Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

MWANZA

Na Paul Mabuga

Wakati huko wanafunzi wakiandika matusi kwenye mitihani yao, kule watoto wameiba simu  janja yenye thamani ya zaidi ya Shilingi 300,000/-, baada ya kumhadaa  mama muuza barafu.
Kwenye daladala, konda kavaa fulana yenye maandishi  ya Kiingereza,  yenye tafsiri kuwa amefurahia uzinzi, na  kwenye mtaa jirani Askari Polisi kaibiwa kuku wanne. Lakini, wenyewe tukikutana, tunasalimiana, ‘Mambo poa’.
Yaani kwamba, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Dk. Saidi anatuambia wanafunzi 17, watatu wakiwa watahiniwa wa  darasa la nne na 12 wakiwa ni wa kidato cha pili, wamefutiwa matokeo  baada ya kuandika matusi katika mitihani waliyoifanya mwaka jana.
Yaani, watoto hawa wametukana, ila tu ni kwamba walikuwa wanatukana nini na wanamtukana nani hatujui.
Hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hili, kwani kwa  kipindi cha miaka  mitano kuanzia mwaka 2018 jumla ya watoto 33 nao walifutiwa matokeo kwa kuandika matusi katika mitihani yao.
Yaani mwaka huu ni hao 17, lakini mwaka 2022 watahiniwa 14 wa kidato cha pili walifutiwa matokeo pia, na wengine wawili wa kidato cha nne, nao walikumbwa na dhahama kama hiyo mwaka 2022.
Angalia, mtoto mwenye umri wa miaka tisa ama 10 akiwa darasa la nne, anaandika matusi, ama tusema anatukana, na kulifanya taifa kusimama kujadili kishindo chake.
Unadhani akifikisha umri wa miaka 22 na akiwa amehitimu Chuo Kikuu kama atafanikiwa, na ikiwa hakurekebishwa, hali itakuwaje katika muktadha wa kujenga kizazi chenye maadili?
Katika mahojiana kwa ajili ya makala haya, Mwalimu John Ndama kutoka Manispaa ya Shinyanga, anasema, “Haya ni mambo yanayotokea katika miaka ya hivi karibuni,” na katika uzoefu wake wa kufundisha kwa karibu miaka 30 kwenye shule za sekondari, hakuwahi kuona mambo kama hayo.
“Hawa ni watoto watukutu, na kwa bahati mbaya wanazidi kuongezeka kadri miaka inavyozidi kwenda. Inawezekana chanzo kikubwa ni wazazi kushindwa kupata muda wa kuwalea kutokana na kubanwa na harakati za kutafuta fedha, baada ya changamoto za kiuchumi kuongezeka, na badala yake, vijana wanalelewa na runinga na mitandao ya kijamii,” anasema Mwalimu Ndama.
Anasema kwamba yaani watoto wanaona vitendo vyenye  maudhui magumu yenye mwelekeo wa matusi kwenye runinga, lakini pia wanaona maandiko na sauti za matusi kwenye mitandao ya kijamii. Lakini baadhi ya familia zinaona haya ni mambo ya kawaida, na hivyo kuyaruhusu yaendelee bia udhibiti! Tunajenge kizazi cha viumbe kisicho na utamaduni, ‘uncultured creatures’.
Katika hali kama hii inakuwaje? Unasafiri kwenda Mtwara kikazi, lakini basi ulilopanda linaharibika njiani katika moja ya vijiji vya mkoa wa Lindi.
Anakuja kijana anauza mahindi ya kuchoma akiwa amevaa fulana yenye maandishi, “Girls for Sex, No offer Rejected,” (yaani Warembo kwa ajili ya ngono, wapo tayari kwa pesa yoyote). Ukimuuliza maana yake anajifanya kufahamu, lakini anakuambia ni zawadi aliyoletewa na baba yake anayeisha jijini Dar es Salaam.
