za Injili kwa maneno na matendo yetu. SOMA ZAIDI...

VATICAN

Na Sr. Angela Rwezaura

Katika Ripoti mpya kutoka UNESCO, inashutumu kuwa mwaka 2022-2023 wafanyakazi 162 wa vyombo vya habari waliuawa,karibu nusu katika maeneo ya vita na kutokujali kungali juu sana.
Idadi ya waandishi wa habari wanawake ambao walikuwa waathiriwa pia iliongezeka,14.
Hii ndiyo sababu hatua ya haraka inaombwa kutoka kwa Mataifa. Kampeni ya”Kuna historia nyuma ya historia”iliandaliwa na mwongozo wa usaidizi wa kisaikolojia ukachapishwa.
“Mnamo 2022 na 2023, kila baada ya siku nne mwandishi wa habari aliuawa kwa kufanya kazi yao: kutafuta ukweli. Katika idadi kubwa ya kesi hakuna mtu anayewajibisha.” Hii iliripotiwa na Audrey Azoulay, mkurugenzi mkuu wa UNESCO, ambaye alichapisha ripoti yake mpya Novemba 2, 2024 wakati wa Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Kutokujali kwa Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari.
Asilimia 85 ya mauaji ya waandishi wa habari ulimwenguni kote hayaadhibiwi, takwimu ambayo inasisitiza uzito wa hali hiyo, licha ya maendeleo madogo tangu 2018, wakati kiwango cha kutokujali kwa mauaji yaliyorekodiwa tangu 2006 kilikuwa asilimia 89.
Asilimia 95 mwaka 2012
Pamoja na ripoti yake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)linatoa wito kwa nchi zote wanachama wake kufanya zaidi ili kuhakikisha kwamba uhalifu huu haukomi bila kuadhibiwa,  Azoulay alieleza zaidi - kushitaki na kuwatia hatiani wenye hatia ni nyenzo ya msingi ya kuzuia mashambulizi ya baadaye dhidi ya waandishi wa habari.”
 Ingawa UNESCO inaona kuboreka kwa mwelekeo huo, ikizingatiwa kwamba kiwango cha kutokujali kilikuwa 95% miaka kumi na miwili iliyopita, inatoa wito kwa Mataifa “kuongeza kwa kiasi kikubwa juhudi zao za kuzuia uhalifu mpya dhidi ya waandishi wa habari.” Katika miaka miwili iliyopita waathirika 162, ambapo 14 wanawake.
Katika kipindi cha miaka miwili 2022-2023, kipindi kilichoakisiwa na ripoti mpya, waandishi wa habari 162 waliuawa, karibu nusu yao katika nchi ambazo migogoro ya silaha ilikuwa ikiendelea, wakati katika kipindi cha miaka miwili iliyopita asilimia ilikuwa asilimia 38.
Katika nchi nyingine, waandishi wa habari wengi wameuawa kwa kujaribu kusema ukweli kuhusu uhalifu wa kupangwa, rushwa au kuripoti maandamano ya umma. UNESCO pia inaripoti ukweli mwingine wa kutisha: idadi ya waandishi wa habari wanawake waliouawa katika kipindi cha miaka miwili, 14 kwa jumla, ni ya juu zaidi tangu 2017.
Kampeni “Kuna historia nyuma ya historia”
Ili kukabiliana na hali ya kutokujali, shirika la Umoja wa Mataifa leo linazindua kampeni mpya ya kila mwaka ya kimataifa ya kuhamasisha umma kuhusu ukatili dhidi ya waandishi wa habari.
Ukiwa na mada “Kuna historia nyuma ya historia, mpango huo unalenga kuleta umakini kwa uhalifu dhidi ya vyombo vya habari, kupitia makala na ushuhuda zilizochapishwa ulimwenguni kote.
Zaidi ya hayo, tarehe 6 Novemba, UNESCO itaandaa mkutano wa kimataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari katika Migogoro na Dharura mjini Addis Ababa, kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika.
Wakati wa hafla hiyo, Daftari la Kimataifa la Mbinu za Kitaifa za Usalama kwa Waandishi wa Habari litawasilishwa, ambalo linakusanya sera za ulinzi wa wanahabari zinazotekelezwa katika nchi 56 na angalau mipango 12 ya kitaifa.
Mwongozo wa msaada wa kisaikolojia
UNESCO pia itachapisha mwongozo kwa wanasaikolojia wanaofanya kazi na waandishi wa habari katika hali za dharura, kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Vyombo vya Habari vya Wanawake (IWMF).
Mwongozo huo, unaolenga hasa wanawake, utawapa wanasaikolojia zana za kuleta utulivu wa michakato ya kihemko na kiakili ya waathiriwa wa matukio ya kiwewe, kuwasaidia kufanya maamuzi ya busara, ya msingi kwa maisha yao, na kupunguza tabia za msukumo ambazo zinaweza kuwaweka hatarini zaidi.
UNESCO, Umoja waonya
Likiwa na nchi wanachama 194, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linachangia amani na usalama kupitia ushirikiano wa kimataifa katika elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na habari.
Ikiwa na makao yake makuu mjini Paris, UNESCO ina ofisi katika nchi 54 na inaajiri zaidi ya watu 2,300.
 Inasimamia zaidi ya Maeneo elfu mbili ya Urithi wa Dunia, Hifadhi za Biosphere na Geoparks za Ulimwenguni, mitandao ya Miji Ubunifu, Jumuishi, ya Kujifunza na Endelevu, na zaidi ya shule elfu kumi na tatu zinazohusiana, viti vya vyuo vikuu, vituo vya mafunzo na utafiti.

