Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

NA CELINA MATUJA

Imeelezwa kuwa waamini wanashindwa kupata mafanikio katika maisha ya kiroho na kimwili kutokana na kusali kwa mazoea.
Hayo yalisemwa na Mlezi wa Karismatiki Katoliki Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, Padri Henry Rimisho katika Kongamano la Uponyaji lililofunguliwa jijini Dar es Salaam.
Alisema hayo katika mada aliyofundisha juu ya toba na Damu ya Yesu Kristo, ambayo ndiyo silaha ya kuondokana na changamoto zilizosababishwa na mazingira au binadamu.
Alieleza namna nzuri ya kufanya toba kwa kutumia Damu ya Yesu Kristo, akisema, “Kwanza, Mwamini anatakiwa kukiri kuwa amekosa; hatua ya pili ni majuto kwa kuwa toba ya kweli inafuata na majuto; kujutia ni ile hali ya kuikataa dhambi na kuumia; tatu, toba ili ikamilike, lazima mdhambi ageuke na kuanza ukurasa mpya na kufanya mema, katika kutenda haki iwe kwa wenzake, kwenye familia, ama kazini kwake.”
Aidha, Padri Rimisho alisema kuwa mtu anapogeuka na kukiri kwa Mungu, anajipatia furaha ambayo itakuwa sehemu ya maisha yake, na Mungu atammiminia neema na baraka tele.
“Hivyo, kwa kutumia Damu ya Yesu, inapata kutakatifuza, kutakasa maeneo, na hiyo ni kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu yanayosema, “Kikombe hiki ni Damu ya Agano Jipya iliyomwagika kwa ajili yenu, ambapo Mwamini anapata kufahamu mambo matatu muhimu ambayo ni; Damu ya Yesu; ya Agano Jipya; na iliyomwagika kwa ajili ya mwanadamu….
“Ikumbukwe kwamba Yesu Kristo mwenyewe alikufa na alifufuka, hivyo katika kufa kwake, alitoa Damu Yake ya gharama kubwa, ili kumkomboa mwanadamu katika maisha hapa Duniani,” alisema Padri Rimisho.
Padri huyo alisema kuwa katika Agano la Kale, damu ya wanyama ilikuwa ni ishara ya kutambuliwa na kutokudhurika, kwa mfano katika kabila, na ilileta upatanisho, ilifunika dhambi, damu hiyo ilitolewa kila wakati na kila mwaka, na hasa pale walipohitaji kushughulikia dhambi.
Aliongeza kuwa Yesu Kristo alijitoa kwa kumwaga Damu yake ili kuondoa dhambi za mwanadamu, na anaiita Damu ya Agano Jipya kwa sababu yeye alikuja baada ya Agano la Kale, ambalo Mtume Paulo analiita Agano Kuu, ni Agano Jipya kwa utendaji wake Yesu Kristo Mwenyewe.
Padri Rimisho alisema kuwa dhambi zilikuwa zinafunikwa tu, haziondolewi wakati huo wa Agano la Kale, ila kwa Agano Jipya, zinaondolewa kabisa.
“Damu hii ya Yesu ambayo tunasema kuwa ni ya Ukombozi, ni kwa sababu Mwanadamu alikuwa utumwani mwa adui shetani. Hivyo, ililipa deni na kutoa uhuru, kwa sasa Yesu anakuwa ni mjumbe wa Agano Jipya,” aliongeza kusema Padri Rimisho.
Aidha, aliwafafanulia Waamini kazi ya Damu ya Yesu, akisema kuwa kwanza inamwondolea mtu agano la uharibifu, yaani la nguvu za giza; inatumika katika hali ya hatari, ama kuota ndoto chafu kwa kusali.
Aliongeza kuwa kwa kupitia Damu ya Yesu, mwanadamu anayelindwa na nguvu za giza, itanena msamaha, inafuta laana na dhambi ambazo mwanadamu anazotenda.
Kadhalika, Padri Rimisho alibainisha kuwa Damu hiyo inafungua maeneo yaliyofungwa na mazingira, na madhara yake ni kwamba mtu anaweza kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine akiwa na mafanikio makubwa maishani mwake, lakini ghafla maisha yake yanakuwa si ya kuridhisha, hivyo anaweza kutumia Damu ya Yesu.
Alisema kuwa Damu ya Yesu Kristo ni ya Agano Jipya, kwa kuwa iwatutoa wanadamu katika utumwa wa dhambi na maonevu ya shetani, hivyo ililipa deni la mwanadamu na Yesu, ambapo sasa ni mjmbe wa Agano Jipya.
Aliongeza kuwa ni lazima kuelewa kwamba Damu ya Yesu inavunja na kuharibu kila nguvu ya giza na agano la shetani, kwani wapo baadhi wanaota ndoto mbaya, na za kutisha.
Hata hivyo, Padri Rimisho alisema kwamba hakuna atakayedhurika ikiwa ataitumia Damu hiyo, kwani ina nguvu, na imemnunua kila mmoja, hivyo ni ulinzi unaofuta laana na dhambi zinazotendwa na mwanadamu.