Kijana anadai anafahamu maadishi, na katika umri wake wa miaka 12, bila shaka ubonge wake ulivyo kama sponji, unamnyinya kila kitu, na kuona kuwa haya ni maisha ya kawaida. Kwa nini huyu asione kuwa kuandika matusi kwenye mitihani, siyo ‘jambo mzungu, [la kustaajabisha]?’.
Unapanda moja ya daladala katika Jiji la Mwanza, konda analifunga kiunoni koti lenye nembo kuonesha kuwa hiyo  ni sare ya kazi. Hali hii inaifanya fulani aliyoivaa na maandishi yake yanayosomeka, “We ejoyed sex overnight!” Hakuna anayemsemesha na kumuonya miongoni mwa abiria, na zaidi wanasalimiana miongoni mwao kuwa ‘mambo poa.’ Fikiria kijana aliyemo ndani ya dalada hiyo, hali hiyo anaichukuliaje?
Katika mtaa mmoja jijini Mwanza, wakati Askari Polisi anamsimulia mama jirani yake juu ya kuibwa kwa kuku wake na vibaka, mama huyo naye anaelezea juu ya watoto wawili wenye umri kati ya miaka tisa na 10, walivyofika kwake na kumuibia simu janja kwa namna ambayo hakuweza kuamini.
Mama huyo, Grace Kezla [43], anasema kwamba alipokuwa ameketi kiambazani nje, walifika watoto wawili na kutaka kununua barafu mbili, na wakatoa shilingi 200.
Mama huyo akaingia ndani kwenda kuchukua hiyo bidhaa kwenye jokofu, kwa bahati mbaya akaacha simu janja kwenye mkeka aliokuwa amekalia. Wale watoto bila kuchelewa walichukua ile simu na kuondoka, na alipotoka nje, hakuona kitu.
“Ni kama vile niliuza simu ya Shilingi 300,000/- kwa Shilingi 200.” Anasema Grace ambaye anapoulizwa kuhusu watoto kuandika matusi kwenye mitahani anasema, “Kwenye jamii yetu kuna vitu haviko sawa, wazazi wameelemewa, na waalimu nao wamezidiwa! Hapo panahitajika juhudi nyingine za ziada, vingenevyo tutapata tabu.”
Anasema, “Wazazi  wapo na shida ya kutumia muda mwingi kutafuta fedha kwa ajili ya mahitaji ya familia. Waalimu nao wanataabika na mzigo mkubwa wa wingi wa wanafunzi kuliko uwezo wao, na hivyo kufanya ‘bora liende’. Wakati hali ikiwa hivyo, bado kwa kila hali, inatakiwa kadri iwezekanavyo, kila kijana amalize elimu ya sekondari.
Anashauri kuwa ingawa mtaala mpya wa elimu una msisitizo juu ya maadili, lakini kuna haja ya jambo hili kuwa mtambuka likihusisha wadau na sekta mbalimbali ili kukikomboa kizazi hiki.
“Kama Waunguja wanaona kuwa kwa mwanamke kukaa kwenye boda, ama kipando kama mwanaume ni sawa na kutukana, badala yake anapaswa kukaa upande, inashindikanaje katika maadili yetu?”
Uzoefu mwingine ni kuhitajika umakini juu ya kusimamia maadili ya kijamii, ni maelezo ya Msese Mwanzalima [80], mkazi wa Shinyanga ambaye anasema kwamba kutokana na waalimu kuzingatia kazi zao enzi hizo, alifukuzwa akiwa darasa ka pili mwaka 1958, enzi za Mkoloni kwa kosa ambalo anadhani pengine leo hii lingevumilika.
“Kwenye madawati, enzi hizo kulikuwa na kitundu kwa jiuu, sasa hapo paliwekwa kidau ambapo kilijazwa wino kwa ajili ya kuchovya ‘pen’ iliyokuwa na ‘nib’, na kuandika.
“Mimi badala yake nilikuwa nachovya kidole katika kidau na kujipaka usoni, ila mchezo huo ulitosha kunifukuzisha shule,” anasema Mzee Mwanzalima akikumbukia hali ilivyokuwa wakati huo, huku akidai kwamba hawa waalimu wa siku hizi, ni wapole sana.

