Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DODOMA

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameiagiza Taasisi zote za ununuzi nchini (Serikali na Binafsi) kuhakikisha zinatoa kipaumbele katika manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa Watanzania, na wazingatie kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo na makundi maalum.
Dk. Biteko alisema hayo Jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (Public Procurement Regulatory Authority: PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (National Economic Empowerment Council: NEEC) ili kujenga ushirikiano unaolenga kuchochea ushiriki wa Wafanyabishara Wadogo, wa kati na Makundi Maalum, katika masuala ya ununuzi wa umma.
“Kusainiwa kwa hati hii leo, kunazidi kuboresha mazingira ya Watanzania kushiriki kwenye uchumi wa nchi yao, hasa watu kutoka makundi maalum. Haya ni  maelekezo ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wote wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, hivyo NEEC, PPRA, Taasisi nyingine za Serikali na Binafsi, wawezesheni Watanzania kushika uchumi wa nchi na muone fahari katika hili,” alisema Dk. Biteko.
Kupitia hafla hiyo, Dk. Biteko aliitaka PPRA kuzidi kuboresha huduma zake kwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa rufaa zinazowasilishwa kwenye mamlaka hiyo, hususan zile zinazohusisha waombaji wa zabuni kutoka makundi maalum ili kuchochea kasi ya ukuaji wa Uchumi wa mtu mmoja mmoja, na hatimaye Uchumi wa Taifa.
Alizitaka mamlaka hizo kujikita zaidi katika uwezeshaji wa wananchi kwa kutoa elimu, badala ya kubaki kuwa wadhibiti pekee.
Dk. BIteko aliongeza kusema kwamba NEEC na PPRA kufanya tathmini na kutoa tuzo kwa watoa huduma wanaofanya vizuri katika uwezeshaji wa makundi maalum suala litakalochagiza ushindani miongoni mwa watoa huduma, na hatmaye kukuza uchumi.
Alisema kuwa makubaliano hayo yatatumika kama jukwaa la kuwahamasisha watu wa kundi hilo kushiriki na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja, kuimarisha wigo wa walipa kodi, na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Aliipongeza PPRA kwa kuweka kanuni ya ushirikishaji makundi maalum kwenye manunuzi ambayo imeelekeza kuwa asilimia 30 ya zabuni zote zitolewe kwa washiriki kutoka makundi maalum, ambao ni wanawake,vijana, wazee na wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, alisema kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya PPRA na NEEC ni ushahidi wa namna Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kwa dhati kushikirisha makundi ya watu maalum kwenye uchumi na ujenzi wa Taifa.
Alisema kuwa makubalinao hayo yataongeza ushiriki wa makundi maalum kwenye manunuzi ya umma, na hii itaongeza uwezo wa Watanzania katika uzalishaji malighafi na bidhaa pamoja na utoaji wa huduma ndani ya nchi.

TUNDURU

Na Salimu Juma

Wananchi wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Rural Water Supply and Sanitation Agency: RUWASA) kwa kutimiza ahadi yake ya kuwapatia maji safi.
Walisema kuwa kwa miaka mingi vijiji vya Wilaya ya Tunduru vilikabiliwa na changamoto kubwa ya huduma ya maji safi na salama kutokana na wananchi kutumia maji ya visima na mito, ambayo hayakuwa salama kwa afya zao.

