Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Joyce Sudi

Wasimamizi wa Vijana Waimarishwa wametakiwa kuwasimamia vizuri ili waweze kukua kiimani na kimaadili.
Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Pili ya Majilio ya Mwaka C wa Kanisa, sambamba na utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa Waimarishwa 185 wa Parokia ya Mtakatifu Bonaventura, Kinyerezi, jimboni humo.
Askofu Mchamungu alisema Wasimamizi wa Ubatizo na Kipaimara, wanalo jukumu la kusimamia watoto ili wakue kiimani hadi watakapokuwa watu wazima.
Kwa mujibu wa Askofu Mchamungu, Waimarishwa hao wa  Sakramenti Takatifu ya Kipaimara wanapaswa kuwa na mahusiano mazuri na Wasimamizi wao, na wanapopata nafasi, wanatakiwa kwenda  kuwasalimia.
Aidha aliwasihi Waimarishwa hao, kuendelea kusali na Waamini wenzao katika makusanyiko ya kanisani na Jumuiya, kwa kuwa wapo baadhi wakishapata Sakramenti hiyo, hawaonekani tena kwenye nyumba za ibada.
“Kila mtu anajua kuwa hataishi milele, hivyo mjitahidi kutubu kila wakati, na kuishi vizuri ili inapofikia siku ya mwisho, msiwe na mateso na mahangaiko,”alisema Askofu Mchamungu.
Alibainisha pia kwamba kwa bahati mbaya, ufahari wa dunia hii hawaondoki nao, wahangaikie roho zao kwa kuwa na mahusiano mazuri na Mwenyezi Mungu.
Askofu Mchamungu aliwataka Waimarishwa hao kabla hawajatoka kitandani wamshukuru Mungu na kuomba Baraka zake, na wajibiidishe katika shughuli mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu utunzaji mazingira, Askofu Mchamungu alisema kuwa vijana hao na Waamini kwa ujumla, wanatakiwa kutunza mazingira, kupitia Waraka wa Baba Mtakatifu Fransisko wa Laudato Si.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Bonaventura, Kinyerezi, Padri Francis Hizza, alisema kuwa neema waliyoipata Waimarishwa hao, ni kubwa, hivyo wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu,wazazi na walezi wao, pamoja na Wasimamizi ambao wamekubali kubeba dhamana ya kuwakuza kiroho.
Padri Hizza alisema kwamba wazazi wanatakiwa kuwahimiza watoto wao kwenda kanisani ili waweze kukua vyema kiroho, kiakili na kimwili, kwani mafanikio yoyote,  ikiwemo ya elimu kwani vyote hivyo chanzo chake  ni Mungu.
Aidha, amewataka Waamini wanaposubiria kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo, wajitayarishe na wafurahie ndani ya mioyo yao, wakijua kwamba anayekuja ni Mfalme na mwenye uweza wa yote.

