Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amewataka Waamini kuwahubiria maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa uhuru wao.
Aliyasema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, katika Dominika ya Januari 26 mwaka huu wa 2025, ambapo ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Dominika ya VI ya Neno la Mungu iliyoanzishwa na Papa mwenyewe mwaka 2019.
Aidha, katika fursa hiyo, ilitolewa pia Huduma ya Usomaji wa Neno la Mungu kwa waamini 40 kutoka mataifa mbalimbali duniani, ambayo pia ilikuwa ni Adhimisho la Misa Takatifu ya Kufunga Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano, iliyoanza tangu Januari 24 kwa ufunguzi wa Misa.
Katika homilia yake Baba Mtatifu Fransisko alisema kuwa Injili waliyoisikia katika Adhimisho hilo inatangaza utimilifu wa unabii unaofurika katika Roho Mtakatifu, na yule anayeitimiza ni Yeye ajaye kwa nguvu za Roho.
“Neno la Mungu liko hai, linatembea nasi kwa karne nyingi, na kupitia nguvu za Roho Mtakatifu linafanya kazi katika historia. Bwana kiukweli siku zote ni mwaminifu kwa ahadi yake, ambayo huiweka kwa sababu ya upendo kwa wanadamu. Hivi ndivyo alisema Yesu katika sinagogi la Nazareti. Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” alisema Baba Mtakatifu.
Baba Mtakatifu alisema kuwa ni bahati iliyoje yenye furaha katika Dominika ya Neno la Mungu, ambapo bado wakiwa mwanzoni mwa Jubilei, ukurasa huo wa Injili ya Luka unatangazwa, ambamo Yesu anajidhihirisha kuwa Masiha aliyewekwa wakfu kwa kupakwa mafuta na kutumwa kutangaza mwaka kwa neema ya Bwana.
Papa alisema kuwa katika Dominika hiyo iliyowekwa maalum kwa ajili ya Neno la Mungu, ni wajibu wa kila mmoja kumshukuru Mungu kwa kuwa amewaelekezea Neno lake lililomfanya mtu kwa wokovu wa ulimwengu.
Aliongeza pia kuwa hilo ndilo tukio ambalo Maandiko yote yanazungumza juu yake, ambayo yana watunzi wao wa kweli, yaani watu na Roho Mtakatifu, na kwamba Biblia nzima inamkumbuka Kristo na kazi yake, na Roho hufanya uwepo katika maisha yao na katika historia.
“Tunaposoma Maandiko, tunapoomba na kuyasoma, hatupokei  habari kuhusu Mungu tu, bali tunamkaribisha Roho ambaye hutukumbusha yote ambayo Yesu alisema na kutenda (Taz Yh 14:26). Hivyo mioyo yetu, ikiwa imewashwa na imani, inangojea kwa matumaini ujio wa Mungu,” Papa alisema.
Aliongeza kuwa kila mwamini lazima awe na mazoea zaidi ya kusoma Maandiko, na kwamba katika hilo, alipendekeza tena kuwa kila mtu awe na Injili ndogo mfukoni ya Agano Jipya, na kubeba katika mfuko, na wakati wa mchana kuisoma.

MOROGORO

Na Angela Kibwana

Mpendwa msomaji, katika mfululizo wa makala haya ya “Wajibu wa Kanisa kwa Watu Wenye Ulemavu katika Huduma za Kiroho,” Makala yaliyopita yalianza na kuonesha kwamba Kanisa kama Jumuiya ya Waamini wanaomwamini Kristo, msingi wake ni Kristo mwenyewe ((Waefeso 5: 29; Wakolosai, 1: 24 na Wakolosai 2:10).
Katika kulithibitisha hilo, makala hayo yalionesha namna Yesu Kristo mwenyewe alivyokasimisha majukumu yake  ya  kulihudumia Kanisa  la hapa duniani  kupitia Mtume Petro, na msingi huo huo ndiyo asili ya uwepo wa  Kanisa Katoliki ((Mathayo, 16:18).
Makala hayo yalisisitiza kwa kuwa Yesu Kristo ndiye msingi wa Kanisa, Kanisa la duniani halina budi kuyaishi maneno, matendo pamoja na kuubeba wajibu ambao Yesu Kristo aliukasimisha kwa Kanisa la hapa duniani, kama ilivyothibitishwa kupitia Biblia Takatifu na mafundisho ya mama Kanisa.
Makala hayo pia yalisisitiza kuwa Kanisa kama Jumuiya ya Waamini wanaomwamini Kristo, Waamini wake wanayo mahitaji tofauti, ambayo ndio msingi wa ustawi wao, kiroho na kimwili.