VISIGA, PWANI

Na Mwandishi wetu

Wabatizwa nchini wametakiwa kuitambua hadhi yao, kwani wao ni hekalu la Mungu, hivyo hawatakiwi kuligeuza hekalu hilo kuwa jalala la dhambi.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi alitoa wito huo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa la Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria – Visiga, mkoani Pwani.
“Tusimshangae sana Suleimani, tuchote fundisho kutoka kwake, kwa nini? Kwa sababu hata sisi tuna kibali machoni pa Bwana, siyo tu kwamba Mungu ameturuhusu tujenge hekalu, bali ametupa haki ya kuwa hekalu lake. Kila Mbatizwa anayo hadhi ya kuwa hekalu la Roho Mtakatifu…
“Kwa hiyo, ewe Mbatizwa, tambua hadhi yako, tambua wito wako, tambua heshima yako, na tunza utakatifu wako mbele za Mungu. Usikubali kukengeuka na ukaligeuza hekalu la Mungu kuwa jalala la dhambi,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Mkuu aliwaasa Waamini kumbeba Kristo na kumpeleka kwa wengine, kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wameinjilisha na wamekuwa wajumbe wa Habari Njema katika maisha yao.
“Maria huyu ni mfano wetu, kwani sisi pia tunaitwa tumbebe Kristo na tumpeleke kwa wenzetu. Kwa maneno mengine, tunaitwa tuwe wainjilishaji, tuwe wajumbe wa Habari Njema,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Aliwashukuru Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), kwa majitoleo yao yaliyoweza kujenga kanisa hilo lililotabarukiwa, akisema kuwa kujituma kwao na kwa ukarimu wao, ndiko kumefanikisha kukamilika kwa ujenzi huo.
Vile vile, Askofu Mkuu aliagiza kuwa kanisa hilo lililotabarukiwa, lisigeuzwe kuwa ukumbi, bali liwe tu kwa ajili ya mambo ya Mungu na Taifa lake Takatifu.
Wakati huo huo pia, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliialika Jumuiya ya Seminari kulitunza kanisa na altare hiyo, ili viendelee kutumika kama ilivyokusudiwa.
Aliwataka Waseminari kutokuona aibu ya kutoa ushuhuda wao, bali wajivunie kwamba wamepata heshima ya kuwa Wakristo, hivyo hawana budi kuutunza uwakfu wao.
“Kwenu Waseminari, tunza uwakfu wako, jilinde kama hekalu Takatifu, toa harufu ya utakatifu na usione aibu kutoa ushuhuda wa Ukristo wako. Jivunie ya kwamba umepata heshima ya kuwa Mkristo, ishi heshima hiyo na shuhudia heshima hiyo na lijenge Kanisa la Kristo,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake, Gombera wa Seminari Ndogo ya Visiga, Padri Philip Tairo, alisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwapa nguvu ya kufanya kazi hiyo ya ujenzi wa kanisa ambayo waliianza Novemba mwaka 2022.
Naye Mwenyekiti WAWATA jimboni humo, Stella Rwegasira alimshukuru Askofu Mkuu kwa kuunganisha tukio lao la shukrani pamoja na la kutabaruku kanisa hilo, huku akisema kuwa kwao kama WAWATA, hiyo ni siku ya furaha kubwa.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas More - Mbezi Beach, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Ladislaus Kapinda amewataka Waamini kuwa watu wa upendo na jirani zao katika jamii wanamoishi.
Padri Kapinda aliyasema hayo hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kanda mpya ya Bethlehemu inayoundwa na Jumuiya nne za Mtakatif Rita wa Kashia; Mtakatifu Monika; Mwenyeheri Isdori Bakanja; na Mtakatifu Michael Malaika Mkuu.
“Kuweni na upendo na jirani zenu katika jamii zenu mnamoishi. Muwe watu wa sala, huku mkiwa na furaha huko mnakoishi, mkiwa kama Jumuiya moja, Kanda au hata Parokia... tambueni kwamba ninyi ni wamoja katika Kristo Yesu, akasema,
“Inawapasa kula chakula pamoja, maana mmekuwa ndugu na Wanajumuiya, hivi ndivyo Kristo anavyotaka, ndiyo maana ametuachia zawadi ya upendo,” alisema Padri Kapinda.
Padri Kapinda alisema kuwa msalaba huo ndio mafanikio makubwa katika imani moja ya Kanisa Katoliki, huku akiwasihi Waamini kutumia msalaba huo ili uwaletee neema katika maisha yao.
Aliongeza kuwa msalaba huo ni alama kwa kila Mkristo, huku akiwakumbusha kufahamu kwamba kila mmoja amekombolewa na msalaba.
“Mimi niwaombe sana muwe Waamini wazuri na wenye kulitunza Kanisa pamoja na kuilinda imani yenu kama Kristo mwenyewe. Kupokea msalaba ndiyo alama kuu kwa Mkristo,” alisema Padri Kapinda.
Wakati huo huo pia, Padri Kapinda aliwakumbusha waamini kuulinda Ukristo wao ili wasije wakaukataa kwa kudanganywa na watu wasio waminifu mbele ya Mungu.
“Waamini nawaomba sana, msiache kutoa michango ili Kanisa letu liweze kuisha kujengwa, maana bila michango yenu, hatutaweza. Kwa hiyo, Kanisa tutajenga bila hofu, maana msalaba umefika na kuzunguka maeneo yote ya Kanda na Jumuiya zetu,” alisema Padri huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Walei Parokia hiyo, Juliana Palangyo alisema kuwa Parokia yao imebarikiwa kuwa na imani, huku akiwaasa Waamini wenzake kwamba kwa kupitia msalaba huo, wamwombe Mungu azidi kuwapa baraka katika maisha yao.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kanda hiyo, Deogratius Kweka aliwasihi Waamini kutambua kwamba kanisa bado halijaisha, hivyo waendelee kutoa michango yao ili kuweza kukamilisha ujenzi huo.
Adhimisho hilo la Misa Takatifu lilikwenda sanjari na kupokea Msalaba wa Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndoko za Kikristo (JNNK), unaoendelea kutembezwa katika Parokia hiyo.