KIGOMA

Na Mathayo Kijazi

Katika kuhakikisha familia, jamii, na hata Kanisa kwa ujumla linaendelea kuwa na watu wenye maadili ya kumpendeza Mungu, ni lazima familia zijengwe vyema, ili ziweze kudumu katika misingi iliyo bora.
Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kujenga jamii iliyo bora kupitia katika familia zao, zikiwemo semina za Kanisa, mikutano, makongamano, pamoja na mafundisho mbalimbali.
Katika jitihada hizo za kujenga familia, Utume wa Uimarishaji wa Familia Tanzania (UFATA), hivi karibuni ulifanya Mkutano wake Mkuu wa Kitaifa katika Jimbo Katoliki la Kigoma.
Vile vile, ndani ya Mkutano huo ilifanyika Semina iliyohusisha mada mbalimbali zilizolenga familia, mwenendo wake, pamoja na tafakari mbalimbali.
Akiwasilisha mada isemayo ‘Familia imara ni msingi wa utu wa mtu’, Mkuu wa Chuo cha Songea Catholic Institute of Technical Education, kilichopo Songea, mkoani Ruvuma, Padri Longino Rutangwelera Kamuhabwa wa Jimbo Katoliki la Bukoba, anasema kwamba kwa kuumbwa kwake na kwa hulka yake, utu wa mtu ni wa kuheshimiwa na umetakaswa.
Padri Kamuhabwa anasema kwamba Familia ni Taasisi ya Kimungu kati ya wanadamu, kwa ajli ya kuendeleza na kulinda heshima ya utu wa mtu, na kwamba kuheshimu familia na utu wa mtu, ni kumheshimu Mungu aliye chimbuko lake.
Anaongeza kwamba mwanadamu anatakiwa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama njia mojawapo ya kumheshimu na kumthamini Mungu, kwani ameumbwa kwa malengo ya kumjua, kumpenda, kumtumikia Mungu na kutafuta Ufalme wake.
Padri huyo anabainisha pia kuwa mwanadamu ni wajibu wake kutambua kwamba ameumbwa pamoja na wanadamu wengine, kwani huo ni mpango wa Mungu kuwa mwanadamu atimize malengo ya kuumbwa kwake akiwa kundini.
Anasema pia kwamba mwanadamu ni muhitaji, mhanga na dhaifu, hivyo, anahitaji kuhubiriwa, kulindwa, kutetewa, kukemewa pamoja na kuelekezwa.
Anabainisha pia kwamba katika kuwa kiumbe muhitaji, mwanadamu kwa hulka yake, Mungu alimuumba mtu akiwa na njaa na kiu ya kufikia ukamilifu, na kuongeza kuwa ni katika hali hiyo, mtu hutafuta, husali, hufanya kazi ili afikie kile cha kumfanya awe mkamilifu. Katika kutafuta huko, Padri huyo anasema kwamba mwanadamu pengine hupatia, na pengine hukosea.
Pia, Padri huyo anasema kwamba nyenzo za kumsaidia wanadamu kufikia kile anachokihitaji, ni pamoja na Sala, Neno la Mungu, Maisha ya sakramenti, pamoja na Maisha ya familia.
Vile vile, anasema kuwa kwa hulka yake, mwanadamu ameumbiwa kwanye jamii (familia), na kwa asili yake, ana mwelekeo wa kuishi au kushirikiana na wanadamu wengine.
“Mwanadamu anafaidika kwa kushirikiana na wanadamu wengine. Kukamilisha na kukamilishwa na wengine (complementarity principle). Kutegemeza na kutegemezwa na wengine (synergy principle). Mtu ni ufunuo na uwepo wa Mungu kati ya watu (transcendental being)…