Makala hayo yakaangazia ni kwa namna gani Kanisa la hapa duniani linaweza au linayatafsiri mahitaji hayo katika utekelezaji wa majukumu yake kiroho na kimwili, pasipo kumwacha Waamini yeyote ambaye ni mwili na Kielelezo cha Kristo nje ya huduma hizo. “Waamini wenye ulemavu na mahitaji yao ya kiroho, ndio ukawa msingi wa makala hayo.”
Katika makala ya toleo hili, tunaendelea kuangazia hali ya upatikanaji wa huduma za kiroho ndani ya Kanisa Katoliki kwa watu wenye ulemavu, pasipo kuyatenga makundi mengine ya watu wenye ulemavu. Makala haya yatajikita kwa undani zaidi kwenye vikwazo vya mawasiliano kwa kundi la watu wenye ulemavu wa kuongea na kusikia, ili kuweka usawa wa kihuduma kiroho, kiafya,kijamii na kimtazamo pia.
Kutokana na takwimu za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 nchini Tanzania, kati ya watu wote wenye ulemavu, ulemavu wa kuona,kusikia, kuongea na kutembea ni 6.5% ya Watanzania wote, ambayo ni sawa na jumla ya watu 3,154,514kuanzia umri wa miaka saba (7)na kuendelea pasipo kujali dhehebu au dini ya mhusika, kwa hiyo kutokana na hali zao watu hawa wanahitaji mipango na mikakati maalum ya kuwafikia kwa huduma za kimwili, kijamii, kiafya, kielimu na kiroho pia.
Mpendwa msomaji wa makala haya katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma za kiroho leo hii nitaangazia wajibu huo kuanzia katika msingi wa familia na  jumuiya ndogondogo za Kikristu.
Kanisa Katoliki linajengwa kuanzia ngazi ya familia halafu jumuiya  ndogondogo za Kikristu ukiwa ni mwito wa kuwakaribisha watu wote  katika jamii ya waamini wanao mwamini Kristo kuwa Kristo ndiyo  kichwa na mwili wa kanisa
Katika waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho, tunakumbushwa kuwa mwili wa Kristo una viungo vingi, na kila kimoja kina thamani na nafasi yake (1 Kor. 12:12-27).
Hili ni somo muhimu linalotufundisha kuwa hakuna anayepaswa kuachwa nyuma katika mpango wa wokovu, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu kwa ujumla.
Huduma za kiroho kwa watu wenye ulemavu wa kusikia ni mwaliko wa dhati wa kuhakikisha kwamba kundi hili linaloshiriki kikamilifu katika maisha ya kiroho ya jumuiya, ikiwa ni haki yao ya kimsingi kama waamini na wana wa Mungu, ambao walibatizwa na kuwa sehemu ya familia ya Kanisa.
Kwa msingi huu, huduma hizi zinapaswa kuwekwa kama kipaumbele katika jitihada za Kanisa za kujenga jumuiya ndogondogo zinazojumuisha watu wote kuanzia ngazi ya familia bila ubaguzi unaotokana na hali zao.
Jumuiya za Kikristo, hasa ndani ya mazingira ya Parokia, zina jukumu la kutambua kuwa ulemavu wa kusikia,kutembea, kuongea au kuona, siyo kikwazo kwa imani, badala yake, ni fursa ya kuthibitisha wito wa Kanisa wa kuwa sauti ya matumaini na mshikamano kwa kundi hilo.
Maandiko Mtakatifu, mfano Warumi, 15:1, inaonesha jinsi ambavyo wana Kanisa wanavyoitwa kuwa na moyo wa huduma na kusaidia wale walio na udhaifu wa aina yoyote, ikiwemo ulemavu.”Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wa wanyonge, wala si kujipendeza wenyewe.”
Kanisa Katoliki linapofanya sensa kujua idadi ya waamini wake, kadhalika sensa hiyo inapaswa kuwajumuisha watu wenye ulemavu ili kujua idadi yao, taarifa na mahitaji yao ili yatafsiriwe katika huduma za kiroho na huduma nyingine.
Kadhalika, Kanisa lina wajibu wa kuandaa mwongozo kwa watu wenye ulemavu, ambao utaonesha namna ya kuwafikia kuanzia ngazi ya familia, jumuiya Ndogo Ndogo,Parokia na taasisi zake  kwa ujumla, ili waweze kupata huduma za kiroho, ikiwa ni pamoja na kuwalinda kwa sababu Kanisa nalo lina wajibu wa kulinda haki kwa maisha ya kila binadamu.

Mzungu hajakubali kuwa bin-Adam wote ni sawa, wala kwamba wote ni wa baba mmoja,  Adam.