VIKINDU, PWANI

Na Mathayo Kijazi

Wagonjwa wametakiwa kumlilia Mungu ili awaponye matatizo yao, badala ya kutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji, kwani Mungu ndiye anayesikia kilio cha kila mmoja na kumwondolea mahangaiko yake.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alitoa wito huo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kuwaombea Wagonjwa na Watoa Huduma kwa Wagonjwa, iliyoadhimishwa katika Kituo cha Mafungo kilichopo Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Vikindu, iliyomo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
“Kwa hiyo ndugu zangu, tunapougua tufahamu kwamba kuugua ni sehemu ya ubinadamu, tunatakiwa tumlilie Mungu kwa sababu Mungu anasikia kilio chetu. Tuache kuhangaikahangaika huko kutafuta mambo ya kidunia, mara kwa waganga wa kienyeji. Tukimlilia Mungu, yeye atatuondolea mahangaiko yetu,” alisema Askofu Mchamungu.
Alibainisha kuwa wengi wanakosa baraka katika maisha yao kwa kuwa hawakumtanguliza Mungu katika mahitaji yao ya kila siku, hivyo akawataka waepuke kutegemea mambo ya kidunia, ili baraka za Mungu ziwafikie.
Aidha, akifafanua kuhusu Sakramenti ya Wagonjwa, Askofu Mchamungu alisema kuwa Sakramenti hiyo siyo tu kwa ajili ya wagonjwa ambao wanakaribia kufa, bali ni Sakramenti ambayo hutolewa kwa wagonjwa wote, bila kuangalia wanaumwa kwa kiasi gani.
“Watu waliogopa sana Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Kwa hiyo hakuna ambaye alikuwa tayari kwa ajili ya kupokea Sakramenti hiyo, kwa sababu dhana ilikuwa kwamba ukishapokea Sakramenti ya Wagonjwa, kinachofuata unakufa…..,
“Na hata sehemu nyingine, mtu akishapatiwa Sakramenti ya Wagonjwa, basi ndugu zake wanaanza kuandaa utaratibu wa mazishi, hata kabla hajafa. Na kabla ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano (1962-1965), watu walikuwa wanasubiri wagonjwa wao hadi wawe mahututi, ndipo wanaanza kumtafuta Padri ili aende akawapake mafuta. Sasa Mtaguso wa Pili wa Vatikano ukabadilisha hayo mambo, kwamba hiyo siyo Sakramenti ya Wanaokufa, bali ni Sakramenti ya Wagonjwa,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu huyo alisema kuwa hata mzee anapoamua kuomba Sakramenti hiyo kutokana na uzee wake, ni vyema akapatiwa, kwani Sakramenti hiyo ni vizuri kutolewa kwa mtu ambaye ana uelewa pindi inapotolewa, kuliko kwa mtu aliyepoteza fahamu.
Vile vile, Askofu huyo aliongeza kuwa Sakramenti hiyo inaruhusiwa kutolewa zaidi ya mara moja, akisema kwamba mgonjwa anapopatiwa Sakramenti hiyo, kisha akapona, na baadaye akaumwa tena, anastahili kupatiwa Sakramenti hiyo kwa mara nyingine.
Wakati huo huo, Askofu alibainisha kwamba mtu anayeishi maisha ya hovyo, na hataki kumrudia Mungu katika maisha yake, huyo hastahili kupatiwa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa, bali atakapotubu na kubadilika, ndipo anastahili kupatiwa.
Aidha, aliongeza kuwa miongoni mwa watu ambao hawawezi kupatiwa Sakramenti hiyo, ni pamoja na watu wanaokwenda vitani, kwani licha ya kwamba wanakwenda kwenye hatari ya kifo, bali kifo hicho hakitokani na ugonjwa wala uzee.
Pia, alisema kuwa licha ya kwamba anayekwenda kunyongwa, anakwenda kwenye hatari ya kifo, bali hawezi kupatiwa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa, kwa sababu kifo chake hakitatokana na ugonjwa wala uzee.
Katika homilia yake, Askofu Mchamungu aliwaasa watoa huduma kwa wagonjwa, kuendelea kutoa huduma hiyo kwa upole na kwa uaminifu mkubwa, akisema kuwa hiyo si kazi rahisi, na si kila mtu anaweza kuifanya.
Aliwasisitiza Madaktari kutoa huduma hiyo kwa upendo, huku wakiepuka kuwa na uso wa ‘mbuzi’ katika utoaji huo wa huduma, kwani wagonjwa wanahitaji zaidi upendo na faraja katika kipindi walicho nacho.
Kwa upande wake Katibu wa Afya Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Pauline Archard, alitoa wito kwa wauguzi kutambua kwamba wanapotoa huduma kwa wagonjwa, wawe wakarimu, na kuwahudumia kwa upendo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mlezi na Mwalimu katika Seminari ya Mtakatifu Antoni wa Padua – Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba, Padri Roland Kashaga, amewataka wazazi na walezi kuwapatia watoto wao malezi bora na yenye kumpendeza Mungu.
Padri Kashaga alisema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyokwenda sanjari na utoaji wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa watoto 90, iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Mateso - Mbezi Msakuzi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Mkiwa mnawalea watoto wenu, mtambue kwamba hamjapoteza chochote, maana msipowapatia misingi bora watoto wenu, baadaye mtakuja kujuta wenyewe kwa sababu hamkuwapatia kile kinachotakiwa kuwapa watoto hao. Mkiwalisha mema na Matakatifu, hasa wawe watu wa kulishika Neno la Mungu, mtakuwa mmefanya vizuri,” alisema Padri Kashaga.
Padri Kashaga aliwasihi watoto waliopokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kuiheshimu, huku akiwasisitiza kuithamini, kwani hicho ni chakula cha uzima katika maisha yao.
Aliwapongeza Waamini wa Parokia hiyo ya Bikira Maria wa Mateso – Msakuzi, kwa kuwa na kanisa jipya ambalo tayari limeshatabarukiwa, akiwasihi kulitumia vyema kanisa hilo, ikiwemo kwenda kusali na familia zao.
Aliwasisitiza Waamini hao kuendelea kupendana katika maisha yao, kwani wao ni wamoja, akiwasihi kutokutengana ili waendelee kuijenga Parokia yao.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia hiyo Padri Fregiel Massawe, aliwaasa wazazi na walezi ambao bado hawajafunga ndoa, wafunge, huku akiwataka kufahamu kwamba kuishi kama mume na mke bila kufunga ndoa, ni dhambi.
Padri Massawe aliwashukuru Waamini wote wa Parokia hiyo kwa majitoleo yao wanayoyatoa kwa Kanisa, akiwaomba wasichoke kujitolea ili maendeleo yazidi kuwa juu katika Parokia hiyo.

