Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Uongozi wa klabu ya soka ya KMC umejitoa katika mbio za ubingwa msimu huu kutokana na kutokuwa na misuli ya kutosha katika kushindana na vilabu vingine.
Mtendaji wa klabu hiyo Daniel Mwakasungura alisema kuwa bado wanaendelea kujitafuta, huku akiweka wazi kuwa bado hawapo katika ramani za waokupambana na wenye uwezo wa kifedha .
Mwakasungura alifunguka kuwa wameliona hilo kwa mwaka huu, na kuamua kuijenga timu yao ili ikishakuwa sawa, waanze kupambana kwa misimu mingine ya ligi huko baadaye lakini kwa sasa bado hawana wachezaji wenye uwezo wa kiushindani.
Alisema kuwa kwenye upande wa soko la usajili, wenzao wamewaacha mbali sana kuliko wao, kwani gharama ambazo wanatumia vilabu vingine katika kusajili wachezaji, ni kubwa kuliko za wao, na hivyo kusababisha hata kupokonywa wachezaji wengi wzuri.
“Unajua kwenye soko la ushindani unatakiwa ujitutumue kweli sasa sisi tunamuona mchezaji, na tunatamani kumsajili lakini unakuta fedha tunayotoa ni ndogo kuliko ambayo wenzetu wakiamua kuitoa kwa mchezaji huyo huyo”, alisema Mwakasungura.
Alisema pia kuwa kwa sasa wao wanajenga timu ili iwe tishio kwa miaka inayokuja, kwani tayari wameshaanza kujipata katika namna ya uchezaji, hivyo vimebaki vitu vichache ambavyo wao kwa kusaidiana na bechi la ufundi, wanavitengeneza.
KMC msimu uliopita ilibaki kidogo kushuka kwenda kucheza Ligi ya Championship, lakini walijipapatua na kuendelea kubaki katika Ligi Kuu. Kwa msimu, na sasa wanachokifanya ni kujihakikishia nafasi ya kutoshuka Daraja ili malengo yao ambayo waliyaweka, yaweze kutimia.

