Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

RUVUMA

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga amesema kwa Serikali imetenga takribani Shilingi bilioni 4.6/- kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi mkoani Ruvuma.
Kapinga (pichani) aliyasema hayo wakati akizindua Kituo cha Mauzo ya Makaa ya Mawe ya kampuni ya Market Insight Limited (MILCOAL), inayojihusisha na uchimbaji, uuzaji na usambazaji wa makaa ya mawe, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

SIMANJIRO

Na Mwandishi wetu

Wachimbaji wa madini ya Green Garnet eneo la Lemshuku, Kata ya Komolo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamelalamikia kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde juu ya changamoto ya ukosefu wa maji, nishati ya umeme na kuwa na ubovu wa barabara.
Mmoja wa wachimbaji madini ya Green Garnet, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chusa Mining Ltd, Joseph Mwakipesile alisema hayo wakati akizungumza na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde baada ya kutembelea machimbo ya Lemshuku.
Mwakipesile alisema kuwa huduma ya maji ni changamoto kubwa kwenye machimbo ya Lemshuku, na hakuna nishati ya umeme, hivyo kushindwa kufanya uchimbaji kwa uhakika.
“Maji yanafuatwa umbali wa kilomita 17 kutoka kijiji cha Komolo hadi hapa machimboni, na tulikuwa na kisima cha maji, ila hivi sasa tuna maji tunafuata mbali, na pia barabara ni mbovu,” alisema Mwakipesile.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini (MAREMA), Tawi la Lemshuku, Swalehe Abdalah aliiomba Serikali kufanikisha utatuzi wa changamoto hizo ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji kwa uhakika.
“Tunakushukuru Waziri Mavunde kwa kufika Lemshuku na kuona mazingira ya hapa Lemshuku, tunaomba serikali imalize vikwazo tulivyonavyo ili tufanye kazi vyema,” alisema Swalehe.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Mavunde alisema atakutana na Mawaziri husika ili kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi kuwawezesha wachimbaji hao waweze kufanya kazi zao ipasavyo, na Serikali iongeze mapato.
Waziri Mavunde alisema miundombinu ikiboreshwa na changamoto zikipatiwa ufumbuzi, Watanzania hao watatajirika kwa kupata fedha nyingi, na serikali itaongeza mapato kupitia kodi.
Hata hivyo, ili kumaliza changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya, ameendesha harambee ya ghafla ya ujenzi wa zahanati na kupatikana Sh23 milioni matofali 3,000 na mifuko 185 ya saruji
Aliuagiza uongozi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro, kuhakikisha pampu iliyozama kisima cha maji Lembole inatolewa ili wachimbaji wapate huduma wakati wakisubiri mradi mkubwa wa maji.
Akizungumza kuhusu mawasiliano alisema kwamba atazungumza na waziri husika ili mnara wa simu ufungwe kwenye machimbo hayo na hivyo mawasiliano yapatikane.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala alisema kuwa hii ni mara ya kwanza Waziri wa madini kufika kwenye machimbo ya Lemshuku, hivyo Waziri Mavunde anapaswa kupongezwa.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini nchini, Femata John Bina alisema Waziri Mavunde ni kiongozi wa pori kwa pori asiyekaa ofisini ndiyo sababu amefika Lemshuku huku Mwenyekiti wa chama cha mabroka Tanzania (Chamata) Jeremiah Kituyo amewaasa wanunuzi wa madini kukata leseni ili waweze kuwa huru na biashara yao.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka naye alisema wachimbaji hao wa Lemshuku wakitatuliwa changamoto zao watanufaika ikiwemo wachekechaji.

