Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mshambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda, amefunguka juu ya ukweli wa maisha yake binafsi, huku akiweka wazi kuwa malengo yake ya kwanza yalikuwa ni kuwa Mhandisi, lakini mwisho wa siku mambo hayakwenda vile ambavyo alikuwa anataka.
Nyota huyo (pichani) ambaye anamudu uwanjani kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati na pembeni alisema kuwa mwanzo alikuwa anataka kuwa Mhandisi kabla ya soka kummbadilishia mwelekeo na hatimaye akaacha kile alichokuwa anatamani kukifanya.
Musonda alisema kuwa alitakiwa kwenda chuo kwa ajili ya kusomea Uhandisi, lakini soka lilimbadilishia mfumo wa maisha na sasa amekuwa mfumania nyavu uwanjani.
“Mwanzo nilitakiwa kwenda chuo kusomea Usanifu wa Majengo, lakini mpira ulinipa mwelekeo mwingine wa maisha ndiyo kama hivi kwa sasa, nachezea Yanga”, alisema Musonda.
Kuhusu kazi yake na majukumu yake uwanjani kama mchezaji sasa wa Yanga, Musonda amepanga kufunga mabao zaidi na kuisaidia Yanga kushinda kila mchezo wake msimu huu.
Lakini, kwa upande mwingine Musonda alifunguka juu ya ugumu anaoupata wa namba tangu asajiliwe ndani ya Yanga huku akiweka wazi kuwa juu ya mkanganyiko wa mashabiki wake, wanaojiuliza juu ya kwa nini hafunguki akiwa na Yanga huku kwenye timu yake ya Taifa akifunga.
Musonda alisema kuwa kwenye timu yake ya Taifa, anapata nafasi sana na ndiyo maana anafunga sana, lakini kwa upande wa klabu imekuwa tofauti, kwani hapati nafasi sana. Mpaka sasa amecheza mara 20 pekee, hali inayopelekea kupata changamoto ya kupachika mabao.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakati wa kufanyika kwa droo na hata baada ya kuanza kwa michuano ya Afrika ambayo Simba na Yanga wanashindania Ubingwa, mashabiki wengi na wadau wa soka walikuwa na maoni tofauti juu ya timu zao wakizichambua katika viwango vya juu, lakini kwa sasa hali imekuwa tofauti, kwani maji na unga vimeanza kujitenga.
Mpaka sasa bado mambo hayajaenda sawa kwa klabu za Tanzania ambazo zinashindana katika michuano hiyo ya Afrika msimu huu, tofauti na ilivyotarajiwa.
Simba inashiriki Kombe la Shirikisho kutokana na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita, huku watani zao klabu ya soka ya Yanga ikishiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika, na hii ni baada ya kuwa Mabingwa msimu iliopita katika Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya soka ya Simba, Ismail Aden Rage, aliweka wazi kuwa klabu ya soka ya Yanga bado hawajawa katika kiwango bora kama walivyokuwa katika misimu miwili ya nyuma na hilo limechangia kuwepo kwenye nafasi waliyopo sasa.
Rage alisema na kuweka wazi mara baada ya kufanya tathmini yake katika mchezo wao uliopita waliocheza katika dimba la Benjamini Mkapa, akidai kuwa walipata nafasi nyingi za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo dhidi ya wapinzani wao TP Mazembe.
Alisema kuwa bado Yanga wana safu mbovu ya ushambuliaji ambayo inawasababisha washindwe kupata matokeo chanya kwenye mechi zake msimu huu.
Yanga ilipata ushinda wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, iliyochezwa Jumamosi, Januari 4 mwaka huu.
Kuhusu Simba, Rage alisema kuwa, bado inajitafuta, japokuwa imefanya vyema katika michezo yake mitatu kati ya minne, ambayo mpaka sasa imeshacheza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, wakipata ushindi huku wakifungwa mchezo mmoja.
Watanzania wengi bado hawana matumaini ya dhati juu ya klabu hizo kutokana na nafasi walizokuwa nazo kwenye misimamo ya makundi yao, huku kwa sasa ni mahesabu ya vidole tu ndiyo yaliyobaki.
Yanga kwa kuchechemea katika michezo minne, ameshinda mchezo mmoja, akipata sare mchezo mmoja huku akifungwa michezo miwili, na amekusanya alama nne, akishika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi lake michuano ya Klabu Bingwa Afrika, hatua ya makundi.
Simba nayo ni kama wanaingia wanatoka, kwani katika michezo minne, ameshinda michezo mitatu, akifungwa mchezo mmoja, akijikusanyia alama tisa, akishika nafasi ya pili kwenye hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Timu zote hizo zinatarajiwa kutupa karata zao nyingine katika viwanja vya ugenini January 12 ambapo klabu ya Simba watawafuata Bravos ya Angola huku klabu ya soka ya Yanga ikiwafuata Al Hillal ya kutokea kule Sudan.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akiwa katika picha ya pamoja na Kamati Tendaji ya Parokia ya Mtakatifu Cesilia, Kisarawe II, jimboni humo. Kulia kwa Askofu ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Roger Kamuzinzi, na kushoto ni Paroko Msaidizi. (Picha na Yohana Kasosi)

Waamini wa Parokia ya Bikira Mama wa Kanisa, Goba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Krismas iliyoadhimishwa hapo hivi karibuni.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akibariki matoleo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Noeli katika Parokia ya Mtakatifu Agustino – Salasala. Kushoto ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter Assenga. (Picha na Mathayo Kijazi)