ROMBO

Na Mathayo Kijazi

Watawa wa Kike wametakiwa kuendeleza karama walizojaliwa nazo, ili kila mmoja aweze kupokea baraka zaidi kupitia karama alizo nazo maishani mwake.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Mhashamu Agustine Shao, alipokuwa akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Masista 39 wa Shirika la Bibi Yetu wa Kilimanjaro (CDNK Sisters), iliyoadhimishwa katika Kanisa la Nyumba ya Asili - Huruma Convent, Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi.
Wakati huo huo, Askofu Shao aliwataka Masista wale ambao ni waalimu, waepuke kuwachapa watoto viboko kupitiliza, bali wawafundishe kwa upole na kwa unyenyekevu, kwani kuwaelimisha siyo lazima kutumia viboko.
“Kwa hiyo, jitahidini sana kuziendeleza karama zenu mlizojaliwa nazo, ili kupitia karama hizo, kila mmoja aweze kupokea baraka zaidi katika maisha yake,” alisema Askofu Shao, na kuongeza…
“Masista waalimu, msiwatandike watoto kupitiliza, waelekezeni kwa upole na kwa unyenyekevu, kwa sababu kuwaelimisha siyo lazima mtumie viboko.”
Aidha, aliwataka Masista hao kufahamu kwamba Jubilei haiwezi kuwa Jubilei kama hawataingia ndani sana, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wengine, na kuwasamehe wale waliowakosea.
Pia, aliwasisitiza kulichukua jukumu la kuishi kama wawekwa wakfu, ikiwa ni pamoja na kuishi maisha yanayompendeza Mungu, kwani hilo ndilo jukumu lao baada ya kuweka Nadhiri zao za Daima.
Vile vile, alilipongeza Jimbo Katoliki la Moshi kwa kuendelea kuzalisha Watawa wengi, akiwasihi wazazi na walezi kuendeleza malezi kuendelea kuwapata Watawa wengi zaidi.
Kwa upande wake Mama Mkuu wa Shirika hilo la Bibi Yetu wa Kilimanjaro (CDNK Sisters), Sista Theresia Buretta aliwashukuru wazazi wa Masista hao, kwani wazazi ndio waliwalea katika malezi ya kumpendeza Mungu tangu wakiwa wadogo.
Aliongeza kwamba uwepo wa Masista waliomshukuru Mungu kwa Miaka 25, 50 na 60 ya Utawa, kwao ni jambo la furaha, huku akimshukuru Askofu Shao kwa kusafiri kutoka Zanzibar hadi jimboni Moshi kuadhimisha Misa hiyo Takatifu.