“Kadiri ya Edith Stein (Mtakatifu Theresa wa Msalaba) mtu ni Epiphania - anafunua wema na upendo wa Kimungu kwa wengine. Kadri ya Mtakatifu Thomas Aquinas, kupitia ubinadamu wetu, Mungu yu pamoja nasi = Emmanuel. Kristu aliutwaa ubinadamu wetu ili sisi tukwezwe na kuushiriki Umungu wake. Kwa hiyo, mtu ni ufunuo wa uwepo wa Mungu kati yetu. Mtu ni zaidi ya yale unayoyaona,” anasema Padri huyo.
Sambamba na hayo, Padri Kamuhabwa anaongeza kwamba mwanadamu ni kiumbe hisia, kwani kwa hulka yake anaweza kufurahi au kukasirika; kupenda au kuchukia; kuwa na vionjo mbalimbali; kukubaliana pamoja na kutofautiana na wengine.
Anasema kwamba hiyo inaleta uhalali wa mtu kupenda na kupendwa, kujali na kujaliwa, kuheshimu mawazo na maoni ya mtu, kumpa mtu nafasi ya kuchagua anachokitaka, na kuacha asichokipenda.
Kwa nini utu wa mtu uheshimiwe na kulindwa?
Padri Kamuhabwa anabainisha kwamba ni vizuri kutumia sababu moja kati ya hizi, ili kujenga hoja ya kulinda heshima na utu wa mtu; Mtu ni sura na mfano wa Mungu (Mwa, 1:26); Mtu kajaliwa akili na utashi wa kumtafuta Mungu (Isaiah, 1:17-19); Mungu kapitia kwa mtu kajifunua kwa viumbe wote (In, 14:8-9); pamoja na; Mungu kamchagua mtu na kuweka agano naye (Mwa, 9:13; Kut. 19:5).
Sambamba na hayo, anasema kwamba familia ni taasisi ya kuenzi na kuheshimu utu wa mtu, kwani hiyo ni taasisi ya wanadamu aliyoianzisha Mungu ili kupitia kwenye taasisi hiyo, watu washirikishane upendo wa Kimungu, na watu washiriki kazi ya Mungu ya uumbaji.
Pia, anabainisha kwamba taasisi hiyo ni ya wanadamu kwa sababu inaundwa na wanadamu (nuclear and extended). Na pia ni ya Kimungu kwa sababu mwasisi, mtegemezaji na malengo yake ni Mungu.
Vile vile, anasema pia kwamba taasisi hiyo ni ya upendo, kwa sababu kiungo chake ni upendo, ni ya uumbaji kwa sababu inaendeleza umbaji.
Njia za kuenzi na kuimarisha familia:
Akitaja njia zinazoweza kutumika ili kuimarisha familia, Padri huyo anabainisha kwamba ni lazima kuwepo na sala, kuiombea na kusali pamoja; ijikite katika kusoma na kuishi Neno la Mungu; Maisha ya Sakramenti; ipate neema za Sakrameti; malezi endelevu; ianze na Mungu na ibaki na Mungu; Maadhimisho endelevu; kushika amri ya mapendo, kufanya kumbukizi za matukio muhimu ya kifamilia, pamoja na kuhuisha mahusiano.
Matishio dhidi ya familia:
Akitaja mambo yasiyofaa na yanayoonekana kuwa tishio katika familia, Padri Kamuhabwa anasema kwamba mambo hayo ni pamoja na familia kuanzishwa kiholela.
Anaongeza kuwa kadri ya mpango wa Mungu, familia huanza kupitia ndoa halali, tofauti na hilo, ni mwanzo potofu, matokeo yake ni matokeo na mwisho potovu.
Vile vile, anasema kwamba upotoshwaji wa sifa za wanafamilia ni moja ya tishio, kwani familia huundwa na baba, mama na watoto. Upotovu katika jinsia za wazazi ni tishio la familia.

