Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na Jimbo Katoliki la Moshi, wakisali mbele ya sanduku lililobeba mwili wa Mwanashirika mwenzao, marehemu Theresia Nicholaus Massawe wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kumwombea, iliyoadhimishwa kijiji cha Maua Kati wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro. (Picha na Yohana Kasosi)

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Wanajumuiya wametakiwa kulishika na kuliishi Neno la Mungu kwa ukamilifu bila kuwa na hofu yoyote katika maisha yao ya kila siku.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri Bonaventure Kisoka, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Somo wa Jumuiya ya Mtakatifu Fabiano, parokiani hapo.
“Waamini muwe watu wa kusali kila mnapokutana, kwa sababu ninyi ni Wakrito, mnapoishi kwa umoja msije mkatengana, endeleeni kusali pamoja kama hivi leo mnaposherehekea Sikukuu yenu mmeungana kitu kimoja, hivi ndivyo inavyotakiwa Wakristo,”alisema Padri Kisoka na kuongeza,
“Tambueni kwamba Jumuiya ni kanisa ndogo la nyumbani, mnakuwa Wakrito wenye umoja. Endeleeni kusali pamoja kama hivi kila wakati, mfuateni Mtakatifu wenu wajumuiya, Mtakatifu wenu alikuwa mtu mwema ambaye alimsikiliza sana Mungu, na ninyi muwe watu wema.”
Aidha, aliwasihi kuungana kwa pamoja ili waweze kuwa na furaha katika Jumuiya yao, Kanda, pamoja na Parokia yao ya Kristo Mfalme, kwa ujumla.
Padri huyo aliwasihi Waamini wenye tabia za kujilimbikizia uongozi, waache kufanya hivyo, akisema kwamba baadhi yao wakipata uongozi, wanajiona ndiyo wameshafanikiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Mtakatifu Fabiano, Alfred Kunambi alisema kuwa kwa sasa Jumuiya yao ni changa ina miezi michache tangu Paroko wa Parokia hiyo awatangaze, bali wanaishi Ukristo wao kwa furaha.
Kunambi aliongeza kuwa mwaka huu mpya, Jumuiya yao imejipanga vyema, hasa katika mavuno ya Parokia na Jimbo, pamoja na kushiriki katika michango mbalimbali wanayoambiwa na Parokia yao.
Hata hivyo, aliwaomba Viongozi wa Vyama vya Kitume kila Parokia na Parokia Teule, kumuunga mkono Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi kwa kutoa michango yao ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa Kuu Mbadala la Gezaulole.

MOSHI

Na Mwandishi wetu

Watanzania wametakiwa kutoruhusu Vyama vya Siasa viwagawe na kuwafanya watengane kwa itikadi hizo, kwani sifa kubwa ya Taifa hilo, ni kuwa na amani.
Hayo yalisemwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria Mshindaji, Jimbo Katoliki la Kigoma, Padri George Muhanuka wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kumuombea marehemu Theresia Nicholaus Massawe, iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni – Kibosho- Singa, Jimbo Katoliki la Moshi.
Aidha, Padri huyo aliwasihi Waamini kuwa wamoja, huku wakiachana na tabia ya ubinafsi katika imani yao.
“Waamini, tujitahidi kuwa wamoja, tuachane na tabia ya ubinafsi katika imani. Lakini pia Vyama vya Siasa CCM, CHADEMA, au chama chochote kile, visitugawe katika umoja wetu tukiwa Watazania wenye amani,” alisema Padri Muhanuka.
Padri Muhanuka aliongeza kwa kusema, “Ndugu zangu Waamini tujiandae, hatujui muda wala saa tutakapoitwa na Mungu, maana tunakuwa Waamini wa Jumapili tu, wala hatupo kama Waamini wa kuwa na Mungu karibu.”
Padri huyo alisema pia kuwa Theresia Massawe enzi ya uhai wake, aliuishi Ukristo wake kwa imani moja ya Kanisa Katoliki, ambaye pia alikuwa mwanashirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, na alijiunga pia na Shirika la Mtakatifu Anna.
“Je, wewe Mwamini umejiunga na chama gani cha Shirika la Kanisa? Jitathmini Ukristo wako unaoishi kwa sasa, Mungu ametuleta hapa duniani ili tumtambue na tumtumikie, ili siku ikifika, tuwe mahali pa wokovu. Huyu mama aliishi kiukamilifu bila shaka lolote,” alisema Padri huyo.
Alibainisha pia kuwa Waamini wengi hawauishi Ukristo wao kikamilifu, kwa sababu ya kutangatanga katika Makanisa mbalimbali kutafuta miujiza.