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Wilbroad Henry Kibozi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Askofu Mteule Kibozi wa Jimbo Kuu hilo aliteuliwa Februari 12 mwaka huu, ambapo hadi uteuzi huo, yeye alikuwa Makamu Gombera na Profesa wa Seminari Kuu ya Familia Takatifu, Kahama.
Askofu Mteule Wilbroad Henry Kibozi (pichani), alizaliwa Aprili 30 mwaka 1973 mjini Dodoma. Majiundo yake baada ya sekondari, alisoma Falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba, na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Kipalapala, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.
Baada ya kufanya shughuli za kichungaji kwa muda wa mwaka mmoja katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji huko Chalinze (Dodoma), aliendelea na masomo na kupata leseni na Shahada ya Udaktari wa Taalimungu katika Kitivo cha Taalimungu cha Italia ya Kati, huko Firenze.
Alipewa Daraja Takatifu la Upadri Julai 9 mwaka 2010, kwa ajili ya Jimbo lake Kuu, Dodoma, Tanzania.
Askofu Mteule Kibozi alishika nyadhifa mbalimbali  kama vile Paroko Msaizidi wa Parokia ya Lumuma, kati ya 2010-2012, Mkurugenzi wa Miito Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma kati ya 2012-2014, Muungamishi katika Nyumba ya Malezi huko Livorno, Italia, kati ya mwaka 2017-2019, Mkufunzi wa Waseminari katika Chuo Kikuu cha Jordan, Jimbo Katoliki la Morogoro, kati ya mwaka 2019-2020. Tangu 2020, amekuwa Makamu Gombera na Profesa katika Seminari Kuu ya Familia Takatifu ya Kahama, Tanzania.