VATICAN CITY, Vatican
Katika mahojiano kwenye kipindi cha luninga cha Italia,Papa Fransisko alisikitikia hatari ya kuongezeka kwa vita katika kona mbalimbali za dunia.
Aidha, alielezea jinsi ambavyo hana mpango wa kujiuzulu na kutangaza ziara za kitume huko Polynesia na Argentina.
Kama katika miezi hii ya migogoro ya Mashariki ya Kati na katika miaka hii ya uchokozi dhidi ya Ukraine, Papa Fransisko alirudi kuelezea juu ya hofu ya vita:
“Ni kweli kwamba ni hatari kufanya amani, lakini pia vita ni hatari zaidi,” alisema. Na alizungumzia mkutano aliokuwa nao Jumatano iliyopita tarehe 10 Januari 2024, na ujumbe wa watoto kutoka Ukraine kwamba:
“Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa akitabasamu. Watoto hutabasamu moja kwa moja, niliwapatia chokoleti na hawakutabasamu. Walikuwa wamesahau tabasamu lao, na kwa mtoto kusahau tabasamu lake, ni uhalifu. Hii inaleta vita: inakuzuia kuota.”

Na Dk. Deoscorous B. Ndoloi

Mpendwa msomaji, katika safu hii, wiki iliyopita tuliona vijitabia zoelefu (offending mannerisms) ambavyo vinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa namna tunavyozungumza katika hadhara. Tulivitaja vijitabia hivi kama sehemu ya mawasiliano silonge.

Kwa kukumbushana tu, na kwa wale ambao hawakupata fursa ya kusoma makala husika, vijitabia hivi vinahusu kuwa na kitu chochote mdomoni (pipi au kimbaka), kujikuna kusikofaa, kutoa kicheko ‘kichafu’, kuwakonyeza ama kuwagusa wasikilizaji, kupiga chafya ama kukuohoa kusiko na staha, nk. Pengine tulishau vilevile kugusia juu ya vijitabia vya kuchezea vitu wakati tunapotoa wasilisho, kwa mfano hutikisatikisa funguo mkononi ama sarafu mfukoni, hutafuna kucha au mfuniko wa kalamu, kutingishatingisha magoti hasa wakati unapotoa wasilisho umemeketi, ‘kuvunja vidole’ (cracking knuckles), kugusagusa simu nk. Haya yote yatakufanya uonekane hujatulia.

Leo, katika safu hii, tushirikishane maarifa kidogo juu ya kujenga uhusiano wenye tija na hadhira (audience). Kwa wale ambao wanafuatilia mada zetu, tulisema kwamba haitoshi tu kwa mwasilishaji kuwa mbobezi katika uwanja wake, na kuwa na weledi katika kuzungumza katika hadhara, ni muhimu vilevile kujua aina ya wasikilizaji na sababu zinazowafanya wakusikilize. Hii itasaidia jinsi ya kujipanga kuwakabili. Tuone kwa kifupi aina za hadhira.

Aina ya kwanza tunaweza kuiita ni ya ‘hadhira-mateka’ (captive audience). Wasikilizaji wa aina hii wanajikuta kwamba, kimsingi, hapo walipo hawakuja kwa ajili ya kukusikiliza wewe. Kwa mfano wanachuo wapo chuoni kwa sababu moja ya msingi – elimu. Lakini, hata kama somo lako hawalipendi, unapoingia darasani, inabidi wakae kimya na kukusikiliza, kinyume na matakwa yao kwa vile sheria inawabana.

Wafungwa wanaweza kuwa mfano mwingine wa hadhira ya aina hii. Wapo kama kundi kwa sababu wanatumikia adhabu kwa makosa mbalimbali, na ‘wamekusanywa’ bila ridhaa yao. Katika sehemu za kazi, wapo wafanyakazi wengine wanaona kama kuhudhuria mikutano inayoitishwa na uongozi ni kama kupotezeana muda. Wafanyakazi wa namna hii, katika mikutano, ni hadhira-mateka. Wapo kwa sababu tu, wasipotii mamlaka, wanaweza kukaripiwa.