Dar es Salaam

Na Laura Chrispin

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amesema kuwa Taifa kwa sasa linapitia kipindi kigumu, kwani kimejaa vilio na wasiwasi mwingi kutokana na vitendo vya watu kutekwa na kuuawa, na miili yao kutupwa.
Kardinali Pengo alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyoadhimishwa Parokia ya Ekaristi Takatifu-Keko Jimboni humo.
“Kipindi tunachopitia sasa kimejaa vilio, wasiwasi na huzuni, kwani watoto na watu wazima wanatekwa, kuteswa na kuuawa. Imefika hatua unatafuta wapi tunaokota mwli wa mtu ambapo hiyo hali hatukuwahi kiiona na hatujaizoea,”alisema Kardinali Pengo.
Akizungumza kuhusu Waimarishwa, Kardinali Pengo, alisema kwamba Wanakipaimra hao wamekubali kuimarishwa, hivyo yawapasa wawe tayari kusikia sauti ya Kinabii na nguvu ambayo inatokana na Sakramenti ya Kipaimara.
Kardinali Pengo aliendelea kusema kwamba vijana hao wanatakiwa kuwa tayari kusikia sauti ya Kinabii ndani yao, kwani Mitume wa mwanzo hawakuwa jasiri wa kutangaza habari njema kwa watu, ndiyo maana walijificha ndani kwa hofu ya Manabii, lakini baada ya kushukiwa na Roho Mtakatifu, walikuwa jasiri kwani walitoka nje na kuanza kufundisha habari njema kwa Mataifa yote Ulimwenguni.
Aidha, aliwasihi Waimarishwa hao kukabiliana na dhambi binafsi, na zile watu wanazotumia kuongozea taifa.
Kardinali Pengo alitoa wito kwa Waamini wote kuwa bega kwa bega na Waimarishwa kwenye kazi zao za kiutume.
Kwa upande wake Katibu Crinton Mushi, alimshukuru Askofu Mstaafu kwa kutoa Sakramenti hiyo, kwa Vijana 13.
Aidha, alimwomba Kardinali Pengo kuwasaidia kuzirudisha Jumuiya zilizochukuliwa na Parokia za jirani ya Kurasini na Chang’ombe.
Naye Paroko wa Parokia hiyo, Padri Meinrad Bigirwamungu Kalikawe, alimshukuru Kardinali Pengo kwa kuadhimisha Misa hiyo kwenye Parokia ya Ekaristi Takatifu.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Makatekista wa Dekania ya Pugu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wameaswa kuishi maisha ya utakatifu ili wawe mfano bora kwa wengine.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma Mji Mpya Relini, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Pius Thomas -MSFS, ambaye ni Mlezi wa makatekista wa Dekania hiyo.
Padri Pius  alisema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani ya Makatekista wa Dekania ya Pugu, kumshukuru Mungu kwa kuumaliza salama mwaka 2024, na kuukaribisha mwaka 2025, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Thomas Mtume-Chanika, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Kila Katekista inampasa atembee zaidi Kisinodi akiufuata mfano bora wa maisha ya Mama Bikira Maria, ambaye mara zote anawasaidia kutenda kazi za uinjilishaji, kwani ninyi mliitwa na mkaitika kwa kazi ya Mungu,”alisema Padri Pius.
Aidha, alisema kuwa hata Mama Bikira Maria alikubali maagizo aliyopewa na Malaika kwani aliitika na kusema,  ‘Mimi mjakazi wa Bwana, nitendee kama ulivyo nena,’ aliendelea kusema Maria alitambua kuwa ile ilikuwa ni kazi ya Mungu, na siyo ya malaika.
Padri Pius aliwataka Makatekista hao kutambua kwamba Bikira Maria, alikubali kila mtu aige mfano bora wa maisha yake kwa kutazama zaidi fadhila za Kimungu.
Kwa mujibu wa Padri Pius Makatekista hao wanatakiwa kufahamu kuwa Kipindi cha Majilio, kila mtu anatakiwa kutafakari na kujiuliza, je anawajibika kama Bikira Maria? Na kumshukuru Mungu kwa kuhitimisha mwaka 2024 na kuomba baraka na neema kwa mwaka ujao 2025.
Aidha, Padri Pius alitoa wito kwa Makatekista hao kutambua kwamba wao ni mzizi wa imani wa Kanisa Katoliki hivyo, hawatakiwi kuwa kikwazo kwa wengine, au chanzo cha kuwapotosha watu katika imani ya Kanisa Katoliki.
Aliwasihi Makatekista hao, kumkabidhi maisha yao Bwana Mungu, ili waweze kupata fadhili zake, wakiendelea kufundisha habari njema kwa watu, wakiliongoza Kanisa, kwani wao ndio wenye kumkuza mtu katika imani tangu kuzaliwa hadi kufa.
“Bikira Maria anafundisha unyenyekevu na utii, na huo huo unauona hata kwa Yesu kwa kutii na kukubali kunywa kikombe cha mateso, na unyenyekevu huo unang’aa ndani yake,”alisema Padri Pius.
Alitumia nafasi hiyo, kuwataka Makatekista kumshukuru Mungu na kumwomba Mama Bikira Maria, kama mwombezi wao, hata katika wakati mgumu pasipo kukata tamaa.
Naye Katibu wa Makatekista Dekania ya Pugu, Katekista Gerald Shukuru, aliwashukuru Makatekista kwa ushirikiano wao.