SOMA ZAIDI....

DAR ES SALAAM

Na Pd. Mujuni Audiphace

(Heri kwenda nyumbani mwa matanga kuliko kwenda nyumbani mwa karamu, maana huko ndiko mwisho wa binadamu wote, na walio hai wataweka moyoni,” Mhubiri 7:2)
Ndugu zangu Tumsifu Yesu Kristo.
Mwezi wa nane mwaka huu (2024) familia yetu tulijengea na kuweka msalaba mpya kwenye kaburi la Baba yetu aliyefariki miaka 37 iliyopita huko Kamachumu Kagera.
Siku moja kabla ya Misa ya kilele cha tukio hili nilifika nyumbani kuona kinachoendelea, nikakuta fundi yupo anakamilisha ujenzi akiwa na mdogo wetu wa mwisho wakiwa wawili tu pale kwenye eneo la makaburi.
Huyu bwana mdogo akawa anajisifia kuwa yeye tu ndiye haogopi makaburi, akaniambia kuwa wengine wote wamekimbia hii kazi ya msaidia fundi sababu inafanyika makaburini na ni ya kujenga kaburi.
Nilimuuliza kuwa: UNAFIKIRI HASA WANAOGOPA NINI KUHUSU MAKABURI?
Akanijibu kuwa: HAWAOGOPI MAKABURI, BALI WANAOGOPA KINACHOSABABISHA MAKABURI KUWEPO, YAANI KIFO. Hivyo wanafikiri kuyasogelea makaburi ni sawa na kukisogelea KIFO kwa makusudi.
NA HUU NDIO MTAZAMO WA BAADHI YETU TULIO WENGI
Wapendwa, makaburi yamekuwapo tangu mwanzo wa uwepo wa mwanadamu. Makuburi yameandaliwa na kutunzwa vyema na binadamu baada ya kuwa wamezikwa humo miili ya wapendwa wao.
Tunasoma Katika kitabu cha Mwanzo 23: 19-20, kuwa Abraham alinunua pango katika shamba la Makpela, na humo yakawa maziko ya watu ( Sarah, Abraham, Isaka, Yakobo, Lea, Raheli, nk). Eneo hili la makaburi liliendelea kutunzwa vizuri sana na watu wa wakati.
Kumekuwepo na Mila za kuyatumia makaburi kwa kufanya mambo ya hovyo na pia kuyahusishanisha na ushirikina kwa baadhi ya makabila ya kiAfrika. Hivyo Kila anayejishughulisha na makaburi anaonekana kuwa ni mtu wa Hovyo na mshirikina.
Kitabu Cha Muhubiri 7:2 kinasema kuwa “ Heri kwenda nyumbani mwa matanga kuliko kwenda nyumbani mwa karamu, maana huko ndiko mwisho wa binadamu wote na walio hai wataweka moyoni.”
Tunahimizwa kutembelea makaburi sababu ni swala la kusali.
