Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Celina Matuja

Maandalizi ya Kongamano la Tano la Ekaristi Kitaifa litafanyikia Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kuanzia tarehe 11-16 Septemba 2024, katika viwanja vya Msimbazi jijini Dar es Salaam yanaendelea kwa kasi huku majimbo ambayo hayajakamilisha michango, yanaombwa kumalizia.
Akizungumza na Tumaini Letu ofisini kwake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alisema kwamba maandalizi kwa sasa yako katika kiwango cha juu.
Aidha, Askofu Mchamungu alitoa wito kwa Majimbo Katoliki yote nchini kukamilisha michango yao, ili kufanikisha tukio hilo kubwa kwa Kanisa Katoliki Tanzania.
Alifafanua kwamba kila Jimbo katika Metropolitani ya Dar es Salaam, linapaswa kuchangia Shilingi milioni 25/=. Majimbo mengine yanapaswa kuchangia Shilingi milioni sita kila moja.
Askofu Mchamungu alisema kuwa Mashirika ya Watawa yanapaswa kuchangia Shilingi 250,000/= kila moja, Mapadri na Walei watakaoshiriki Kongamano hilo na kupewa malazi, wanapaswa kuchangia Shilingi 250,000/= kila mmoja, na watoto ni Shilingi  65,000/= kila mmoja.
Aidha, kwa Mapadri na Walei ambao watashiriki kwa kutwa tu bila kuhitaji malazi, wanapaswa kuchangia Shilingi 50,000/- tu. Idadi ya washiriki watakaopata chakula na malazi, inatarajiwa kuwa watu 2,811, na idadi ya washiriki wa matukio ya kila siku inatarajiwa kuwa watu 4,811.
Askofu Mchamungu alizitaja mada zitakazofundishwa kwa siku tatu ili kukuza kiwango cha imani kwa Waamini wakiwemo vijana na watoto, ni pamoja na Ekaristi na Maadili, Udugu wa Kikristo kama Nguzo y a Kukuza Utu wa Mwanadamu; Ekaristi na Uponyaji katika Familia. Nyingine ni Ekaristi na Jumuiya Ndogo Ndogo; Historia ya Uinjilishaji katika Kanda ya Mashariki; Ukuu wa Adhimisho la Misa Takatifu; Changamoto ya Upentekoste na Mkatoliki wa Leo.
Kongamano hilo litatanguliwa na Maandamano ya Ekaristi Asubuhi siku ya Jumamosi Septemba 25 mwaka huu.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amesema kuwa watu waliolishwa kwa mikate mitano na samaki wawili, walikuwa ni wadau wakuu walioshuhudia mang’amuzi ya msingi katika hija ya maisha yao ya kiroho.
Baba Mtakatifu alisema hayo katika Dominika ya 18 ya Mwaka ‘B’ wa Kanisa katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.
“Katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 18 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Kristo Yesu anapenda kuwaalika wafuasi wake kutambua kwamba Yeye ndio ule Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, unaozima njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele. Wayahudi walionja pia ukarimu wa Mwenyezi Mungu wakati walipokuwa Jangwani alipowapatia mana iliyoshuka kutoka mbinguni, waliyokula wakashiba wakati wote wa safari yao, hadi pale walipofika kwenye nchi ya ahadi.
“Yesu anawahakikishia wafuasi wake kwamba Yeye ndiye ule Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, unaomkirimia Mwamini maisha ya uzima wa milele, kwani Yeye ni Mwana mpendwa wa Mungu aliyekuja hapa duniani kumkirimia mwanadamu utimilifu wa maisha yake, na hatimaye kumwingiza katika maisha ya Kimungu.”
Baba Mtakatifu aliongeza kuwa Waisraeli walitambua kwamba wao walishibishwa kwa namna ya pekee na Sheria pamoja na Neno la Mungu, mambo ambayo yaliwatofautisha na Makabila mengine, kwani wao walikuwa na uwezo wa kutambua utashi wa Mungu, na hivyo walipaswa kuwa na dira makini kuhusu maisha yao.
Aliongeza kuwa Kristo Yesu ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, na ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, akibainisha kwamba huo ni mwaliko kwa Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutekeleza mapenzi ya Mungu maishani mwao, ila kikawa kitendo cha Wayahudi kupinga kuhusu Yesu kuwa ni Chakula cha uzima wa milele.
Baba Mtakatifu aliongeza kuwa mkate unaotolewa na Kristo Yesu, Neno wa Mungu, unahitaji kiu na njaa ya undani wa maisha ya binadamu, hivyo huo ni mwaliko wa kujiuliza ikiwa kama Waamini wana njaa na kiu ya kweli ya Neno la Mungu, pamoja na kufahamu maana halisi ya maisha.
Aliongeza kwamba huo ni mwaliko kwa waamini kujiachilia mikononi mwa Kristo mwenyewe, ili aweze kuwafundisha namna ya kumwamini, kukutana, na hatimaye, kulishwa naye, ili kufanikisha jitihada za kupata maisha ya kweli na njia inayoelekeza maana ya maisha, haki, ukweli na upendo, na ni changamoto kwa waamini kumwamini Kristo Yesu, ili waweze kupata maisha mapya.