Pamoja na kwamba alituletea Msahafu wa dini – Biblia wenye kusisitiza “upendo,” hiyo ni ghiliba tupu kwa sababu inawabagua wana-Adam kati ya walio wana wa Taifa teule la Mungu (Israeli), na wana wa Mataifa yasiyo teule. Huko ni kukweza ngozi nyeupe.
Kwa kutumia Mungu wa kujiundia (Yahweh) na Msahafu wa kibeberu, wanaidhinishwa kutugeuza watumwa wao, eti kwamba:
“Na wageni watakuwa watumwa wa kulisha mifugo yenu; na wana wa Mataifa watawalimia na kutunza mashamba ya mizabibu yenu”. Huo ndio ubaguzi wa ubeberu wa kimataifa ambao umedumu hadi leo.
Ubaguzi huo kwa misingi ya rangi ulioasisiwa, kusimikwa na kukomazwa Kimataifa na Mjerumani Johann Friedrich Blumenbach (1752 – 1840) unawagawa bin-Adam kwa viwango vya ubora katika makundi sita ya Watu weupe (Coucassians) kama daraja la kwanza; Wamongolia (Mongoloid) daraja la pili; Watu weusi (Ethiopoid); Wamarekani wenye asili ya Kihindi (Red Indians) na Wahimalaya (Malayans) kama daraja la mwisho kwa ubora.
Wamefika mbali kwa kudai kuwa Mwafrika si Mwana-Adam, yaani hakuzaliwa na Adam. Dhana hiyo mpya inayoitwa “Pre-Adamisma inadai kuwa Mwafrika alikuwepo kabla ya kuumbwa Adam na alikuwa kiumbe asiye na roho.
Mwasisi na Mwenezi wa dhana hiyo inayoshika kasi kipindi hiki cha utandawazi ni Mfaransa Isaac La Peyrere (1596 – 1676). Dhana hiyo inapinga usahihi wa Biblia juu ya uumbaji, ikidai kuwa kulikuwa na watu kabla ya kuumbwa kwa Adam na Hawa.
Anasema kwamba kulikuwa na uumbaji mbili za watu: uumbaji wa kwanza ulikuwa wa dunia nzima na Mwafrika kama mtu wa kwanza; na uumbaji wa pili ulihusu Wayahudi kama Taifa ambalo Adam alikuwa mkuu wake.
Anadai kuwa, Mataifa yote hayatokani na Nuhu, kwamba watu wa Mataifa (wasio wa Taifa teule) hawakutenda wala hawahusiki na dhambi ya asili kwa sababu walikuwepo kabla ya Adam, na hivyo hawakupokea “Sheria” au Maagizo ya Mungu, bali ni Adam na uzao wake pekee. Chini ya dhana hiyo Wazungu ni Wana-Adam, na Mwafrika siye.
Dhana hii ina watetezi wengi miongoni mwa Mataifa ya Ulaya: Mathew Fleming Stephenson, katika kitabu chake “Adamic Race” anasema, “Mungu alitumia mamilioni ya miaka kuumba mtu duni (Mwafrika) kabla ya kuumba mtu bora aina ya Mzungu (Caucasian) juu yake”. Wengine, kwa kutaja wanataaluma wachache tu, ni pamoja na John Harris (The Pre-Adamite Race), Isabelle Duncan (Adamites and Pre-Adamites), na wengine.
Iwe ni kwa mtizamo wa dhana ya “Pre-Adamite”, “Uumbaji” au “Mageuko” (evolution), hakuna ubishi mpaka sasa, kwamba binadamu (mtu) wa kwanza aliishi Loliondo/Ngorongoro zaidi kabla ya mwaka 10,000, Kabla ya Vizazi (KV) ambao ndio mwaka unaosemekana Adam aliumbwa.
Ustaarabu wa mtu huyu ulianza na shughuli za Kilimo, ufugaji, ibada na makazi eneo ambalo sasa linajulikana kama Nubia, au Sudan Kaskazini. Utawala wa kwanza ulianzia Ta-Seti eneo hilo; watu hawa walijulikana kama “Anu”.
Nchi waliyokalia ilijulikana kwa majina mengi, kama vile, Nubia, Kermet, Kush, Ethiopia au Egypt (Misri) na Mji Mkuu ulikuwa Kerma. Nubia imetajwa kwenye Biblia, Kitabu cha Mwanzo 2:11 kama nchi ya Havillah.
Ni Ufalme ulioundwa na watu weusi kutoka eneo la Maziwa Makuu (ANU) miaka ya 5900 Kabla ya Vizazi (KV) na maelfu ya miaka kabla ya Kristo (KK). Hapa ndipo Gharika (la Nuhu) lilipowakuta watu hawa, wakaangamia isipokuwa mtu mmoja – Nuhu na wanae watatu – Yafeti, Shem na Hamu. Hiyo ilikuwa Mwaka 5000 KK. SOMA ZAIDI KWA KUNUNUA TUMAINI LETU.

