Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliendelea kuwaletea historia ya Uasi wa Martin Luther na historia ya maisha yake ya uasi.
Leo tunaendelea kuwaletea historia ya uasi wa Luteri hata kwa Shirika lake, na mafundisho yake ya dini. Sasa endelea…
Februari 3, mwaka 1518, Luteri aliitwa na Mkutano Mkuu wa Shirika lake, lakini kwa kulindwa na Frederick, hakuudhiwa na hata ndugu zake wengine shirikani walimshangilia.
Tarehe 16/05/1518, Luteri akiogopa kutengwa na Kanisa, alihubiri akipinga uwezo wa Papa kumtenga Mkristo.
Hapo Papa alimwita afike Roma kwa hukumu, lakini Frederick wa Saxony, aliweza kumfanya Papa akubali, asikilizwe huko huko Ujerumani na Kardinali Kajetani.
Luteri alikataa kuacha uzushi, na baadaye akakimbilia kwa Frederick asikamatwe. Bahati mbaya Papa hakufanya lolote, akihofia kupoteza urafiki wa Frederick.
Mambo yalifikia kilele mwaka 1519, Luteri alipobishana na Mdominikani makini sana John Eck, aliyemzidi akili na utundu.
Kabla ya hapo, Luteri alikuwa akijificha katika maneno magumu ya teolojia, lakini sasa ilibidi aseme wazi, kujibu maswali makali ya John Eck.
Pale alikiri, mawazo yake na kusema kwamba, siyo tu Papa lakini hata Mtaguso Mkuu, unaweza kufanya makosa na mtu binafsi akaupinga.
Sasa ikawa wazi kwamba, ni mzushi na vyuo vikuu vikubwa vikamkana kama mzushi. Ni tokea wakati huo, sasa Luteri akahesabika rasmi kama mzushi katika Kanisa.
Tarehe 15/06/1520, Papa Leo X, alituma hukumu ya kumtenga na Kanisa kwa Luteri, akimpa siku 60 akane uzushi.
Luteri badala ya kukana uzushi, akaichoma ile hukumu hadharani, kama dharau kwa Papa. Mwaka 1521, aliitwa na Mfalme Mkuu Karoli V, kukana uzushi na alipokataa alihukumiwa, lakini akakimbizwa na Frederick na kufichwa.
Wakati huo, ambapo Mfalme Mkuu Karoli angefuatilia kwa matendo, ilimbidi aondoke haraka kurudi Hispania kwa shida maalumu.
Hispania ilikuwa ikigombana na Ufaransa, na wakati huo huo Waturuki walitaka kuiteka Ulaya. Mfalme Mkuu Karoli, hakuweza kurudi Ujerumani mpaka baada ya miaka 9, yaani mwaka 1530.
Katika muda huo, Luteri aliachwa kueneza mafundisho yake, kwa sababu hakuna mwingine ambaye angelimsema au kumshika, kwa sababu alilindwa na Frederick wa Saxony.