DAR ES SALAAM

Na Jonas Abel

Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tanzania Revenue Authority: TRA), imesema kuwa mfumo mpya wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS), utarahisisha uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuingia ndani kwa haraka, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na watafanyakazi mchana na usiku.
Mfumo huo uliozinduliwa hivi karibuni, umebuniwa ili kuboresha ufanisi, kuhakikisha usahihi, na kupunguza ucheleweshaji katika shughuli za forodha.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha, Januari 26 mwaka huu, yenye kaulimbiu “Forodha itatimiza ahadi yake ya usalama na ustawi”.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alieleza maboresho makubwa yaliyofanywa kwenye mfumo huo alisema,
“Mfumo mpya wa TANCIS unatumia teknolojia ya akili bandia kwa ajili ya uchakataji wa data kwa usahihi, uwazi zaidi, na urahisi wa operesheni…TRA tumejipanga kuboresha mifumo yetu na taratibu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuboresha shughuli za forodha.”
Alisema kwamba mfumo ulioboreshwa, ambao ulianza kufanya kazi rasmi Januari 20, 2025, umekumbana na changamoto ndogo wakati wa uzinduzi wake wa awali. Hata hivyo, Kamishna Mkuu (Commissioner General) aliwahakikishia wadau kuwa mafundi wanashughulikia changamoto hizo kwa bidii.
Alisisitiza pia kuwa mfumo mpya utapunguza kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa ukaguzi wa mizigo na gharama zisizo za lazima, hivyo kuboresha ufanisi kwa ujumla.
“Ahadi yangu, pamoja na timu yangu, ni kuwa kuanzia Februari, mfumo huu ulioboreshwa utaanza kufanya kazi kikamilifu na kuwafaidisha watumiaji wote,” alisema, akibainisha kuwa maboresho hayo pia yatahakikisha thamani ya bidhaa inakokotolewa kwa haki na usahihi zaidi.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio, alionyesha matumaini kuhusu mfumo mpya wa TANCIS, akipongeza uwezo wake wa kuboresha ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa mapato.
“Tunaamini mfumo huu utaongeza uwazi na ufanisi,” amesema Urio. Hata hivyo, amekiri kuwa baadhi ya wanachama wamekumbana na changamoto, kama vile gharama za ziada kutokana na ucheleweshaji wa kuhifadhi na kusafirisha mizigo wakati wa awamu ya awali ya utekelezaji wa mfumo huo.
Kwa upande mwingine, Kamishna wa Forodha, Juma Bakari alisema kuwa mfumo mpya wa ukaguzi wa bidhaa umeboreshwa zaidi ukilinganisha na ule wa awali uliotumika tangu mwaka 2014.
“Unarahisisha shughuli za kibiashara, hasa katika uagizaji na usafirishaji wa bidhaa,” alisema Bakari.
Alibainisha pia kuwa mfumo huo unaziunganisha taasisi 36 zinazoweza kuutumia, hivyo kuboresha mawasiliano kati yao.
Aidha, alisema kwamba kutakuwa na matumizi bora ya taarifa, kwani data zitasimamiwa vizuri, hivyo kusaidia maafisa wa forodha na taasisi nyingine kufanya maamuzi sahihi.
Mfumo mpya wa TANCIS ni hatua muhimu katika kuboresha taratibu za forodha nchini Tanzania, kuhakikisha taifa linaendelea kufanikisha malengo yake ya usalama na ustawi.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakili wa Kujitegemea Dk. Aloys Rugazia amesema eneo la jinai la kubambikiwa kesi ni eneo linalosumbua watu wengi katika jamii.
Amesema kuwa Wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba hiyo ni changamoto wanayokutana nayo katika maisha yao.
Dk Rugazia (pichani) alisema hayo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam wakati wa maandalizi ya kutoa elimu ya sheria bure na kuandaa nyaraka katika kuadhimisha wiki ya sheria kwa lengo la kuwafikia wananchi ambao hawana fedha za kupata huduma za sheria.
“Tunapokutana na wananchi wanatueleza changamoto nyingi katika eneo la jinai kwamba kuna kubambikiwa kesi kuna kuonewa ndiyo maana tunawataka waje hapa tuwape elimu ya kutosha wajue haki zao ni zipi na watakiwa kufanya nini,” alisema Dk. Rugazia
Aidha, alisema changamoto nyingine ambayo wananchi wanapata ni eneo la ardhi na mirathi wajane, wazee na watoto yatima wanapata shida kupata haki zao za msingi kwa wakati.
“Ardhi ni maisha ni moja kati ya mali muhimu katika mustakabali wa watu mara nyingi ardhi imekuwa ikileta msuguano waliyonacho na wasio nacho, mara nyingi wanajikuta katika hali ngumu ndiyo maana kwa wiki hii tunatoa msaada bure watu waje,” alisema Dk. Rugazia.
Aliongeza kwamba wapo kwenye wiki ya sheria ambayo ilizinduliwa Januari 25, 2025 kwa kawaida wanaadhimisha kwa kujaribu kuifikia jamii kuhakikisha inapata haki kwa sababu sio kila mtu anauwezo wa kulipia gharama za kupata huduma za kisheria.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alianzisha mpango maalumu wa kusaidia wananchi wa Mama Samia Legal Aid, mkakati wa kutoa msaada wa kisheria kwa watu wanaishi kwenye jamii wenye kiu ya kudai haki ambao hawawezi kuipata.