Padri Denis Kunambi, Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam akikabidhi vitendea kazi kwa Kamati Tendaji ya Kigango cha Kuzaliwa Bikira Maria, Kisukuru, Parokia ya Roho Mtakatifu, Segerea, wakati wa Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kigango hicho.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba -OSA, akimbatiza mtoto Kiernani James katika Parokia ya Mtakatifu Boniventura, Kinyerezi jimboni humo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ambapo watoto 93 walibatizwa, na Watoto 43 walipata Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. (Picha na Yohana Kasosi)

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akiumwagia maji mti baada ya kuupanda katika Parokia ya Mtakatifu Cesilia, Kisarawe II, Kigamboni jimboni humo. Wengine ni Mapadri, Viongozi wa Halmashauri ya Walei, na baadhi ya Waamini. (Picha na Yohana Kasosi)

Baadhi ya Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu-Mtume, Kijitonyama, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakitoa sadaka kwa Mtoto Yesu katika Pango alimolazwa, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Mkesha wa Krismas parokiani hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA) wametakiwa kujadiliana na kupambanua kuhusu mambo msingi, ili waendelee kuwa nguzo imara katika Kanisa.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri Vincent Sabiit –SDS, wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Siku ya UWAKA (UWAKA Day) Parokia ya Mtakatifu Polycarp Askofu na Shahidi – Kilamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Ipo haja ya UWAKA kujadiliana na kupambanua juu ya mambo mbalimbali yenye tija, ili muendelee kuwa nguzo imara katika Kanisa...
“Katika kujadiliana huko, ipo haja ya kujadiliana pia kuhusu mambo yanayomhusu Mungu, ikiwemo kuwatia moyo wale wote wanaochechemea kiimani,” alisema Padri Vincent.
Padri huyo aliwasihi UWAKA kutenga muda na kuamua kujadili mambo yenye tija, huku wakiepuka kuwa na mijadala inayosababisha mipasuko na huzuni katika maisha ya watu.
Pia, aliwasisitiza kusaidiana wao kwa wao, huku wakihakikisha pia wanawasaidia vijana, hasa wale wanaosumbuliwa zaidi na malimwengu katika maisha yao.
“Sisi kama UWAKA tunaposherehekea leo, tunapaswa kujiuliza kwamba, je, kweli sisi ni nguzo imara? Je, sisi ni nguzo iliyosimama sawasawa au imeelemea upande mmoja na inataka kuanguka?
“Tukumbuke kwamba tunalo jukumu kubwa la kuendelea kujadiliana juu ya mambo yaliyo mema, ili tuzidi kuwa nguzo imara katika Kanisa letu na katika familia zetu, na pia kuweza kuwa na vijana bora watakaolisaidia Kanisa letu siku zijazo,” alisema Padri huyo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Kilamba, Padri Timothy Nyasulu Maganga alimshukuru Padri Vincent kwa homilia yake aliyoitoa katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Padri Nyasulu aliwashukuru UWAKA kwa kufika kwa wingi katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu, akiwasihi kuendeleza umoja na mshikamano wao, ili kuendelea kukuza chama hicho cha kitume parokiani hapo.
Naye Mwenyekiti wa UWAKA Taifa, Cassian Njowoka, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika siku hiyo ya UWAKA Parokiani hapo, aliwapongeza wana UWAKA wa Parokia hiyo kwa kuandaa Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Siku yao.
Njowoka aliwashauri wanaume kujiunga na chama hicho cha kitume cha UWAKA, kwani kuna faida kubwa watakazozipata ndani ya chama hicho, ikiwemo kusaidiana wakati wa magonjwa na matatizo mengine.
Vile vile, alitumia nafasi hiyo kuwaasa Wanaume Wakatoliki na Waamini wengine, kushiriki katika suala zima la Uchaguzi Mkuu mwaka ujao 2025, ikiwemo kujiandikisha na kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaowaongoza.
Aliwasisitiza pia kuwaunga mkono Waamini wenzao pale wanapohitaji kugombea nafasi wanazozihitaji, kwani kwa kupitia viongozi hao, watampeleka Kristo katika nafasi watakazozipata.
“Kwa hiyo, tunaaswa na Mababa tujitokeze, tujiandikishe kwa wingi, tupige kura, na kama una sifa ya kupigiwa kura, jitokeze ugombee. Na kama tunaona mwenzetu amejitokeza anataka kugombea nafasi fulani, ‘tum-support’ tusianze kupambana naye, ili ampeleke Kristu katika nafasi ambayo yeye atakuwa ameipata,” alisema Mwenyekiti huyo wa UWAKA Taifa.
Aliongeza kwamba Mungu Mwenyezi amewapa Wakristo Wakatoliki uwezo mkubwa wa kutambua mambo mbalimbali, hivyo yeyote atakayejitokeza, awe mwanaume au mwanamke, ana haki ya kuungwa mkono katika nafasi anayowania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWAKA Parokia ya Kilamba, Venance Kavishe, ambaye pia ni Mwenyekiti UWAKA Dekania ya Mbagala, alimshukuru Padri Timothy Nyasulu Maganga kwa kuendelea kuwaunga mkono katika kila wanalolifanya wana UWAKA parokiani hapo.