Ukujikuta unazungumza na hadhira kama hii, kwanza, unakuwa na kazi ngumu sana kuwabadilisha mtazamo/msimamo na kuwasabibishia kiu ya kukusikiliza. Katika mazingira haya, dakika chache za mwanzo za kutoa wasilisho ni muhimu sana – waaminishe kwamba una uzoefu na ujuzi katika mada husika, lakini pia washawishi kwamba mada yenyewe ni ya muhimu mno katika maisha yao na hasa katika kuimarisha mahusiano. Ikiwezekana tumia mifano ya watu ambao walishawahi kufanikiwa kimaisha kwa sababu walizingatia unayozungumza.

Aina ya pili ya hadhira ni ‘hadhira-chuki (hostile audience). Hadhira ya namna hii inaweza kuwa inaonesha dalili zote za chuki na kukosa shauku ya kutaka kujua/kuambiwa jambo. Chuki hii inaweza kulenga katika mada yenyewe; kwa mfano, wasilisho linalohusu kuwahamisha na kuwapeleka sehemu nyingine ya nchi kupisha suala ya maendeleo kama ujenzi wa miundombinu ama kuendeleza hifadhi ya wanyama pori.

Kama hadhira hii haioni faida ya haraka na ya moja kwa moja, utapata shida sana kuzungumza nao. Katika hali isitotegemewa, hadhira hii inaweza hata kuzua tafrani, uhasama ama ushari (wa maneno au matendo). Tumeona kwa mfano viongozi wakijaribu kuzungumza na hadhira wakati wa migomo. Wakati mwingine katikati ya mgomo kunaweza hata kuzuka mapigano. Hali ikidorora vya kutosha hadhira kama hii kuamua kutojihusisha na jambo lolote (apathy).

Hadhira-chuki inaweza kuelekeza uhasama wake kwa mtoa mada binafsi, endapo atasema jambo linalowafedhehesha wasikilizaji. Ikumbukwe kwamba hadhira inaweza kuanza vizuri kwa usikivu wa kutosha, halafu polepole au ghafla hadhira inageuka kuwa na chuki, na kuamua kutotoa ushirikiano na mtoa mada.

Ni vizuri ukiwa unatoa mada kugundua iwapo kuna mabadiliko ya tabia-fiche kati ya wasikilizaji inayoashiria kwamba sasa ‘joto linapanda’ na hadhira inaanza kubadilika kihisia. Matendo na maneno yao madogomadogo yataashirika kinachoenda kutokea.

Vilevile tuliona juu ya mawasiliano silonge (non-verbal communication) na jinsi watu wanavyoweza kuzungumza hata kwa ‘kupiga kelele’ bila kufungua mdomo. Ukiwa mwasilishaji uwe hodari kugundua hili na kutumia mbinu zote kurudisha hali ya hewa katika hali ya utulivu.

Wakati mwingine hadhira inaweza kuwa na chuki na mamlaka yenye uhusiano na mwasilishaji, kama serikali. Hivyo kwamba chuki hii haielekezwi kwa mzungumzaji moja kwa moja, bali kwa serikali kupitia kwa mzungumzaji. Ni vema kama wewe ni mzungumzaji kujua uhasama au chuki hii inaelekezwa wapi, usije ‘ukanunua’ tatizo lisilokuhusu.

 Ni lazima kuwa mwangalifu na kuwa na weledi wa kisaikolojia kuweza kukabiliana na hadhira ya namna hii. Ni vema kutojitenga na tatizo, lakini ni vema zaidi kujua jinsi ya kukabili mabadiliko ya usununu wa hadhira. Kumbuka mhemko huambukiza; hivyo inasaidia kuukabili inavyofaa, pale unapoanza kwa mtu mmojammoja.