BAGAMOYO

Na Mathayo Kijazi

Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), wametakiwa kufahamu kwamba kushiriki Hija, ni kukutana na Mungu, waongee naye, wamshirikishe shida zao.
Hayo yalisemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Hija ya WAWATA, iliyoadhimishwa katika Kituo cha Hija - Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro.
“Ndugu zangu wapendwa, tumekuja kufanya Hija hapa Bagamoyo kama WAWATA. Tumekuja kwenye Hija hii, lengo ni kukutana na Mungu katika mazingira haya ambayo ndipo Injili iliingilia kwetu Tanganyika,” alisema Askofu Musomba, na kuongeza…,
“Tunakutana na Mungu huyu ili tuongee naye, tumshirikishe shida zetu, tumshirikishe mambo ya familia zetu, tumshirikishe juu ya udhaifu wetu tulio nao, na tutafakari pamoja naye imani yetu, hasa katika tathmini kwamba tupo katika njia sahihi, au tumepotea, au tuna mahangaiko, au tumekengeuka, yeye mwenyewe atunyanyue na atuinue ili atuweke sehemu nzuri. Tumjue vizuri, tumtambue vizuri katika maisha yetu.”
Sambamba na hayo, Askofu Musomba aliwataka WAWATA kufahamu kwamba Hija hiyo waliyoshiriki siyo utalii, bali ni jambo la kiroho zaidi, kwani wanakutana na Mungu wanayemtafakari katika maisha yao.
“Na kwa sababu hiyo, Hija hii siyo utalii, ni jambo la kiroho zaidi. Mungu huyu tunayekutana naye, ni yule ambaye kwanza tunamtafakari katika maisha yetu, tunamtafakari katika roho zetu, na hivyo tunaingia kwake katika utulivu.
“Tunatambua kwamba ndiye aliyetuumba, tunatambua kwamba ndiye aliyeumba kila kitu. Kwa hiyo katika Hija, tunawiwa kumtambua zaidi na kumjua zaidi. Tumpende na kumtumikia ipasavyo tukiwa na lengo la kwenda kwake, ndiyo maana ya Hija hii kumwelekea yeye,” alisema Askofu huyo.
Pia, aliwataka WAWATA hao kutoukaribia uovu, ikiwa ni pamoja na kushawishika kwenda kwa waganga wa kienyeji, kwani katika Hija hiyo wapo katika mazingira ambayo Injili iliingilia.
Sambamba na hayo, aliwasisitiza kuendelea kumjua Mungu kwa kusoma Maandiko Matakatifu, kusoma Mafundisho ya Mama Kanisa, pamoja na kuyafuatilia inavyotakiwa.
Pia, aliwaasa kushiriki vizuri katika Liturujia za Mama Kanisa, kwani katika hiyo, wanaadhimisha maisha yao wenyewe pamoja na imani yao.
Katika homilia yake, Askofu Msaidizi Musomba aliwataka WAWATA kuendelea kusikiliza yale wanayoshauriwa na wenzao, pamoja na kuyachanganua, kwani kuna faida kubwa ya kupata mawazo mapya katika maisha.
“Tuendelee kusikiliza kila mara wenzetu wanatushauri nini katika maisha yetu, na vile vile kuchanganua kwamba rafiki wa kweli anatuongoza. Rafiki anayesema acha kusali, huyo siyo rafiki, na wala siyo wa kweli. Lakini yule anayesema tusali Rozari, tutafakari maisha ya Yesu na Mama Bikira Maria, huyo ndiye rafiki wa kweli,” alisema Askofu Musomba.
Kwa upande wake Mlezi wa WAWATA Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Joseph Mosha, ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas wa Akwino – Chuo Kikuu, alimshukuru Askofu Msaidizi Musomba kwa kuadhimisha Misa hiyo, na kusema kwamba kwa muda mrefu walikuwa wanatamani wawe na Askofu katika Maadhimisho ya Misa hizo.
“Nichukue nafasi hii kumshukuru Baba Askofu kwa kutuongozea Ibada ya Misa Takatifu, imepita miaka kadhaa tulikuwa tunakosa Maaskofu wa kutusindikiza, lakini mwaka huu tunashukuru sana Baba umetusindikiza, wakinamama wamepata nguvu kweli kweli, asante sana Baba,” alisema Padri Mosha.
Naye, Mwenyekiti wa WAWATA jimboni humo, Stella Rwegasira aliwataka wanawake wenzake kutambua maana ya Hija pamoja na umuhimu wake, akiwasihi kuepuka kuifananisha Hija na safari nyingine za starehe.
“Tumepata mada inayohusu Hija, tumeweza kujua Hija maana yake nini, maandalizi yake yaweje, na kwamba tumefundishwa Hija siyo ‘piknik’, na Hija siyo kuja kuogelea, kwa mfano tunaokuja Bagamoyo…
“Kuna wenzetu wengine pia wamepata bahati ya kwenda Hija za nje ya Nchi, na kuna wengine ambao walijua wanakwenda ‘shopping’, ingawa kuna wakati fulani nilipata kesi, lakini haikufanikiwa, kuna mtu anakwenda Hija halafu anataka kuzamia, sasa wakiwa kule wanapiga simu, ‘Mama… kuna WAWATA wako huku,’ sasa kama wewe ni mama, ukienda kuzamia huko, huwi tena hujaji, unakuwa mama ni wale WAWATA wako,” alisema Stella Rwegasira, Mwenyekiti huyo wa WAWATA.
Stella Rwegasira alimshukuru Askofu Musomba kwa kuadhimisha Misa hiyo Takatifu, akiwashukuru pia Mapadri, WAWATA, pamoja na wote walioshiriki katika Adhimisho hilo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddeus Ruwa’ichi, amewataka Waamini kujitathmini kikamilifu maisha yao, kama ni kweli ya Ukristo au ya ubabaishaji.
Wito huo aliutoa hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, iliyofanyika parokiani hapo.
Askofu Ruwa’ichi alisema kuwa Mungu anampenda kila mmoja, na wala hana ubaguzi, chuki, lakini Waamini ndio wenye kumchukiza Mwenyezi kwa mambo mabaya wanayofanya.
Askofu Ruwa’ichi aliwasihi Waamini hao kuhakikisha wanabadilika na kuwa Wakrito wema, na wenye kupenda maendeleo ya Kanisa lao.
“Mimi na ninyi Wanaparokia hii ya Mtakatifu Nicholaus ni mapacha, pia ni ndugu, Mimi nilipata Daraja Takatifu la Uaskofu siku moja, na ninyi mnatangazwa kuwa Parokia, hongereni sana,”alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo,Padri Faustino Maganga, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kukubali mwaliko wao, na kufungisha ndoa hizo.
Padri Maganga alisema kwamba amepokea maagizo yote ya  Askofu Mkuu, na atajitahidi kuleta maendeleo katika Parokia hiyo.
Katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia hiyo, Askofu Ruwa’ichi alifungisha Ndoa jozi 10.