Biblia inaendelea kutugundisha kuwa waliokufa sio adui zetu na wala sio mikosi kwetu tukiendelea kuwa karibu nao hata kwa kubeba masalia yao pale inapobidi, Yoshua 24:32 “mifupa ya Yosefu anazikwa Shekhem baadae ya waIsrael kusafiri nayo kutoka Misri. Eneo la Maziko linakuwa urithi wa Wana wa Yosef.”
Makaburi sio UCHURO ndugu zangu. Tunzeni maeneo yenu ya makaburi.
Kadiri ya maelekezo ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Nabii Elia, kutokuzikwa kaburini ni ishara ya kufa kifo kibaya (ukiwa mdhambi), Wafalme 9:33-44, “mdhambi mmoja anayeotwa Yezebel anakufa na mwili wake unaliwa na mbwa mitaani sababu ya wingi wa dhambi zake.”
Hivyo, kutokuzikwa baada ya kufa ni ishara ya laana, lakini waliozikwa vizuri ni ishara ya baraka.
Kuogopa makaburi ni sawa na kuogopa “kisichokuwepo.”
Kwa Kihaya uwa kuna methali inasema “kyakutinisa kita’kurwe”, jibu lake uwa ni “Mwilima.”
Tafsiri: “Kuna kitu kinakutisha lakini hakina nguvu ya kukula(kukuua),” na jibu lake ni “Giza.”
Kuogopa makaburi ni sawa na kuwa na “wasiwasi wa Bure” katika maisha, ni tatizo la AFYA YA AKILI. Tibu tatizo hili kwa kutunza vyema kumbukumbu za wapendwa wetu.
Wapendwa, shetani hakai makaburini, tukisoma Injili ya Mt. Marko 5:2-3, “Yesu baada ya kumtoa mapepo mtu aliyeishi makaburini akiwazuia watu wasiende makaburini, wale pepo walikimbilia baharini (sio makaburini).”
Tujifunze kwa Bwana wetu Yesu Kristo aliyekwenda makaburini kumfufua Lazaro (pamoja na kwamba dada yake Lazaro alimkataza Yesu kwenda makaburini, lakini Yesu alienda tu na Ufufuo ukafanyika).
Wapendwa tusisikilize kelele za wanaotuzuia/ kutucheka tunapokwenda makaburini kuyasafisha na kuwaombea waliolala huko, maana wote waliolala katika Kristo, watafufuliwa naye.
HITIMISHO
“Hata siku ya kwanza ya Juma, alfajiri na mapema, walikwenda kaburini wakiyachukua manukato waliyokuwa wameyatoa tayari,...” Luka 24: 1.
Wanawake watakatifu walienda”wakashuhudia UFUFUKO.
Makaburini.”  walimuona yesu mfufuka kwenye bustani za makaburi, hawakumuona shetani.
Tuwaombee waliolala makaburini waone uso wa Mungu.
Bwana awe nanyi nyote.
Pd. Mujuni Audiphace, Padri wa Jimbo Katoliki la
Bunda.