VATICAN

Na Angela Rwezaura

Kitabu hiki kinapatikana katika lugha ya Kijerumani, ambacho kinasimulia historia ya Ukristo katika dunia.
Kitabu hicho kimeeleza kwa kina kuhusu safari za Papa Fransisko alizotimiza nchini Iraq mwaka 2021, na kuhusu diplomasia ya Vatican katika nchini Iraq.
Matthias Kopp ni mwandishi na Mtaalimumgu ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini Ujerumani.
Desemba mwaka 2024, Baba Mtakatifu Fransisko alimteua kuwa mshauri wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano.
Dibaji ya Papa Fransisko:
Kwa shukrani ya kumbukumbu ya ziara yangu ya kitume nchini Iraq, ambaye licha ya janga la Uviko 19, na mashaka ya usalama, nilitimiza ziara hiyo kunako Machi 2021 ili kueleza kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema katika Nchi hiyo, upendo wangu na mshikamano wangu.
Nchi hiyo inachukua nafasi daima na kila wakati katika moyo wangu katika sala.
Licha ya matatizo mengi ambayo Iraq inakabiliana nayo, ninatazama  Nchi hiyo kwa matumaini, kwa sababu inayo nguvu maalum.
Nguvu hiyo awali ya yote, ni watu hao hao  nchini Iraq, wale wote wanaoshiriki ujenzi wa jamii ya raia, ambao wanahamasisha demokrasia katika Nchi na ambao wanajibidiisha kwa ajili ya mazungumzo ya wazi na ya kweli kati ya dini.
Kwa njia hiyo, ziara yangu kwa Mkuu Ayatollah wa Najaf, Sayyid Ali Al-Sistani, ilikuwa muhimu na ya maana. Mkutano ule ulikuwa unataka kuwa alama kwa ulimwengu wote kwamba : kufanya vurugu katika jina la dini, ni matumizi mabaya ya dini.
Kama watu wa dini, tunawajibika kuelekeza amani, na lazima kuiishi, kufundisha na kuieneza amani hii.
Katika muktadha huo ninafikiri hata ziara yangu huko Ur, Kusini mwa Iraq, kwa maana kama wawakilishi wa dini mbali mbali, tulizungumza na kusali pamoja, chini ya maelfu na maelefu ya nyota zilizotazamwa na  baba yetu Ibrahimu alipoinua macho yake angani.
Urithi wa utajiri katika historia ya Bimillenaria del Cristianesimo kisayansi, karibu haijavumbuliwa.
Ninafikiri shule za kiteknolojia za Wakristo wa kwanza wa Mesopotamia, uwepo wa amani kwa mamia ya miaka kati ya Wakristo, na Waislamu kati ya Eufrate na Tigri, na tamaduni mbali mbali za ibada ya Kikatoliki katika kanda.
Aidha, mapambano kati ya Madhehebu ya Kikristo, katika nyakati za mateso mwanzoni mwa karne ya 20,  na visasi vingine vya kisiasa  na kwa mwendelezo wa uwepo wa Kikristo, hadi sasa.
Haya yote yanapendeza kwamba katika kazi ya Matthias Kopp, urithi huu na historia hiyo inakuja kuonesha katika muktadha wao mafunzo ya kidini, katika wingi na kwa kuzingatia fasihi nzito.
Mwandishi kwa namna ya pekee anaweka umakini katika jitihada za Kikanisa nchini Iraq na katika shughuli za Vatican,  kwa wawakilishi wake wa kidiplomasia, ambao wanamulika uhasishaji mwingi wa Mapapa kwa ajili ya Iraq na Wakristo wanaoishi ndani mwake.
Kwa njia hiyo, imezaliwa zawadi kama anavyoandika mwandishi mwenyewe, kwa Wakristo nchini Iraq, ambao ninawatia moyo kujihusisha kwa kina zaidi utajiri wao mkubwa wa kihistoria na kudumisha uhai wa urithi wao:
Kwa wakati ujao ambao hata leo hii unahatarishwa kwa sababu ya uhamiaji na ukosefu wa uhakika kisiasa.
Ninataka kueleza kwa kina na kuamini kwamba  haiwezekani kufikiria Iraq bila Wakristo, kwa sababu pamoja na Waamini wengine wote wanawakilisha kwa nguvu utambuzi maalum wa Nchi, ambao tangu karne za kwanza pamekuwa ni mahali pa kuishi, kuvumiliana na kukubaliana wao kwa wao.
Kwa hiyo, Iraq inaweza na kwa watu wake, kuonekana, katika Mashariki ya Kati na katika Ulimwengu kwamba inawezakana kuishi pamoja kwa amani, licha ya tofauti zao.