KHARTOUM, Sudan
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabaraza ya Maaskofu Wanachama Afrika Mashariki (AMECEA), Askofu Charles Sampa Kasonde ametoa wito kwa Makongamano ya Wanachama kuwasilisha Nchi ya Kaskazini -Mashariki mwa Afrika, ya Sudan, mbele ya Bwana ili amani na upatanisho viweze kutawala.
“Kwa mshikamano na Kanisa linaloteseka na watu wa Sudan, ninawasihi kwa unyenyekevu na Maaskofu wote wa mkutano wenu kujitolea sala maalum kwa ajili ya amani na upatanisho nchini Sudan. Tuombe Mungu aingilie kati vita hivi, aponye madonda ya migawanyiko, na kurejesha maelewano katika taifa hili lenye matatizo,” Askofu Charles Sampa Kasonde alishiriki katika ujumbe wake alioutoa kwa uongozi wa makongamano katika kanda ya AMECEA.
Rufaa hiyo inakuja kufuatia shambulio la hivi majuzi dhidi ya Askofu Yunan Tombe Trille Kuku wa Jimbo Katoliki la El-Obeid, na Shemasi waliojeruhiwa vibaya na Vikosi vya Haraka.
“Tunasikitishwa sana na taarifa kwamba Neema yake Askofu Mkuu wa Khartoum (Askofu Mkuu Michael Didi Adgum Mangoria) bado hawezi kuishi katika Jimbo lake Kuu kutokana na vita,” Askofu Kasonde wa Jimbo Katoliki la Solwezi, nchini Zambia alisimulia, kisha akafichua.
Taarifa zinaeleza kuwa mzozo wa zaidi ya mwaka mmoja nchini Sudan ulianza Aprili 2023, kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), ambapo tangu wakati huo, watendaji mbalimbali duniani kote wamekuwa wakishirikiana kuelekea kupatikana kwa suluhu endelevu kwa nchi yenye matokeo machache.