DAR ES SALAAM

Na Deus Helandogo

Uongozi wa klabu ya soka ya Simba kupitia kwa Meneja wake Ahmed Ally, umefunguka sakata la kuachana ghafla na mshambuliaji wao Fredy Michael, ambaye amedumu ndani ya klabu hiyo kwa miezi michache tu.
Ahmed Ally aliweka wazi kwamba sababu za kuachana na nyota huyo ni kutokana na kuwa alishindwa kufundishika, mara baada ya kocha wao Fadlu Davis kumfanyia mazoezi mengi na kuzungumza naye, lakini bado kiwango chake kilikuwa hakiridhishi.
Ahmed alisema kuwa moja kati ya wachezaji ambao wao kama uongozi walikuwa wanafikiri a kuwa atakuwa kiongozi kwa wachezaji wengine, ni yeye, lakini kutokuwa timamu kimwili kumesababisha kocha kuomba kutafutiwa mchezaji mwingine.
Alisema pia kuwa wakati wa maandalzi ya msimu mpya wa ligi walipoweka kambi kule Misri, kocha Fadlu alikuwa akimfuatilia na kuzungumza naye mara kwa mara, lakini bado hakuwa katika utimamu wa mwili.
“Kocha alizungumza naye mara kwa mara tangu alipowasili kambini lakini hakuweza kufanya zaidi atu alikuwa akishuka kila siku na ndiyo maana kocha alitaka kutafutiwa mchezaji mwingine haraka zaidi, ndipo tukamtafuta mwamba Christian Lionel Ateba”, alisema Ahmed.
Alisema pia kwamba suala la kuachana na Fredy, ni kutokana na matakwa ya kocha na ni kutokana na kutopedezwa na kiwango chake alichoonyesha kwenye mazoezi laini. Kwa sasa wamemalizana naye na hivyo wanaanza upya.
Aidha, alizungumzia juu ya kulidhishwa na kikosi chao, huku akiweka wazi kuwa msimu huu, pamoja na kuwa wanajenga timu, lakini wana mipango ya kuchua ubingwa msimu huu na kurudisha ufalme wao ambao waliupoteza kwa watani zao Yanga, lakini watahakikisha wanafanya vyema.
Mpaka sasa, klabu ya Simba imefanikiwa kucheza michezo miwili ya ligi dhidi ya Tabora United na Fountaine Gate na kufanikiwa kubeba alama zote 6 na kujikusanyia mabao 7 wakiwa juu katika msimmo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Papa  Fransisko katika  tafakari  yake, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2024 anasema, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumtafakari Bikira Maria baada ya  kupashwa  habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu aliondoka, akaenda hata nchi ya mlimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti, binamu yake! Rej Lk, 1: 39-56. Shuhuda wa furaha, matumaini na uzima wa milele.
Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili (1939-1958: wa 260) katika Waraka wake wa kitume.
 “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani,” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki.
Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya, huku akihusishwa na Adam mpya, Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo.
Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa, na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika  mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.”
Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio,” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae.”
Hii ni Sherehe inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila Mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti.
Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni, hiki ni kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu kama alivyokiri Mtakatifu Yohane Paulo II (1978-2005 wa 264) mnamo mwaka 1997.
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2024 anasema, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumtafakari Bikira Maria baada ya kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, aliondoka, akaenda hata nchi ya mlimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti, binamu yake! Rej Lk, 1: 39-56.
Taarifa kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, ili kumsukuma kuondoka kwa haraka, kwenda kutangaza na kushuhudia ile furaha iliyomwilishwa katika huduma.
Tangu wakati huo, Bikira Maria alianzisha mchakato wa kumfuasa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu, kama mfuasi halisi wa Ufalme wa Mungu, akadiriki hata kusimama chini ya Msalaba, na hatima ya hija hii ya maisha ya kiroho ni Kupalizwa kwake mbinguni, ambako huko juu mbinguni wanaendelea kufurahia pamoja na Kristo Yesu, maisha ya uzima wa milele.
Bikira Maria ni mfano wa mwamini anayesoma alama za nyakati, akawa tayari kufuata nyayo za Mwanaye mpendwa, akakutana na wafuasi wa Kristo Yesu, na baadaye safari yake ya kutangulia kwenda mbinguni, kwenye utukufu wa Baba wa milele.
Huu ni mwaliko kwa waamini kutambua kwamba maisha yao huku bondeni kwenye machozi, ni safari endelevu itakayofikia hatima yake kwa kukutana na Kristo Yesu, huko mbinguni.
Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba wanatunza moyoni mwao, kwamba Mwenyezi Mungu amewaumba, ili hatimaye, waweze kuwa na furaha ya uzima wa milele na kwamba, ndoto yake ni kuwachukua waja wake wote, ili wakaishi naye katika maisha ya uzima wa milele.
Safari ya maisha ya binadamu ni sehemu ya mpango wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Hii ni hija inayowaongoza siku hadi siku, ili kukutana na Mwenyezi Mungu, chemchemi ya furaha isiyokuwa na mwisho; furaha ambayo amewaandalia waja wake.
Baba Mtakatifu Fransisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanarutubisha safari hii kwa matumaini na hasa pale, wanapokumbana na magumu pamoja na changamoto za maisha.
Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho, iwe ni fursa makini kwa Waamini kujiuliza swali la msingi, ikiwa kama katika safari ya maisha yao hapa duniani, wanaendelea kuirutubisha kwa matumaini, kwa kutambua kwamba, mwisho wa safari yao, yuko Kristo Yesu anayewangoja.
Au katika safari hii ya maisha, tayari wamekwisha “kubweteka?” Je, Waamini wanakumbuka kwamba wameumbwa kwa ajili ya kufurahia maisha ya uzima wa milele; kwa kuwapenda na kuwathamini ndugu na jirani au Mwamini amejikuta akiwa amezama zaidi katika uchoyo na ubinafsi, na hatimaye kuzama katika malimwengu?
 Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Fransisko amewaalika Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwangalia, na hatimaye, kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwaombea, ili kamwe wasisahau kwamba hatima ya maisha yao ni furaha na matumaini ya uzima wa milele. “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika Watakatifu jinsi ulivyo.” Efe 1:18.
Katika hatua nyingine, Kardinali Pierbattista Pizzaballa, O.F.M. Patriaki wa Yerusalemu na Mlinzi Mkuu wa Nchi Takatifu na Mlima wa Sion, katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni Mwili na Roho, yaliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mateso lililoko kwenye Mlima wa Mizeituni ulioko Mashariki mwa mji wa Yerusalemu.
Papa Fransis alitumia fursa hii kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini zaidi huko Mashariki ya Kati.
Katika mahubiri yake amewaalika Waamini kumtafakari Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho kama zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, changamoto kwa Walimwengu ni kuondokana na : vita, ghasia, machafuko; Utumwa mamboleo na biashara ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, pamoja na ukoloni mamboleo.
Bikira Maria, Mama wa Yesu akiwa amekwisha kutukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura na mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao. Kadhalika anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja kwa taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja. LG 68.
Amezungumzia kuhusu madhara ya vita yanayowatumbukiza watu katika umaskini wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, kwa kusigina, uhuru, utu, heshima na haki zao msingi. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni, awaombee Walimwengu haki, amani na upatanisho.