MOROGORO

Na Angela Kibwana

Katika nyumba moja huko Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, Lucy Patrick (siyo jina lake halisi), mfanyakazi wa majumbani, anajikuta akifanya kazi kwa saa 18 kila siku, bila kupumzika.
Hajawahi kulipwa mshahara wake wa miezi mitatu, sasa, ambapo malengo yake ya awali ilikuwa ni kujiongezea kipato kusaidia familia yake na mara nyingi anakula mabaki ya chakula cha familia.
Kwa muda mrefu, sauti yake haikusikika, lakini sasa, juhudi za Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki (CWW) zimeanza kuleta matumaini kwake baada ya kutoa mafunzo ya kuboresha mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi.”
Wafanyakazi wa majumbani wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo kutolipwa mishahara inayoendana na kazi zao, kunyimwa chakula, kupigwa, na kudhulumiwa haki zao za msingi.
Aidha, wengi wao hawana mikataba ya ajira, jambo linalowafanya kukosa ulinzi wa kisheria, hivyo wanajikuta wakifanya kazi kwa mazingira magumu bila msaada wowote wa kisheria au kijamii.
Victor Mackyao, mwanasheria na mwezeshaji wa mafunzo yaliyoandaliwa na (Chama cha Wafanyakazi Majumbani: CWM), anasema kuwa wafanyakazi wa majumbani, mara nyingi hawajui sheria za ajira, wala haki zao za msingi.
Wafanyakazi wa majumbani wengi wao ukiwauliza wanasema wanakumbana na vipigo, wananyanyapaliwa, wanatengwa,wanateswa maeneo wanayoishi siyo rafiki, wanakosa fursa ya matibabu wanapougua, wengine kukosa chombo maalum cha kuwasemea” alisema Mackyao.
Alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwaelimisha wafanyakazi hao wa majumbani ili kujua nini maana ya haki, lakini pia waajiri watambue wajibu wao ni upi kwa wafanyakazi hao ili kujenga usawa katika makundi yote mawili.
Alifafanua kuwa moja ya changamoto zinazochangia wafanyakazi hao wa majumbani kukosa hali zao msingi ni kutokana na vyombo au mamlaka mbalimbali ambazo zina dhamana ya kuwasimamia haki zao, kutowafikia kwa wakati kwa sababu wafanyakazi hao wanatoka kwa waajiri tofauti na maeneo tofauti.
Alisema kuwa tangu Cwm ilipoanza kutoa mafunzo hayo wamebaini kwamba baadhi ya wafanyakazi wa majumbani wanapohojiwa, ambao wanakaa kwao nje ya mwajiri wake, baada ya kuulizwa, wamedai kwamba wanalipwa kiasi cha shilingi elfu 30 au 50, wakati sheria inamtaka alipwe kuanzia 120,000/=.
“Wafanyakazi ambao wanakaa kwa waajiri wao sheria inawataka walipwe shilingi elfu 60, lakini hawalipwi kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo changamoto hizo ndizo zilizotufanya tuweze kupita na kutoa elimu kwa jamii lakini tutoe rai na tuviombe vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia masuala ya wafanyakazi wa majumbani, waweze kutumia mbinu kama tunazotumia sisi, ili waweze kuwafikia kujua changamoto zao na kazitatua wasikae tu mijini.”
Alisema kwamba kazi za majumbani si rahisi, na sheria inakataza ajira ya watoto katika kazi hizi kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, Sura ya 13, Hata hivyo, bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,
Kwa kutambua changamoto hizi, CWM jimbo la Morogoro limeanza kutoa mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi wa majumbani katika Dekania ya Kilosa.
Kwa mujibu wa CWM, kati ya wafanyakazi 161 waliopata mafunzo, asilimia 70 hawakuwa wanajua haki zao za msingi, na wala hawajui lolote kuhusu haki yao ya kuwa na mikataba ya kazi, ili kulinda haki zao.
Lengo ni kujenga mahusiano bora kati ya waajiri na wafanyakazi wa majumbani, kwa kuhakikisha haki na wajibu vinazingatiwa pande zote mbili.
Mratibu wa CWM, Edson Yeyeye, alisema kuwa mafunzo haya yalianza mwishoni mwa mwaka 2024 katika Dekania za Kihonda, Morogoro mjini, na sasa yamefikia Kilosa. Tayari wafanyakazi 161 na waajiri 62 wamepatiwa mafunzo hayo, huku Viongozi wa Dini na serikali 27 wakiungwa mkono katika juhudi hizi.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mfanyakazi wa majumbani anapata elimu ya haki zake na waajiri wanajua wajibu wao,” alisema Yeyeye.