LINDI

Na Mwandishi wetu

Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, (NEEC) limewataka viongozi wa Mkoa wa Lindi, kutengeneza mkakati kabambe utakaozuia mimba za utotoni kwa wasichana kuwakatiza masomo na kuzima ndoto zao.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Beng’i Issa wakati baraza hilo lilipozindua programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA)mkoani humo.
“Mkoa huu una matatizo ya wasichana kuacha masomo, hata wakiwa wamefaulu kujiunga na shule za sekondari hawaendi na inakadiriwa asilimia 30 yao hukatisha masomo kutokana na mimba za utotoni…mimba za utotoni zinakatisha ndoto za kiuchumi za wasichana,”alisema Beng’i.
Alisema programu ya IMASA imekuja kuwezesha Makundi ya kinamama, vijana, na makundi maalum. Hivyo makundi ya vijana yakipata elimu, ni nyenzo kubwa ya kufikia malengo yao ya kiuchumi na ukizingatia mkoa huo una fursa nyingi za kiuchumi.
Beng’i alisema kwamba mkoa huo wananchi wanajishughulisha na kilimo cha korosho,alizeti,uvuvi, mazao ya mwani, hivyo programa hiyo itashirikiana na mkoa huo kuweka vipaumbele ili kuandaa programu kwa ajili ya uwezeshaji wake.
Alisema pia kuwa program ilipokelewa vizuri mkoani humo na wananchi walitamani sana programu ianze haraka, na washiriki wengi walikuwa ni wafanya biashara, wakulima, wakulima wa kuongeza thamani mazao, na madalali wa kilimo.
Aidha, aliutaka uongozi wa Mkoa huo kuendelea na programu zao za kawaida katika kilimo cha korosho, ubanguaji korosho kuongeza thamani mazao na uvuvi, na zile za uwezeshaji za asilimia kumi na kuendelea, kufuata maelekezo ya serikali.
Naye Katibu wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Manispaa ya Lindi, Zuhura Meza alisema anamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hiyo ambayo imekuja kuwainua kiuchumi wanawake kupitia mafunzo ya ujasiriamali na uwezeshaji watakaopewa.
“Nikirirudi nyummbani naenda kuwaelimisha watu wenye ulemavu, wale ambao hawajajisajili na programu ili nao waende kujisajili ili kupata fursa ya mafunzo na uwezeshaji,” alisema.
Naye Mkulima wa Mwani kutoka Kata ya Lindi Mjini ya Kitumbi, Kwela, Manispaa ya Lindi, Rukia Selemen alisema yeye ni mkulima na mchakataji wa bidhaa za mwani. Anashukuru ujio wa program hiyo kufika katika manispa yao kutoa elimu ya ujasiriamali na itamwezesha kufanya vizuri zaidi.
Mjasiriamali toka Kilwa Masoko Fatuma Juma alisema anajishughulisha na usindikaji wa mazao mbalimbali, yakiwemo ya maziwa (yogati), juice ya mwani na anatengeneza bidhaa za urembo kama nguo, na alidai kwa kusema kuwa programu hiyo imewaingiza katika mfumo na hivyo kufanya kazi kwa ubora.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewaasa Waamini kutambua kwamba ufukara na umaskini isiwe ni sababu ya wao kuikana imani.
Kardinali Pengo (pichani), alitoa wito huo hivi karibuni wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyoadhimishwa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima-Msimbazi, jimboni Dar es Salaam.