Na Arone Mpanduka

Alizaliwa Antoine Nedule Monswet mnamo Desemba 25, 1940, huko Leopoldville (sasa Kinshasa), jina la kisanii la Papa Noel kulikuwa na maelezo kuwa jina Noel lilikuja kutokana na  kuzaliwa kwake kwa Siku ya Krismasi. Papa Noel mwenyewe alifafanua kuwa kinyume na imani ya wengi, jina la Papa Noel (aliyezaliwa Antoine Nedule Monswet) halina uhusiano wowote na siku ya Krismasi, lakini jina hilo ni la kisanii kutoka kwa mshauri wake Leon Bukasa.Papa Noel Alianza kucheza gitaa ambalo mama yake alimpa, na mnamo 1957 aliombwa kufanya kazi na Léon Bukasa kwenye studio yake ya rekodi.
Papa Noel alisema kuwa ni gwiji Leon Bukasa ambaye alimpa jina la kisanii la “Papa Noel’, ambalo liliandikwa kinyume cha jina lake la Leon.
Mara baada ya hapo, aliombwa ajiunge na kikundi kipya cha Rock-A-Mambo,katika miaka iliyofuata, alikuwa mwanamuziki katika bendi kadhaa zilizokuwa maarufu wakati huo , Orchester Les Bantous de la Capitale kutoka Brazzaville, African Jazz, na Orchester Bamboula, ambapo alikuwa kiongozi wa bendi.
Kuanzia 1978 na kuendelea, alikuwa mpiga gitaa katika T.P.O.K iliyokuwa chini ya gwiji Franco ambapo alidumu na kundi hilo kwa miaka kumi na moja hadi kifo cha Franco mnamo 1989. Mwaka 1984 Papa Noel alitengeneza albamu yake binafsi inayoitwa “Bon Samaritain”, ambayo haikumfurahisha Franco ambaye hakupenda washiriki wa bendi yake kuwa na albamu zao binafsi .
Mnamo 1991, baada ya kifo cha Franco, TPOK Jazz ilizuru Ulaya, mwishoni mwa ziara hiyo, baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo waliamua kuhamishia makazi yao jijini Brussels nchini Ubelgiji na kuunda bendi ya Bana OK, Papa Noel alikuwa miongoni mwao. Alishiriki katika albamu ya Rondot ya Bakitani , ambayo ilitolewa kwa jina la Bana OK.
Papa Noel anaonekana kama mpiga gitaa anayeheshimika, katika upigaji wa magita yote yaani solo, rhythm na mi-solo ambaye alijizolea sifa kubwa ulimwenguni kote. Licha ya kutoa albamu yake binafsi mwaka 1984, Papa Noel amefanikiwa kushiriki katika albamu ya Sam Mangwana  Galo Negro (1998) uliovuta hisia zaidi kwake.
Mnamo 2000, albamu ya mkusanyiko << Bel Ami » ilitoka, ikifuatiwa na albamu ya kwanza ya Kékélé mnamo 2001.
Miradi mipya ilianzishwa, kama vile vipindi vya kurekodi na wanamuziki wa Cuba Adan Pedroso na Papa Oviedo, kujaribu kuchunguza mizizi ya pamoja ya muziki wa afro-cuba na rumba ya Kongo. Ugonjwa wa Papa Noël (Nedule ana kisukari) ulimzuia kwa muda kushiriki katika tamasha zaidi na ubia mpya. Hata ilimbidi kukosa albamu ya Kékélé ya 2003. Mnamo 2004, hata hivyo, alizunguka na kikundi kilichoitwa Bana Congo, na waimbaji Nana na Baniel (wote waliwahi kuwa na OK Jazz) na bendi ya Cuba nzima.
Maisha ya Papa Noel yanakaribia historia nzima ya muziki maarufu wa Kongo alianza kuonyesha uwezo wake katika muziki akiwa na umri wa miaka kumi na saba , aliingia studio ya Léopoldville’s (Kinshasa) ili kumsaidia mwimbaji- gitaa mwanzilishi Léon Bukasa.
Rekodi yao ya 1957 kuhusu mwanamke anayeitwa “Clara Badimwene” ilikuwa ya kwanza kwa Noel na mwaka uliofuata alihamia studio ya Esengo na kucheza na bendi iitwayo Rock’a Mambo iliyoongozwa na wanamuziki kutoka Kongo-Brazzaville, mkali Jean Serge Essous na mpiga sax Nino Malapet.
Mwaka wa uhuru wa kisiasa wa Kongo hizo mbili, 1960, Noel huko Gabon alishirikiana na Mbrazzaville mwingine, Guy-Léon Fylla, na bendi yake Makina Loka. Mwishoni mwa mwaka huo huo Noel alihamia katika bendi ya Bantous de la Capitale huko Brazzaville ambapo sifa yake ilipata mng’ao wa kwanza. Akiwa na bendi ya Bantous, Papa Noel alishiriki kikamilifu kwenye kundi hilo katika nyimbo kama vile “Basili Koyokana” (hawaelewi tena) na “Mobali Liboso” ( mwanaume kwanza).