Bahati Ramadhani, mmoja wa waajiri walioshiriki mafunzo hayo, alisema, “Ni muhimu elimu hii kufika vijijini kwa sababu huko ndiko wafanyakazi wengi wa majumbani wanatoka, Wengi wanapokuja mjini, wanakosa haki zao kwa sababu hawana mikataba wala hawajui sheria”.
Maria Chalalika, mshiriki mwingine, aliongeza kuwa kunahitajika kuundwa vyombo maalum vya kushughulikia haki za wafanyakazi wa majumbani, hasa kwa wale wanaopelekwa nje ya nchi, bila kujua wanachokwenda kukifanya
Kwa upande wake, Hosea Nikodemas Mgunda, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani Boma, aliwapongeza CWM kwa juhudi zao za kutoa elimu hiyo kwa jamii, ili haki za wafanyakazi wa nyumbani ziweze kulindwa na kuthaminiwa.
“Wafanyakazi wa majumbani wanapitia madhila mengi, hivyo tunahitaji kuwa na chama chao maalum ili kuwatetea na kuhakikisha wanapata haki zao.ili kupunguza vitendo vya ukatili miongoni mwao
Hata hivyo, Mgunda aliahidi kutumia mikutano yake ya kijamii kutoa elimu kuhusu haki za wafanyakazi wa majumbani ambavyo anatarajia kufanya kuanzia tarehe mosi Februari mwaka huu 2025.
Mafunzo haya yameongeza uelewa miongoni mwa wafanyakazi na waajiri, ambapo wengi wao sasa wanatambua umuhimu wa mikataba ya ajira, haki ya likizo, na mishahara inayotambulika kisheria.
Hata hivyo, changamoto bado zipo, hasa katika kuwafikia wafanyakazi walioko maeneo ya vijijini, na wale wanaofanyiwa ukatili wa kimya kimya.
Washiriki wa mafunzo hayo walipendekeza kuundwa kwa vyombo maalum vya kushughulikia haki za wafanyakazi wa majumbani, Kuongeza uhamasishaji kuhusu sheria za kazi vijijini na mijini, Kuwapatia wafanyakazi wa majumbani elimu ya malezi na maadili, kwani mara nyingi wao ndio walezi wa karibu wa watoto katika familia nyingi
Mratibu wa CWM, Edson Yeyeye, alisisitiza kuwa jitihada hizi zitaendelea hadi sauti za wafanyakazi wa majumbani zisikike na kuheshimiwa kikamilifu.
 “Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha haki na heshima kwa kila mfanyakazi wa majumbani, kwani mchango wao katika familia na jamii hauwezi kupuuzwa,” alisema Yeyeye.
Sasa ni wakati wa jamii kushirikiana ili kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi wa majumbani anapata heshima anayostahili, na mahusiano ya kazi yanajengwa kwa misingi ya haki na usawa.
Nashauri wafanyakazi wa majumbani wapewe elimu ya malezi na maadili mara kwa mara, kwa sababu katika nyumba nyingi za mijini na hata vijijini, sauti ya mfanyakazi wa majumbani ndiyo inayopokelewa kwanza asubuhi, ikiongoza familia katika maandalizi ya siku.
Wakati mwingine, wao ndio waangalizi wa karibu wa watoto; wanahakikisha wanakula, wanavaa, na mara nyingi hata wanasaidia katika kujenga maadili ya msingi kwa watoto hao, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha kusoma au kuandika. Hata hivyo, mchango huu wa kipekee mara nyingi unapuuzwa, ukifichwa na mwanga wa jukumu lao la kazi za nyumbani.

MELBOURNE, Australia
Alexander Zverev amekerwa na shabiki kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa hafla ya kupokea tuzo ya Australian Open.
Mchezaji huyo namba mbili wa Ujerumani, alishindwa kwa seti moja kwa moja kutoka kwa nambari moja duniani, Jannik Sinner huko Melbourne.
Alipopiga hatua kupokea kombe lake la washindi wa pili, shabiki mmoja alipaza sauti: “Australia inaamini katika Olya na Brenda.”
Mchezaji huyo alishitakiwa kwa kumnyanyasa mpenzi wake wa zamani Olya Sharypova mnamo mwaka 2020, na unyanyasaji wa nyumbani mnamo 2023 aliyofanya kwa Brenda Patea, ambaye alizaa nae mtoto mmoja.
Zverev mara kwa mara amekuwa akikanusha kesi zote mbili za madai, na kesi ya mahakama ya Berlin iliyoletwa na Patea ilikomeshwa mwaka jana.
Mnamo Oktoba 2020, mpenzi wa zamani Sharypova, alimshtaki Zverev kwa vurugu na unyanyasaji wa kihemko wakati wa uhusiano wao. Zverev alikanusha madai hayo na kusema, “hayana msingi”.