Kisarawe

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Viwanda Dk. Selemani Jaffo ameiagiza Mamlaka ya Maji Vijijini (Ruwasa) kuchimba Kisima kirefu Kata ya Bwama iliyopo Wilayani Kisarawe, Mkoani Pwani.
Dk. Jaffo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe alitoa agizo hilo alipofika Bwama kwenye kuzindua Zahanati ya Bwama iliyogharimu Shilingi milioni 77/- hadi kukamilika kwake tangu ujenzi ulipoanza mwaka 2010.

DAR ES SALAAM

Na Salehe Said

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (United Nations: UN), Amina Mohamed ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mkakati wa kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia na utafutaji madini nchini.
Amina alitoa pongezi hizo hivi karibuni wakati wa mkutano wa pembeni wa Mkutano wa Nishati, alipokutana na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waandishi wa Habari wametakiwa kutumia vyema kalamu zao kuandika habari zenye ukweli, na si zenye kuwachafua wengine, kwani wana jukumu la kueneza ujumbe wa matumaini, upendo na amani.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Joseph Massenge, katika homilia yake wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa Wanamawasiliano wa Jimbo hilo, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bikira Maria, Mama wa Fatima, Msimbazi.
“Wanahabari tumieni vyema kalamu zenu kuandika habari zenye ukweli, epukeni kuandika habari zenye kuwachafua wengine. Mnatakiwa kueneza ujumbe wa matumaini, upendo na amani,” alisema Padri Massenge.
Padri Massenge ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tumaini Media, na Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu - Makongo Juu, alitoa wito huo kwa wanahabari kuhakikisha Injili inafika kwa kila kiumbe.
Ageukia utunzaji mazingira:
Aliwasihi kupitia kazi zao wanahabari hao wahamasishe pia kuhusu  utunzaji wa mazingira, kwani kwa kutunza mazingira, watakuwa wamepeleka Injili kwa kila kiumbe.
“Hakikisheni Injili inafika kwa kila kiumbe, siyo kwa kila binadamu tu, ni kwa kila kiumbe. Kupitia kazi zenu hizo, nendeni mkahamasishe pia kuhusu utunzaji wa mazingira…Tunzeni mazingira ili yawatunze, mkifanya hivyo mtakuwa mmetangaza habari njema kwa kila kiumbe,” alisema Padri Massenge.
Aidha, aliwasisitizia wanahabari hao kuepuka kuwa waandishi wenye kuandika habari zenye maslahi ya papo kwa papo, bali wafanye kazi zao wakizingatia maadili ya uandishi wa habari.
Padri Massenge aliwasihi wanamawasiliano hao kuwaombea waandishi wote waliotangulia mbele za haki kutokana na kazi zao, akiwataka kuendelea kusimamia ukweli katika uwajibikaji wao.
Padri Mujuni awafunda Waandishi:
Kwa upande wake, Padri Audiphace Mujuni, Padri wa Jimbo Katoliki la Bunda, anayechukua masomo yake katika fani ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT), Tawi la Msimbazi, jijini Dar es Salaam, alisema kwamba vyombo vya habari vina haja ya kuchangia kuleta upendo na mshikamano katika jamii.
Aidha, Padri Mujuni aliongeza kuwa waandishi wa habari ni vyombo vya matumaini katika ulimwengu, hivyo ni wajibu wao kufanya kazi kwa kufuata misingi inayowaongoza.