JUBA, Sudan Kusini

Askofu Yunan Tombe Trille Kuku wa Jimbo Katoliki la El-Obeid nchini Sudan, ameelezea uzoefu wake wa kiwewe kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea katika nchi hiyo ya Kaskazini-Mashariki mwa Afrika, kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Katika ujumbe wake, Askofu huyo (pichani) pamoja na Shemasi Joseph, walieleza jinsi walivyonyanyaswa na wanajeshi walipofika El-Obeid kutoka sehemu isiyojulikana, wakisema:
“Pamoja na shemasi, tulikosa kifo cha kishahidi pale kiongozi mmoja aliposema inatosha! “Nimefika tu El Obeid pamoja na Shemasi Joseph, Wakati huu, nilitendewa vibaya,” Askofu huyo alisimulia akirejelea tukio hilo alipokutana na wanajeshi wa Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ambao wamekuwa kwenye vita tangu Aprili 2023.
Alisema kuwa kwa upande wa Vikosi vya Haraka, alipigwa mapigo mengi mazito kwenye shingo, paji la uso, usoni, pamoja na pande mbili za kichwa chake.
Aliongeza kwamba hivi majuzi, wajumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Sudan na Sudan Kusini (SSSCBC) walilalamika kwamba mzozo huo wa muda mrefu umesababisha uhalifu wa kutisha wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na pande zote mbili, na hivyo kupelekea watu wa nchi hiyo inayokabiliwa na mzozo kupata maafa ya kibinadamu.
Pia, alibainisha kuwa tabia ya jamii ya Sudan imesambaratika, huku watu wakishtushwa, wametiwa kiwewe, na kutoamini kiwango cha jeuri na chuki, ambapo Maaskofu walifichua katika ujumbe wao katikati ya mwaka huu na kufafanua kwamba vita si kati ya majenerali wawili tu, kwani jeshi limejikita katika maisha ya kiuchumi ya nchi, na SAF na RSF kila moja ina mtandao wa matajiri wasomi wa Sudan na watu binafsi na mashirika ya kimataifa.