Sharypova hakufungua mashtaka, na uchunguzi wa miezi 15 wa ATP Tour ya wanaume uligundua kuwa hakuna “ushahidi wa kutosha” kuthibitisha madai yaliyotolewa na Sharypova, na hivyo Zverev hakukabiliwa na hatua za kinidhamu.

LEICESTER, Uingereza
Baraza la majaji limestaafu kuanza mashauri yake katika uchunguzi wa vifo vya watu watano waliofariki katika ajali ya helikopta nje ya Uwanja wa King Power wa Leicester City.
Mwenyekiti wa Foxes, Vichai Srivaddhanaprabha alifariki pamoja na abiria wenzake Kaveporn Punpare, Nusara Suknamai, rubani Eric Swaffer na mshirika wake Izabela Roza Lechowicz, Oktoba 27 mwaka 2018.
Siku ya Jumatatu, mchunguzi wa maiti Catherine Mason, alihutubia baraza la majaji, huku uchunguzi ukiingia wiki ya tatu katika Ukumbi wa Jiji la Leicester.
Prof Mason aliita ajali hiyo “msiba mbaya”, huku akiagiza baraza la mahakama kwamba hitimisho la bahati mbaya tu, lingeweza kufikiwa.
Aliwaambia majaji 11 kwamba watajibu maswali manne. Kila mtu aliyekufa alikuwa nani? Walikufa lini? Walifia wapi? Na, walikujaje na kifo chao?
“Hilo lisijumuishe mambo kama mifumo, taratibu, na tahadhari ambazo zingeweza kusababisha helikopta na kubeba kubuniwa kwa njia tofauti,” aliongeza.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Tenisi ni mchezo unaofurahiwa na washiriki wa rika zote na viwango vyote. Mchezo huo umekuwa ukivutia watazamaji na wachezaji tangu mwanzoni mwa karne ya 12.
Hapa kuna ukweli na maendeleo ya kupendeza ambayo yametokea tangu historia ya mapema ya tenisi.
RAKETI:
Raketi ni kifaa cha kuchezea mchezo wa tenisi, ambacho kazi yake ni kupigia mpira huo.
Kabla ya wachezaji wa tenisi kutumia raketi, watu walianza kutumia kiganja cha mikono yao kupiga mpira na kuurudisha juu ya wavu.
Watu katika karne ya 12 waliteseka kutokana na kuvimba mikono  katika mchezo wa jamii ya tenisi ulioitwa ”jeu de paume” unaomaanisha “mchezo wa mitende.”
Hali hiyo haikuchukua muda mrefu, kwani ilikwenda hadi karne ya 16 ambapo ‘racquets’ zilitumiwa ingawa kabla ya raketi walitumia matawi ya mnazi yaliyosukwa kupigia mpira.
RANGI ZA MIPIRA:
Kabla ya mipira ya tenisi yenye rangi ya njano kuletwa mchezoni, kulikuwa na mipira myeupe.
Mipira myeupe ilitumika tangu mchezo huo unatambulishwa duniani, hadi pale iipoanzishwa michuano ya Wimbledon mnamo mwaka 1986, wakati mipira ya tenisi ya njano ilipotumiwa.
Maafisa waliamini kuwa mpira wa njano ungekuwa rahisi kwa watazamaji kutazama kwenye TV, na hiyo ndiyo ikawa sababu ya kutumia mipira ya rangi hiyo.
MAILI TATU:
Wakati wa mechi ya tenisi, mchezaji kwa wastani hukimbia maili 3.
Kwa sababu ya udogo wa uwanja wa tenisi, hiyo ni maili 3 ngumu zaidi ya mchezaji kwenda mbele na kurudi nyuma mara zote.
MKANGANYIKO WA RAKETI:
Raketi ya tahajia ndiyo njia ya kawaida ya kutamka kifaa kinachotumika katika michezo ya wavu, kama vile tenisi.
Kwa Kiingereza, kuna maneno mawili yanatofautiana kwenye kuandika, lakini yanafanana kimatamshi. Racket na racquet hutofautiana kwenye matumizi, ambapo Racket ni kifaa ambacho hutumika kwa kuchezea tenisi, na Racquet hutumika kuchezea michezo mingine, kama vile skwashi.
Ingawa tovuti nyingi zitakuambia kuwa raketi ni tahajia sahihi, USTA mara kwa mara hutumia raketi ya tahajia.
DADA WA FAMILIA MOJA:
Venus na Serena Williams walikuwa seti ya kwanza ya kina dada kushinda medali za dhahabu za Olimpiki katika historia ya tenisi.