DAR ES SALAAM

Bondia wa Masumbwi nchini, Hassan Mwakinyo amesema kuwa ujio wa pambano lake la ‘Usiku wa Utetezi wa Mkanda” ni sehemu ya kudhihirisha utemi wake kwenye mchezo huo.
Mwakinyo anautetea mkanda wake wa WBO Afrika aliouweka kama rehani ili kurudisha hadhi yake kwenye viwango vya ubora vya mchezo huo.
Pambano hilo litakalo fanyika Tarehe 16 Novemba 2024 katika ukumbi wa Werehouse Masaki Jijini Dar es Salaam, na litakuwa pambano ambalo litatoa taswira ya ubora wa bondia huyo kutoka hivi karibuni kuingia katika mvutano mkubwa na baadhi ya mabondia wenzake.
Hassan Mwakinyo amewaomba wadau na wapenzi wa mchezo wa ngumi kujitokeza kwa wingi siku hiyo kuona ukubwa wake kwenye masuala ya ngumi.
“Maisha yangu siku zote mimi ni mapigano kutokana na dunia ninayoishi, hivyo hata mpinzani wangu atambua hilo kuwa sitamuacha salama kutokana  na maandalizi niliyoyafanya”, alisema Mwakinyo.

DAR ES SALAAM

Klabu ya soka ya Tabora United imesema kwamba timu yoyote inayotaka huduma ya mchezaji wao Offen Chikola, inapaswa kutoa kitita cha shilingi bilioni moja ili imsajili.
Chikola kwa sasa anaimbwa na wapenzi wa soka nchini kwa mabao yake mawili aliyofunga hivi karibuni kwenya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga katika uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam.
Akizungumza na gazeti Tumaini Letu kwenye mahojiano maalum hivi karibuni, Afisa Habari wa Tabora United ambaye pia anakaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu, Christina Mwagala, alisema Chikola ana thamani kubwa kuliko watu wanavyodhani, na kwamba hiyo haitokani na kuifunga Yanga, isipokuwa thamani yake ni ya muda mrefu.
Alisema kwamba kwa kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba wa muda mrefu na Tabora United, timu inayomtaka inabidi ijipange vilivyo kuvunja kibubu ili kumsajili.
“Sisi kila mchezaji wetu ana thamani kubwa.Huyu Chikola ni Mtanzania mwenzetu kutoka Morogoro tu pale. Wapo wale wa kimataifa, nao ukitaka kuwasajili bei yao imechangamka.Na thamani yao inaendana na wanachokifanya uwanjani.Sote tunaona Tabora United jinsi inavyocheza,”alisema Christina.
Alisema kuwa wachezaji wote wa Tabora wana ubora mkubwa, na kwamba hicho ndicho wanachojivunia kwa sasa huku wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri katika msimu huu.
“Sisi malengo yetu ni kuwa mabingwa, na si vinginevyo.Tunaziheshimu sana timu za Simba na Yanga, lakini safari hii tunataka zitupishe kidogo ili na sisi tutambe na taji la ubingwa,”alisema.
Chikola ambaye ni kiungo mshambuliaji wa Tabora United, hadi sasa amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu, huku akionyesha nia ya kutaka kuendelea kufunga mabao mengine.
Mabao hayo yote matatu amefunga kwa kutumia mguu wake wa kushoto, sawa na Nassoro Saadun wa Azam FC, na Joshua Ibrahim wa Ken Gold.