“Kuna baadhi ya watu kutokana na umaskini na ufukara wao, wamediriki kuikana imani yao ili mradi wapate baadhi ya vitu walivyokuwa wakihitaji,”alisema Kardinali Pengo.
Aliendelea kusema, “Nanyi Waamini na watoto mnaopokea Sakramenti ya Kipaimara, inawapasa kufahamu, hata Yesu alikuwa ni mtu fukara zaidi, lakini bado aliishi katika imani…hivyo basi nanyi inawapasa  kuishi katika imani hiyo hiyo aliyokuwa nayo Yesu Kristo mwenyewe, ikiwa kama kielelezo na mfano bora wa maisha ya Mkatoliki.”
Kardinali Pengo alisema wanatakiwa kutambua kuwa Mwenyezi Mungu hana shida na fedha za mtu yeyote, bali anahitaji watu waongoke na kuiamini Injili.
Inawapasa kufahamu “maskini anayeongelewa na Muinjili Mathayo, si maskini wa mavazi, malazi au makazi, bali ni maskini yule asiyelifahamu Neno la Mungu”
Kardinali Pengo alisema kwamba Yesu Kristo alikuja duniani kwa kazi moja ya kuwahubiria Injili watu maskini na kuwakomboa wanadamu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba-OSA, amesema kuwa vijana wanapopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, wanapokea ili watambue wajibu wao.
Askofu Musomba alisema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 60 katika Parokia ya Mtakatifu Paulo VI-Mikwambe, jijini Dar es Salaam.
Alitoa wito kwa Waamini wa Mikwembe kuepuka kiburi na majivuno, kwani tabia hizo zimetajwa kuwa ni vyanzo vinavyosababisha watu washindwe kumwelekea Mungu katika maisha yao.
Vile vile, alitoa msisitizo kwa Waamini kuepuka kuusaliti Ukatoliki wao kutokana na kudanganywa na waganga wa kienyeji wanaodai kwamba wanasafisha nyota.
Aliwasihi Wakristu kutenga muda maalum wa kuombea familia zao, kwani familia nyingi hukosa utulivu kutokana na kutokuwa karibu na Mungu katika maisha yao.
Askofu Musomba aliwakumbusha Waamini kutokufanya shughuli binafsi siku ya Jumapili zitakazowafanya washindwe kwenda kanisani, akiwataka kutambua kwamba Mungu ndiye anayewapa nguvu kila wakati.
Vile vile, aliwataka kuondoa vikwazo vinavyowafanya wawe mbali na Mungu, bali wajitahidi kuwa karibu naye ili waweze kuishi maisha yaliyo mema.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Gregory Kijanga alisema kuwa ni furaha kwao kutembelewa na Askofu Musomba, ambaye ni mara yake ya kwanza kufika parokiani hapo.
Padri huyo aliwasihi vijana walioimarishwa katika Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kuyaishi yale waliyofundishwa, kwani hiyo itawasaidia kuiishi vyema imani yao.
Naye Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Stefano Shirima alimshukuru Askofu Msaidizi Musomba, akiwasisitiza wazazi na walezi kuwa karibu na vijana hao katika ukuaji wao, kwani wasipowasimamia vyema, wataharibika.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Viongozi wa Dini na Wanasiasa nchini, wanatakiwa kuzingatia hekima ili waweze kutenda vyema, kwani wasipokuwa na hekima, watasababisha vurugu na taharuki katika jamii kwa kuongea mambo mabaya dhidi ya watu wengine, hata kama mambo hayo hayapo.