NAIROBI, Kenya

Afisa wa Shirika la Kikatoliki la Maendeleo ya Nchi za Nje (CAFOD), Mwila Mulumbi (pichani) amesema Kanisa linatakiwa kuweka mikakati zaidi katika utetezi ili kudumisha mamlaka yake ya kimaadili katika jamii.
Akizungumza katika kongamano la siku mbili la Kukuza Maendeleo ya Kibinadamu (PIHD), katika Jumuiya ya Mabaraza ya Maaskofu Wanachama Afrika Mashariki (AMECEA), Mwila alisema kuwa mamlaka ya kimaadili ina haki ya kujitolea kwa dhati kuchukua jukumu la kimkakati zaidi katika utetezi.
Alisema kwamba kushindwa kushughulikia masuala hayo, ikiwa ni pamoja na ajira kwa watoto, dawa za kulevya, ukosefu wa ajira kwa vijana, itikadi za kijinsia, misimamo mikali ya kidini, ubaguzi wa kikabila, ubaguzi wa afya ya akili kunaweza kusababisha watu kuhisi Kanisa halina umuhimu.
Taarifa zinaeleza kuwa masuala hayo pia yanapinga imani na mila za muda mrefu ndani ya Kanisa, na zinaathiri moja kwa moja jumuiya na ustawi wa wao binafsi.
Akiwaasa washiriki zaidi ya 30 waliokusanyika kwa ajili ya mkutano huo katika Roussel House Donum Dei, Nairobi, Kenya, Bi. Mulumbi alisema kuwa Kanisa linafaa kuchukua mtazamo ulioratibiwa zaidi, unaoeleweka, na wenye kusudi na washirika ili kushughulikia masuala hayo kwa ushawishi zaidi na kupata athari chanya.
Katika mada yake ya Novemba 28 iliyoitwa “Mkakati wa Kukumbatia Utetezi Katika Kushirikiana na Washirika na Kujibu Mahitaji ya Kanisa”, Bi. Mulumbi aligusia kuwa upinzani dhidi ya mitazamo ya imani, upinzani wa kisiasa na upinzani wa umma, ni miongoni mwa mengine yanayoweza kujitokeza.
Ili kukabiliana na changamoto ya mitazamo ya imani inayopingana, Afisa huyo wa CAFOD mwenye makao yake mjini Lusaka, Zambia alisema Kanisa linahitaji kushirikiana na mashirika ya kiekumene yenye nia moja au vikundi vinavyoshiriki malengo sawa na kukusanya rasilimali, maarifa, na mitandao kwa ajili ya matokeo makubwa.
Aliongeza kuwa Kanisa linaweza kuwezesha mazungumzo ambayo yanahimiza uelewano kati ya watu kutoa taarifa tofauti.
Kwa kutokuwa na imani na Serikali, alisema kuwa Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwashirikisha Viongozi wa Kisiasa wanaoaminika na kuonyesha faida za utetezi ili kujenga imani na Serikali.
Bi. Mulumbi alisema zaidi kwamba Kanisa linapaswa kushirikiana na wataalamu na kuwekeza katika tafiti za kina, ili kuziba mapengo ya maarifa.
Afisa huyo wa CAFOD alisema kushirikiana kwa ajili ya utetezi wa kimkakati ni muhimu, kwani Kanisa haliwezi kushughulikia masuala ya kijamii pekee.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amehimiza kazi ya Washiriki wa Kongamano la Pili la Ekaristi Kitaifa lililofanyika nchini Rwanda, kuwa Ishara ya Matumaini inayoonekana, baada ya Mungu wa Utatu na asili yake ya uhusiano.
Papa aliyasema hayo katika Ujumbe wake uliotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, akihimiza kazi ya washiriki wa Kongamano la Pili la Ekaristi Kitaifa, na kwamba ndani yake watu katika jumuiya wanakusanyika, wakivunja vizuizi vya rangi, lugha au utamaduni, na kuwa Wamisionari wa udugu.
Katika Ujumbe ulioelekezwa kwa Askofu Vincent Harolimana wa Jimbo Katoliki la Ruhengeri, na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Rwanda (Episcopal Conference of Rwanda: CEPR), kwa ajili ya Kongamano la II la Ekaristi Takatifu kitaifa, Baba Mtakatifu Fransisko anaungana kwa furaha na shukrani za Waamini wote wa Kikristo nchini humo.
Katika ujumbe wake huo kwa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Rwanda, Baba Mtakatifu Fransisko alisisitiza juu ya uwajibikaji kwa kukabiliana na njia ya kimwili na hadhi ya binadamu.
Akitazama Kaulimbiu ya Kongamano hilo isemayo “Tumkazie macho Yesu katika Sakramenti ya Ekaristi: chemchemi ya matumaini, udugu na amani”, Papa Fransisko alibainisha kuwa inatoa fursa ya kutafakari Ushirika, ambacho ni kitovu cha maisha yote ya Kikristo, na ishara inayoshikika ya upendo wa Kristo kwa wanadamu wote.
Baba Mtakatifu aliwahimiza Waamini kujitoa kama zawadi kwa wengine, huku wakifanya kazi kwa makubaliano ya pamoja, ili kujenga ustaarabu wa upendo.
Kwa kuzingatia Jubilei na Miaka 125 tangu uinjilishaji ulipoanza nchini Rwanda, Baba Mtakatifu Fransisko aliwaalika Waamini wote nchini humo kuanza tena kwa Kristo na mkate wa uzima, huku akisisitiza kuonesha mshikamano kwa yeyote anayejikuta katika mazingira magumu.
Baba Mtakatifu alibainisha kuwa Ekaristi inakumbusha wajibu wa kawaida kuelekea mahitaji ya kimwili na ya kiroho ya binadamu, huku ikichochea matumaini katika Utatu.