Akina dada hao walishinda medali yao ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki katika Michezo ya Olimpiki ya Sydney mwaka 2000.
Sasa wana medali mbili za ziada za dhahabu kutoka Beijing 2008 na London 2012.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Mtibwa Sugar ya Morogoro imesema kwa ubora inayouonyesha kwenye Ligi ya Chamionship kwa sasa, ni kama vile walitoka Ligi Kuu mara moja na kwenda kutalii, ili kuona hali ya hewa ya huko.
Mtibwa imekuwa ikionyesha kiwango bora tangu msimu wa Championship uanze, Ligi ambayo zamani ilifahamika kama Daraja la Kwanza, ambayo huzipokea timu zinazoshuka daraja kutoka Ligi Kuu.
Mtibwa ambayo ipo kileleni mwa Ligi hiyo, endapo itaendelea kukaza uzi, itafanikiwa kurejea tena Ligi Kuu, ambapo msimu uliopita ilishuka daraja baada ya kuwa na matokeo mabovu.
Afisa Habari wa ‘Wakata miwa’ hao. Thobias Kifaru alisema kwamba ushiriki wao wa Championship ni kama wanafanya utalii, ili kujua mandhari yake, na kisha kurudi Ligi Kuu kuwasimulia wengine maisha ya huko.
“Huku ni kama tumekuja kutalii na kujionea maisha ya Chamionship yalivyo, halafu tutarejea zetu Ligi Kuu tukiwa tuna taarifa zote za kinachoendelea huko kwa sababu kwa sasa hatukamatiki na tunajihisi hatuna mpinzani wa kutusumbua,”alisema Kifaru.
Alisema kwamba imani yao ni kuona wanarejea kwenye Ligi Kuu msimu ujao na kujiwekea mipango ya kuhakikisha hawashuki tena daraja kwa sababu chanzo wameshakijua, na wamejifunza.
Hivi karibuni Mtibwa ilicheza mechi ya kirafiki na Azam FC na kuiadabisha kwa kuichapa bao 1-0 kwenye mchezo uiopigwa Manungu Complex mjini Morogoro.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Siku chache baada ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kupaa hadi nafasi ya nne kwa ubora barani Afrika, timu shiriki za Ligi hiyo zimeshauriwa kuongeza ushindani ili kuondoa mazoea ya timu zile zile kupokezana ubingwa.
Hayo yamesemwa na beki wa zamani wa Taifa Stars Bakari Malima wakati akitoa mtazamo wake kuhusiana na ubora wa Ligi hiyo ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya zamani.
Alisema kuwa bado kumekuwa na kasumba ya Ligi hiyo kuwa na ushindani wa timu tatu ama nne zinazowania ubingwa kila msimu, huku timu zingine zikiwa zinashiriki kuwania kutoshuka daraja.
“Ligi Kuu ni bora, lakini kila msimu kumekuwa na ushindani wa timu tatu ama nne pekee, ambazo zinawania ubingwa.Sasa kwenye hilo, kunahitaji uboreshaji hasa kwa timu zenyewe kuongeza ushindani ili kuleta uimara,”alisema Malima.
Alisema pia kuwa ifike wakati bingwa wa Ligi Kuu asitabirike kirahisi, kwa maana ya kwamba ikitokea Yanga ameyumba, basi Simba anapewa nafasi, au ikitokea Simba kayumba kwenye msimu, Yanga anapewa nafasi ya ubingwa katika wakati ambao hata msimu haujafika katikati.
Malima alisema kwamba hata mechi zinazohusisha Simba, Yanga na Azam FC dhidi ya timu zingine, bado imekuwa ni rahisi sana kutabiri nani atashinda, tofauti na ilivyo katika Ligi zingine.
Alitolea mfano Ligi Kuu ya Uingereza, ambayo kila msimu imekuwa ni ngumu kumtabiri bingwa pamoja na mechi moja moja zinazochezwa ambazo mshindi amekuwa haeleweki, na hivyo kuwapa shida watu wanaobashiri mechi hizo.
Katika hatua nyingine, Malima alisema kuwa uongozi bora na ubora wa miundombinu, ndiyo silaha kubwa ya kupanda viwango kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Alisema kwamba katika miaka ya zamani ambayo yeye alicheza soka, Chama cha Soka nchini FAT (Football Association of Tanzania) kwa wakati ule, kilitawaliwa na migogoro ya mara kwa mara, huku viwanja vingi vya kuchezea vikiwa chakavu.
“Ninakumbuka zamani uwanja mzuri ambao wachezaji tulikuwa tunapenda kuuchezea ni wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza lakini zaidi ya huo, hakukuwepo na uwanja mwingine mzuri. Hata wa Uhuru haukuwa sawa kwenye eneo la kuchezea,”alisema Malima.