Hayo yalisemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Maria Salome, Kimara, jimboni Dar es Salaam, iliyokwenda sanjari na kumsimika Parokoa mpya wa parokia hiyo, Padri Boniphace Omondi.
“Wazingatie hekima, kwani watatenda kama vile Mungu anavyotaka, asiye na hekima anaweza kuingia katika mambo ya ulevi, hana cha maana sana sana ataongelea ya wengine na tena ya ajabu ajabu,”alisema Askofu Mchamungu, baada ya kumsimika Parokia mpya, Padri Omondi.
Viongozi wasiokuwa na hekima fujo:
Akiwazungumzia Viongozi wa Kanisa na Serikali ama Wanasiasa, Askofu Mchamungu alisema,
“Katika Nchi Rais aliyemaliza muda wake anapoondoka anakuja  mwingine yule aliyestaafu hatakiwi kuingilia mambo ya Rais aliyopo madarakani, anapaswa kuendelea na shughuli zake bila kumwingila mwingine, hiyo ndiyo itakuwa hekima,”alisema Askofu Mchamungu.
Askofu Mchamungu alibainisha kuwa hata katika Kanisa, Viongozi wakiwemo Maaskofu na Maparoko wanapomaliza muda wao na kustaafu, wanapaswa kutulia na kuendelea na shughjuli zao bila ya kuwaingilia wengine ambao wapo madarakani, kwani kwao kufanya hivyo, hiyo ndiyo hekima, lakini kinyume chake ni vurugu katika jamii.
“Hata katika Kanisa, Askofu anapomaliza muda wake na kustaafu, kwa mwenye hekima, anapaswa kutulia na kuendelea na shughuli zake huko aliko, bila kumuingilia mwingie ambaye yupo madarakani, endapo atamwingi maana yake atakuwa amekosa hekima, na hiii italeta vurugu, kwani atakuwa anafanya uchochezi kwa kusema wengine vibaya, hata kama mambo husika hayapo,”alisema Askofu Mchamungu na kuongeza,
“Katika Parokia, hata Paroko aliyemaliza muda wake, naye ni hivyo hivyo, anapaswa kukumbatia hekima na kuendelea na kazi zake, bila ya kumuingilia mwingine ambaye anayeendelea na kazi zake katika Parokia,”alisema.
Kwa mujibu wa Askofu Mchamungu, Kiongozi wa namna hiyo asiyeingilia wenzake kwenye majukumu madarakani, ndiye anayoonekana kuwa mwenye hekima...popote pale, lakini endapo atakwenda kinyume, atakuwa mchochezi dhidi ya mwenzake.
“Kiongozi mjinga ni yule mwenye kupita chini chini na kuchochea watu kwa kusema maneno mengi ya uongo dhidi ya viongozi waliopo madarakani... hiyo ni mbaya, kwani hata Mtume Paulo mwenyewe anataka tuache kufanya hivyo, na kutekeleza mapenzi ya Mungu.”
Aidha, Askofu Mchamungu aliwataka Waamini kuhakikisha katika nafasi zao, wanakumbatia hekima ya Mungu, na kuendelea na kazi zao bila ya kuwaingilia wenzao waliopo madarakani na kuwafanyia vurugu za chini kwa chini katika nafasi zao za Uongozi, kwani kufanya hivyo, ni kusababisha vurugu katika uongozi.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba-OSA katika Kigango cha Mtakatifu Antoni wa Padua – Nyeburu, Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II – Buyuni, Adhimisho la Misa Takatifu ya Somo wa Kigango hicho. (Picha na Michael Ally)