MWANZA

Na Paul Mabuga

Maureen Mwanawasa, Mke wa Rais wa zamani wa Zambia, Levy Mwanawasa [2002 – 2008], amefariki  Agost 13, 2024, jijini Lusaka nchini humo baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kama ulipata nafasi ya kumfahamu, bila shaka utajiuliza kwa nini akina mama huku kwetu wanashindwa kuwashawishi wanaume wanne wao kwenda kanisani hasa baada ya kuonekana mahudhurio yao ni hafifu na yenye kulalamikiwa.
Fikiria mama wa ‘kibongo’ anaweza kumshawishi mume wake, kulipia hadi shilingi elfu 30 ama hata hamsini, kwa ajili ya kusuka nywele ili apendeze, ama anunulie gauni la mtoko la hadi shilingi 60,000/- na kumsaidia marejesho ya mikopo ya kausha damu, lakini anashindwa kumbembeleza mwanaume ahudhurie kanisani, jambo ambalo hata hivyo haligharimu fedha yoyote.
Safari yangu ya kukutana na Maureen Mwanawasa ilianzia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Keneth Kaunda jijini Lusaka, ambapo wakati natoka nje  nikiwa miongoni mwa wageni waliowasili, nilipokelewa na mzee mmoja raia wa Tanzania. Nilishangaa baada ya kuwa licha ya mzee huyo kunizidi umri, lakini alipokea begi langu   ambalo lilikuwa mzigo wangu pekee, na kunielekeza kwenye gari ndogo tukielekea katikati ya jiji la Lusaka. Juhudi zangu za kukataa mzee huyu kunibebea mzigo ili kulinda mila za Kiafrika, zilizogonga mwamba.
Hapo safari ikawa moja kwa moja hadi katika hoteli ya Pamodzi [yaani pamoja] ambayo baadaye niliambiwa kuna Marais na Wakuu wa Nchi 14 wanalala hapo, na ndiyo maana ulinzi ulikuwa mkali. Nikajisemea kimya kimya, itakuwaje siye kwa mazoea ya kabila letu kwamba ukinywa hata kabia kamoja, unaanza kuimba. Lakini kwa bahati, mratibu wa mambo akaniambia, “Bwana mdogo twende huku.’’ Nikapelekwa hoteli nyungine jirani ambayo nayo ilikuwa kubwa. Hii ilikuwa ni Agosti 15, 2007.
Jioni hiyo kukawa na zoezi ambapo watu wote waliokuwa wanatarajia kuingia katika vikao vya Marais na wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika [SADC], walitakiwa kufika katika kituo maalum, ambapo baada ya kuhakikiwa, walipigwa picha na kupewa Kitambulisho maalum. Hakuna aliyekuwa akiachwa kwenye hatua hii, isipokuwa mabwana wakubwa.
Wakati nimefikia hatua ya kupigwa picha, akaingia mama mmoja aliyevaa kitamaduni, na baadaye nikabaini kuwa ni mmoja wa wafanyakazi katika Ikulu wa King Mswati lll wa Eswatini. Kwa heshima yake na kwamba anatoka katika familia ya kifalme, jambo ambalo inaelekea Wazambia wanalijali, nikaambiwa nimpishe ahudumiwe kwanza yeye. Nikafanya hivyo, na mimi baadaye nikapata kitambulisho changu.
Asubuhi wakati nakwenda kwenye mkutano, ile naingia geti la kwanza, nikakutana na askari ambaye baada ya kutambua kuwa ninatoka Tanzania, akanionesha kitambulisho cha mmoja wa Mawaziri wa  huku kwetu ambacho kumeokotwa. Akaniuliza, unamjua huyu na mimi nikamwambia, naam namjua ni mmoja wa mawaziri wetu, na akanionya, mtafute umpe hiki kitambulisho, vinginevyo hataingia humo ndani. Niliifanya kazi hiyo na baadaye kumkabidhi kitambulisho chake.
Wakati wa mapumziko, nilifanikuwa kuwa karibu na aliyekuwa Rais wa Namibia, Hifikipunye Pohamba, jamaa mrefu hivi, baada ya kumsalimia kwa Kiingereza na kuonesha nia ya kufanya naye mahojiano, aliinama na kusoma kutambulisho changu ambacho kilikuwa kikionesha pia ninatoka nchi gani. Baada ya kugundua ninakotoka akabadili lugha na kuniambia kwa Kiswahili, “habari za Dar es salaam, vipi Buguruni, mambo poa” Wakati naendelea kutafakari hatua ya kufuata, akaanza kuondoka na kuniaga. “Haya bwana, kazi njema!”
Jioni wakati wa mpango wa kazi, nikaitwa na mkuu wangu, nakwambiwa kuwa siku inayofuata, nitaambatana na wake wa Marais na Wakuu wa Nchi ambao watakuwa katika ziara wakiongozwa na mwenyeji wao, Mke wa Rais wa Zambia Maureen Mwanawasa. Siku hiyo ilipofika, tulianza ziara tukiwa katika mabasi mawili, moja likiwa la hao akina Mama Waheshimiwa na jingine la watu waliokuwa  kwenye kazi mbali mbali, tukiwemo wanahabari wachache.