NA MWANDISHI WETU

Mtandao wa Jinsia Tanzania (Tanzania Gender Networking Program: TGNP) umesema kwamba utaendelea kutekeleza kwa kishindo mpango wake wa kupinga vitendo vya ukatili ili kutokomeza ukeketaji nchini.
Afisa wa Idara ya Ujenzi Nguvu za Pamoja na Harakati, Flora Ndaba, akizungumza katika Kongamano la kupinga vitendo hivyo alisema kuwa wamejadili mada mbalimbali na kuona kwamba kuna jinsi ya kuwekeza katika wanawake na kwa mabinti walionusurika kukeketwa.
Alisema kuwa wametumia Bonanza na Sinema ambayo imeandaliwa na Mtandao huo kwa lengo la kupaza sauti zao kuujulisha Umma kuhusiana na Janga hilo la ukeketaji.
“Tupo kwenye Soko la Kivule, na hapa tupo na wadau ambapo kuna sinema ambayo imeandaliwa na TGNP,” alisema Flora.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii, Magdalena Msaki alibainisha kwamba wao wamejipanga kuzuia ukeketaji, kwani kisheria hasa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, ukeketaji ni kosa la jinai.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, ukeketaji ni kosa la jinai, kwa hiyo tunataka kutoa elimu kwa jamii inayotuzunguka katika Kata hizi tatu,” alisema Magdalena.
Kwa upande wake mmoja wa Wanaharakati wa Masuala ya Jinsia, Seleman Bishangazi alisema kuwa wameamua kushirikisha Vijana kwa madhumuni ya kupaza sauti zao ili jamii itambue kuwa ni jambo baya, na hivyo kuachana na jambo hilo.
Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu “Sauti yangu, Hatma yangu” na kufanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam wilayani Ilala.

KASESE, Uganda

Askofu Francis Aquirinus Kibira Kambale wa Jimbo Katoliki la Kasese nchini Uganda, amewatahadharisha Wakristo dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya Dini na kabila.
Aidha, amewasihi waamini hao kuhakikisha wanazingatia maendeleo na elimu kwa manufaa ya jamii husika, badala ya kuendekeza ubaguzi miongoni mwao.
Askofu Kibira alitoa onyo hilo katika hotuba yake baada ya kuadhimisha Misa Takatifu ya Shukrani ya Mchungaji Restetuta Biira Katusabe, binti wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu “Madada wa Banyateresa”, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Nyabirongo, jimboni humo.
Katika hotuba yake, Askofu Kibira anayehusishwa na kusaka maendeleo, kuchukia umaskini na chuki miongoni mwa jamii kwa Wakristo waliopoteza ubinadamu kati yao, aliwataka waishi pamoja kwa amani.
Askofu Kibira alirejelea onyo lake la awali kwa wakuu wa familia dhidi ya kugawanya vipande vya ardhi miongoni mwa watoto, lakini kutumia ardhi iliyopo kwa tija ambayo itasaidia kuongeza mapato, ikiwemo karo ya shule kwa watoto wao.
Katika Misa hiyo, Askofu Kibira Kambale alimteua na kumtuma Padri Leosio Masereka kwenda kufanya utume katika Seminari Kuu ya Kitaifa ya Mtakatifu Paulo-Kinyamasika, baada ya kuhitimu Shahada yake ya Uzamivu (PhD) ya Liturjia kutoka Roma.
Askofu Kibira aliwaomba wazazi kuwatoa watoto wao ili wafanye kazi za Kanisa na kuwasaidia hasa katika elimu rasmi na isiyo rasmi, na kutaja familia kuwa shule ya kwanza, na wazazi ndio waalimu wa kwanza.
Akiongoza hotuba wakati wa Jubilei ya Fedha katika maisha ya Kidini ya shukrani ya Misa ya Mchungaji Jacinta Mbambu pamoja na kuadhimisha viwango tofauti vya elimu katika familia ya Padri Leosio, Askofu Kibira alibainisha kuwa kasisi huyo alimaliza PhD yake huko Roma, kabla ya kumteua kuwa Mhadhiri wa Seminari Kuu ya Kitaifa ya Mtakatifu Paulo.
Katika Homilia yake, Askofu Kibira aliwataka wazazi na walezi kufanya kazi ya kuwajenga watoto wao ili kuendana na huduma ya Kanisa na kuwekeza katika malezi ya watoto, huku akiwakumbusha kuendeleza upendo, msamaha na uvumilivu miongoni mwa mambo mengine.