Jambo ambalo ningetaka kumalizia nalo, ni kwamba kama mwasilishaji mada, utakuwa umefeli kabisa ukiruhusu mhemko wa hadhira ukakuingia, na wewe ukapata hasira au ukaanza kuonyesha chuki, kwa sababu eti unahusishwa na masuala yasiyokuhusu.

Katika hali yoyote ile ya mhemko wa chuki toka kwa hadhira, uwe na busara ya kujizuia na usikubali kurubuniwa kisaikolojia, ukafanana na hadhira ya namna hii. Unapotoa mada uwe na utulivu ambao wasikilizaji wataona kwamba unayoyaona yahajakufanya ukatetereka toka kwenye kusudio lililokupeleka.
Tumsifu Yesu Kristu!
Itaendelea wiki ijayo.

Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Gaspari, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ambaye pia Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, jimboni humo, Padri Dominic Somola (kushoto), akiwaonyesha Mapadri wenzake maendeleo ya ujenzi wa kanisa jipya la parokia hiyo. (Picha na Yohana Kasosi)

Waamini wa Parokia ya Familia Takatifu – Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyoadhimishwa parokiani hapo.

Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu – Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Vitalis Kassembo akiwabariki Waamini waliotoa Zaka wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyoadhimishwa parokiani hapo.

Viongozi wa Halmashauri ya Walei ya Parokia ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe – Mwenge, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Adhimisho la Misa Takatifu.

Waamini kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo Katoliki la Mtwara, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyoadhimishwa hivi karibuni katika viwanja vya Kanisa Kuu jimboni humo. (Picha zote na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Chama Cha Pool Tanzania (Tanzania Pool Association: TAPA) kimepata mwaliko kwa wachezaji binafsi kushiriki mashindano ya JOY Grand Masters Final yatakayofanyika kuanzia Machi 24 hadi 29 mwaka huu huko Qinhuangdao nchini China.
Katika mashindano hayo, Tanzania itawakilishwa na Melckzedeck Amadeus aliyemaliza kama mchezaji bora wa Bara la Afrika katika mashindano ya Afrika yaliyofanyika Afrika Kusini mwaka 2023.
Msemaji wa Chama hicho Akida Kilango alisema kuwa mchezaji atakayependa kushiriki katika mashindano hayo anaweza kupata fursa hiyo kwa kujigharamia nauli ya ndege kwenda na kurudi, malazi, pamoja na chakula.
Alisema kuwa mchezaji huyo atatakiwa kuwasiliana na TAPA ili kuweka mambo sawa juu ya ushiriki wake.
TAPA itamsaidia katika upatikanaji wa nyaraka muhimu ikiwemo mwaliko kwa ajili ya safari na itagharamia gharama ya kupata VISA.

DAR ES SALAAM

Na Nicholaus Kilowoko

Wamiliki wa timu ya soka ya wanawake inayoshiriki Ligi ya Wanawake Tanzania Bara, Amani Queens yenye maskani yake mkoani Lindi, wameamua kuiuza timu yao kutokana na ukata wa kifedha ambao umesababaisha washindwe kuiendesha.
Wakizungumza kutokana na kukutana na changamoto hiyo, wamiliki hao walisema kuwa mpira kwa sasa unahitaji fedha, hivyo wao ilifika wakati wanakosa kabisa stahiki za wachezaji, hali ambayo imewafanya waamue kuiuza timu hiyo.
Walisema kuwa kipindi cha nyuma walikuwa wanaomba michango kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kuiendesha timu hiyo, lakini kwa sasa imefikia mwisho na kuamua kuiuza timu hiyo kwa Jeshi la Wananchi Tanzania JWTZ.
Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Lindi, Hosea Lugano alisema kuwa kutokana na mwenendo mbovu ulikokuwa nao timu hiyo, wamiliki wake walimaua kuiuza timu hiyo kwa wawekezaji wengine ambao ni JWTZ.