DAR ES SALAAM

Na Israel Mapunda

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Sekta Binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi, ili kuhakikisha Sekta ya anga inakua na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa.
Waziri Kihenzile (pichani), alisema hayo jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea anga ya kampuni ya Ndege ya Precision, kukutana na kuzungumza na Wakurugenzi watendaji wa Coastal Aviation na Flightlink.
Katika ziara yake hiyo, Naibu Waziri Kihenzile alisema kwamba uwekezaji unaofanywa na Serikali kwenye eneo la kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege, utakuwa na matokeo makubwa pale ambapo sekta binafsi pia itawekeza katika ununuzi wa ndege.
Kihenzile aliongeza kuwa Serikali ipo katika hatua mbalimbali ya kufanya maboresho kwenye sera ya Uchukuzi na Sheria ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kwa lengo la kuimarisha sekta ya usafiri wa anga.
Naye Mkurugenzi wa Precision, Patrick Mwanri alisema kwamba katika mpango kazi wake, imepanga kuongeza ndege ambazo zitakwenda sambamba na ongezeko la vituo ambavyo kampuni itakuwa ikitoa Huduma nchini.
Mkurugenzi Mwanri aliiomba Serikali kupitia Naibu Waziri Kihenzile, kuzisaidia kampuni binafsi za ndege kuweza kupata mikopo kupitia benki za ndani, ili kuziimarisha kwenye uendeshaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Flightlink, Kapteni Munawer Dhirani aliishukuru Serikali kwa kutekeleza dhamira yake ya kuweka mazingira mazuri ya sekta ya anga, na kuhakikisha makampuni binafsi yanaendelea kuwekeza kwa kununua ndege nchini.
Kapteni Munawer aliongoza kuwa  mazingira yaliyowekwa yameiwezesha Kampuni ya Flightlink kuweka mipango ya  kuongeza mtandao wa safari, ambapo mapema mwisho wa mwaka, Kampuni hiyo itaongeza kituo cha Mwanza.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwai’chi amewataka waimarishwa kuwa Manabii wa kweli na kusikiliza sauti ya kichungaji wanapoitwa na Mungu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mwenyeheri Antonio Rosmini - Mpigi Magoe, jimboni humo.
“Muimarishwa unaitwa kuhubiri Habari Njema za Kristu, pamoja na kufanya mambo yaliyo mema na yenye kumpendeza Mungu, na si kuwa nabii wa uwongo,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Aliongeza kuwa zama za sasa zimekuwa na manabii wengi wa uongo, ambao lengo lao ni kudanganya, na si kutangaza Neno la Mungu.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwai’chi alisema kuwa Mkatoliki aliyebatizwa, hapaswi kuwaamini manabii wa uongo, bali anatakiwa kuishi katika imani yake.
Aliwakumbusha Waamini kwamba manabii wa uwongo wamekuja kwa kazi ya kutafuta fedha tu, na si kwa ajili ya kuhubiri Neno la Mungu, akiwasisitiza kusimama imara katika imani yao.
“Nabii wa kweli hutokana na kusema ukweli, na siku zote maisha yao si rahisi, kwa sababu ndani yao mara zote kumejaa manyanyaso ya kusakamwa, ya kusutwa, pamoja na kudhulumiwa,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza,
“Hata katika Somo la Kwanza anazungumziwa Nabii Yeremia ambaye ni kati ya manabii mahiri zaidi katika Agano la Kale, ambaye mara zote alikuwa anawaambia watu wamrudie Mungu kutokana na mambo yao waliyokuwa wakitenda.
“Lakini, kwa sababu alikuwa ni nabii aliyesimama katika ukweli zaidi, watu hao walimkamata na kumuhukumu kifo, lakini ni kwa sababu Yeremia aliwataka watu wabadilike kwa kutubu ili yasije kujitokeza tena yale ya Sodoma na Gomora. Hiyo inaonesha fika ni kwa jinsi gani Manabii wa ukweli wanavyoteseka.”
Aidha, Askofu Ruwa’ichi aliwakumbusha Waamini kutubu na kuamini Injili, ikiwa kama ujumbe wa Yesu aliowaachia wanafunzi wake, akiwataka kutokufanya maamuzi ya haraka, bali wafikiri zaidi na kutenda ili baadaye wasije kujuta.
Aliwakumbusha Waimarishwa kuwa siku ya Ubatizo walizaliwa mara ya pili kama hekalu la Roho Mtakatifu, akiwataka watambue na wajiheshimu kwa kuuishi vyema wito wao.
Aliwasisitiza kushuhudia matendo makuu ya Mungu, akiwaasa kuwa kipaumbele ni kuzungumza habari njema kwa watu, na kuwakumbusha kutokuwa manabii waliokufa, wala manabii wasiokuwa na uthubutu.
Hata hivyo, Askofu Mkuu aliwataka wazazi na wasimamizi kuwa mfano bora wa kuigwa na watoto, kwa kuwasaidia kuishi vyema wito wao siku zote za maisha yao.

DODOMA

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amewaasa wataalamu wa sekta za mifugo na uvuvi kupeleka na kufundisha teknolojia za sekta hizo vijijini, ili kuwapa elimu wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa, na hivyo kuleta tija.
Alisema hayo alipotembelea kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa (Nane Nane) yaliyofanyika Kitaifa mkoani humo.