NEW DELHI, India
India imeliarifu Baraza la Kimataifa la Kriketi kwamba haitasafiri kwenda kwenye Kombe la Mabingwa, kulingana na wenyeji Pakistan.
Mvutano wa kisiasa unaoendelea, unamaanisha kuwa nchi hizo mbili hazijacheza nje ya mashindano makubwa ya wanaume tangu mwaka 2013, wakati India haijacheza nchini Pakistan kwa miaka 16.
Pakistan inatazamiwa kuandaa hafla ya kimataifa kwa mara ya kwanza tangu 1996 mwezi Februari, na Machi mwaka ujao, timu nane, zaidi ya 50 ya Mabingwa.
Lakini, Bodi ya Kriketi ya Pakistani (PCB) ilisema Bodi ya Udhibiti wa Kriketi nchini India imeiambia ICC timu ya India haitavuka mpaka.
“TAKUKURU imepokea barua pepe kutoka kwa ICC, ikisema kwamba BCCI imewafahamisha kwamba timu yao haitasafiri hadi Pakistan kwa ajili ya Kombe la Mabingwa wa ICC 2025”, alisema msemaji wa PCB.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza baada ya siku mia moja, tarehe 19 Februari. Ratiba bado inapaswa kuthibitishwa na ICC.
ICC haijajibu moja kwa moja taarifa ya PCB, lakini iko kwenye majadiliano na Pakistan na mataifa mengine saba yanayoshindana juu ya ratiba. BCCI imeombwa majibu.

LONDON, Uingereza
Mwamuzi wa Premier League, David Coote (kushoto) amesimamishwa baada ya video inayodaiwa kumuonyesha akitoa kauli za dharau kuhusu Liverpool na meneja wa zamani wa klabu hiyo Jurgen Klopp, kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Bodi ya Waamuzi PGMOL inasema kusimamishwa kutaanza kutumika mara moja na inasubiri uchunguzi kamili.
Video hiyo, iliyosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii, haijathibitishwa na haijulikani ni lini ilirekodiwa au uhalisi wake.
Coote, 42, alichezesha ushindi wa 2-0 wa Liverpool dhidi ya Aston Villa Jumamosi na ni mmoja wa maafisa wa Premier League walio na uzoefu mkubwa, na amekuwa waamuzi katika ligi kuu tangu 2018.
Video inayoshirikiwa inaonekana kurejelea mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza ambayo Coote alisimamia mechi kati ya Liverpool na Burnley mnamo Julai 2020, ambayo iliisha 1-1.
Klopp alimkosoa Coote baada ya mechi, akisema mwamuzi alishindwa kutoa faulo kwa changamoto zilizowakabili wachezaji wa Liverpool.

Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Salamu Maria umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa.

Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.

Ndimi mtumishi wa Bwana, Nitendewe ulivyonena.

Salamu Maria umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa.

Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.

Neno wa Mungu akatwaa mwili, Akakaa kwetu.

Salamu Maria umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa.

Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu.

Amina.
Utuombee mzazi Mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe:
Tunakuomba Ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika, kwamba Kristo mwanao amejifanya mtu;

kwa mateso na msalaba wake, utufikishe kwenye Utukufu wa ufufuko.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Atukuzwe baba na mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina x3

Raha ya Milele, uwape Ee Bwana na Mwanga wa Milele uwaangazie, Wapumzike kwa amani. Amina x3