LILONGWE, Malawi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Lilongwe nchini Malawi, Mhashamu George Desmond Tambala, amewataka Watawa kujiandaa na kazi ya Kimisionari ya Kimataifa.
Alisema hayo katika Parokia ya Mtakatifu Andrew Kaggwa Jimboni humo, wakati akihubiri katika Misa Takatifu ya Wanovisi wawili Apronia Mahowe na Stella Mkwezalamba, wa Shirika la Wamisionari wa Mary Mediatrix.
Alisisitiza kuwa wanaume na wanawake waliowekwa wakfu wenye asili ya Malawi, lazima waondoe hofu ya kuacha ardhi yao ili kumtumikia Bwana katika nchi nyingine.
“Lazima nisisitize hili, hasa kwako wewe Amidi (Dean) mwenzangu wa Malawi. Tujitenge na upendo wa ardhi yetu, na tuwe tayari kuwatumikia wengine nje ya nchi yetu...wengi wenu huwa na tabia ya kukataa uteuzi wa kimataifa kwa sababu ndogo.
“Unaona, Wamisionari wa Maria Mpatanishi walipaswa kuja kutoka Ulaya na Asia kufanya kazi kati yetu. Wanasaidia Kanisa la mahali hapo bila ubinafsi, na kwa hivyo wakati umewadia kwako kufanya vivyo hivyo mahali pengine,” alisema Askofu Tambala.
“Chukua mfano wa Ibrahimu na Mariamu ambao walitenda tu kwa mapenzi ya Mungu. Unakumbuka Yesu alichosema kuhusu Petro aliposema ‘ulipokuwa kijana, ulikuwa unavaa na kutembea popote unapotaka, lakini ukishakuwa mzee utanyoosha mikono, na mwingine atakuvika na kukupeleka popote pale,” alisema.
Kwa mujibu wa Askofu Tambala, hali hiyo ndiyo inahusu kufanya kazi katika shamba la mizabibu la Bwana kwa lazima, ili watu wajifunze kubadili mitazamo yao na kuchukua changamoto.
Akiwa aliunganishwa na jambo hilohilo, kasisi huyo alikazia hotuba yake kwenye usomaji wa kwanza wa siku hiyo unaotoka kwenye kitabu cha Mwanzo, 12:1-4.
Alisema kwamba Abramu aliombwa aondoke katika nchi yake, watu wake na nyumba ya baba yake hadi nchi ambayo Yehova angemwonyesha.
Kwa upande wake,Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Andrew Kaggwa Monsinyo Patrick Thawale, aliwashauri Wachungaji wawili - Sista Apronia Mahowe na Mchungaji Stella Mkwezalamba, wawe na kasi ya kuitikia wito wao wa kila siku.

LUSAKA, Zambia
Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Zambia (Zambia Conference of Catholic Bishops: ZCCB), limetoa shukrani za dhati kwa wanaume na wanawake wa Dini nchini Zambia kwa michango yao isiyoyumba kwa Kanisa la Mitaa na Universal.
Katika ujumbe maalum kuhusu Siku ya Dunia ya Maisha ya Kuwekwa Wakfu, Askofu George Lungu wa Jimbo la Chipata, alisema kuwa zipo changamoto kubwa katika utume wao.

VATICAN CITY, Vatican

Imeelezwa kuwa watu wengi wamekuwa wakinyimwa haki ya matibabu, na haki ya kuishi.
Hayo yalisemwa na Baba Mtakatifu Fransisko wakati akizungumza baada ya Sala ya Malaika wa Bwana katika kuadhimisha Siku ya Wagonjwa Duniani.
Alisema kuwa kutokana na umaskini uliokithiri au kuteswa chini ya mabomu, katika mataifa ya Ukraine, Palestina, Myanmar na katika migogoro mingine, watu wengi wamekumbwa na matatizo.
Baba Mtakatifu alisema kuwa jamii inatakiwa kuwa karibu, na kuwa na huruma na wagonjwa au watu dhaifu, wakiwahudumia kwa upendo.
“Leo ametangazwa Mtakatifu María Antonia wa Amani wa Figueroa, Mtakatifu wa Argentina, tumpigie mikono Mtakatifu Mpya tunapoadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, sanjari na Siku ya Wagonjwa Ulimwenguni, ambayo mwaka huu inazingatia umuhimu wa uhusiano katika ugonjwa,” alisema Baba Mtakatifu, na kuongeza,
“Sote tunaitwa kuwa karibu na wale wanaoteseka, kuwatembelea wagonjwa, kama Yesu anavyotufundisha katika Injili. Hii ndiyo sababu leo nataka kueleza ukaribu wangu na ule wa Kanisa zima kwa wagonjwa wote, au watu dhaifu zaidi.
Baba Mtakatifu alisema kuwa jamii inatakiwa kutosahau mtindo wa Mungu wa ukaribu, huruma na upole, kwani haiwezi kupuuza ukweli kwamba kuna watu wengi walionyimwa haki ya kutunza, na haki ya kuishi.