Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

VIWAWA wapata viongozi wapya wa Taifa

Na Mathayo Kijazi

Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) ngazi ya Taifa, kimefanya Uchaguzi Mkuu, na hivyo kuwapata viongozi wapya, watakaoongoza chama hicho hadi mwaka 2029.
Akizungumza hivi karibuni, katika Mkutano wa makabidhiano, uliofanyika katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwenyekiti mpya wa VIWAWA Taifa, Elia Mshana, alisema kwamba Dira Kuu waliyonayo ni kumjenga kijana mwenye nafasi katika jamii na katika Kanisa.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa walezi, wanaowalea vijana hao kuanzia ngazi za Parokia pamoja na Majimbo, kuwapa nafasi vijana katika Halmashauri za Walei, kwani wanaweza kufanya kazi katika maeneo hayo.
“Wito wangu kwa walezi wanaowalea vijana, kuanzia ngazi za Parokia mpaka Majimbo, Wakurugenzi wote wawape nafasi vijana. Lakini pia katika Halmashauri za Walei kwenye Parokia zao, vijana wapewe nafasi kubwa zaidi, kwa sababu wakiaminiwa wanaweza,” alisema Mwenyekiti, Elia Mshana.
Aliongeza kwamba, imekuwa ni desturi ya Viongozi wa VIWAWA Taifa, kukutana Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kufanya makabidhiano kati ya Viongozi Wastaafu na Viongozi wapya, kwa ajili ya kuanza rasmi majukumu yao ya kiuongozi.
Mwenyekiti huyo aliwashukuru viongozi waliomaliza muda wao, kwani wamefanya kazi kubwa, katika kipindi chote cha uongozi wao, wakiahidi kwenye kuendeleza yale yaliyoanzishwa na uongozi uliopita.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mstaafu VIWAWA Taifa, Mwalimu Leonard Mapolu, alimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufanya shughuli zao za kitume, katika Chama hicho tangu walipoanza mwaka 2023 mpaka 2026.
Mwalimu Leonard Mapolu kutoka Jimbo Katoliki la Shinyanga, ambaye pia ni Mratibu wa VIWAWA Afrika, alisema kwamba katika utume wanashirikishwa, hivyo wana wajibu wa kutii na kufuata miongozo ya Kanisa, lengo likiwa ni kumpeleka Kristo kwa wengine.
Pia, alitoa wito kwa vijana kuendelea kushiriki Makongamano mbalimbali ya Kanisa, pamoja na Semina pale wanapopata nafasi, kwani kupitia matukio hayo, wanapata utatuzi wa changamoto zao.
Mwalimu Mapolu alitoa wito kwa Viongozi wapya wa VIWAWA, kuendeleza mradi wao wa kitenge cha VIWAWA, hasa katika kukizalisha kwa ubora mzuri, kwani kwa kufanya hivyo, watakiendeleza vema Chama hicho.
Naye Katibu Mstaafu wa VIWAWA Taifa, Benedict Agustino, alimshukuru Mungu kwa kutumikia katika mihula miwili, ambapo alianza mwaka 2020–2023, kisha 2023-2026, akisema kuwa katika vipindi hivyo, walijitahidi kutekeleza majukumu yao kama ilivyokusudiwa.
Kwa mujibu wa Benedict, miongoni mwa miradi waliyofanikiwa kuitekeleza, katika kipindi cha uongozi wao, ni pamoja na kununua shamba la VIWAWA, lenye ukubwa wa ekari 50, lililopo katika Jimbo Katoliki la Singida, pamoja na shamba jingine lililopo Kibiti, ndani ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.