Tulipomaliza ziara iliyochukua hadi muda wa mchana, tulirudi katika hoteli ya Pamodzi, ambapo kulikuwa na maonesho ya bidhaa mbali mbali  zinazozalishwa na wanawake nchini humo, ikiwa ni pamoija na vito. Mama Maureen hakusita kuwaambia kwa lugha yao akina mama wale, wafanye biashara, kwani hao waliowatembelea ni wake wa Marais. Nilitafsisriwa hicho alichokisema na mwandishi wa gazeti moja la nchini humo.
Baada ya ziara hiyo, akina mama hao wakawa na kikao chao, Mama Maureen Mwanawasa ambaye alikuwa Mwenyekiti wao, alisimama na kuwaambia juu ya ajenda muhimu, iliyohusu azimio lao la kutaka  wanawake kupewa nafasi ya madaraka katika kile kinachojulikana kama hamsini kwa hamsini, yaani kama mkakati wa kijinsia wanawake wapewe nafasi katika ngazi mbali mbali katika kiwango cha uwiano sawa na wanaume.
Cha kufurahisha ni kwamba aliwaambia kesho yake watawasilisha hoja, na kwamba kila mmoja aitangulize hoja hiyo kwa mwenzi wake. Na inawezekana kila mmoja aliwasilisha hoja hiyo, maana ilipowasilishwa  na Mama Maureen Mwanawasa siku iliyofuata mbele ya  Wakuu wa Nchi, hakukuwa na mjadala bali Viongozi hao  walipiga makofi kama ishara ya kuiunga mkono, na ikapita, na kuanzia hapo imekuwa ajenda ya kudumu katika Nchi hizo.
Ukiacha hilo, lakini Maureen Mwanawasa amekuwa na ushawishi mkubwa katika mambo mbali mbali enzi ya uhai wake, ikiwa ni pamoja na harakati ya kupambana na umaskini, na pia akiongoza Wake wa Marais na Wakuu wa Nchi katika Jumuiya ya SADC katika kupambana na madhira ya UKIMWI na Virus vya UKIMWI.
Ni Mwanamke ambaye alitumia nguvu ya ushawishi wake katika kupeleka ajenda. Anasifika pia katika kuendesha kampeni za kisiasa kupigania ushindi wa mume wake katika chaguzi.
Maureen alizaliwa April 28. Mwaka 1963 katika eneo la Kabwe nchini Zambia. Aliolewa na Mwanasheria Levy Mwanawasa Mei 07, 1987. Mumewe alifariki mwaka 2008 akiwa madarakani, na Mwenyezi Mungu aliwajalia  watoto wanne, ambapo watatu ni wa kike na mmoja ni wa kiume.
Kwa njia ya ushawishi wa akina mama kwenye hamsini kwa hamsini, dada zetu, shemeji zetu, shangazi na mama zetu wanashindwaje kuwashawishi wanaume kushiriki kwenda kanisani? Kwa nini nguvu hii ambayo haihitaji rasilimali fedha, haitumiki kupunguza changamoto hii, ambayo inaelekea kuwa sugu?
Kuna wakati ukihudhuria kanisani, unakuta uwiano ni wanawake kuwa theluthi mbili na wanaume theluthi moja. Unakaa kwenye jumuia unakuta ni wanawake na watoto, labda na mwanume mmoja. Kama akina mama wanaweza kuzengea fedha ya kucha, nywele na marejesho wanashindwaje kuwashawishi wanaume kwende kanisani?

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo ll, Buyuni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Padri Bartazari Minde akibariki vipaji wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Bikira Maria, iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akikata utepe Hospitali ya Saratani ya Good Samaritan iliyopo katika Jimbo Katoliki la Ifakara. Wa pili kulia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Ifakara, Mhashamu Salutaris Libena (mwenye miwani) na kushoto kwa Kardinali ni Mhashamu Lazarus Msimbe, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro. (Picha na Michael Ally)

Baadhi ya Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Paul II, Buyuni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Bikira Maria iliyoadhimishwa parokiani hapo.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, akiongoza Sala wakati wa utoaji wa Daraja Takatifu la Upadri kwa Shemasi Peter Masaga (aliyelala kifudifudi), wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Gaspar Del Bufalo, Mbezi Beach, jimboni humo. (Picha na Yohana Kasosi)

Padri Peter Masaga akipokea zawadi kutoka kwa Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia ya Mtakatifu Gaspar Del Bufalo, Mbezi Beach Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, iliyofanyika hivi karibuni parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu (katikati aliyeshika fimbo ya Kichungaji) na Mapadri, wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia ya Mtakatifu Maria Salome, Kimara, Jimboni humo.