TAFAKARI SOMO LA INJILI DOMINIKA YA 19

Amani na Salama!
“Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye, hataona kiu kamwe.” Haya ndiyo maneno ya hitimisho la somo la Injili ya Dominika iliyopita. Yesu anajitambulisha kwa wasikilizaji wake kwa namna ambayo iliwakwaza, ni maneno yaliyoweka imani yao njia panda, na hapa ndipo tunaona wasikilizaji wake ambao Mwinjili anawatambulisha kama “Wayahudi,” walimnung’unikia Yesu kutokana na maneno hayo.
Wayahudi waliamini kuwa na ukweli wote, na ndiyo Torati na Manabii. “Atamlisha mkate wa ufahamu, na kumnywesha maji ya hekima.” (Yoshua bin Sira, 15:3) Hivyo, ndiyo kusema kuwa mkate wa uzima ni Neno la Mungu ambalo Wayahudi waliamini kuwa nalo katika ukamilifu wake, ndiyo Torati na Manabii na Vitabu vingine vya Maandiko Matakatifu.
Kwao ilikuwa ni makwazo makubwa, kwani Yesu leo anajitambulisha kuwa ni Yeye aliye mkate wa uzima wa milele utokao mbinguni, ni kwa kulisikiliza na kulishika Neno lake, kila mwenye njaa na kiu atashibishwa, na hivyo hataona njaa wala kiu tena.
Wayahudi walishindwa kuupokea utambulisho wa Yesu kama chakula cha uzima, na wakabaki kumwona kama mwana wa Yusufu tu, na tena waliyemfahamu vyema hata kazi na ujira wake kuwa ni ule duni kabisa, na zaidi sana hata mama yake pia walimfahamu. Ni watu waliomfahamu vyema na vizuri, na kwa nini basi anajitambulisha na kujifananisha kuwa ni Mungu, ni kutoka mbinguni?
“Wakasema, huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, ameshuka kutoka mbinguni?” Na tunasikia manung’uniko haya hawakumwelekezea Yesu, bali yalikuwepo baina yao, miongoni mwao, kati yao wenyewe.
Kunung’unika siyo kitendo kile cha kulalamika tu. Naomba kieleweke, na Mwinjili anakitumia kitenzi hicho kuonesha mkwamo wao wa kiimani, kukwazika na kujikwaa kwao kwa fundisho lenye utambulisho mpya kumhusu Yesu, utambulisho ambao unamfunua Yesu kuwa si tu mwanadamu kweli, bali pia ni Mungu kweli, ametoka kwa Mungu, amekuja kuifunua katika ukamilifu sura halisi ya Mungu. Kwao haikuwa jambo rahisi na lenye kueleweka kuwa kwa njia ya Yesu, hekima ya Mungu imejimwilisha na kukaa kati yao, na kuwa katikati yao. Soma zaidi Tumaini Letu.

Vijana Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu, Makongo Juu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti hiyo.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, akiwa katika picha ya pamoja na Mapadri na vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara katika Parokia ya Mtakatifu Rita wa Kashia – Temboni, jimboni humo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu. Kulia kwa Askofu, ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Festo Ngonyani. (Picha na Mathayo Kijazi)

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi akimbariki mtoto katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu, Makongo Juu, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa parokiani hapo. Kulia kwa Askofu Mkuu, ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Massenge, na aliyesimama ni Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, Padri Canisius Hali.

Watoto wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu wa Parokia ya Mwenyeheri Antonio Rosmini, Mpiji Magoe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara. Kushoto aliyesimama ni Mlezi wa Shirika hilo, Krista Kimalio.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akiwa katika picha ya pamoja na Mapadri  na Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu, Makongo Juu jimboni humo, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo. (Picha zote na Yohana Kasosi).

Vijana Waimarishwa wa Parokia ya Mwenyeheri Antonio Rosmini, Mpiji Magohe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo.

Waamini wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu, Makongo Juu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa parokiani hapo hivi karibuni.