“Waandishi wa habari, tambueni kwamba ninyi ni vyombo vya matumaini katika ulimwengu. Kwa hiyo, ni wajibu wenu kufanya kazi kwa kufuata misingi na taratibu zinazowaongoza. Mnapaswa kuwa watumishi wa kweli, mkifahamu kwamba kila neno linaweza kuleta athari katika jamii,” alisema Padri Mujuni.
Aliwasisitiza wanamawasiliano kufanya kazi zao, huku wakimtanguliza Mungu, wakitambua kwamba uandishi wao usiwe sababu ya kuikosa mbingu.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, amewasihi Watawa kutambua kwamba wito ni zawadi ya thamani kutoka kwa Mungu, hivyo wasifanye mzaha.
Alisema hayo hivi karibuni  wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kupandishwa hadhi ya Utawa kwa Wapostulanti kuwa Wanovisi, iliyofanyika katika Kituo cha Kiroho -Mbagala, jimboni humo.
“Wito ni zawadi ambayo usipoitambua, utaipoteza, na baadaye utajutia, kwani utakuwa umepoteza tunu ya thamani zaidi kwa sababu ya kufuata mikumbo katika jumuiya, kwa kusikiliza maneno ya wengine na kusahau ulichoitiwa na Mungu, kwa sababu ya tamaa ya ulimwengu na uwongo wa watu wa nje,” alisema Askofu Musomba.
Aidha, alisema kuwa kuongoka ni kutoka katika fikra zisizo njema, na kuanza kufikiria mambo yanayofaa na kumpendeza Mungu, kwani hata Mtume Paulo aliyekuwa akiitwa Sauli, alikuwa ni mtu aliyewachukia Wakristo, na aliwatesa.
Na hata wakati mwingine alidiriki kuyabomoa makanisa, na hata alipokuwa njiani akielekea Damaskasi nchini Syria kuwatafuta Wakristo, ajabu alisikia sauti ikimwita ‘Sauli Sauli, mbona unanitesa’ na yeye hakutambua ni nani, na sauti imetokea wapi.
Aliendelea kusema kuwa ile sauti ilimjibu na kumwambia, Mimi ni Yesu; na baada ya kuingia Damaskasi, alibatizwa na kupewa maelekezo ya kulijenga Kanisa na kubadilishwa jina na kuitwa Paulo, badala ya Sauli.
Askofu Musomba aliwasihi Watawa wote kupenda kujitoa zaidi kwa kuwatumikia wengine kwa unyenyekevu mkubwa, bila kujibakiza wala kujali chochote au kusema wanaonewa na wengine au kuteswa, badala yake wanatakiwa kutambua wapo kwa ajili ya kutumwa, kwani waiitwa na wakaitika.
Askofu Musomba alisema umoja na upendo unaweza kuharibika kwa sababu ya udanganyifu na hisia, na kuwasihi kuwakemea Watawa wengine ambao watakuwa wanaenda tofauti na mapenzi ya Mungu, na kuwataka watambue wakifanya hivyo itawafanya waishi vizuri zaidi.
Aliendelea kusema kuwa Mungu hapendi kuona jumuiya yenye magomvi na masimango, wala kuona jumuiya ya watu wenye roho mbaya, badala yake wanatakiwa kutengeneza jumuiya yenye upendo na upatanisho.
Askofu Musomba aliwapongeza Wapostulanti watano kwa kuvuka hatua na kuwa Wanovisi, na kuwataka wawe ni watu wenye unyenyekevu na furaha kama ya wakati ule walipoandika barua ya kuomba kujiunga katika shirika, na kusikia wamekubaliwa ombi lao.
Askofu Musomba alisema kwamba ukiona mwenzako anafanya vibaya, alafu unampongeza na kufurahia ujue hiyo ni tabia mbaya, na kuwaasa wasidanganyike katika safari yao ya Utume bali wazidi kumwomba Mungu ili wazidi kukua kiimani.