NDOLA, Zambia

Jimbo Katoliki la Ndola nchini Zambia, limeweka historia kubwa kutokana na Jengo jipya la Kanisa katika Parokia ya Mtakatifu Antonio Fasani wilayani Ndola, ambalo limebarikiwa na kuwekwa wakfu.
Akihubiri katika adhimisho la Misa Takatifu ya uzinduzi wa kanisa hilo, Askofu Benjamin Phiri wa Jimbo hilo, alisema kuwa kiini cha wongofu wa kweli, ni kusika Neno la Mungu.
Alisema pia kuwa utakatifu wa kweli unaenea zaidi ya kuta za kanisa, akisema unyofu wa mioyo kama kipaumbele kuliko ukuu wa jengo lolote, kukumbusha kutaniko umuhimu mkubwa wa imani thabiti na ya kujitolea.
“Baraka na kuwekwa wakfu kwa jengo jipya la kanisa, siyo tu kuwa ni wakati wa kusherehekea, bali pia ni ukumbusho wa kuhuzunisha wa imani ya kudumu na roho ya Jumuiya ambayo inapaswa kuunganisha Parokia pamoja,” alisema Askofu Phiri.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Charles Tembe, aliwashukuru waamini wa Parokia hiyo kwa kujitolea kwao bila kuyumbayumba katika kulisaidia Kanisa.
“Tukio hili linasimama kama ushuhuda wa dhamira isiyoyumba ya Jumuiya ya Parokia ya Mtakatifu Antonio Fasani, ikiashiria sura mpya katika safari yao ya kiroho ndani ya kuta zilizowekwa wakfu za kanisa lao jipya lililobarikiwa,” alisema Padri Tembo.
Padri Tembo alisema kuwa huo ni wakati muhimu katika sherehe hiyo ya kuwekwa wakfu kwa madhabahu na Askofu Phiri, ambaye aliipaka mafuta na kuchoma uvumba, kuashiria utakaso wa nafasi hiyo takatifu.
Miongoni mwa watu waliohudhuria kuwekwa wakfu kanisa hilo ni Mkurugenzi wa Kichungaji, Padri Ephraim Mapulanga; Waziri wa Mkoa wa Copperbelt, Elisha Matambo, na Makuhani wengi na wanadini.

ZOMBA, Malawi
Jimbo Katoliki la Zomba nchini Malawi limetoa msaada wa unga wa mahindi uliosindikwa kwa watu walioathirika na njaa katika jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa kuchangia unga katika Parokia za Chipini na Lisanjala, Askofu wa jimbo hilo, Mhashamu Alfred Chaima aliwataka wanufaika wa msaada huo kuwaombea wananchi walioweka rasilimali pamoja katika kuchangia unga huo.

Viongozi wa Watawa wanaofanya Utume katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Watawa iliyoadhimishwa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo.

Viongozi wa Halmashauri ya Walei na Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Dominiko – Mbezi Juu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa parokiani hapo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya kuchangia Tumaini Media.

Mapadri kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakiingia kanisani kuadhimisha Misa Takatifu ya Sikukuu ya Watawa iliyoadhimishwa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo.

Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu, Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Vitalis Kassembo, akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi na Wadau wa Tumaini Media, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa Redio Tumaini kutimiza Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, iliyoadhimishwa katika Parokia hiyo. (Picha na Michael Ally)

Masista Wanajubilei ya Miaka 25 ya Utawa, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupongezwa na Watawa wenzao wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Watawa iliyoadhimishwa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam hivi karibuni. (Picha zote na Yohana Kasosi)