Dar es Salaam
Na Nicolaus Kilowoko
Mkurugenzi wa Utawala wa Shirikisho la Mpira wa Wavu Tanzania (TVF) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Riziki Godwin, amekiri kuwa miundombinu waliyoiweka kwa sasa hasa mara baada ya kuupata Uwanja wa Mwembeyanga, imechangia kwa kiasi kikubwa uimara wa mchezo huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Riziki alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na Ligi ya Wavu ambayo kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa sana kutokana na timu ambazo zimekubali ushiriki wake na hilo linatokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya uwanja ambapo hapo awali ilikuwa ni changamoto kubwa kwao.
Alisema ushindani wa ligi hiyo ambayo kwa sasa inaendelea umeongezeka, kwanza ni kutokana na timu shiriki kutamani kuonesha uwezo na mabadiliko yao kutokana na ligi hiyo inafanyika kila mwaka hapa nchini.
Aliongeza kuwa mbali na hilo, ligi hiyo inatumika kwa kuandaa timu wakati wa mashindano ya msimu ujao hivyo hata ushindani wake umeongezeka kiasi kikubwa na timu zinaelewa kabisa kama zitashindwa kufanya vizuri kwa sasa zitakuwa na wakati mgumu msimu ujao wa ligi hiyo.
Riziki alisema ubora wa viwanja mara ya kwanza ulikuwa kikwazo kwa timu kuonesha uwezo wao lakini kwa sasa wanajivunia kuona maendeleo makubwa yanafanyika katika timu hizo.
