DAR ES SALAAM

Na Rosemary Daniel

Imeelezwa kuwa Wakristo wengi wamekuwa na tabia ya kumiliki Bibilia nyingi kama fasheni, pasipo na faida yoyote katika maisha yao hasa kwa kuisoma, kuielewa na kupata ujumbe wa Mungu.
Hayo yalielezwa na Dekano wa Dekania ya Ubungo, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Gallen Mvungi wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu aliyoadhimisha katika Parokia ya Maria Mtakatifu, Kimara.
Padre Mvungi ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Utatu Mtakatifu, Changanyikeni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, alisema,
“Kuwa na Bibilia nyingi bila kusoma, siyo tija kama hatujitaabishi na kijibidiisha kuisoma, kuelewa na kupata ujumbe wa Mungu. Unakuta Mkristo ana Bibilia nyumbani, kwenye gari, kwenye mkoba na hata ofisini kwake, ila imekaa kama pambo tu bila kusomwa.”
Padri Mvungi (pichani) alisema kuwa Wakristo wengi hawampatii Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yao, bali wanamweka Mungu kama pambo la kuthibitisha kile wanachokifikiri.
“Pale tunaposoma na kuyaelewa Maandiko Matakatifu, huwa yanapenya ndani kabisa na kuichoma mioyo yetu na kuinua Imani yetu, ndipo tunapopokea majibu ya maombi yetu, njia zetu za kiimani zinafunguka na kuleta amani na uzima tele,”alisema Padri Mvungi.
Alisema kuwa Maadiko Matakatifu pia yanafundisha, kuonya, kurekebisha na kuasa wanadamu waliokengeuka kwa namna ya kipekee kulingana na karama na vipawa vyao, na jinsi walivyoguswa na maandiko hayo.
“Ndani ya Maandiko Matakatifu, jumbe tofauti ambazo zinamgusa Mkristo mmoja mmoja kulingana na kipawa na karama yake kwa jinsi Mungu alivyomjalia, kama vile kila kiungo kilivyo na kazi yake katika mwili wa binadamu,”aliongeza kusema Padri Mvungi.
Alisema kwamba endapo Wakristo hao watakapoyaelewa na kuyashika Maandiko Matakatifu ya Mungu,hakika hawawezi kudanganyika, na wala Ulimwengu hautawahadaa kwa kutafuta mambo ya kidunia, kukimbilia makanisa mengine kutafuta miujiza.